Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.

Bofya kuelekea tovuti kuu

Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data

Moja kwa moja, Iran yaonya nchi za Ghuba juu ya ushirikiano na Marekani

Abdullahi amesema "ni jambo lisilowezekana kwamba idadi kubwa ya ndege za kijeshi, hasa ndege za mafuta, ziwekwe katika vituo vya kanda hiyo bila nchi wenyeji kujua."

Muhtasari

Moja kwa moja

Na Ambia Hirsi

  1. UAE yasitisha biashara na Iran

    Falme za Kiarabu, UAE, zimesitisha biashara na miamala yote ya kifedha na Iran hadi hapo itakapotangaza vinginevyo, kutokana na kuongezeka kwa mvutano katika eneo hilo.

    Wizara ya Mambo ya Nje ya UAE imesema uamuzi huo umetokana na kuongezeka kwa mzozo unaotishia amani na usalama wa eneo hilo na kimataifa.

    Saa chache kabla ya tangazo hilo, Wizara ya Ulinzi ya UAE ilisema imegundua makombora mawili ya balistiki yaliyorushwa kutoka Iran kuelekea UAE.

    Kwa mujibu wa wizara hiyo, kombora moja lilianguka nje ya maji ya eneo la UAE, huku jingine likianguka katika ardhi ya UAE.

    Tangu kuanza kwa mashambulizi ya Marekani na Israel dhidi ya Iran, UAE imekuwa miongoni mwa nchi za eneo hilo zilizoathiriwa na mashambulizi ya Iran.

    Hatua hiyo mpya imeongeza zaidi wasiwasi wa kiusalama nchini UAE, wakati mvutano kati ya pande hizo ukiendelea.

  2. Korea Kusini yapunguza muda wa mazoezi ya kijeshi na Marekani

    Korea Kusini imesema mazoezi yake ya pamoja ya kijeshi na Marekani yatamalizika siku sita kabla ya muda uliopangwa, huku pia yakipunguzwa kwa kiwango.

    Hatua hiyo inafuatia agizo la Rais wa Marekani Donald Trump la kupunguza mazoezi hayo, akisema hayafai na yanaweza kuchukuliwa kuwa ya uchokozi dhidi ya Korea Kaskazini.

    Ripoti ambazo hazijathibitishwa zinaeleza kuwa Trump anatarajia kukutana na kiongozi wa Korea Kaskazini, Kim Jong Un, baadaye mwaka huu.

    Rais wa Korea Kusini, Lee Jae Myung, amesema nchi yake inahitaji kujenga uwezo imara na huru wa kijeshi, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kupunguza utegemezi wake kwa Marekani katika masuala ya ulinzi.

  3. Serikali Tanzania yawapa wazalishaji wa saruji siku nane kushusha bei

    Serikali ya Tanzania imewapa wazalishaji wa saruji muda wa siku nane kuongeza usambazaji na kushusha bei, baada ya mfuko wa saruji wa kilo 50 kufikia hadi shilingi 26,000 pesa za Tanzania sawa na dola 9.8 katika baadhi ya maeneo.

    Wizara ya Viwanda na Biashara iliitisha kikao cha dharura na wazalishaji tarehe 18 Agosti, na kuwapa hadi Agosti 28 kuchukua hatua za kukabiliana na upungufu wa saruji na kupunguza bei.

    Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Rajabu Salum, amesema serikali itafuatilia kwa karibu bei na upatikanaji wa saruji kabla ya kuamua iwapo hatua zaidi zitahitajika.

    Wazalishaji wamehusisha upungufu wa bidhaa hiyo na hitilafu katika baadhi ya mitambo mikubwa ya uzalishaji wa klinka, ikiwemo kiwanda cha Maweni mkoani Tanga na Dangote. Wasambazaji, kwa upande wao, wametaja kupanda kwa gharama za mafuta na usafirishaji.

    Hata hivyo, tofauti kati ya bei ya saruji kutoka kiwandani na ile ya rejareja imeibua maswali kuhusu ongezeko la bei katika mnyororo wa usambazaji.

