China, Urusi na Marekani zakubaliana kulinda usalama wa dunia

Rais wa China Xi Jinping amesema kuwa, "historia inatufundisha kuwa mataifa yenye nguvu yanapoishi kwa maelewano, dunia huwa na amani. Mataifa yenye nguvu yanapozozana, dunia huingia katika machafuko."

Muhtasari

Ruka Video uendelee
  • xx
  • Wicknell Chivayo
  • Kijanangoma
  • xx
  • Besigye
  • .
  • xx
  • xx
  • xx
  • Lungu
  • xx
  • xx
  • d
  • s
  • Sonko
  • xx
  • xx
  • xx
  • xx

Moja kwa moja

Na Faidha Ngaga & Beldeen Waliaula

  1. Kufikia hapo tunatamatisha matangazo yetu ya moja kwa moja. Kwaheri.

  2. Marekani na Venezuela zakubaliana kushirikiana kijeshi

    .
    Maelezo ya picha, Picha ya Rais wa Venezuela Delcy Rodríguez na Pete Hegseth

    Marekani na Venezuela zimekubaliana tena kushirikiana kijeshi, mwaka mmoja tu baada ya vikosi vya Marekani kumkamata aliyekuwa kiongozi wa nchi hiyo, Nicolás Maduro, katika operesheni ya uvamizi iliyofanyika katika mji mkuu wa Caracas.

    Serikali ya mpito inayoongozwa na Delcy Rodríguez, aliyekuwa makamu wa rais wa Maduro, imetia saini makubaliano ya ushirikiano wa kijeshi na Waziri wa Ulinzi wa Marekani Pete Hegseth.

    Hadi sasa, maelezo machache kuhusu makubaliano hayo yametolewa. Hata hivyo, Hegseth amesema kuwa ndani ya kipindi kisichozidi miezi 12, Venezuela imebadilika kutoka kuwa "tishio kubwa zaidi la kiusalama katika eneo letu hadi kuwa mshirika anayeshirikiana nasi katika masuala ya usalama."

    Rais wa mpito Rodríguez amesema makubaliano hayo yatasaidia kukabiliana na "vitisho vya pamoja."

    Ushirikiano wa kijeshi kati ya mataifa hayo mawili ulikatizwa mwaka 2005 na Hugo Chávez, aliyekuwa rais wa Venezuela na mwanasiasa wa mrengo wa kushoto wakati huo.

    Chávez alidai kuwa wanajeshi wa Marekani waliotumwa nchini Venezuela kutoa mafunzo, walikuwa wametoa matamshi ya kuidharau serikali yake.

    Pia aliishutumu ofisi ya kijeshi ya Marekani iliyokuwa katika kituo cha Fuerte Tiuna, eneo kubwa zaidi la kijeshi nchini Venezuela, kwa kuwa "chombo cha kijasusi cha CIA kinachopanga njama dhidi ya serikali."

    Chini ya utawala wa Nicolás Maduro, aliyechukua uongozi baada ya kifo cha Chávez kutokana na saratani, uhusiano kati ya Marekani na Venezuela ulizidi kuzorota.

    Soma pia:

  3. Somalia yamuamuru balozi wa UAE kuondoka nchini humo

    .

    Somalia imeamuru balozi wa Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE) kuondoka nchini humo ndani ya saa 72 na kumrejesha balozi wake kutoka Abu Dhabi kwa mashauriano, hatua inayozidisha mzozo wa kidiplomasia kati ya mataifa hayo mawili.

    Uamuzi huo ulitangazwa hii leo na Waziri wa Habari wa Somalia, Abdulfatah Qasim, baada ya mkutano wa baraza la mawaziri ulioongozwa na Waziri Mkuu Hamza Abdi Barre.

    Akizungumza na waandishi wa habari mjini Mogadishu, Qasim alisema serikali imepitisha hoja tano kujibu kile ilichokitaja kuwa ni kuendelea kwa UAE kuingilia masuala ya ndani ya Somalia na kukiuka mamlaka yake ya kujitawala.

    Soma pia:

  4. China, Urusi na Marekani zakubaliana kulinda usalama wa dunia

    .

    Rais wa Marekani Donald Trump, pamoja na viongozi wenzake wa China na Urusi, Xi Jinping na Vladimir Putin, wamehitimisha mkutano wa kihistoria wa pande tatu hii leo, ambapo walijadili vita nchini Ukraine na udhibiti wa silaha za nyuklia.

    China, Urusi na Marekani zimetoa taarifa ya pamoja kufuatia mkutano wa pande tatu kati ya viongozi wa nchi hizo, huku mambo makuu yaliyojadiliwa yakibainishwa.

    Katika taarifa hiyo, Rais wa China Xi Jinping, Rais wa Urusi Vladimir Putin na Rais wa Marekani Donald Trump wamesema kuwa wanaendelea kujitolea kulinda utulivu wa kimkakati na usalama wa kimataifa.

    Kwa mujibu wa taarifa hiyo, viongozi hao pia walijadili masuala yanayohusiana na usalama wa nishati na kukubaliana kuhusu mipango ya kuongeza uzalishaji na usambazaji wa bidhaa za mafuta yaliyosafishwa.

