Kwa nini tunapaswa kuitunza mifupa mapema?

Fahamu vyakula vinavyosaidia kuimarisha mifupa kadiri umri unavyoongezeka

d

Huenda ulizoea kuambiwa unywe maziwa ukiwa mtoto ili uwe na mifupa imara. Lakini je, unajua kuwa mifupa yako huanza kupoteza uimara mapema kuliko unavyoweza kudhani? Kuna vyakula unavyoweza kula sasa ili kusaidia kuilinda mifupa yako na kupunguza hatari ya kudhoofika kadiri unavyozeeka.

Huenda bado unakumbuka jinsi ulivyohimizwa kumaliza glasi yako ya maziwa ukiwa mtoto, kwa kuambiwa kuwa yatakusaidia kukua na kuwa na mifupa imara.

Na kwa hakika, maziwa ni chanzo kizuri cha kalisiamu, madini muhimu katika kujenga na kudumisha uimara wa mifupa.

Lakini kuna jambo ambalo wengi wetu hatulizingatii sana tunapokuwa watu wazima. Afya ya mifupa haihusu tu kile tunachokula tukiwa watoto. Ni jambo tunalopaswa kuendelea kulizingatia katika maisha yetu yote.

Kadiri umri unavyoongezeka, mifupa huanza kupoteza msongamano wa madini na hivyo kuwa dhaifu zaidi. Hali hii inaweza kuongeza uwezekano wa kuvunjika kwa mifupa, hata kutokana na kuanguka kwa namna ambayo huenda isingesababisha madhara makubwa hapo awali.

Kwa bahati nzuri, bado unaweza kuchukua hatua za kuilinda mifupa yako, bila kujali una umri gani.

Na si lazima utegemee maziwa pekee. Kuna vyakula mbalimbali, vikiwemo samaki, mboga za majani, soya, matunda na mbegu, ambavyo vina virutubisho muhimu kwa afya ya mifupa.

Lakini kwa nini ni muhimu kuanza kuitunza mifupa mapema? Na ni vyakula gani unapaswa kuvijumuisha katika mlo wako ili kuifanya iendelee kuwa imara?

Kwa nini tunapaswa kuitunza mifupa mapema?
Iliyochapishwa
Muda wa kusoma: Dakika 8
Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili WhatsApp bofya kutufuatilia
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Huenda usifikirie sana kuhusu afya ya mifupa yako ikiwa bado huna maumivu au matatizo ya kutembea. Lakini wataalamu wanasema usisubiri dalili zijitokeze ndipo uanze kuchukua hatua.

Afya ya mifupa ya mtu anapokuwa mzee huathiriwa kwa kiasi kikubwa na jinsi mifupa yake ilivyojengwa tangu utotoni na mwanzoni mwa utu uzima.

Katika kipindi hicho, mifupa hukua na kujenga msongamano mkubwa wa madini kabla ya kufikia kiwango chake cha juu cha uimara mwanzoni mwa utu uzima.

Kate Ward, profesa wa afya ya mifupa na misuli katika Chuo Kikuu cha Southampton nchini Uingereza, anasema akiba ya madini na uimara wa mifupa tunayojenga katika miaka hiyo ya awali ina mchango mkubwa katika afya ya mifupa yetu tunapozeeka.

Baada ya kufikia kiwango chake cha juu cha uimara, mifupa huanza kupoteza msongamano wa madini kadiri umri unavyoongezeka.

Tatizo hili ni kubwa zaidi kuliko wengi wanavyoweza kudhani. Takribani watu milioni 500 duniani wanaishi na osteoporosis, ugonjwa unaofanya mifupa iwe myembamba, dhaifu na rahisi kuvunjika.

Changamoto ni kwamba mara nyingi ugonjwa huu hauonyeshi dalili za wazi. Mtu anaweza kuendelea na shughuli zake za kawaida bila kujua kuwa mifupa yake inadhoofika, hadi pale anapovunjika mfupa.

Julie Thompson, kutoka Shirika la Kifalme la Osteoporosis nchini Uingereza, anasema magonjwa kama osteoporosis na osteopenia mara nyingi hugunduliwa baada ya mtu kuvunjika mfupa, jambo ambalo linaweza kuwa na madhara makubwa kwa maisha yake.

Hasa inapohusu mifupa ya nyonga. Zaidi ya visa milioni 10 vya kuvunjika kwa mifupa ya nyonga huripotiwa kila mwaka duniani miongoni mwa watu wenye umri wa zaidi ya miaka 55.

Kuvunjika kwa mfupa wa nyonga kunaweza kusababisha matatizo mengine makubwa ya kiafya, yakiwemo nimonia na mshtuko wa moyo.