    Utafiti wa hivi karibuni umeonyesha kuwa saruji ilikuwa ikiuzwa kwa wastani wa shilingi 321,251 pesa za Tanzania sawa na dola 121.47 kwa tani kabla ya kodi ya ongezeko la thamani, sawa na takriban shilingi 16,063 kwa mfuko wa kilo 50.

    Baraza la Taifa la Ujenzi linasema ongezeko la mahitaji ya ujenzi, gharama za usafirishaji na kuvurugika kwa usambazaji ni miongoni mwa sababu zinazochangia kupanda kwa bei.

    Hatua ya serikali inakuja wakati bei ya saruji ikiwa na athari kwa gharama za ujenzi, huku watumiaji na wafanyabiashara wakisubiri kuona iwapo agizo hilo litashusha bei katika siku zijazo.

  4. EU yasema mchakato wa kujumlisha kura za uchaguzi Zambia ulikuwa na dosari

    Ujumbe wa Waangalizi wa Uchaguzi wa Umoja wa Ulaya nchini Zambia umesema mchakato wa kujumlisha kura ulizorota kwa kiasi kikubwa baada ya Tume ya Uchaguzi ya Zambia, ECZ, kusimamisha zoezi hilo kutokana na visa vya vurugu.

    Kwa mujibu wa ujumbe huo, kujumlisha matokeo kulifanyika katika vituo 226 vya kujumlisha kura katika ngazi ya majimbo ya uchaguzi, huku zoezi likiendelea katika baadhi ya vituo vilivyosalia.

    Tarehe 14 Agosti, siku moja baada ya uchaguzi, ECZ ilisimamisha kujumlisha na kutangaza matokeo kote nchini kuanzia saa sita mchana hadi saa kumi na mbili jioni.

    ECZ ilisema kusimamishwa huko kulitokana na visa vya vurugu vilivyowalenga maafisa wa vituo vya kupigia kura na, katika baadhi ya maeneo, madai ya kuibiwa kwa masanduku ya kura.

    Hata hivyo, ujumbe wa Umoja wa Ulaya umesema haukupewa maelezo zaidi kuhusu maeneo yaliyoathiriwa au iwapo matukio hayo yalikuwa ya pekee au yalikuwa yameenea.

    Waangalizi wa Umoja wa Ulaya walifuatilia zoezi la kujumlisha kura katika vituo 64.

    Kabla ya zoezi kusimamishwa, asilimia 43 ya vituo vilivyofuatiliwa vilitathminiwa kuwa vinaendesha mchakato huo kwa kiwango “kizuri sana”.

    Hata hivyo, baada ya zoezi kurejelewa tarehe 14 Agosti, ujumbe huo unasema:

    “Waangalizi wa EU EOM walitathmini kwamba mwenendo wa jumla wa kujumlisha kura ulizorota kwa kiasi kikubwa.”

    Ujumbe huo umeeleza kuwa katika idadi kubwa ya vituo, maafisa walishindwa kurekodi matokeo kwenye fomu za kujumlishia kura mara tu yalipotangazwa na afisa msimamizi, kama inavyotakiwa na kanuni za uchaguzi wa nchi hiyo.

    Kwa mujibu wa waangalizi hao, hali hiyo ilishuhudiwa katika asilimia 42 ya vituo walivyofuatilia baada ya kusimamishwa kwa zoezi, ikilinganishwa na asilimia 30 kabla ya kusimamishwa.

    Pia, idadi ya vituo ambako maafisa walihakikisha kuwa takwimu zilizowekwa katika mfumo wa kidijitali wa usimamizi wa matokeo zinaendana na zile zilizo kwenye fomu za kujumlishia kura ilishuka kutoka asilimia 100 kabla ya kusimamishwa hadi asilimia 81 baadaye.

    Ujumbe huo unasema: “Waangalizi wa EU EOM waliripoti mapumziko marefu wakati wa mchakato wa kujumlisha kura katika karibu nusu ya vituo walivyofuatilia, huku maafisa wasimamizi wakionekana kusubiri na kupokea maelekezo kutoka makao makuu ya ECZ kabla ya kutangaza matokeo.”