    Suala la kinga dhidi ya mashtaka ya kisheria kwa maafisa wa serikali pia lilijadiliwa. Taarifa hiyo imesema viongozi hao walikubaliana kuwa Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC) na taasisi nyingine zinazofanana nayo hazipaswi kutumia vibaya mamlaka yake ya kisheria.

    Kuhusu masuala ya nyuklia, viongozi hao watatu walisisitiza msimamo wao kwamba "vita vya nyuklia haviwezi kushindwa na havipaswi kamwe kupiganwa."

    Viongozi hao walielezea mkutano huo kuwa wa kihistoria.

    "Tumeandikisha historia kweli," Trump alisema mwanzoni mwa mkutano huo. Aliongeza kuwa, "Hakuna amani iliyowahi kupatikana kwa kukataa fursa za mazungumzo."

    Putin, ambaye hivi karibuni amekumbwa na pigo katika vita vyake dhidi ya Ukraine kufuatia kuharibiwa kwa daraja muhimu linalounganisha eneo la Crimea na Urusi, amesema nchi hizo tatu zina "maslahi mengi ya pamoja katika kutatua migogoro ya kikanda, ikiwemo mzozo wa Ukraine."

    Tofauti na Trump na Putin, Xi Jinping, ambaye kwa mujibu wa vyombo vya habari vya serikali ya China alikuwa akiongoza mkutano huo, hakutaja moja kwa moja vita vya Ukraine.

    Hata hivyo, alisema, "historia inatufundisha kuwa mataifa yenye nguvu yanapoishi kwa maelewano, dunia huwa na amani. Mataifa yenye nguvu yanapokinzana, dunia huingia katika machafuko."

    Ikulu ya Kremlin imetoa video inayoonyesha Rais wa Urusi Vladimir Putin akiondoka katika eneo la mkutano huo na kumuaga Rais wa China Xi Jinping.

    "Asante kwa kuandaa mkutano huu," Putin alisema. "Sidhani kama kuna mtu aliyetarajia kuwa kila kitu kingeenda vizuri kiasi hiki."

    Kwa mujibu wa shirika la utangazaji la taifa la China, CCTV, Rais Xi Jinping ameelezea mkutano wake na Rais wa Urusi Vladimir Putin na Rais wa Marekani Donald Trump kuwa "mzuri, wenye tija na matokeo makubwa."

    Mkutano huo haukuguzia vita vya Iran.

    Soma pia:

  5. Idadi ya Waislamu inatarajiwa kuzidi ya Wakristo ifikapo 2035

    .

    Na Caro Robi

    Watafiti wanabashiri ifikapo mwaka 2035,Uislam utakuwa dini kubwa zaidi duniani ikiipiku Ukristo.

    Utafiti huo uliofanywa na kituo cha utafiti cha Marekani cha Pew kinaonesha kuwa idadi ya Wakristo bado inakua lakini idadi jumla ya Waislamu inakua kwa kasi zaidi kutokana na kasi ya kuzaana.

    Inakadiriwa kuwa Mwanamke wa Kiislamu ana zaidi ya watoto watatu ikilinganishwa na mwanamke wa Kikiristo anayejifungua kwa wastani watoto wawili au wasiozidi watatu.

    Katika mataifa 53,tayari Waislamu walikuwa ndiyo wengi miaka sita iliyopita.Ukuaji huo wa Waislamu unatarajiwa kutoka katika mataifa hayo kwa zaidi ya Waislamu Bilioni 1.2 ifikapo 2070 hiyo ikiwa sawa na ukuaji wa asilimia 74 ya idadi jumla ya Waislamu Duniani.

    Licha ya hayo,ukuaji wa idadi ya Waislamu hautarajiwi kudumaza ule wa Wakristo huku makundi yote mawili yakitarajiwa kushuhudia ukuaji katika muongo mmoja ujao.

    Watafiti wa Pew wanasema, idadi ya Waislamu inaongezeka kwa kasi kuliko watu wa dini nyingine kwasababu wanapata watoto wengi zaidi.

    Kati ya mwaka 2020 hadi 2070,inakadiriwa kuwa Waislamu wataongezeka kwa bilioni 1.6 huku Wakristo wakiongezeka kwa Milioni 792 katika kipindi hicho.

    Watu kubadili dini pia kunatajwa kuwa miongoni mwa mambo yatakayoathiri ukuaji wa dini hizo mbili kubwa lakini athari yake inatarajiwa kuwa ndogo ikilinganishwa na suala la kuzaana.

    Katika kipindi cha muongo mmoja ujao,baadhi ya watu waliozaliwa Waislam au Wakristo,watabadili dini au hata kuachana kabisa na dini yoyote.

    Watafiti wanasema kutokana na tafiti za nyuma,inatarajiwa kuwa ni idadi ndogo tu ya Waislam watakaobadili dini ikilinganishwa na Wakristo wataosilimika.

    Inabashiriwa Watu milioni 8 wataachana na Uislamu huku Wakristo Milioni 105 wataachana na Ukristo.Wengi wa hao watakaoachana na Ukristo wanasemekana kuwa hawatataka kujitambulisha na dini yoyote ile.

