Kwanini Saudi Arabia inatafuta washirika wapya wa ulinzi?

.
Iliyochapishwa
Muda wa kusoma: Dakika 8

Hatua ya Saudi Arabia kuimarisha ushirikiano wake wa kiusalama sasa si suala la mipango ya baadaye tena.

Tarehe 5 Oktoba, Saudi Arabia, Uturuki na Pakistan zilitangaza kuanza mara moja kutekeleza kwa vitendo makubaliano yao ya pamoja ya ulinzi chini ya mfumo wa Muungano wa Makkah. Nchi hizo zilisema zitachukua hatua za kuandaa vikosi na uwezo wa kijeshi uliokubaliwa, pamoja na kuwezesha kupelekwa kwake kwa haraka nchini Saudi Arabia.

Uamuzi huo ulifikiwa katika mkutano wa dharura wa Kamati ya Kisiasa na Kimkakati ya Ulinzi ya Muungano wa Makkah, ulioitishwa kujadili hali ya usalama na vitisho vinavyoikabili Saudi Arabia.

Hatua hiyo inakuja wakati vita vya Yemen vikizidi kushika kasi tena, huku Saudi Arabia ikiendelea kulengwa na mashambulizi ya kundi la Ansar Allah (Wahouthi), linaloungwa mkono na Iran.

Awali, ripoti za vyombo vya habari zilidai kuwa Rais wa Marekani Donald Trump alikuwa amekataa maombi ya mara kwa mara ya Saudi Arabia ya kupata msaada wa moja kwa moja wa kijeshi dhidi ya Wahouthi.

Kwa mujibu wa ripoti hizo, Washington haijakubali kushiriki moja kwa moja katika mashambulizi dhidi ya Wahouthi kwa kushirikiana na Saudi Arabia. Hata hivyo, imeendelea kuiunga mkono Riyadh kwa kutoa taarifa za kijasusi na upelelezi zinazosaidia operesheni zake dhidi ya kundi hilo.

Marekani yaunga mkono ulinzi wa mipaka

Baada ya zaidi ya miaka minne ya utulivu uliofuatia makubaliano ya kusitisha mapigano yaliyoungwa mkono na Umoja wa Mataifa mwaka 2022, Yemen imeingia tena katika awamu ya mapigano makali.

Hatua muhimu katika mabadiliko hayo ilijitokeza mwezi Julai, wakati vikosi vya serikali ya Yemen vikisaidiwa na Saudi Arabia viliposhambulia uwanja wa ndege wa Sanaa unaodhibitiwa na Wahouthi. Vikosi hivyo vilisema lengo la shambulio hilo lilikuwa kuzuia ndege kutoka Iran kutua katika mji mkuu huo.

Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili WhatsApp bofya kutufuatilia
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Tangu wakati huo, hali ya usalama mpakani imezidi kuzorota, huku mashambulizi ya Wahouthi dhidi ya Saudi Arabia yakiongezeka na kuzua wasiwasi mpya kuhusu kuenea kwa mzozo huo katika eneo la Ghuba.

Saa chache baadaye, Wahouthi walirusha makombora kusini mwa Saudi Arabia, huku mzozo huo ukichukua mkondo mpya baada ya kundi hilo kupanua udhibiti wake katika maeneo ya pwani ya magharibi mwa Yemen. Hatua hiyo imeongeza uwezo wa Wahouthi kutishia usafiri wa baharini katika mlango wa Bab al-Mandab, njia muhimu ya biashara inayounganisha Bahari ya Hindi na Bahari ya Mediterania kupitia Bahari ya Shamu na Mfereji wa Suez.

Mnamo Oktoba 5, vikosi vya serikali ya Yemen vinavyoungwa mkono na Saudi Arabia, kwa msaada wa mashambulizi ya anga ya Riyadh, vilianzisha operesheni kubwa ya kijeshi ya kuyarejesha maeneo yaliyo chini ya udhibiti wa Wahouthi.

Mtafiti wa masuala ya Mashariki ya Kati, Mitchell Plitnick, anaamini matukio ya wiki za karibuni yamekuwa mtihani mpya kwa uhusiano wa kiusalama kati ya Riyadh na Washington.

"Hapa ndipo Marekani ilipoiangusha Saudi Arabia," anasema.

Kwa mujibu wake, tangu mwisho wa Vita Kuu ya Pili ya Dunia, Saudi Arabia ilijenga uhusiano wake wa kiusalama na Marekani kwa msingi wa kubadilishana uthabiti wa soko la mafuta na usalama wa nishati kwa mwavuli wa ulinzi kutoka Marekani na washirika wake wa Magharibi.

