Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Mfungwa aliyeepuka kunyongwa mara nane, afariki dunia
Francis Clifford Smith aliandaliwa "mlo wake wa mwisho" mara nane tofauti.
Hata hivyo, utekelezaji wa hukumu yake uliahirishwa katika kila moja ya nyakati hizo, na akawa mfungwa aliyekaa gerezani kwa muda mrefu zaidi nchini Marekani kabla ya kufariki dunia mwezi Juni akiwa na umri wa miaka 101.
Smith alihukumiwa kwa kosa la mauaji mwaka 1950, akiwa na umri wa miaka 25, ingawa aliendelea kusisitiza kuwa hana hatia, kulingana na watu waliomfahamu waliozungumza na BBC.
Andrius Banevicius, afisa habari wa Idara ya Magereza ya Connecticut, alisimulia jinsi Smith alivyokuwa akiwalisha ndege alipokuwa katika gereza la Osborn.
Jambo hilo lilimfanya ajulikane kwa jina la utani la "Osborn's Bird Man" .
"Aliificha mikate yote aliyoweza kupata ndani ya nguo zake," alisema Banevicius, huku akiongeza kuwa, "Kila mtu alijifanya haoni kwa sababu walijua alikuwa akiwalisha ndege."
Uhalifu
Smith alikuwa kijana mdogo mwenye historia ya uhalifu wa viwango vidogo.
Mnamo mwaka wa 1949, alishutumiwa kwa mauaji ya Grover Hart, mlinzi wa usiku katika klabu ya boti huko Connecticut.
Alikuwa mmoja wa wanaume wawili waliokamatwa kuhusiana na mauaji hayo, lakini mwenzake alifikia makubaliano na upande wa mashtaka na kutoa ushahidi dhidi ya Smith, ambaye baadaye alikutwa na hatia ya mauaji ya kukusudia ya daraja la kwanza.
Hatia ya Smith na ushahidi uliotumika kumtia hatiani vimehojiwa kwa miaka mingi, hasa baada ya mashahidi kubadili kauli zao na mfungwa mwingine baadaye kukiri kuhusika na mauaji hayo.
Mmoja wa maafisa waliomhoji Smith baada ya kukamatwa kwake baadaye alitoa ushahidi kwamba aliamini kuwa hakuwa na hatia.
"Sina uhakika hata kama nilikuwepo eneo la tukio la mauaji hayo," Meja Leo Carroll aliambia Bodi ya Msamaha, kulingana na gazeti la Boston Globe.
Mashaka hayo yalimwezesha kupata msamaha dhidi ya hukumu kadhaa za kunyongwa zilizokuwa zimeratibiwa, hadi pale hukumu yake ya kifo ilipobadilishwa na kuwa kifungo cha maisha jela mwaka wa 1954.
Maisha gerezani
Smith alitumikia zaidi ya miaka 70 gerezani, isipokuwa kwa vipindi vitatu vifupi alipokuwa huru.
Alitoroka gerezani mwaka wa 1967, lakini alikamatwa tena siku 12 baadaye. Mwaka wa 1974, alirudi nyumbani kwa ajili ya mkesha wa Krismasi na kurejea gerezani siku iliyofuata, alisema Banevicius.
Kisha, mwaka wa 1975, alipewa ruhusa ya kuishi nje ya gereza, na kuwa huru kwa takriban miezi 10, lakini punde si punde alikamatwa kwa kosa la wizi mdogo na kumiliki silaha, mambo ambayo yalikiuka masharti ya uhuru wake wa muda, kulingana na gazeti la Boston Globe.
Richard Sparaco, aliyekuwa mkurugenzi mtendaji wa chombo kinachojulikana sasa kama Bodi ya Msamaha , aliliambia gazeti la Hartford Courant kuwa Smith alikataa majaribio kadhaa yaliyofuata ya kupata tena uhuru wa kuhudumia kifungo nje ya gereza hadi mwaka wa 2020, alipopewa uhuru huo wenye uangalizi na kuhamishwa katika kituo cha utunzaji wa wazee kilicho chini ya mfumo wa mahakama.
Dkt. Stephanie Prost, mtafiti aliyebobea katika masuala ya wazee na mazingira ya magereza katika Chuo Kikuu cha Louisville huko Kentucky, aliambia BBC kuwa magereza mengi yana wafungwa kama Smith.
"Sisi si eneo pekee linalokabiliwa na tatizo hili linalohusiana na kuongezeka kwa idadi ya watu wenye umri mkubwa, kwa sababu matatizo kama hayo yanaibuka pia nchini Australia na Uingereza," alisema.
Kulingana na utafiti wa mwaka wa 2025, idadi ya watu wenye umri wa miaka 55 na zaidi walio gerezani iliongezeka kwa ktakriban asilimia 400 kati ya mwaka wa 1991 na 2021.
Ofisi ya Sensa ya Marekani inatabiri kuwa kufikia mwaka wa 2030, angalau theluthi moja ya idadi ya wafungwa itakuwa na umri wa zaidi ya miaka 50.
Watafiti kama Prost wanapendekeza suluhisho bora zaidi na kile wanachokiita "mfumo mzuri wa kuwaachilia wafungwa" , sawa na ilivyotokea katika kesi ya Smith.
Hii inaweza kujumuisha sera kama vile kuachiliwa kwa misingi ya kibinadamu na kuhudumia kifungo ukiwa nje ya gereza kwa watu wazee au wenye matatizo ya kiafya.
Programu hizi huzingatia umri na mahitaji ya utunzaji, kwani wafungwa wazee hukabiliwa na viwango vya juu vya matatizo ya kiafya yanayohitaji gharama kubwa, jambo linalowafanya washindwe kumudu maisha katika mazingira magumu ya gereza,matatizo hayo ni pamoja na hatari ya kuanguka, kushindwa kudhibiti haja, na matatizo ya kusikia.
Hata hivyo, kulingana na wataalamu, kuna magereza machache kama lile alilopelekwa Smith ambayo yako tayari kupokea wafungwa waliohukumiwa.
Hatimaye
Smith alikuwa mmoja wa watu wa kwanza kupata huduma za matibabu kupitia mpango wa MissionCare Health, ambao unalenga hasa kutoa huduma kwa watu waliofungwa gerezani.
Kwa sasa, mpango huo una vituo vitatu katika eneo la kaskazini mashariki mwa Marekani.
David Skoczulek, msemaji wa 60 West,kituo ambacho Smith aliishi miaka yake ya mwisho aliambia BBC kuwa Smith alifariki dunia akiwa amelala hapo mwezi Juni na baadaye mwili wake ukachomwa .
"Kimsingi, alifariki kutokana na uzee," alisema. "Familia yake haikuhusika sana katika siku za mwisho kabla ya kifo chake, lakini tulihakikisha kuwa kila kitu kinafanyika kwa njia inayofaa na yenye heshima, na kwamba matakwa yake yanaheshimiwa."
Skoczulek alieleza kuwa jukumu la kituo hicho lilikuwa kumpatia Smith huduma za kitaalamu za uuguzi na matunzo ya muda mrefu alizohitaji.
Utafiti unaonyesha kuwa kufungwa gerezani kunaweza kusababisha "kuzeeka kwa kasi" na kwamba hali kama vile shida ya kupoteza kumbukumbu, inaweza kujitokeza mapema zaidi ikilinganishwa na watu ambao hawajawahi kufungwa.
Imetafsiriwa na Sarafina Robi