    Kwa mfano,nchini Pakistan,idadi ya Waislamu inatarajiwa kuongezeka maradufu kutoka milioni 227 ilivyokuwa mwaka 2020 hadi milioni 461 ifikapo 2070, na hivyo kulifanya kuwa taifa lenye Waislamu wengi zaidi duniani.Kwa sasa ndilo taifa la pili duniani.

    Ukuaji wa Wakristo utakuwa katika mataifa 120 ambako tayari ndiyo wengi.Kwa jumla,idadi ya Wakristo katika Mataifa hayo inatarajiwa kuongezeka kwa milioni 630,ikiwa ni 92% ya idadi jumla ya Wakristo duniani.

    Kwa mfano,Katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC),idadi ya Wakristo inatarajiwa kukua mara tatu kutoka milioni 92 ilivyokuwa mwaka 2020 hadi milioni 299 ifikapo 2070.

    Marekani ndilo taifa lenye idadi kubwa zaidi ya Wakristo duniani na inatarajiwa kushuhudia kupungua kwa idadi hiyo ya Wakristo kutoka milioni 217 ilivyokuwa 2020 hadi milioni 174 ifikapo 2070.

    Watafiti wa Kituo cha Pew wanasema ifikapo 2070,Waislamu watakuwa 95% Mashariki ya Kati na Afrika Kaskazini.

    Eneo ambalo linatarajiwa kuwa na mabadiliko makubwa ya dini ni Asia Pasific ambako Waislam wanatarajiwa kuongezeka na kuwapiku wasiofungamana na dini yoyote.

  6. Myanmar ilikuwa na nia ya kuwaangamiza jamii ya Rohingya - ICJ

    .

    Mahakama Kuu ya Kimataifa ya Haki (ICJ) imesema kuwa Myanmar ilitekeleza mauaji ya kimbari dhidi ya jamii ya Warohingya katika jimbo la Rakhine Kaskazini.

    Mahakama ya ICJ imesema kuwa, Myanmar ina wajibu wa kutoa fidia kwa waathiriwa kutokana na vitendo vyake, ingawa haijabainisha kiasi cha fedha kinachopaswa kulipwa.

    Jaji Iwasawa, amesema fidia hiyo inapaswa kuzingatia ukubwa wa madhara yaliyosababishwa.

    Jaji Iwasawa ameongeza kuwa Myanmar inapaswa kuwasilisha ripoti ndani ya miaka miwili tangu kutolewa kwa hukumu hiyo, ikieleza namna itakavyotekeleza wajibu wake wa kutoa fidia.

    Gambia, ambayo iliwasilisha kesi hiyo, ilikuwa imesema kuwa Myanmar inapaswa kutoa fidia kamili kwa waathiriwa wote wa jamii ya Warohingya kutokana na vitendo vilivyokiuka sheria.

    Jaji Iwasawa amesema hukumu ilifikiwa baada ya Myanmar kushindwa kuchunguza, kuwafungulia mashtaka na kuwaadhibu watu waliohusika na makosa ya mauaji, chini ya Kifungu cha 3 cha Mkataba wa Umoja wa Mataifa kuhusu kuzuia na kuadhibu mauaji ya kimbari, wakiwemo makamanda wa kijeshi.

    Kifungu hicho kinatambua mauaji ya kimbari, njama za kutekeleza mauaji hayo, uchochezi wa moja kwa moja na wa hadharani, jaribio la kutekeleza mauaji ya kimbari pamoja na kushiriki katika vitendo hivyo kuwa makosa yanayopaswa kuadhibiwa.

    Iwasawa ameongeza kuwa Myanmar imeshindwa kutekeleza wajibu wake wa kuadhibu mauaji ya kimbari chini ya vifungu vya 1, 4 na 6 vya mkataba huo.

    AidhaJaji Iwasawa amesema Myanmar ilihusika na "uharibifu mkubwa wa ushahidi" kwa kuchoma miili ya watu waliouawa au kuitupa.

    Jaji huyo pia amesema maeneo ambako operesheni za kijeshi za kuwaondoa Warohingya zilifanyika yalichomwa moto na kubomolewa kwa tingatinga, hatua iliyozuia uchunguzi wa kina kuhusu matukio ya mwaka yaliyotokea mwaka wa 2017.

    Iwasawa amesema ukubwa na aina ya vitendo vya Myanmar vilionyesha nia ya kuangamiza sehemu kubwa ya jamii hiyo.

    Mahakama ya ICJ imebaini kuwa takriban Warohingya 815,000 waliokuwa wakiishi katika jimbo la Rakhine Kaskazini kabla ya operesheni za kijeshi za mwaka 2017 walilengwa na Myanmar.

    Historia ya jamii ya Warohingya

    Warohingya ni jamii ya watu wachache ambao wengi wao ni Waislamu na wanaishi katika jimbo la Rakhine nchini Myanmar.

    Kwa miongo kadhaa, jamii hiyo imekabiliwa na ubaguzi na ghasia nchini Myanmar, ambayo kwa kiasi kikubwa ina wakazi wanaofuata dini ya Ubuddha.

    Serikali ya Myanmar pia haiwatambui Warohingya kama raia chini ya sheria zake za uraia, hali iliyowafanya kuwa miongoni mwa jamii kubwa zaidi duniani zisizo na utaifa.

    Mawimbi ya mateso kwa miongo kadhaa, yakiwemo operesheni kubwa ya kijeshi ya mwaka 2017, yamelazimisha karibu Warohingya milioni mbili kuikimbia nchi hiyo.