    Waangalizi pia wamesema uwepo mkubwa wa wanajeshi katika vituo vya kujumlisha kura baada ya zoezi kurejelewa uliwatia hofu washiriki wengi.

    Kwa mujibu wa ujumbe huo, hali hiyo ilisababisha kupungua kwa idadi ya mawakala wa vyama na waangalizi wa wananchi waliokuwepo katika vituo hivyo ikilinganishwa na kipindi cha kabla ya kusimamishwa kwa zoezi.

    Ujumbe wa Umoja wa Ulaya pia umesema umepokea taarifa kuhusu visa vya vurugu katika baadhi ya vituo vya kujumlisha kura.

    Katika mji wa Lusaka, ujumbe huo unasema:

    “Kundi lenye silaha lilivamia kituo cha kujumlisha kura cha Makeni tarehe 15 Agosti na kuchukua karibu fomu zote za matokeo kutoka vituo vya kupigia kura.”

    Katika Mkoa wa Kati, waangalizi wamesema mashahidi kadhaa waliowaona na kuwahoji waliripoti kuwa watu wanaodaiwa kuwa wafuasi wa UPND walivamia vituo viwili kati ya vitatu vya kujumlisha kura katika Kabwe tarehe 16 Agosti.

    Ujumbe huo unasema uvamizi huo: “Ulivuruga kwa kiasi kikubwa mchakato wa kujumlisha kura.”

    Umoja wa Ulaya pia umeikosoa ECZ kwa kutoweka hadharani matokeo ya vituo vya kupigia kura kupitia tovuti yake.

    Ujumbe huo umesema: “ECZ haikuchapisha matokeo ya awali kwenye tovuti hiyo. Siku ya uchaguzi, ECZ ilithibitisha kwamba haitachapisha matokeo yaliyogawanywa kwa kila kituo cha kupigia kura, licha ya kuwa hatua hiyo ni muhimu kwa uwazi kwa sababu inaruhusu kila mtu kulinganisha matokeo ya vituo vya kupigia kura na yale yanayotangazwa na ECZ.”

    ECZ ilitangaza matokeo ya awali ya urais muda mfupi kabla ya saa tisa usiku wa Agosti 18.

    Umoja wa Ulaya sasa unasisitiza umuhimu wa ECZ kuchapisha matokeo yaliyogawanywa kwa kila kituo cha kupigia kura.

    “EU EOM inarudia wito wake wa kutaka kuwepo kwa uwazi wa hali ya juu katika hatua hii na katika sehemu nyingine za mchakato, na inasisitiza kwamba kuchapishwa kwa matokeo yaliyogawanywa kwa kila kituo cha kupigia kura na ECZ katika ngazi ya kitaifa kunaweza kusaidia kujenga imani katika mchakato.”

    Waangalizi wa Umoja wa Ulaya bado wako Zambia na wanaendelea kufuatilia mchakato wa uchaguzi katika majimbo yote 10 ya nchi hiyo.

    Haya yanajiri baada ya Tume ya Uchaguzi ya Zambia (ECZ) ilitangaza matokeo ya mwisho yaliyojumuishwa kutoka majimbo yote 226, yakionyesha kuwa Hichilema, wa chama cha United Party for National Development, alipata kura 2,965,326 (asilimia 60.49). Mpinzani wake mkuu, Brian Mundubile wa chama cha National Reconciliation Party for Unity and Prosperity, alipata kura 1,856,217 (asilimia 37.87). Tofauti ya kura kati ya Hichilema na mpinzani wake ni kura 1,109,109.

  5. Watu 107 wafariki dunia kwa maporomoko katika mpaka wa Cameroon na Jamhuri ya Afrika ya Kati

    Takriban watu 107 wamefariki dunia kufuatia maporomoko ya ardhi katika eneo la uchimbaji madini huko Zamboï, eneo lililo kwenye mpaka kati ya Cameroon na Jamhuri ya Afrika ya Kati, Meya wa eneo hilo ameiambia BBC.

    Amadou Abdon, Meya wa Garoua-Boulaï katika eneo la mashariki mwa Cameroon, alisema tukio hilo lilitokea mchana wa Jumanne.