Hata hivyo, anasema utawala wa Donald Trump umeonyesha tangu muhula wake wa kwanza kuwa mpangilio huo si dhamana ya moja kwa moja ya msaada wa kijeshi, hasa pale ambapo maslahi mengine ya Marekani yanapokuwa mbele ya mahitaji ya usalama ya Saudi Arabia.

Plitnick anatolea mnfano mashambulizi ya Septemba 2019 dhidi ya miundombinu ya mafuta ya Saudi Arabia, ikiwemo vituo vya Aramco, yaliyoathiri kwa muda sehemu kubwa ya uzalishaji wa mafuta wa nchi hiyo. Ingawa Marekani na Saudi Arabia ziliilaumu Iran kwa mashambulizi hayo na Tehran ikakanusha, Washington haikuchukua hatua za kijeshi dhidi ya Iran.

Kwa mtazamo wake, tukio hilo lilizidi kuimarisha hisia nchini Saudi Arabia kwamba ushirikiano wa kiusalama na Marekani haumaanishi Washington itaingilia kati katika kila mzozo ambao Riyadh inaona kuwa tishio kwa usalama wake.

Naye Aaron David Miller, aliyewahi kuwa mshauri wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani kwa takribani miaka 25, anaamini kuwa Washington ina sababu za kuisaidia Saudi Arabia, lakini imekuwa makini kutokana na mzozo mpana na Iran na nia ya kuepuka kufungua uwanja mpya wa vita nchini Yemen.

Anasema uzoefu wa operesheni ya Marekani dhidi ya Wahouthi mwaka 2025, iliyodumu kwa siku 52 na kuhusisha zaidi ya mashambulizi 1,000, uliwaonyesha viongozi wa Marekani kuwa nguvu za kijeshi pekee hazitoshi kudhoofisha uwezo wa kundi hilo kwa kiwango cha kuleta matokeo ya haraka.

Miller pia anaona kuwa siasa za ndani za Marekani, hasa kuelekea uchaguzi wa katikati ya muhula wa Bunge, zimechangia tahadhari ya Washington kutotumbukia katika mzozo mwingine wa kijeshi.

Utiaji saini wa Mkataba wa Makka kati ya Pakistan, Saudi Arabia na Uturuki.

Kwa upande mwingine, Amr Hamzawy wa Taasisi ya Carnegie anaamini kukataa kwa Marekani kutoa msaada wa moja kwa moja wa kijeshi kwa Saudi Arabia hakumaanishi kuwa uhusiano wa kimkakati kati ya nchi hizo mbili umebadilika au kwamba Washington inaiacha Riyadh.

Kwa mujibu wake, Marekani imechagua kuendelea kutoa msaada wa kijasusi, ikiwemo taarifa kuhusu uwezo na maeneo ya Wahouthi, huku ikiepuka ushiriki wa moja kwa moja vitani. Anaona hatua hiyo kuwa inaonyesha mipaka ya jukumu la kijeshi la Marekani badala ya mabadiliko ya msingi katika dhamira yake kwa Saudi Arabia.

Kauli za maafisa wa Marekani pia zimeendelea kusisitiza mshikamano huo. Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Marco Rubio, alisema Septemba 23 kwamba nchi hiyo ina "makubaliano imara sana ya ulinzi" na Saudi Arabia na itaendelea kutekeleza wajibu wake chini ya makubaliano hayo.

Siku chache baadaye, Waziri wa Ulinzi wa Saudi Arabia, Mwanamfalme Khalid bin Salman, na Waziri wa Ulinzi wa Marekani, Pete Hegseth, walijadili ushirikiano wao wa kimkakati wa ulinzi na njia za kuimarisha usalama na uthabiti wa eneo hilo.

Kwa upande wa Saudi Arabia, Salem Al-Yami, mshauri wa zamani wa Wizara ya Mambo ya Nje ya nchi hiyo, anakataa hoja kwamba Marekani imeitelekeza Riyadh.

"Marekani haiwezi kuachana na mshirika kama Saudi Arabia bila kuathiri maslahi yake yenyewe," anasema.

Kwa mujibu wake, matukio ya karibuni yameathiri mahusiano ya nchi hizo katika ngazi ya kiutendaji, lakini hayajabadilisha msingi wa ushirikiano wao wa kimkakati na wa kihistoria.

Hata hivyo, Al-Yami anasema kuwa tangu mwaka 2015 Saudi Arabia imekuwa ikifuata mkakati wa kupanua ushirikiano wake wa kisiasa, kibiashara, kiusalama na kijeshi ili kupunguza utegemezi kwa mshirika mmoja na kujenga uwiano mpana wa kimkakati.