    Maelfu ya wengine wanaendelea kuondoka nchini humo kila mwaka, wengi wakisafiri kwa kutumia boti zilizojaa watu na kukabiliwa na hatari kubwa baharini, mwaka jana watu 900 walifariki katika ajali ya boti.

    Zaidi ya wakimbizi milioni moja wa Rohingya waliohama makwao wanaishi katika kambi za wakimbizi za Cox's Bazar nchini Bangladesh.

    Umoja wa Mataifa umewataja Warohingya kuwa "jamii ya watu wachache inayoteswa zaidi duniani."

    Soma pia:

  7. Kampuni ya Marekani yashinda zabuni ya uchimbaji madini Mrima Hill Kenya

    .

    Kampuni ya Marekani ya Frontier Minerals, imetangazwa mshindi wa zabuni ya mradi wa uchimbaji madini katika eneo la Mrima Hill, eneo la Pwani ya Kenya.

    Zabuni hiyo ilikuwa ikishindaniwa vikali na kampuni kutoka China na Australia.

    Eneo la Mrima Hill linaaminika kuwa na akiba kubwa ya madini ya niobium, ambayo hutumika katika utengenezaji wa teknolojia za kijeshi na vifaa vya kielektroniki.

    Ushindi wa kampuni hiyo ya Marekani inaonyesha juhudi za Rais wa Marekani Donald Trump za kuhakikisha nchi yake inapata fursa kubwa zaidi ya kufikia rasilimali za madini muhimu barani Afrika.

    Upatikanaji wa madini hayo ni sehemu muhimu ya sera ya Marekani kuhusu Afrika.

    Hatua hiyo inamaliza miaka kadhaa ya ushindani wa kutaka kudhibiti eneo hilo, ambalo lina ukubwa wa takriban ekari 390 za msitu karibu na pwani ya Bahari ya Hindi.

    Hata hivyo, mradi huo bado unakabiliwa na utata. Jamii ya wenyeji wa Digo inalitambua eneo la Mrima Hill kuwa takatifu, na baadhi ya wanajamii wamewahi kupinga shughuli za utafiti wa madini wakihofia kufurushwa kutoka kwa makazi yao bila kulipwa fidia.

  8. Mwanariadha wa Kenya Peres Jepchirchir apigwa marufuku kwa miaka mitatu kwa matumizi ya dawa za kusisimua misuli

    .
    Maelezo ya picha, Picha ya Peres Jepchirchir

    Mwanariadha nyota wa Kenya Peres Jepchirchir amepigwa marufuku kushiriki mashindano ya riadha kwa kipindi cha miaka mitatu kutokana na matumizi ya dawa za kusisimua misuli.

    Bingwa huyo wa zamani wa Olimpiki na bingwa mtetezi wa dunia alikutwa na dawa aina ya EPO, ambayo imepigwa marufuku. Jepchirchir alikubali mashtaka yaliyohusiana na kupatikana na matumizi ya dawa hiyo.

    Kutokana na marufuku hiyo, Jepchirchir ambaye pia amewahi kushinda mbio za marathoni za New York, Boston na London, amevuliwa ubingwa wa mbio za Sydney Marathon alioutwaa mwezi Agosti.

    Waandaaji wa mbio hizo wamesema Mkenya mwenzake Irine Cheptai, aliyemaliza katika nafasi ya pili, atatangazwa mshindi iwapo hakutakuwa na rufaa ndani ya siku 30.

    Marufuku hiyo pia inamaanisha kuwa Jepchirchir hataruhusiwa kushiriki mashindano yoyote ya World Marathon hapo baadaye.

    Kesi yake inaongeza changamoto ya matumizi ya dawa za kusisimua misuli nchini Kenya, wakati ambapo taifa hilo linajiandaa kuandaa mashindano ya dunia ya riadha ya mwaka 2029, yatakayokuwa ya kwanza kufanyika barani Afrika.

    Kwa mujibu wa Kitengo cha Uadilifu katika Riadha (AIU), zaidi ya wanariadha 140 wa Kenya kwa sasa wanatumikia adhabu za kusimamishwa kushiriki mashindano kutokana na masuala yanayohusiana na matumizi ya dawa hizo.

  9. Boti iliyokuwa na wahamiaji 100 yazama pwani ya Senegal

    .

    Mamlaka nchini Senegal zinaendelea na shughuli za kuwatafuta manusura baada ya boti inayodaiwa kuwa imewabeba wahamiaji Zaidi ya 100 kupinduka baharini karibu na pwani ya nchi hiyo.

    Taarifa za awali zilisema kuwa mtu mmoja alikuwa amefariki dunia, lakini baadhi ya vyombo vya habari vimeripoti kuwa miili ya watu wanne imepatikana. Makumi ya watu bado hawajulikani walipo.

    Shughuli za uokoaji ziliendelea siku nzima hapo jana na zimerejelewa pia hii leo.

    Tukio hilo limetokea chini ya wiki mbili baada ya ajali nyingine ya boti kuzama karibu na mji wa Thieppe, kaskazini-magharibi mwa nchi hiyo, iliyosababisha vifo vya watu wasiopungua 39.

