Uingereza yaongeza vikwazo zaidi dhidi ya Urusi, makampuni yanayoisaidia Urusi katika vita yalengwa

Chanzo cha picha, Getty Images
Serikali ya Uingereza imetangaza upanuzi mpya wa orodha yake ya vikwazo dhidi ya Urusi. Vikwazo hivyo vinalenga makampuni mapya katika sekta ya mafuta na meli za mafuta zinazosafirisha mafuta ya Urusi nje ya nchi, makampuni katika sekta za fedha na fedha za kidijitali, na mashirika yanayosambaza bidhaa muhimu kwa jeshi la Urusi.
Kulingana na Wizara ya mambo ya nje ya Uingereza, vikwazo hivyo vitaathiri safari za Zarubezhneft na INK Capital, pamoja na meli zingine 12 za mafuta (jumla ya meli zilizowekewa vikwazo sasa zinazidi 600).
Vikwazo vimetolewa kwa masoko matatu ya sarafu za kidijitali na majukwaa mawili ya malipo. Imebainika kuwa majukwaa haya huenda yaliunganishwa na mtandao unaojulikana wa soko la fedha za kidijitali la A7, ambao unaaminika kuisaidia mamlaka ya Urusi kuepuka vikwazo vya kifedha vilivyowekwa hapo awali.
Katika sekta ya wauzaji wa bidhaa zinazotumiwa na Urusi kupigana vita, vikwazo vipya vitatumika kwa vyombo 17 na watu binafsi waliotambuliwa na Uingereza, Marekani, na EU kama wanaohusika katika biashara hiyo. Hii ni pamoja na waagizaji wa Urusi wa zana za mashine, vifaa vya elektroniki, na vifaa muhimu kwa uzalishaji wa makombora na ndege zisizo na rubani za Urusi.
"Ukiisaidia Urusi kufadhili au kusambaza vita hivi, itabidi ujibu," Wizara ya mambo ya nje ya Uingereza ilisema.
Ubalozi wa Urusi nchini Uingereza ulijibu kuhusu habari za vikwazo vilivyopanuliwa, ukitangaza kwamba havitailazimisha Moscow kubadilisha mkondo wake wa sera za kigeni. Ikibainisha kwamba vikwazo hivyo vitaathiri makampuni kutoka China, Kyrgyzstan, Thailand, na Uturuki.
Ulisema kwamba uamuzi wa London unaonyesha "mtazamo wa wasomi wa Uingereza wa ukoloni mamboleo kuelekea ulimwengu unaoendelea."
Unaweza pia kusoma:

































