Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Tanzania inavyoijenga upya historia ya ardhi
- Author, Yusuph Mazimu
- Akiripoti kutoka, BBC Dar es Salaam
- Iliyochapishwa
- Muda wa kusoma: Dakika 5
Miaka zaidi ya thelathini iliyopita nilikuwa mwanafunzi nikiishi katika Kijiji cha Ilonga, Wilaya ya Kilosa, Morogoro. Vijiji vya Rudewa, Mbwade, Chanzuru na Kimamba A na B, vilikuwa sehemu ya maisha yetu ya kila siku, lakini pia vilikuwa sehemu ya hofu iliyotanda baada ya migogoro ya wakulima na wafugaji kugeuka kuwa mapigano ya mara kwa mara. Hapo ndipo nilipoanza kuelewa kwamba mgogoro wa ardhi hauishii kwenye mipaka ya mashamba; unaweza kugusa maisha ya jamii nzima.
Mnamo Desemba 8, 2000, mapigano kati ya wakulima na wafugaji katika Kijiji cha Rudewa-Mbuyuni yaliua wakulima 38. Tukio hilo, pamoja na migogoro iliyofuata katika maeneo ya Dumila na Mbigili, liliifanya Kilosa kuwa moja ya vielelezo vinavyotajwa mara nyingi katika historia ya migogoro ya matumizi ya ardhi nchini.
Juma Shomvu, mkazi wa Kilosa aliyeshuhudia kipindi hicho, anasema kumbukumbu hizo bado hazijafutika. "Nakumbuka ukitoka Ilonga kwenda Rudewa au Kimamba kupitia Mbugani, kila safari ilikuwa imejaa hofu. Tulikuwa tunaingia majumbani mapema kwa sababu hakuna aliyejua nini kingetokea," anasema.
Zaidi ya miaka ishirini baadaye, niliporudi Kilosa, nilikuta picha tofauti. Vijiji vingi vina mipango ya matumizi ya ardhi, wananchi wanapewa hati za kimila na mipaka imeainishwa. Shomvu anasema: "Leo unaweza kunywa chai Ilonga, ukala chakula cha mchana Rudewa na ukalala Chanzuru bila hofu. Sitaki hata kuyakumbuka maisha yale."
Kilosa kama mfano, lakini maeneo mengi ya Tanzania, upimaji na hati za umiliki wa ardhi zinatolewa zikiwemo za kimila. Ni hatua hii inayoendelea inaandika historia mpya ya ardhi Tanzania?
Historia ya migogoro mpaka mipango
Kwa miaka mingi, migogoro ya ardhi nchini Tanzania imekuwa ikichochewa na ukosefu wa mipaka iliyo wazi, matumizi yanayokinzana ya ardhi na udhaifu wa mipango ya matumizi ya maeneo ya vijiji. Hali hiyo iliwakutanisha wakulima na wafugaji kwenye rasilimali zilezile bila utaratibu unaokubalika na pande zote.
Kuna wakati ulifanyika utafiti wa African Capacity Building Foundation (ACBF) kuhusu migogoro ya wakulima na wafugaji Tanzania, ambao ulibainisha kuwa chanzo kikuu cha migogoro mingi ni ukosefu wa usalama wa umiliki wa ardhi, kutokuwepo kwa mipango ya matumizi ya ardhi katika vijiji vingi pamoja na mapungufu ya sera na usimamizi wa rasilimali hiyo.
Utafiti huo ukaonya kuwa bila kurejesha uhakika wa umiliki wa ardhi kwa wakulima na wafugaji, migogoro itaendelea kujirudia. Serikali ikaliona hilo.
Katika jitihada za kukabiliana na changamoto hizo, Serikali imehakiki mipaka ya vijiji 974 katika wilaya mbalimbali nchini na kuendelea kuandaa mipango ya matumizi bora ya ardhi katika maelfu ya vijiji. Hatua hizo zinakusudia kupunguza migongano ya matumizi ya ardhi kabla haijazaa migogoro.
Athari za hatua hizo zinaanza kuonekana katika maeneo kama Kilosa. Aliyewahi kuwa Afisa Mtendaji wa Kijiji cha Madizini, Cosmas Tayari, alisema kabla ya upimaji na utoaji wa hati za kimila kijiji hicho kilikuwa kinapokea migogoro mingi ya ardhi, lakini baada ya wananchi kupimiwa maeneo yao na kupewa umiliki rasmi, migogoro hiyo ilipungua kwa kiasi kikubwa.