    Katika miaka ya hivi karibuni, maelfu ya watu kutoka Afrika Magharibi wamefariki au kupotea baharini wakijaribu kukimbia migogoro, utawala wa kimabavu na umaskini.

    Shirika la Umoja wa Mataifa la Uhamiaji (IOM) lilisema mwezi uliopita kuwa lilikuwa limerekodi vifo na kutoweka kwa watu wasiopungua 454 katika pwani ya Afrika Magharibi mwaka huu pekee.

  10. Taiwan yaripoti ndege za kijeshi za Urusi kuingia katika anga lake

    .

    Wakati Rais wa Russia, Vladimir Putin, akijiandaa kukutana na Rais wa Marekani, Donald Trump, na Rais wa China, Xi Jinping, mjini Shenzhen, Wizara ya Ulinzi ya Taiwan imesema ndege mbili za kijeshi za Russia aina ya Tu-95 ziliingia katika eneo lake la anga mapema leo.

    Katika taarifa iliyochapishwa kwenye mtandao wa X, wizara hiyo imesema ndege hizo ziliingia katika eneo la utambuzi wa ulinzi wa anga la Taiwan (ADIZ) kupitia upande wa kusini, zikaruka katika anga la mashariki mwa Taiwan na baadaye kuondoka katika eneo hilo upande wa kaskazini-mashariki mwa Keelung.

    Vikosi vya Taiwan vimesema vilifuatilia mwenendo wa ndege hizo na kuchukua hatua stahiki kukabiliana na hali hiyo.

    Tukio hilo linajiri siku moja baada ya Japan kusema kuwa ilirusha ndege zake za kivita na kuwasilisha malalamiko makali kufuatia tukio la Jumanne, ambapo ndege mbili zinazoshukiwa kuwa za Russia ziliripotiwa kukiuka anga lake.

    Korea Kusini pia ilipeleka ndege zake za kivita, huku Taiwan ikisema ilichukua hatua baada ya kubaini ndege za kijeshi za Russia katika maeneo yake ya utambuzi wa ulinzi wa anga.

    Maeneo hayo ya ADIZ ni maeneo ya kiusalama yasiyo rasmi yanayoanzia nje ya anga la kitaifa, ambako serikali hufuatilia na kutambua ndege zinazokaribia kwa madhumuni ya kiusalama.

    Hadi sasa, Moscow haijatoa tamko lolote kuhusu tukio hilo.

  11. Je, kuna uwezekano China, Russia na Marekani kufikia makubaliano kuhusu silaha za nyuklia?

    .

    Taarifa zinaeleza kuwa Rais wa Marekani, Donald Trump, anataka kujadili suala la silaha za nyuklia na upunguzaji wake na viongozi wa China na Russia. Hata hivyo, suala hilo ni miongoni mwa ajenda ambazo viongozi wengine wanaoshiriki katika mkutano huo hawaonekani kuwa na hamu kubwa ya kuzizungumzia.

    China haina silaha za nyuklia zinazolingana kwa idadi na zile za Russia na Marekani, hivyo haioni sababu ya kupunguza uwezo wake wa kijeshi katika eneo hilo kufikia kiwango sawa na mataifa hayo mawili. Hata haionekani kuwa tayari kujadili suala hilo.

    Vita vya Ukraine pia vimeonesha kuwa silaha za nyuklia ni nyenzo ya Russia ya kuzuia mataifa ya kimataifa kukubaliana kuchukua hatua za kukabiliana nayo, au hata kuingilia kijeshi. Silaha hizo zinaipa Moscow uwezo wa kujilinda dhidi ya hatua kama hizo.

    Hata hivyo, Rais Trump, ambaye anaamini katika uwezo wake wa kufanya mazungumzo na kufikia makubaliano, na ambaye kwa miongo kadhaa amekuwa akitetea upunguzaji wa akiba ya silaha za nyuklia, anataka kujaribu kupiga hatua katika suala hilo.

    Huenda hiyo ndiyo sababu alisema mwanzoni mwa mkutano wake wa pande mbili na Rais wa Russia, Vladimir Putin: "Ninaamini mkutano huu unaweza kuzaa matokeo ya kipekee, au angalau kuwa mwanzo wa matokeo hayo."

    Ikulu ya Marekani (White House) iliwahi kusema kuwa hakuna makubaliano yatakayofikiwa katika mkutano huo, lakini unaweza kuwa mwanzo wa mazungumzo kuhusu makubaliano ya silaha za nyuklia.

    Hapo awali, marais wa Marekani na Umoja wa Kisovieti, na baadaye Russia, waliwahi kufanikiwa kufikia makubaliano kuhusu suala hilo.

    Hata hivyo, ukweli kwamba miongo kadhaa baadaye upokonyaji wa silaha za nyuklia bado ni miongoni mwa ajenda zinazojadiliwa na viongozi wa mataifa hayo unaonesha kuwa, kihistoria, mazungumzo ya aina hiyo hayajakuwa yakizaa makubaliano makubwa mara nyingi.

  12. Xi afananisha uhusiano wa Marekani na China na mageuzi ya mji wa Shenzhen

    .

