Mageuzi ya ardhi yanavyobadili uchumi Tanzania

    • Author, Yusuph Mazimu
    • Akiripoti kutoka, BBC Dar es Salaam
  • Iliyochapishwa
  • Muda wa kusoma: Dakika 4

Wakazi wa Kijiji cha Ngea, Wilaya ya Kilwa, Lindi wanaitazama hati zao za ardhi kwa makini kana kwamba wameshika kitu cha thamani kuliko karatasi. Kwa miaka mingi waliishi na kuendesha shughuli zao kwenye ardhi hiyo bila uthibitisho rasmi wa umiliki, hali iliyowafanya kuwa na wasiwasi wa rasilimali hiyo kwenye kujiletea maendeleo.

Leo, hati hiyo imebadili mtazamo wao. "Kwa miaka mingi tulikuwa tunaishi kwenye ardhi hii, lakini leo nina uhakika kwamba ni mali yangu halali. Nikitaka kuwekeza au hata kwenda benki, sasa nina kitu cha kuonyesha," anasema mmoja wao.

Wananchi wa Ngea siyo peke yao. Katika maeneo mbalimbali nchini Tanzania, wananchi wanaanza kuitazama ardhi kwa mtazamo tofauti. Badala ya kuiona kama sehemu ya kujenga nyumba au kulima pekee, wanaiona kama mali inayoweza kuzalisha mtaji, kuongeza uzalishaji na kubadili maisha yao.

Mtazamo huo unaibuka wakati Serikali ikiendelea kutekeleza mageuzi makubwa ya sekta ya ardhi kupitia upimaji wa viwanja, utoaji wa hatimiliki, urasimishaji wa makazi na matumizi ya mifumo ya kidijitali katika usimamizi wa ardhi.

Unaweza kujiuliza, mageuzi ya ardhi yanaweza kweli kuwa kichocheo cha ukuaji wa uchumi wa Tanzania?

Ardhi: Rasilimali inayobadili uchumi

Ardhi ndiyo msingi wa karibu kila shughuli ya uzalishaji nchini. Kilimo, makazi, viwanda, uchimbaji madini, miundombinu na uwekezaji vyote hutegemea namna rasilimali hiyo inavyopangwa na kusimamiwa. Ndiyo maana wataalamu wa maendeleo wanaiona ardhi kama mtaji ambao kwa muda mrefu haukutumika kikamilifu.

Kwa mujibu wa Sera ya Taifa ya Ardhi ya mwaka 1995 (Toleo la 2023), takribani asilimia 65 ya Watanzania wanategemea kilimo kwa maisha yao, huku karibu asilimia 80 ya wananchi wa vijijini wakitegemea ardhi kwa uzalishaji wa chakula, kipato na ustawi wa familia zao.

Hata hivyo, sehemu kubwa ya ardhi hiyo imekuwa ikitumika bila umiliki rasmi au mipango madhubuti ya matumizi.

Kwa mwekezaji wa sekta ya ardhi, Philipo Mushi wa Mwendapole Real Estate, thamani ya ardhi huanza pale inapokuwa mali inayoweza kutambulika na kutumika kiuchumi. "Ardhi ni maisha yako ya leo na kesho na ya vizazi vyako. Unaweza kuigeuza kuwa kitega uchumi, na ndicho kitu pekee ambacho ukikinunua leo kinaendelea kupanda thamani kila siku," anasema.

Mtazamo huo unaungwa mkono na mtaalamu wa maendeleo ya uchumi wa jamii, Raphael Kugesha, ambaye anasema: "Hati ya ardhi si karatasi; ni pasipoti ya uchumi." Kwa maoni yake, umiliki ulio salama unafungua milango ya uwekezaji, mikopo na matumizi yenye tija ya ardhi.

Ndiyo msingi wa mageuzi yanayoendelea nchini. Lengo lake si kuongeza idadi ya hati pekee, bali kuifanya ardhi itambulike kama mtaji unaoweza kuchochea uzalishaji, kuvutia uwekezaji na kuongeza mchango wake katika maendeleo ya taifa.