Tafiti zinaonyesha kuwa takribani asilimia 30 ya wagonjwa wenye umri wa zaidi ya miaka 60 hufariki dunia ndani ya mwaka mmoja baada ya kuvunjika mfupa wa nyonga. Hata hivyo, umri na magonjwa mengine ambayo mtu alikuwa nayo kabla ya kuvunjika kwa mfupa huo yanaweza pia kuchangia.

Wanawake wako katika hatari kubwa zaidi ya kupoteza msongamano wa madini kwenye mifupa, hasa wanapofikia ukomo wa hedhi. Hii inahusishwa na mabadiliko ya homoni yanayotokea katika kipindi hicho.

Lakini wanaume pia wanaweza kupata osteoporosis. Bess Dawson-Hughes, profesa wa tiba katika Chuo Kikuu cha Tufts, anasema kwa muda mrefu ugonjwa huo ulionekana zaidi kama tatizo la wanawake kwa sababu wanaume wengi hapo awali hawakuishi muda mrefu kiasi cha kuonyesha dalili zake.

Kwa hiyo, ni vyakula gani vinaweza kutusaidia kuimarisha mifupa yetu?

Maziwa, jibini na mtindi

s

Tuanze na vyakula ambavyo huenda tayari unavifahamu. Maziwa, jibini na mtindi ni vyanzo vizuri vya kalisiamu, madini yanayohitajika katika kujenga na kudumisha mifupa imara.

Kwa mfano, glasi moja ya maziwa yenye ujazo wa mililita 200 ina takribani miligramu 260 za kalisiamu.

Lakini kalisiamu si kirutubisho pekee unachopaswa kuzingatia. Mwili pia unahitaji vitamini D ili kusaidia kufyonza kalisiamu, pamoja na protini inayosaidia kudumisha afya ya mifupa na misuli.

Virutubisho vingine kama vitamini K, magnesiamu, zinki na fosforasi pia vina mchango muhimu.

Utafiti mmoja uliowahusisha wazee 7,195 waliokuwa wakiishi katika vituo vya kulea wazee ulichunguza manufaa ya kuongeza matumizi ya bidhaa za maziwa na protini.

Baada ya miaka miwili, watafiti walibaini kuwa washiriki waliotumia bidhaa nyingi zaidi za maziwa walikuwa na uwezekano mdogo kwa asilimia 11 wa kuanguka. Hatari yao ya kuvunjika mifupa ya nyonga pia ilikuwa chini kwa asilimia 46.

Watafiti wanadhani huenda mchanganyiko wa kalisiamu na protini ndio uliosaidia kupata matokeo hayo.

Kuhusu kiasi cha kalisiamu kinachohitajika kila siku, mapendekezo hutofautiana kulingana na umri, jinsia na nchi.

Nchini Uingereza, watu wazima wanashauriwa kupata takribani miligramu 700 za kalisiamu kila siku. Kwa walio katika hatari ya kupata osteoporosis, kiwango kinachopendekezwa ni miligramu 1,000 kwa siku.

Wanawake ambao wamefikia ukomo wa hedhi wanashauriwa kulenga kupata miligramu 1,200 kila siku.

Nchini Marekani, watu wazima wanashauriwa kutumia kati ya miligramu 1,000 na 1,200 za kalisiamu kila siku, kutegemea umri na jinsia zao.

Soya

Ikiwa hutumii maziwa au unapenda kubadilisha aina ya vyakula unavyokula, soya inaweza kuwa chaguo jingine zuri.

Vyakula kama tofu na maharagwe ya edamame vina kalisiamu. Kwa mfano, gramu 100 za tofu zina takribani miligramu 200 za madini hayo.

Tafiti zinaonyesha kuwa ulaji wa vyakula vya soya unaweza kupunguza hatari ya kuvunjika kwa mifupa.

Soya ina aina ya kemikali asilia inayopatikana kwenye mimea, inayofanana na homoni ya estrogeni, inayojulikana kama isoflavone.

Tafiti pia zimeonyesha kuwa wanawake waliokoma hedhi wanaotumia virutubisho vya soya kwa wingi wanaweza kuwa na msongamano mkubwa zaidi wa madini kwenye mifupa.

Uchambuzi wa tafiti mbalimbali uliohusisha zaidi ya wanawake 9,000 waliokoma hedhi ulibaini kuwa wale waliotumia virutubisho vya isoflavone vinavyopatikana kwenye soya walionyesha ongezeko dogo la msongamano wa madini kwenye mifupa ya uti wa mgongo, nyonga na sehemu ya chini ya mkono.