    "Miili 107 ilitolewa kutoka kwenye vifusi," aliambia BBC, akiongeza kuwa tukio hilo "lilitokea katika eneo la uchimbaji madini lililoko ndani ya ardhi ya Jamhuri ya Afrika ya Kati, si mbali na mpaka na Cameroon."

    Haijulikani mbado kilichosababisha maporomoko hayo ya ardhi. Video zinazosambaa mtandaoni zinaonekana kuonyesha udongo ukiangukia wachimbaji kadhaa wa dhahabu wa kiwango cha chini waliokuwepo eneo hilo.

    Juhudi za uokoaji zinaendelea huku kukiwa na hofu kuwa idadi ya vifo inaweza kuongezeka.

    Uchimbaji wa dhahabu kwa njia za zisizo sawa ni chanzo kikuu cha mapato kwa jamii nyingi mashariki mwa Cameroon. Hata hivyo, mazingira ya kazi ni duni, huku wachimbaji mara nyingi wakikabiliwa na hatari za kiafya na kimazingira.

    Maporomoko ya migodi na ardhi ni matukio ya mara kwa mara nchini humo, ambapo mashimo ya uchimbaji mara nyingi huachwa wazi na mvua kubwa huathiri udongo.

  6. Serikali Tanzania yasitisha leseni ya gazeti la MwanaHALISI kwa miezi sita

    Serikali ya Tanzania imesitisha leseni ya kuchapisha na kusambaza gazeti la MwanaHALISI kwa kipindi cha miezi sita kuanzia leo, Agosti 19, 2026.

    Taarifa ya Idara ya Habari Maelezo imesema gazeti hilo limekiuka masharti ya utendaji kwa kuchapisha maudhui yaliyokosa usahihi, mizania na uthibitisho wa kutosha.

    Hatua hiyo imehusishwa na toleo namba 571 la gazeti hilo la Agosti 6 hadi 12, 2026, lililokuwa na habari yenye kichwa “Nchimbi agoma kujiuzulu.” Gazeti hilo lilimtaja Makamu wa Rais wa Tanzania, Emmanuel Nchimbi, katika habari hiyo bila kumuhoji au kumnukuu, kwa mujibu wa Maelezo.

    Kwa mujibu wa Idara hiyo, uamuzi huo umechukuliwa chini ya Kifungu cha 9(b) cha Sheria ya Huduma za Habari, Sura ya 229, baada ya kubainika kuwa gazeti hilo limeendelea kurudia makosa ya kitaaluma licha ya kupewa maonyo ya awali.

    Kabla ya uamuzi huo, uongozi wa MwanaHALISI ulipewa fursa ya kujieleza katika kikao kilichofanyika Agosti 7 katika ofisi za Maelezo, Dar es Salaam.

    Gazeti hilo lilipewa muda kuwasilisha maelezo ya maandishi kuhusu mazingira yaliyopelekea kuchapishwa kwa habari hiyo, lakini Maelezo imesema majibu hayo hayakutosha kuondoa hoja zilizowasilishwa dhidi yake.

    Kwa mujibu wa Idara hiyo, katika mwaka 2026 pekee, MwanaHALISI imeitwa kutoa maelezo mara tatu, mwezi Februari, Mei na Agosti, kuhusu habari mbalimbali zilizochapishwa.

    Miongoni mwa habari zilizotajwa ni “Samia 2021 atakutana lini na Samia wa 2026?”, iliyochapishwa Februari, pamoja na “ICC haikwepeki” na “Hawa kuchongewa na watangoka tu”, zilizochapishwa Mei 2026.

    MwanaHALISI pia iliwahi kusitishiwa uchapishaji kwa miezi miwili mwaka 2017 kutokana na makosa ya aina hiyo, kwa mujibu wa Maelezo.

    Hadi sasa, MwanaHALISI haijatoa maelezo kuhusu uamuzi huo wa Serikali.

    Kwa hatua hiyo, gazeti hilo halitaruhusiwa kuchapisha na kusambaza matoleo yake kwa kipindi cha miezi sita kuanzia Agosti 19, 2026.