Muungano wa Makka: Mbadala wa Marekani au tabaka lingine la Usalama?

Kwa mujibu wa Salem Al-Yami, makubaliano ya ulinzi yaliyotiwa saini na Saudi Arabia, Uturuki na Pakistan mjini Makkah mwezi Agosti ni miongoni mwa hatua muhimu zaidi zinazoonyesha juhudi za Riyadh kupanua wigo wa washirika wake wa kiusalama.

Chini ya makubaliano hayo, shambulio dhidi ya mojawapo ya nchi hizo tatu linachukuliwa kuwa shambulio dhidi ya zote, katika mfumo wa ushirikiano wa pamoja wa ulinzi.

Hata hivyo, tangu yaliposainiwa, zimekuwepo hoja kuhusu jinsi yatakavyotekelezwa kwa vitendo, hasa baada ya Saudi Arabia kushambuliwa na Wahouthi bila Uturuki au Pakistan kuonyesha nia ya kuingilia kati kijeshi.

Mwezi Septemba, Pakistan ilisema hakuna hatua ya haraka ya kijeshi iliyokuwa imejadiliwa chini ya makubaliano hayo kujibu mashambulizi ya Wahouthi, ingawa ilisisitiza kuwa inaendelea kutekeleza wajibu wake chini ya mkataba huo.

Lakini mkutano wa Oktoba 5 ulionyesha mabadiliko ya wazi. Nchi hizo tatu zilitangaza kuanza mara moja utekelezaji wa ahadi zao za pamoja za ulinzi, ikiwemo maandalizi ya vikosi na uwezo wa kijeshi uliokubaliwa pamoja na taratibu za kuvipeleka kwa haraka nchini Saudi Arabia pindi itakapohitajika.

Aidha, Jenerali mstaafu Noman Mahmood wa Pakistan aliteuliwa kuwa Katibu Mkuu wa kwanza wa Muungano wa Makkah kwa muhula wa miaka mitatu, hatua inayoonekana kama juhudi za kuupa muungano huo msingi wa kudumu wa taasisi.

Kwa mujibu wa Aaron David Miller, muungano huo haupaswi kupuuzwa. Unaziunganisha Saudi Arabia, mojawapo ya wazalishaji wakubwa wa mafuta duniani; Pakistan, taifa lenye silaha za nyuklia; na Uturuki, mojawapo ya nguvu kubwa za kijeshi ndani ya NATO.

Hata hivyo, anaonya kuwa hilo halimaanishi kuwa nchi hizo tatu ziko tayari kuingia katika makabiliano ya moja kwa moja na Iran kwa ajili ya kuitetea Saudi Arabia, wala hazina kwa sasa uwezo unaolingana na ule ambao Marekani huipa Riyadh katika nyanja za kijeshi, ujasusi na ulinzi wa anga.

Naye Amr Hamzawy anaona Muungano wa Makkah kama sehemu ya mkakati mpana wa Saudi Arabia wa kujenga upya mfumo wake wa usalama kupitia miungano mipya ya kikanda, huku ikiendelea kudumisha ushirikiano uliopo.

Kwa mtazamo wake, makubaliano hayo yamejikita zaidi katika kuimarisha ulinzi wa ardhi, mipaka na miundombinu ya Saudi Arabia kuliko kuunda muungano wa kuendesha operesheni za kijeshi nchini Yemen.

Hamzawy pia anabainisha kuwa ingawa vikosi vya Pakistan tayari vina uwepo nchini Saudi Arabia, hali hiyo haimaanishi kwamba Islamabad au Ankara ziko tayari kushiriki moja kwa moja katika vita vya Yemen au kuingia katika mzozo wa wazi na Iran.

Mitchell Plitnick anakubaliana na tathmini hiyo. Anasema Muungano wa Makkah bado uko katika hatua za awali na mifumo yake ya utekelezaji haijakomaa kikamilifu.

Kwa mujibu wake, Saudi Arabia, Uturuki na Pakistan zinafahamu vema mipaka ya uwezo wa muungano huo. Ndiyo maana kwa sasa umeundwa zaidi kama ngao ya kujihami na kulinda mipaka, maeneo muhimu na miundombinu ya Saudi Arabia, badala ya kuwa muungano wa mashambulizi kwa ajili ya vita vya muda mrefu nchini Yemen.