Kwa Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Adam Malima, maboresho ya usimamizi wa ardhi yameongeza uwezo wa serikali kushughulikia migogoro. "Kuwa na kumbukumbu nzuri za wamiliki wa ardhi jambo hili limetusaidia kama Mkoa wa Morogoro kutatua migogoro ya ardhi pale inapojitokeza," anasema
Historia mpya huanzia kwenye ramani
Mageuzi ya sasa hayajajikita kwenye utoaji wa hati pekee, bali kwenye kujenga mfumo wa kisasa wa usimamizi wa ardhi. Kwa mujibu wa Taarifa ya Mafanikio ya Serikali ya Awamu ya Sita (2020–2025), viwanja 1,427,005 na mashamba 11,699 vimepimwa, huku hatimiliki 356,642 na nyaraka nyingine za kisheria 444,447 zikitolewa.
Aidha, hati za kimila 318,868 zimeandaliwa na kusajiliwa katika vijiji 236 vya wilaya za Songwe, Chamwino, Mufindi, Mbinga, Maswa na Tanganyika, hatua inayolenga kuongeza usalama wa umiliki wa ardhi kwa wananchi wa vijijini.
Serikali pia imeidhinisha maombi 719 ya ardhi kwa ajili ya uwekezaji yenye ukubwa wa zaidi ya hekta 146,363,240, ikionyesha kwamba usimamizi bora wa ardhi unaonekana pia kama nyenzo ya kuvutia uwekezaji na kuchochea ukuaji wa uchumi.
Sambamba na hilo, Wizara ya Ardhi imeanza kutumia mfumo wa kidijitali wa e-Ardhi katika majiji ya Dar es Salaam, Dodoma, Arusha, Mbeya na Tanga. Aliyekuwa Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Deogratius Ndejembi, alitoa taarifa kwamba mfumo huo utasaidia kupunguza migogoro ya ardhi na kuondoa changamoto ya kugawa eneo moja kwa watu zaidi ya mmoja. "Master plan zetu zitakuwa ndani ya mfumo. Hii inatusaidia kuondoka na migogoro ambayo haina ulazima wa kutokea," anasema.
Na hata Waziri wa sasa wa Ardhi Dkt. Leonard Akwilapo, amekuwa aihimiza usimamizi mzuri wa matumizi ya mifumo hii, pamoja na kusaidia kupunguza migogoro, lakini kurahisisha ufanisi.
Kwa wataalamu wa mipango miji, ramani na taarifa sahihi za ardhi si nyaraka za kiutawala pekee; ndizo msingi wa kupanga makazi, huduma za jamii, uwekezaji na matumizi endelevu ya ardhi kwa vizazi vijavyo.
Je, historia mpya imeanza kuandikwa?
Kwa mtaalamu wa maendeleo ya uchumi wa jamii, Raphael Kugesha, mageuzi ya ardhi hayawezi kupimwa kwa idadi ya hati zinazotolewa pekee. "Kama kuna mahali nchi inaweza kufanya mapinduzi makubwa ni kwenye ardhi," anasema, akisisitiza kuwa usimamizi bora wa ardhi unaweza kubadili uchumi, ustawi wa jamii na utulivu wa taifa.
Mtazamo huo unaungwa mkono na mashirika ya kimataifa kama UN-Habitat, ambayo yanaeleza kuwa usimamizi bora wa ardhi ni msingi wa miji endelevu, maendeleo jumuishi na kupunguza migogoro inayotokana na matumizi ya rasilimali.
Hata hivyo, changamoto bado zipo. Kasi ya ukuaji wa miji, ongezeko la watu, migogoro ya matumizi ya ardhi na utekelezaji wa mipango katika baadhi ya maeneo vinaonyesha kuwa safari ya mageuzi bado haijafika mwisho. Mfumo mpya utahitaji kuendelea kuimarishwa ili uendane na mahitaji ya baadaye.
Lakini tofauti na miaka ya nyuma, mjadala wa leo hauishii kwenye nani anamiliki ardhi. Unazidi kuelekea kwenye namna ardhi itakavyotumika kwa tija, kwa haki na kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho.
Wachambuzi wanasema huenda historia mpya ya ardhi Tanzania isiandikwe kwa idadi ya hati zitakazotolewa wala kilomita za mipaka zitakazowekwa. Itaandikwa na uwezo wa mageuzi haya kuendelea kupunguza migogoro, kujenga imani ya wananchi katika mfumo wa usimamizi wa ardhi na kuweka msingi wa maendeleo yatakayodumu kwa vizazi vijavyo.