    Pia unaweza kusoma:

  7. Iran yaonya nchi za Ghuba juu ya ushirikiano na Marekani

    Ali Abdollahi, Mkuu wa Wafanyakazi wa Jeshi la Iran, ameonya kuhusu uwepo wa kijeshi wa Marekani katika vituo vilivyoko katika nchi za Ghuba ya Uajemi, kupitia ujumbe aliouchapisha kwenye mtandao wa kijamii wa X.

    Abdullahi aliandika: "Ni jambo lisilowezekana kwamba idadi kubwa ya ndege za kijeshi, hasa ndege za mafuta, ziwekwe katika vituo vya kanda hiyo bila nchi wenyeji kujua."

    Alisema kuwa Iran itachukulia "msaada" wowote kwa jeshi la Marekani kama "ushirikiano" na vikosi vya kijeshi vya nchi hiyo.

    Wakati wa vita kati ya Iran, Israel na Marekani, Iran ilifanya mashambulizi ya mara kwa mara dhidi ya kambi za kijeshi katika nchi za Ghuba zilizokuwa zikishirikiana na Marekani.

    Soma Zaidi Hapa:

  8. Angélique Kidjo aweka historia, awa msanii wa kwanza Mwafrika kupata nyota Hollywood

    Nyota wa muziki Angélique Kidjo amekuwa msanii wa kwanza Mwafrika mwenye asili ya Afrika kuchaguliwa kupewa nyota kwenye eneo maarufu la Hollywood Walk of Fame.

    Kidjo, ambaye anatoka nchi ya Benin iliyo Afrika Magharibi ameshinda tuzo tano za Grammy, alikuwa miongoni mwa majina 35 yaliyotangazwa katika orodha ya mwaka 2026 ya Walk of Fame.

    Msanii huyo mwenye umri wa miaka 64 alitajwa kama "mwimbaji nyota wa kipekee" wa Afrika wakati wa mkutano na waandishi wa habari uliotangaza orodha hiyo siku ya Jumatano.

    Mwimbaji Miley Cyrus, muigizaji Timothée Chalamet, mwigizaji Demi Moore na mchezaji wa zamani wa mpira wa kikapu Shaquille O'Neal pia ni miongoni mwa wale watakaotunukiwa nyota kwenye njia hiyo maarufu ya Los Angeles.

    Kidjo anapokea heshima hiyo baada ya kufanya muziki kwa zaidi ya miongo minne na kutoa albamu 16.

    Mwimbaji huyo amejipatia mashabiki kote duniani kutokana na sauti yake yenye nguvu na uwezo wa kuchanganya mitindo ya Afrika Magharibi na aina nyingine za muziki kama vile funk, jazz na R&B.

    Orodha yake ndefu ya wasanii aliowahi kushirikiana nao inajumuisha majina makubwa kama vile Burna Boy, Philip Glass, Sting na Alicia Keys.

    Kidjo anaungana na Charlize Theron, mwigizaji mzungu kutoka Afrika Kusini, katika kuiwakilisha Afrika kwenye Walk of Fame, ambayo ina jumla ya nyota zaidi ya 2,700.

  9. FIFA imejiharibia yenyewe kwa mpango wa Kombe la Dunia - Mkuu wa Ligi Kuu ya Uingereza

    Mtendaji mkuu wa Ligi Kuu ya England, Richard Masters amekosoa mpango wa Rais wa shirikikisho la soka duniani Fifa, Gianni Infantino wa kuuza hisa za Kombe la Dunia, akisema shirikisho hilo "limebonyeza kitufe cha kujiangamiza.

    Infantino yuko chini ya shinikizo kubwa kuhusu jaribio lake, ambalo baadaye lilishindikana, la kuunda kampuni mpya ya kusimamia haki za kibiashara na tiketi za mashindano yote ya Fifa, ikiwa ni pamoja na Kombe la Dunia, huku asilimia 21 ikipangwa kuuzwa kwa kampuni bnafsi ya uwekezaji.

    Mpango wa Fifa Forward Enterprise (FFE) ulisitishwa baada ya ukosoaji mkubwa wa mashirikisho kadhaa, yanayoongozwa na Uefa, ambayo yametishia kususia mashindano yote ya Fifa.