Faida kubwa zaidi zilionekana miongoni mwa waliotumia virutubisho hivyo kwa viwango vya juu kwa angalau mwaka mmoja. Hata hivyo, tafiti zaidi zinahitajika ili kubaini manufaa ya kula vyakula vya soya ikilinganishwa na kutumia virutubisho vyake.

Chanzo kingine cha soya ni tempeh, chakula kinachotengenezwa kwa njia ya uchachushaji. Mchakato huo huvunja baadhi ya kemikali zinazojulikana kama vizuia ufyonzwaji wa virutubisho, ambazo zinaweza kuathiri uwezo wa mwili kufyonza madini muhimu kwa afya ya mifupa.

Matokeo yake ni kwamba mwili unaweza kufyonza kalisiamu kwa urahisi zaidi kutoka kwenye tempeh.

Mbegu za chia

d

Huenda umezoea kuziona mbegu za chia zikiongezwa kwenye uji, mtindi au vinywaji mbalimbali. Lakini mbegu hizi pia zina virutubisho vinavyohitajika kwa afya ya mifupa.

Chia zina kalisiamu, magnesiamu na fosforasi. Kijiko kimoja cha chakula kina takribani miligramu 95 za kalisiamu.

Pia zina mafuta ya omega 3, ambayo husaidia kupunguza uvimbe mwilini.

Kwa nini hilo ni muhimu kwa mifupa?

Uvimbe wa muda mrefu unaweza kuvuruga uwiano kati ya kuvunjwa kwa tishu za zamani za mifupa na kujengwa kwa tishu mpya. Mwili unapovunja mifupa kwa kasi zaidi kuliko unavyoweza kuijenga upya, hatari ya kupata osteoporosis inaweza kuongezeka.

Katika utafiti uliofanywa kwa wanyama, panya waliolishwa mbegu za chia kwa zaidi ya mwaka mmoja walikuwa na kiwango kikubwa zaidi cha madini kwenye mifupa ikilinganishwa na wale waliolishwa chakula cha kawaida.

Hata hivyo, bado haijathibitishwa iwapo matokeo kama hayo yanaweza kupatikana kwa binadamu.

Matunda yaliyokaushwa kama plamu na tini

Unapofikiria vyakula vya kuimarisha mifupa, huenda matunda yaliyokaushwa yasiwe miongoni mwa vitu vya kwanza vinavyokuja akilini.

Lakini matunda kama tini, parachichi na plamu yana virutubisho vinavyoweza kusaidia afya ya mifupa.

Kwa mfano, tini mbili zilizokaushwa zina takribani miligramu 100 za kalisiamu. Hata matunda freshi kama machungwa yanaweza kuchangia upatikanaji wa madini hayo.

Tini na parachichi pia yana magnesiamu, ambayo husaidia katika uundaji wa mifupa na kudumisha uwiano wa madini mwilini.

Aidha, matunda mengi yana kemikali asilia zinazojulikana kama polyphenols. Kemikali hizo zina uwezo wa kupambana na vioksidishaji na kupunguza uvimbe mwilini, jambo ambalo linaweza kusaidia kupunguza kasi ya kudhoofika kwa mifupa.

Utafiti mmoja uliohusisha wanawake ulibaini kuwa wale waliokula gramu 50 za plamu zilizokaushwa kila siku kwa mwaka mmoja walipoteza kiwango kidogo cha madini kwenye mifupa ikilinganishwa na wale ambao hawakula tunda hilo.

Utafiti mwingine pia ulihusisha ulaji mkubwa wa matunda na mboga na msongamano mkubwa zaidi wa madini kwenye mifupa, pamoja na kupungua kwa hatari ya kuvunjika kwake.

Samaki wa kwenye makopo

Kopo dogo la dagaa linaweza kutoa hadi asilimia 30 ya kiwango cha kalisiamu kinachohitajika kwa siku. Kwa mfano, kopo lenye gramu 60 za dagaa lina takribani miligramu 240 za kalisiamu.

Samaki aina ya salmoni wa kwenye makopo pia wana kalisiamu kwa wingi, pamoja na protini ambayo ina mchango muhimu katika kudumisha afya ya mifupa, kuhifadhi misuli na kusaidia mwili kujirekebisha.

"Mifupa na misuli vinapaswa kuchukuliwa kuwa sehemu ya mfumo mmoja," anasema Dawson-Hughes.

"Ukiweza kudumisha uimara wa misuli, utapunguza hatari ya kuanguka na kwa kiwango kikubwa pia kupunguza hatari ya kuvunjika kwa mifupa."

