Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Kenya yathibitisha kisa cha kwanza cha Ebola, mgonjwa afariki dunia
Kenya imethibitisha ungonjwa wa Ebola kwa mara ya kwanza, ikimhusisha raia wake aliyekuwa akiishi Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) kwa miaka saba iliyopita.
Waziri wa Afya, Aden Duale, amesema mgonjwa huyo alianza kuugua takriban mwezi mmoja uliopita na alipata matibabu katika hospitali kadhaa nchini Congo kabla ya kusafiri kuja Kenya.
Kwa mujibu wa waziri huyo, mgonjwa huyo alifariki dunia siku chache baada ya kuwasili Nairobi, huku mamlaka za afya zikianza hatua za kufuatilia waliotangamana naye na kuimarisha tahadhari na kudhibiti kusambaa kwa ugonjwa huo.
Waziri wa Afya, Aden Duale, alisema: "Mgonjwa aliyebainika kuwa na virusi vya Ebola aina ya Bundibugyo alisafiri kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo kupitia Kampala nchini Uganda kabla ya kuwasili Nairobi tarehe 3 Oktoba."
Kwa mujibu wa Duale, mgonjwa huyo alipitia ukaguzi wa kawaida wa afya na taratibu za uhamiaji katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Jomo Kenyatta (JKIA) kabla ya kupelekwa hospitali na jamaa zake.
Taarifa zaidi zinasema mtu huyo alikiwa hospitalini Nairobi, aliwekwa katika kitengo maalumu cha wagonjwa kilichojengwa wakati wa janga la Covid-19.
Baadaye alianza kuonyesha dalili zinazohusishwa na Ebola, ikiwemo homa, baridi kali, uchovu, maumivu wakati wa kumeza, maumivu ya misuli na kuvuja damu chini ya ngozi. Vipimo vilivyofanywa vilithibitisha kuwa alikuwa ameambukizwa virusi vya Ebola aina ya Bundibugyo.
Duale ameongeza kuwa mgonjwa huyo alifariki usiku wa Jumatatu, huku maandalizi ya mazishi salama na yenye heshima yakiendelea kwa mujibu wa taratibu za kudhibiti Ebola.
Mamlaka za afya zimewatambua watu 28 waliokuwa wametangamana naye, wakiwemo jamaa zake na wahudumu wa afya. Wakati huo huo, juhudi zinaendelea kuwatafuta abiria wengine 23 na wafanyakazi wanne wa ndege waliosafiri naye.
Waziri Duale aliongeza kuwa Kenya imeendelea kuwa katika hali ya tahadhari dhidi ya dhidi ya Ebola tangu mlipuko wa ugonjwa huo ulipoanza mwezi Mei 2026.
Kufikia Oktoba 6, 2026, wasafiri 652,584 walikuwa wamefanyiwa uchunguzi katika mipaka na viwanja vya ndege nchini. Aidha, sampuli 267 zimefanyiwa vipimo katika maabara tano, zikiwemo Maabara ya Kitaifa ya Marejeo ya Virusi (NVRL), maabara za KEMRI Nairobi na Kisumu, pamoja na maabara mbili za muda zilizowekwa katika mpaka wa Busia na mpaka wa Lwakhakha, Kaunti ya Bungoma.
Kwa mujibu wa Waziri Duale, ni sampuli moja pekee iliyopatikana na virusi vya Ebola.
Kenya pia imeandaa kituo cha karantini na kuimarisha ufuatiliaji wa ugonjwa huo, ikieleza kuwa imekuwa ikifuatilia kwa karibu mlipuko wa Ebola nchini DRC tangu ulipoanza.
Zaidi ya watu 4,000 wamefariki dunia kutokana na Ebola nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo mwaka huu, katika mlipuko unaotajwa kuwa miongoni mwa milipuko mikubwa zaidi ya ugonjwa huo kuwahi kushuhudiwa nchini humo.
Ebola ni nini?
Ebola ni ugonjwa adimu lakini hatari unaosababishwa na virusi.
Virusi vya Ebola kwa kawaida huambukiza wanyama, hasa popo wa matunda, lakini milipuko kwa binadamu wakati mwingine huanza pale watu wanapokula au kushika wanyama walioambukizwa.
Huchukua siku mbili hadi 21 kwa dalili kujitokeza. Dalili huanza ghafla na kufanana na mafua, kama vile homa, maumivu ya kichwa, na uchovu