    Masters aliunga mkono uamuzi wa Shirikisho la Soka la England (FA) kuondoa uungwaji mkono wake kwa Infantino, na akatoa wito wa kupatikana kwa mgombea mpya wa urais wa FIFA ambaye anaweza kuiunganisha dunia ya soka.

    Soma Zaidi Hapa:

  10. Meli ya mafuta ya UAE iliyozuiliwa Hormuz inaelekea Bandar Abbas

    Vyombo vya habari vya Iran vinaripoti kuwa meli ya mafuta ya Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE) iliyozuiliwa katika Mlango- wa Bahari wa Hormuz imebadilisha mkondo kuelekea Bandar Abbas.

    Awali, meli hiyo ilikuwa imezuiliwa kaskazini mwa Mlango-bahari wa Hormuz.

    Kwa mujibu wa ripoti za vyombo vya habari vya Iran, meli hiyo ilikuwa inaelekea Bandar Jebel Ali, lakini sasa imebadilisha njia yake kuelekea Bandar Abbas.

    Hatua hiyo mpya inakuja wakati Umoja wa Falme za Kiarabu ikitangaza kusimamisha shughuli zote za kibiashara na kifedha na Iran hadi pale itakapotoa taarifa nyingine.

    Wakati wa kuanza kwa vita kati ya Marekani na Israel dhidi ya Iran, Umoja wa Falme za Kiarabu ililengwa na mashambulizi ya Iran zaidi kuliko nchi nyingine za eneo la Ghuba, lakini baada ya kusaini hati ya makubaliano, Iran haikuishambulia nchi hiyo.

    Soma zaidi:

  11. Waziri wa Ulinzi wa Ukraine aliyefukuzwa kazi aitisha uchaguzi wa urais

    Aliyekuwa Waziri wa Ulinzi wa Ukraine, Mykhailo Fedorov, ametoa wito wa kufanyika kwa uchaguzi wakati wa vita, hatua ambayo wengi wanaiona kuwa changamoto kubwa zaidi kwa uongozi wa Rais Volodymyr Zelensky tangu vita dhidi ya Urusi vilipoanza mwezi Februari 2022.

    "Demokrasia haiwezi kushikiliwa mateka na Urusi," alisema Fedorov, aliye na umri wa miaka 35, katika video iliyowekwa kwenye mtandao wa YouTube siku ya Jumanne, akiongeza kuwa Ukraine inapigana "hasa ​​kwa sababu tunataka kubaki kuwa taifa huru la Ulaya".

    Tangu Urusi Iilipoanza uvamizi wake, Ukraine imekuwa chini ya sheria za kijeshi, hali iliyosababisha uchaguzi kusimamishwa.

    Fedorov, ambaye hakumtaja Zelensky moja kwa moja katika video hiyo, aliondolewa ghafla katika wadhifa wake wa Waziri wa Ulinzi mwishoni mwa mwezi Julai, miezi sita tu baada ya kuteuliwa.

    Zelensky bado hajatoa tamko lolote kuhusiana na video hiyo ya Fedorov, ambaye kufutwa kwake kazi kulichochea maandamano makubwa.

    Fedorov alisifiwa kwa kuimarisha wizara hiyo, kuongoza juhudi za kupambana na ufisadi, na kutumia takwimu kuchambua na kujaribu kuboresha utendaji kaziwakati wa vita.

    Inasadikiwa kuwa kufutwa kwake kulitokana na mvutano kati yake na kamanda mkuu wa jeshi, Oleksandr Syrskyi.

    Katika video hiyo ya YouTube, Fedorov hakuelezea mipango yake ya kisiasa, badala yake alijikita katika umuhimu wa kuwepo kwa "utaratibu halali, salama na unaotekelezeka ambao utaiwezesha Ukraine kurejesha mchakato kamili wa kidemokrasia hata katikati ya vita vinavyoendelea kwa muda mrefu".

    Fedorov ndiye mwanasiasa wa kwanza kigogo kuitisha uchaguzi mkuu ambapo kulingana na sheria za Ukraine,ni marufuku kuandaa uchaguzi wakati wa vita.