Ramani mpaka thamani ya uchumi

Katika kipindi cha Serikali ya awamu ya sita, mageuzi ya usimamizi wa ardhi yameanza kuonekana kupitia takwimu na mifumo mipya ya utoaji huduma. Kwa mujibu wa Taarifa ya Mafanikio ya Serikali ya Awamu ya Sita (2020–2025), viwanja 1,427,005 na mashamba 11,699 vimepimwa, huku hatimiliki 356,642 na nyaraka nyingine za kisheria 444,447 zikitolewa.

Aidha, hati za kimila 318,868 zimesajiliwa katika vijiji 236, hatua inayolenga kuongeza usalama wa umiliki wa ardhi vijijini.

Mbali na umilikishaji, Serikali imeidhinisha maombi 719 ya ardhi yenye ukubwa wa zaidi ya hekta 146,363,240 kwa ajili ya uwekezaji. Takwimu hizo zinaonyesha kuwa usimamizi bora wa ardhi hauhusiani tu na wananchi binafsi, bali pia na uwezo wa nchi kuvutia mitaji katika sekta za kilimo, viwanda, utalii na maendeleo ya miundombinu.

Mageuzi hayo yanaenda sambamba na matumizi ya teknolojia. Wakati akiwa Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Deogratius Ndejembi, alisema mfumo wa e-Ardhi umeanza kutumika katika majiji ya Dar es Salaam, Dodoma, Arusha, Mbeya na Tanga ili kuboresha usimamizi wa taarifa za ardhi. "Tayari tumeanza kutumia mfumo wa e-Ardhi. Huu utasaidia kupunguza migogoro ya ardhi na changamoto ya double allocation. Master plan zetu zitakuwa ndani ya mfumo," anasema.

Kwa mtaalamu wa ardhi Afrika Mashariki, Reginald Okumu, hatua hizo zina maana kubwa kuliko kuhamisha taarifa kutoka kwenye makabrasha kwenda kwenye kompyuta. "Ukifanikiwa kupima ardhi unaipa thamani ya dhahabu. Unarahisisha mipango ya maendeleo na kuongeza thamani yake kiuchumi," anasema.

Waziri wa sasa wa ardhi, Dkt. Leonard Akwilapo, na yeye anasisitiza kuhusu matumizi ya mifumo hii, akipigia chapuo pia wanawake kutoachwa nyuma.

"Ardhi ni msingi wa uchumi wa mwananchi na Taifa. Mwanamke anapomiliki ardhi kisheria anapata uwezo mkubwa wa kuwekeza, kufanya shughuli za uzalishaji na hata kupata mikopo katika taasisi za fedha," alisema.

Je, mageuzi yanaonekana?

Kwa Jane Ndesi wa Kilosa, mabadiliko hayo si takwimu kwenye ripoti za serikali, bali ni sehemu ya maisha yake. "Sikuamini kama kuna siku ningekuja kumiliki ardhi. Imebadilisha kila kitu; leo naitumia kwenye biashara, nimejenga na hata nakopea. Kwangu ni kama mgodi wa dhahabu," anasema.

Katika Kijiji cha Ngea, Kilwa, Mwenyekiti wa kijiji hicho Ally Kinunge aliwakumbusha wananchi waliokabidhiwa hati za ardhi kwamba thamani yake ipo katika namna watakavyoitumia. "Si utajiri huo! Mzitunze. Mkitaka kwenda benki, hizi ndizo zitawasaidia," aliwaambia wakati wa hafla ya ugawaji wa hati.

Na hata kwa upande wa Jacob Ernest wa Mwanza, uzoefu wake unaonyesha jinsi ardhi inaweza kuwa chanzo cha utajiri inapopata thamani ya soko. "Niliwahi kununua ardhi na kuiuza, nikapata faida karibu mara nne ndani ya miaka mitano. Najuta sikununua eneo kubwa zaidi; leo ningekuwa zaidi ya milionea," anasema.

Hata hivyo, wataalamu wanaeleza mafanikio katika sekta ya ardhi yatapimwa kwa uwezo wa wananchi kuzitumia hati za umiliki wanazopata kuongeza uzalishaji, kupata mitaji, kuanzisha biashara na kuvutia uwekezaji unaozalisha ajira na mapato.

Mtaalamu maendeleo ya uchumi wa jamii, Raphael Kugesha, anasema hilo ndilo litakuwa kipimo halisi cha mageuzi. "Kama kuna mahali nchi inaweza kufanya mapinduzi makubwa (ya kiuchumi) basi ni kwenye ardhi."