Samaki wenye mafuta mengi pia ni chanzo kizuri cha vitamini D, ambayo husaidia mwili kufyonza kalisiamu.

Upungufu wa vitamini hii mwilini unahusishwa na uchovu, kupungua kwa uwezo wa misuli kufanya kazi na kuongezeka kwa hatari ya kuanguka.

Je, unahitaji kutumia virutubisho vya ziada?

Mboga za madini ya ziada

Huenda ukajiuliza ikiwa kula vyakula hivi kunatosha au unahitaji pia kutumia vidonge vya kalisiamu na vitamini D.

Jibu linategemea mahitaji ya mwili wako na kiwango cha virutubisho unachopata kupitia chakula.

Amelia Moore, mtafiti katika Kitengo cha Osteoporosis cha Hospitali ya Guy's jijini London, anasema manufaa ya virutubisho vinavyolenga afya ya mifupa bado yanajadiliwa na wataalamu kutokana na matokeo yanayotofautiana katika tafiti.

Kwa mfano, tafiti zinaonyesha kuwa virutubisho vya vitamini D huenda visizuie kuvunjika kwa mifupa kwa watu wenye afya nzuri. Hata hivyo, baadhi ya tafiti zimeonyesha kuwa vinaweza kupunguza hatari ya kuanguka miongoni mwa wazee.

Lakini kutumia vitamini D kwa kiwango kikubwa kupita kiasi kunaweza kuwa na madhara.

Matumizi ya zaidi ya mikrogramu 100 kwa siku, kiwango ambacho ni kikubwa zaidi ya kipimo cha mikrogramu 10 hadi 15 kinachopendekezwa kwa matumizi ya kila siku, yanaweza kuongeza hatari ya kuanguka.

Hii inaashiria kuwa kuongeza kiwango cha matumizi si lazima kuongeze manufaa, anasema Dawson-Hughes.

Anaeleza kuwa watafiti bado hawajabaini sababu kamili, lakini matumizi ya kupita kiasi yanaweza kuongeza homoni inayopunguza kiwango cha vitamini D kinachopatikana kwa matumizi ya mwili.

Nchini Marekani na Uingereza, watu wazima wanashauriwa kutumia virutubisho vya vitamini D. Hata hivyo, baadhi ya wataalamu wanaamini kuwa ni wazee pekee au watu walio katika hatari ya upungufu wa vitamini hiyo wanaopaswa kuvitumia, hasa wale wasiopata mwanga wa jua wa kutosha.

Kwa ujumla, takribani asilimia 15 ya watu duniani wana upungufu wa vitamini D, hali ambayo hutokea zaidi wakati wa majira ya baridi.

Kwa upande mwingine, virutubisho vya kalisiamu vinapendekezwa zaidi kwa watu ambao hawawezi kupata kiwango cha kutosha cha madini hayo kupitia chakula wanachokula.

"Ikiwa mlo wako unajumuisha bidhaa za maziwa, protini, mboga za majani na samaki pamoja na nyama, utakuwa unapata vitamini na madini yote unayohitaji. Hata hivyo, kuna watu ambao hawana mlo wa aina hiyo na huenda wakahitaji kutumia virutubisho vya ziada," alisema Sagen Zac-Varghese katika podikasti ya BBC ya What's Up Docs.

Bila shaka, kuna vyakula vingi vya mimea vinavyofaa kwa walaji wasiokula bidhaa za wanyama na ambavyo vina kalisiamu kwa asili. Miongoni mwavyo ni mboga za majani, mbegu za ufuta na aina mbalimbali za kunde.

Hata hivyo, uchambuzi wa tafiti mbalimbali ulibaini kuwa walaji wa vyakula vya mimea pekee, wanaojulikana kama vegans, huwa wanapata kiwango kidogo zaidi cha kalisiamu ikilinganishwa na watu wanaokula vyakula vya mimea na wanyama au walaji wa vyakula vya mimea pamoja na bidhaa za maziwa.

Wataalamu wanasema kuwa watu wanaofuata mfumo huo wa ulaji wanaweza kuhitaji kuzingatia vyakula vilivyoongezwa virutubisho au kutumia virutubisho vya ziada.

Kwa ujumla, Moore anasema kuwa njia bora za kudumisha afya ya mifupa ni kula mlo bora, wenye uwiano na unaojumuisha aina mbalimbali za vyakula.

Bila shaka, ni muhimu pia kuambatanisha mlo huo na mazoezi ya mara kwa mara yanayohusisha kubeba uzito wa mwili, kama vile kutembea, kukimbia na kupanda ngazi.

Imetafsiriwa na Mariam Mjahid