    Pia unaweza kusoma:

  12. Ufaransa yawafukuza wanadiplomasia wawili wa Iran

    Ufaransa imetangaza kuwa inajiandaa kuwafukuza wanadiplomasia wawili wa Iran kutoka nchini humo katika siku chache zijazo.

    Waziri wa Mambo ya Nje wa Ufaransa Jean-Noël Barrot alidokeza taarifa hizo Jumanne kwenye mtandao wa kijamii X.

    Hatua hiyo inakuja siku moja baada ya Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran kutangaza kwamba wafanyakazi wawili wa ubalozi wa Ufaransa waliohusika katika mzozo wa kidiplomasia huko Tehran mwezi Julai hawataruhusiwa kurudi Iran.

    Hapo jana Jumanne Wizara ya Ujasusi ya Iran iliishutumu serikali ya Ufaransa kwa "kuingilia masuala ya ndani ya Iran na kujaribu kuleta ushawishi."

    Mnamo Julai 20, Waziri wa Mambo ya Nje wa Ufaransa alivituhumu vikosi vya usalama vya Iran kwa kukiuka kinga yao ya kidiplomasia kwa "kuwatisha vikali" wawili hao.

  13. Marekani yatangaza vikwazo vipya kwa viongozi wakuu wa ICC

    Waziri wa mambo ya kigeni wa Marekani Marco Rubio ametangaza vikwazo dhidi ya Tomoko Akane, Rais wa Mahakama ya Kimataifa ya kushughulikia kesi za uhalifu wa kivita na uhalifu dhidi ya ubinadamu ICC.

    Hatua hiyo ni ongezeko la hivi karibuni zaidi la msimamo mkali wa utawala wa Trump katika kampeni yake ya “kuivunja” mahakama hiyo, ambayo imepewa mamlaka na zaidi ya nchi wanachama 120 kuchunguza uhalifu wa kivita.

    Rubio alisema kuwa Marekani ilikuwa ikiweka vikwazo dhidi ya Rais wa ICC, Tomoko Akane wa Japan, na Mwanasheria Mkuu wa Mashtaka wa ICC, Abdoulaye Seye wa Senegal, kwa kushiriki katika juhudi za ICC za “kuwafungulia mashtaka maafisa ambao serikali zao hazijaridhia kuwa wanachama wa mahakama hiyo ya ICC.”

    ICC ilisema inaendelea kuwaunga mkono wafanyakazi wake na inaamini kwamba hatua kama zile zilizotangazwa na Rubio “zinadhoofisha utawala wa sheria.”

    Soma zaidi:

  14. Vita vya Ukraine: Raia 62 wa Ghana wauawa wakiipigania Urusi

    Waziri wa mambo ya nje wa Ghana Samuel Okudzeto Ablakwa, amesema raia 62 wa nchi hiyo wameuawa wakiipigania Urusi katika vita vya Ukraine huku wengine 15 wakiwa hawajulikani waliko.

    Bwana Ablakwa ambaye yuko Moscow kwa mazungumzo na mwenzake wa Urusi Sergei Lavrov, amewaambia waandishi wa habari kuwa kusajiliwa kwa raia wa mataifa ya kiafrika kupigana katika vita kati ya Urusi na Ukraine kunapaswa kukoma.

    Kulingana na maafisa wa Ukraine, zaidi ya Waghana 272 wamesajiliwa na Urusi tangu mwaka 2022.

    Ukraine inasema takriban Waafrika 2,000 kutoka mataifa 36 ya Kiafrika wanapigana kwa niaba ya Urusi.

    Maafisa wa Urusi wanakanusha kuwa wanawasajili waafrika kinyume na sheria.

    Maelzo zaidi:

  15. Meta yashtakiwa kwa 'kuwateka kimawazo' watoto kwenye Facebook na Instagram

    Matumizi ya mitandao ya kijamii kwa vijana na watoto unamulikwa darubini kali katika kesi ambayo imeanza kusikilizwa huko California Marekani.