    Rais wa China, Xi Jinping, amefananisha uhusiano wa nchi yake na Marekani na mageuzi makubwa ya mji wa Shenzhen, akisema kujenga uhusiano wenye tija kati ya mataifa hayo mawili kunahitaji ujasiri wa kuanzisha mambo mapya na kufanya majaribio.

    Akizungumza na Trump, Xi alisema katika kipindi cha zaidi ya miaka 40, kijiji kidogo cha wavuvi kimebadilika na kuwa jiji kubwa la kimataifa.

    Alisema siri ya mageuzi hayo ni ujasiri wa kuanzisha mambo mapya, kufanya majaribio na kuwa mstari wa mbele katika mabadiliko. Aliongeza kuwa mafanikio hayo pia yamechangiwa na juhudi kubwa za kufanya kazi.

    Kwa mtazamo huo huo, Xi alisema kujenga uhusiano wenye tija kati ya China na Marekani ni jukumu jipya lisilo na mfano wa awali.

    Aliongeza kuwa hatua hiyo inahitaji pande zote kuwa na ujasiri wa kuanzisha mambo mapya, kufanya majaribio, kuzingatia uhalisia na kuhakikisha kazi zinazopangwa zinakamilishwa kwa mafanikio.

    Mafanikio ya Shenzhen, ambayo ni kitovu cha teknolojia nchini China, yalisifiwa na Xi jana alipohutubia viongozi wa biashara na siasa kutoka sehemu mbalimbali duniani.

    Unaweza pia kusoma:

  13. Putin ‘anafuraha sana’ baada ya mazungumzo na Trump, asema mshauri wake mkuu

    .

    Rais wa Russia, Vladimir Putin, yuko katika hali ya furaha sana kufuatia mkutano wake na Rais wa Marekani, Donald Trump, kwa mujibu wa mshauri wake mkuu wa masuala ya sera za nje, Yuri Ushakov.

    Akizungumza na kituo cha televisheni cha serikali ya Russia cha Vesti, Ushakov amesema mazungumzo kati ya marais hao wawili yalikwenda vizuri.

    Vyombo vya habari vya Russia vimesambaza kwa wingi video inayoonesha Trump akiingia katika chumba cha mkutano na kumuelekea Putin huku akisema: "Huyu ni nani? Huyu ni rafiki yangu!"

    Kwa mujibu wa Ushakov, vita vya Ukraine vilikuwa ajenda kuu ya mkutano huo uliochukua kati ya dakika 35 na 40. Viongozi hao pia walijadili uhusiano wa pande mbili kati ya Marekani na Russia.

    Ikulu ya Kremlin imesema kuwa hakuna kiongozi yeyote kati ya hao wawili aliyetoa tamko lolote kubwa baada ya mkutano huo, huku pande zote mbili zikijiandaa kwa mkutano na Rais wa China, Xi Jinping, unaotarajiwa kufanyika baadaye leo.

    Unaweza pia kusoma:

  14. Trump: Marekani na China zinataka vita vya Ukraine vikome

    .

    Akizungumza na Rais wa China, Xi Jinping, Rais wa Marekani Donald Trump amesema nchi zote mbili zinataka kuona vita kati ya Russia na Ukraine vikimalizika.

    Trump amesema Marekani na China zinatafuta namna ya kusaidia kumaliza vita hivyo, akiongeza kuwa kila mwezi watu 25,000, wengi wao wakiwa wanajeshi, wanauawa.

    Amesema alikutana na Rais wa Russia, Vladimir Putin, mapema kwa ajili ya kuweka mazingira ya mazungumzo ya pande tatu yanayotarajiwa kufanyika baadaye leo.

    Trump amesema ana matumaini kuwa mkutano huo unaweza kufanikiwa.

    Akihitimisha hotuba yake, Trump amemtaja Xi kuwa rafiki yake na kusema wana uhusiano wa kipekee.

    Amesema: "Nadhani mradi mimi na wewe tunaendelea kuongoza mambo, hatutakuwa na tatizo lolote."

    Unaweza pia kusoma:

  15. Mwalimu wa kike afungwa jela baada ya kujifungua mtoto aliyezaa na mvulana wa miaka 12

    .

    Mwalimu wa zamani nchini Australia amehukumiwa kifungo cha miaka minane na miezi sita jela baada ya kumnyanyasa kingono mvulana aliyekuwa na umri wa miaka 12 wakati unyanyasaji huo ulipoanza na baadaye kumzaa mtoto wake.

    Naomi Tekea Craig, mwenye umri wa miaka 34, alikiri makosa 12 ya unyanyasaji wa kingono kwa watoto huko Magharibi mwa Australia.

    Mahakama ilisikia kwamba Craig alikutana na mvulana huyo alipokuwa akifanya kazi kama mwalimu wa muziki katika shule yake huko Mandurah, kusini mwa Perth, mwaka wa 2023.

    Baadaye alijenga uhusiano wa karibu na familia yake, akawa rafiki na mama yake na kusaidia mara kwa mara na usafiri wa shule.

    Licha ya mvulana huyo kuhamia shule nyingine, Craig aliendelea kutumia muda pamoja naye na hatimaye akapewa ufunguo wa nyumba ya familia hiyo.

    Unyanyasaji huo ulianza wakati mvulana huyo akiwa na umri wa miaka 12 na uliendelea kwa zaidi ya mwaka mmoja.