Hata kama muungano huo utaimarika katika miaka ijayo, Plitnick anaamini kuwa hilo halimaanishi Riyadh imepata mbadala wa Washington, bali inaendelea kupanua chaguo zake za kiusalama huku ikipunguza utegemezi wake kwa mshirika mmoja.

Hata hivyo, wachambuzi wanaonya kuwa hata kama Muungano wa Makkah utaendelea kuimarika, hauwezi kwa sasa kuchukua nafasi ya Marekani kama mdhamini mkuu wa usalama wa Saudi Arabia.

Katika muktadha huo, suala la Israeli linaendelea kujitokeza katika mijadala kuhusu mustakabali wa usalama wa eneo hilo.

Israel katika hesabu mpya za usalama za Saudi Arabia

"Hatimaye, njia zote zinaishia kwa Israeli," anasema Mitchell Plitnick.

Kwa maoni yake, kadri Saudi Arabia inavyozidi kutafuta njia za kupunguza utegemezi wake kwa Washington, ndivyo uwezekano wa kuimarika kwa ushirikiano wake na Israeli unavyozidi kupata uzito katika mahesabu ya kimkakati ya Marekani. Lengo ni kujenga mtandao mpana wa ushirikiano wa kikanda unaoweza kukabiliana na ushawishi wa Iran.

Hili si wazo jipya. Kwa miaka kadhaa, Marekani imekuwa ikihamasisha Saudi Arabia kuhalalisha uhusiano wake na Israeli, huku makubaliano hayo yakihusishwa na dhamana za usalama, ushirikiano wa nyuklia kwa matumizi ya kiraia na manufaa mengine ya kimkakati kwa Riyadh.

Kwa mujibu wa Aaron David Miller, viongozi wa Saudi Arabia wamekuwa wakitaka kuimarisha nafasi ya nchi yao kama mshirika muhimu wa Marekani katika Mashariki ya Kati, lakini hawajakuwa tayari kuhalalisha uhusiano na Israeli kama sharti la kudumisha uhusiano huo.

Suala la ushirikiano wa nyuklia kwa matumizi ya kiraia pia limeendelea kuwa sehemu ya mazungumzo mapana kati ya Washington na Riyadh. Hata hivyo, makubaliano yoyote ya aina hiyo yanahitaji idhini ya Bunge la Marekani, jambo linaloongeza uzito wa kisiasa katika maamuzi hayo.

Mwezi Septemba, kulizuka ripoti za mkutano wa siri uliowahusisha maafisa wa kijeshi kutoka Marekani, Israeli, Saudi Arabia na baadhi ya nchi za Kiarabu kujadili Iran na hali ya usalama katika eneo hilo. Serikali zilizohusishwa hazikuthibitisha rasmi taarifa hizo.

Kutoka upande wa Israeli, Chuck Freilich, aliyewahi kuwa mshauri wa usalama wa taifa wa nchi hiyo, anaamini kuwa juhudi za Saudi Arabia kupanua ushirikiano wake wa kiusalama zinaweza kuipa Israeli nafasi kubwa zaidi katika eneo hilo. Anasema nchi hizo mbili zinaiona Iran kama tishio la pamoja.

Kwa mtazamo wake, Israeli inaweza kuwa mshirika muhimu wa Saudi Arabia katika maeneo kama ulinzi wa anga na kukabiliana na mashambulizi ya makombora. Anaongeza kuwa ushirikiano wa kiusalama kati ya nchi hizo unaweza kuongezeka hata kabla ya kuhalalishwa rasmi kwa uhusiano wa kidiplomasia.

Lakini Amr Hamzawy anaona kuna kikwazo kikubwa cha kisiasa. Anasema Saudi Arabia imehusisha wazi kuhalalisha uhusiano na Israeli na maendeleo ya suala la Palestina, jambo linaloifanya Riyadh kuwa makini katika hatua zozote za kusonga mbele.

Kwa upande wake, Salem Al-Yami anasisitiza kuwa kupanua ushirikiano na washirika tofauti hakumaanishi Saudi Arabia imebadili misingi ya sera yake ya nje. Kwa mujibu wake, uamuzi wowote kuhusu uhusiano na Israeli utaongozwa na maslahi ya Saudi Arabia na masharti ambayo Riyadh itaona yanafaa kutimizwa.

Kwa sasa, dalili zinaonyesha kuwa Saudi Arabia inaendelea kutafuta uwiano mpya wa usalama: ikidumisha uhusiano wake wa muda mrefu na Marekani, huku ikipanua ushirikiano na washirika wengine kama Uturuki na Pakistan, na kuacha wazi uwezekano wa ushirikiano mpana zaidi wa kikanda katika siku zijazo.