    Mawakili wa majimbo29 ya Marekani wanaishutumu Kampuni ya Meta kwa kusababisha watoto kutumbukia katika uraibu wa kutumia visivyo mitandao yao ya Facebook na Instagram huku wakiupotosha umma kuhusu hatari zake.

    Meta inakanusha madai hayo, lakini imekiri kwamba baadhi ya watumiaji wa mitandao ya kijamii wanakabiliwa na changamoto.

    Majimbo hayo ya Marekani yanataka Meta kutozwa mabilioni ya dola. Mahakama pia inaweza kuamuru mabadiliko katika jinsi Facebook na mitandao mingine ya kijamii inavyofanya kazi.

    Mahakama imesikia hoja kutoka kwa mawakili wanaowakilisha majimbo hayo kwamba Meta ilikusudia kukiteka kimawazo kizazi cha sasa cha watoto kwenye Facebook na Instagram.

    Baraza la majaji huko Oakland, California litatumia wiki sita zijazo kuchunguza madai ya mawakili wakuu kutoka majimbo kadhaa ya Marekani, na mawakili wa kampuni hiyo ya mitandao ya kijamii, ambao kila mmoja alipinga hoja za mwenzake wakati kesi hiyo ikifunguliwa hapo jana Jumanne.

    Wakili wa jimbo la California alidai Meta iligundua mamilioni ya watoto wenye umri wa miaka 11 na 12 walikuwa kwenye Instagram na haikuchua hatua za kutosha kuwazuia watoto hao. Hata hivyo, Wakili wa Meta alisema ni takriban watumiaji laki moja tu wa umri huo waliogunduliwa na pia alidai uraibu wa mitandao ya kijamii haupo.

    Baada ya wakili wa jimbo la California kusema Meta ilifahamu majukwaa yake yanadhuru afya ya akili ya vijana, upande wa Meta ulisema kampuni hiyo inapuuzwa kutokana na jinsi ilivyochangia vijana wengi zaidi kuwa na wakati mzuri na wanavyonufaika na mitandao hiyo.

    Kesi hiyo inatokana na kesi iliyofunguliwa mwaka 2023 na majimbo 29 ya Marekani, yanayodai ukiukwaji mkubwa wa sheria za Serikali kuu na za majimbo kuhusu kulinda faragha za watoto.

    Si tu kwamba majimbo hayo yanadai mabilioni ya dola kutoka kwa Meta, pia yanaitaka ifanye mabadiliko kwenye Instagram na Facebook, ikiwa ni pamoja na kukomesha idadi ya "likes" na mfumo wa kusogeza mbele maudhui bila kikomo.

    Soma pia:

  16. UAE yasitisha biashara na miamala yote ya kifedha na Iran

    Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE) imesema kuwa imesitisha shughuli zote za kibiashara na kifedha na Iran hadi itakapotangazwa tena.

    Kwa mujibu wa mashirika ya habari, Wizara ya Mambo ya Nje ya UAE ilitangaza kuwa uamuzi huo umefikiwa kutokana na kuongezeka kwa mivutano katika eneo hilo, mivutano inayodhoofisha amani na usalama.

    Saa chache zilizopita, Wizara ya Ulinzi ya UAE ilisema kuwa Iran ilirusha makombora mawili ya masafa marefu) kuelekea nchi hiyo; moja liliangukia nje ya maji ya eneo la mamlaka ya UAE na la pili liliangukia ndani ya maji ya nchi hiyo.

    Hata hivyo Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amekanusha madai ya UAE kwamba Iran imerusha makombora kuelekea nchi hiyo.

    Ismail Beqai alieleza katika taarifa kwamba "madai ya Umoja wa Falme za Kiarabu hayana msingi."

    Tangu kuanza kwa vita vya Marekani na Israel dhidi ya Iran, UAE imekuwa ikilengwa na mashambulizi ya Iran zaidi kuliko nchi nyingine yoyote katika eneo la mashariki ya kati.

    Hata hivyo, Iran haikuishambulia UAE katika operesheni hiyo baada ya kusainiwa kwa mkataba wa maelewano.

    Soma zaidi:

  17. Natumai hujambo. Karibu kwa matangazo ya moja kwa moja.