    Vitendo hivyo viligundulika baada ya mama wa mvulana huyo kupata mashaka na kuweka kamera za usalama ndani ya nyumba ya familia. Picha kutoka kwenye kamera hizo zilikabidhiwa kwa polisi.

    Craig alikamatwa mnamo Desemba 2025 na akajifungua mtoto wa kike mwezi uliofuata. Vipimo vya vinasaba (DNA) vilithibitisha kuwa mvulana huyo ndiye baba wa mtoto huyo.

    Wakati wa kutoa hukumu katika Mahakama ya Wilaya ya Perth mnamo tarehe 17 Novemba 2026, Jaji John Prior alielezea vitendo vya Craig kama ukiukaji mkubwa wa imani.

    Mahakama ilielezwa kuwa Craig alikuwa akimnunulia mvulana huyo zawadi, akifuatilia shughuli zake kwenye mitandao ya kijamii, na kumwambia kuwa anataka kupata watoto zaidi naye.

    Waendesha mashtaka walisema kuwa unyanyasaji huo una uwezekano wa kuacha madhara ya kudumu kwa mvulana huyo na familia yake.

    Craig atakuwa na sifa za kuomba kuachiwa kwa masharti (parole) baada ya kutumikia kifungo cha miaka sita na miezi sita.

    Utambulisho wa mvulana huyo hauwezi kuwekwa wazi kwa sababu za kisheria na kwa ajili ya usalama wake

  16. Lissu kurejea mahakamani katika kesi nyingine ya uhalifu wa mtandaoni

    .

    Kiongozi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Tundu Antiphas Lissu, anatarajiwa kufikishwa tena katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam, leo Alhamisi, Novemba 19, 2026, kwa ajili ya kutajwa kwa kesi nyingine ya makosa ya mtandaoni inayomkabili.

    Lissu anakabiliwa na mashtaka matatu yanayohusiana na madai ya kuchapisha taarifa za uongo kupitia mtandao wa YouTube, akituhumiwa kutoa kauli hizo Aprili 3, 2025.

    Katika kauli hizo zinazodaiwa kuwa na makosa, Lissu anadaiwa kuzungumzia kuenguliwa kwa wagombea wa upinzani katika uchaguzi wa Serikali za Mitaa wa mwaka 2024, matumizi ya polisi katika masuala ya uchaguzi pamoja na kutokuwa na upendeleo kwa baadhi ya majaji.

    Kesi hiyo inakuja siku 13 baada ya Mahakama Kuu kumwachia huru Lissu dhidi ya shtaka la uhaini, lakini kumtia hatiani kwa kosa la uchochezi na kumhukumu kifungo cha miaka minne jela, Novemba 6, 2026.

    Macho na masikio yanaelekezwa katika mwenendo wa kesi hiyo ya leo, huku ikisubiriwa kufahamu hatua zitakazochukuliwa na mahakama pamoja na tarehe nyingine itakayopangwa kwa ajili ya kuendelea na shauri hilo.

    Endelea kufuatilia ukurasa huu kwa taarifa za moja kwa moja kutoka mahakamani....

    Unaweza pia kusoma:

  17. Elon Musk asema kutumia kiasi kikubwa cha fedha katika uchaguzi wa katikati ya muhula Marekani ilikuwa 'kosa la kipumbavu'

    .

    Elon Musk amesema Jumatano kwamba anajiona "mpumbavu kwa kiasi kikubwa" kutokana na kiasi kikubwa cha fedha alichotumia katika uchaguzi wa katikati ya muhula nchini Marekani, kufuatia chama cha Republican kupata kipigo kikubwa.

    Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni za Tesla na SpaceX alikuwa mfadhili binafsi aliyechangia fedha nyingi zaidi katika uchaguzi huo, akitoa dola milioni 446 (pauni milioni 339) kuunga mkono chama cha Rais Donald Trump, hususan katika jimbo la Texas ambako kampuni zake nyingi zina makao yake.

    Musk, ambaye aliunga mkono azma ya Trump ya kurejea Ikulu kwa muhula wa pili, pia amesema yeye si sehemu ya vuguvugu la MAGA (Make America Great Again) linalohusishwa na rais huyo.

    Chama cha Democratic kimefanikiwa kupata udhibiti wa mabunge yote mawili ya Congress ya Marekani, baada ya kushinda katika majimbo yaliyokuwa na ushindani mkali na kupata mafanikio makubwa ya kihistoria katika maeneo ambayo kwa miongo kadhaa yamekuwa yakidhibitiwa na chama cha Republican.

    Matokeo hayo yalionekana kuwa pigo kubwa kwa Trump, ambaye amekuwa akikabiliwa na shinikizo kutokana na athari za sera zake katika gharama za maisha nchini Marekani.

    Musk alikuwa akizungumza kwa njia ya mtandao katika mkutano wa DealBook Summit wa gazeti la New York Times, mkutano wa kila mwaka unaofanyika mjini New York na kuhudhuriwa na viongozi wakuu wa biashara na siasa.

    "Sipo katika MAGA," alisema Musk, akirejelea vuguvugu hilo la kisiasa la mrengo wa kulia.

    Aliongeza: "Sina uhakika MAGA ina maana gani... lakini kama inamaanisha kufuata kwa upofu sera za chama cha Republican, basi kwa hakika mimi sifanyi hivyo."

