Bruno Fernandes asitisha mazungumzo ya mkataba mpya Manchester United

Chanzo cha picha, Getty Images
Nahodha wa Manchester United, Bruno Fernandes, amesema klabu hiyo imempa ofa ya mkataba mpya, lakini ameamua kusitisha mazungumzo kwa sasa akiamini kuwa si wakati mwafaka kujadili mustakabali wake.
Kiungo huyo mwenye umri wa miaka 32 anatarajiwa kumaliza mkataba wake mwishoni mwa msimu huu, ingawa Manchester United ina kipengele kinachoiruhusu kuongeza mkataba wake kwa mwaka mmoja zaidi, hadi mwaka 2028.
Fernandes amesema hakuna mazungumzo yanayoendelea kwa sasa na amekanusha madai kwamba amekuwa akitaka kuongezewa mshahara au muda wa mkataba.
Amesema kama angekuwa anatafuta fedha nyingi zaidi, angeondoka Manchester United kutokana na nafasi alizokuwa nazo za kujiunga na klabu nyingine ambazo zingemlipa zaidi.
Ameongeza kuwa katika misimu kadhaa iliyopita, ikiwemo majira ya kiangazi miaka miwili na mitatu iliyopita pamoja na msimu uliopita, alikuwa na nafasi ya kuondoka, lakini aliamua kubaki Old Trafford.
Mkurugenzi Mtendaji wa Manchester United, Omar Berrada, hivi karibuni alithibitisha kuwa klabu ilikuwa na mazungumzo kuhusu mkataba mpya wa Fernandes, lakini akasema angependa suala hilo libaki kuwa la siri.
Fernandes alijiunga na Manchester United akitokea Sporting mwaka 2020 na tangu wakati huo amefunga mabao 75 katika Ligi Kuu England. Msimu uliopita pia aliweka rekodi ya kutoa pasi nyingi za mabao katika msimu mmoja wa ligi hiyo.
Hata hivyo, kiwango chake kimeonekana kushuka msimu huu, wakati Manchester United ikianza vibaya ligi.
Akizungumzia mazungumzo ya mkataba, Fernandes amesema suala hilo lilianza kujadiliwa mwishoni mwa msimu uliopita na kuendelea mwanzoni mwa msimu huu, lakini aliamua kuliweka pembeni kutokana na hali ya klabu na timu kwa ujumla.
Amesisitiza kuwa kwa sasa si wakati mzuri kwake wala kwa klabu kuendelea na mazungumzo hayo.