  18. Angel Wariael, binti aliyejeruhiwa kwa risasi Oktoba 29, afariki dunia Muhimbili

    .

    Angel Wariel, aliyekuwa akipatiwa matibabu katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) baada ya kujeruhiwa kwa risasi wakati wa matukio ya Oktoba 29 akiwa nyumbani kwao Manzese, amefariki dunia.

    Kifo chake kimethibitishwa Novemba 18, 2026 na Hospitali ya Taifa Muhimbili kupitia Mkuu wa Kitengo cha Uhusiano na Mawasiliano, Irene Charles Mbonde, pamoja na mmoja wa wanafamilia wake.

    Katika taarifa yake kwa vyombo vya habari, MNH imetoa salamu za pole kwa familia, ndugu, jamaa na wote walioguswa na msiba huo, huku ikiwaombea faraja na uvumilivu katika kipindi hiki kigumu cha maombolezo.

    Angel alikuwa amelazwa hospitalini hapo kwa wiki kadhaa akipatiwa matibabu kufuatia majeraha aliyoyapata kutokana na risasi iliyompata akiwa nyumbani kwao Manzese. Angel alipata majeraha yaliyoathiri maeneo mbalimbali ya mwili wake ikiwemo begani na uti wa mgongo.

    "Toka nilivyopigwa risasi siwezi kutembea, napungukiwa na damu, nimepata vidonda vinavyonifanya nilale tu kitandani na nimeshindwa kuendelea na shule" alisema Angel katika mahojiano yake na The Chanzo

    The Chanzo ilichapisha taarifa kuhusu hali yake na ya mama yake mzazi, Mnamo Oktoba 31, 2026, ikieleza kuwa walikuwa wakihitaji msaada wa matibabu kutokana na changamoto za kiafya zilizomlazimu Angel kusitisha masomo yake. Baada ya taarifa hiyo, alipata msaada uliomwezesha kuanza matibabu katika Hospitali ya Taifa Muhimbili hadi kifo chake kilipotokea.

    Matukio ya Oktoba 29 yalihusisha vurugu na matumizi ya silaha katika maeneo mbalimbali, nchini Tanzania.

    Unaweza pia kusoma:

  19. Trump asema Putin na Xi Jinping “wanapendana”

    .

    Rais wa Marekani, Donald Trump, ameonesha imani kuhusu uhusiano kati ya Rais wa China, Xi Jinping, na Rais wa Urusi, Vladimir Putin, kabla ya mkutano wao wa pamoja. Amesema viongozi hao wawili pia “wanampenda Trump”.

    Viongozi hao watatu wanatarajiwa kukutana mjini Shenzhen, China, pembezoni mwa mkutano wa kikanda unaofanyika katika eneo hilo.

    China imesema viongozi hao watabadilishana mawazo kuhusu masuala yanayohusu amani duniani katika mkutano huo.

    Ajenda rasmi ya mkutano huo bado haijawekwa wazi kikamilifu, lakini unatarajiwa kujadili vita vya Ukraine na Iran, pamoja na suala la upokonyaji silaha za nyuklia.

    Baadhi ya wachambuzi wa masuala ya Magharibi wameeleza wasiwasi kuwa mkutano huo unaweza kuchangia kugawanywa kwa dunia katika maeneo ambayo kila moja yatakuwa chini ya ushawishi wa mojawapo ya mataifa makubwa.

    .
  20. Trump asema alizungumza kwa kifupi na Xi kuhusu Jensen Huang

    .

    Wakati tukisubiri mkutano kati ya Rais wa Marekani, Donald Trump, na Rais wa China, Xi Jinping, tunakuletea baadhi ya dondoo kutoka kwenye mahojiano na Trump yaliyorushwa hewani saa chache zilizopita.

    Trump amesema alizungumza kwa kifupi tu kuhusu hali ya aliyekuwa mkuu wa kampuni ya Nvidia, Jensen Huang, na Xi wakati wa chakula cha jioni cha viongozi wa APEC Jumatano usiku.

    “Hatukujadili suala hilo. Huenda nililigusia kwa kifupi tu kwa sababu ni jambo la kusikitisha sana. Ni msiba. Yeye ni mtu mwenye akili nyingi sana,” Trump alisema katika mahojiano na kipindi cha The Ingraham Angle cha kituo cha Fox News.

    Huang, ambaye ni miongoni mwa watu muhimu zaidi katika sekta ya akili mnemba (AI), alijiuzulu wiki iliyopita kufuatia tuhuma za kuwa na mahusiano ya kimapenzi nje ya ndoa, ikiwemo uhusiano unaodaiwa kuwa na jasusi wa China.

    Tukio hilo limekuwa likifuatiliwa kwa karibu kutokana na uwezekano wa kuathiri mazungumzo kati ya Trump na Xi katika mkutano wa APEC.

    “Baadhi ya watu hawawezi kubadilishwa. Huang alikuwa mbele kwa miaka 10,” Trump alisema katika mahojiano hayo.

    Trump aliongeza kuwa sehemu kubwa ya mazungumzo yao wakati wa chakula hicho cha jioni ilihusu akili mnemba (AI).

    Unaweza pia kusoma: