Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
'Ulimweleza Akili Mnemba siri zako, Je, ziko salama?'
Huenda umeshawahi kuishirikisha akili mnemba changamoto za ndoa yako, matatizo ya kifedha, hofu zako, masuala ya afya au hata siri za familia yako. Lakini umewahi kujiuliza nini kitatokea kampuni inayohifadhi mazungumzo hayo ikifilisika? Nani atapata taarifa zako, na je, maisha yako ya faragha yanaweza kugeuka kuwa bidhaa ya kibiashara?
Hebu fikiria umemweleza mtu siri yako kubwa kabisa, ukiamini kwamba mazungumzo yenu yatabaki kuwa ya faragha. Kisha, siku moja, unagundua kwamba mtu huyo hayupo tena, na siri ulizomweleza zimeachwa mahali ambapo mtu mwingine anaweza kuzipata.
Hili ndilo swali tata linalozuka kufuatia matatizo ya kifedha na hatua za kufilisika kwa kampuni ya Character.AI, mojawapo ya majukwaa maarufu ya akili mnemba yanayowawezesha watumiaji kuzungumza na wahusika wa kidijitali.
Tukio hili linaibua tahadhari inayovuka mipaka ya kampuni moja: Taarifa tunazozikabidhi kwa akili mnemba zinaweza kuendelea kuwepo hata baada ya kampuni iliyozikusanya kutoweka.
Rafiki yako wa kidijitali anaweza kujua mengi kukuhusu
AI ni jukwaa linalowawezesha watumiaji kuzungumza na wahusika walioundwa kwa kutumia akili mnemba. Wahusika hao wanaweza kuwa watu wa kubuni, watu maarufu au marafiki wa kidijitali waliobuniwa kulingana na matakwa ya mtumiaji.
Tofauti na injini za kawaida za utafutaji, ambazo hasa hutoa majibu ya maswali, mifumo hii imeundwa kuiga mazungumzo na mahusiano ya kibinadamu.
Baadhi ya watumiaji huitumia kutafuta ushauri, wengine huitazama kama rafiki, mshauri au hata mwenzi wa kimapenzi.
Fikiria kuwa na rafiki wa kidijitali anayekumbuka mazungumzo yenu, anayekujibu kwa upole na anayepatikana kila unapomhitaji.
Kwa kijana anayekabiliwa na upweke au mtu anayepitia changamoto za maisha, mawasiliano hayo yanaweza kuonekana kuwa ya karibu sana.
Lakini kuna jambo moja ambalo halipaswi kusahaulika: Urafiki huo unafanyika ndani ya mfumo wa kiteknolojia unaomilikiwa na kampuni ya kibiashara.
Nyuma ya majibu hayo ya kirafiki kuna kampuni inayokusanya na kuchakata taarifa za watumiaji.
Kampuni inapokosa fedha, taarifa zako zinakuwa na hatima gani?
arehe 12 Oktoba 2026, Character Technologies, kampuni inayomiliki Character.AI, iliwasilisha maombi ya ulinzi wa kisheria wa kufilisika chini ya Sura ya 11 ya sheria za Marekani.
Hatua hiyo ilikuja wakati kampuni ikikabiliwa na gharama kubwa za uendeshaji, changamoto za kisheria na shinikizo la kifedha.
Kwa mujibu wa taarifa za nyaraka za mahakama zilizoripotiwa na Reuters, kampuni ilikuwa ikipata hasara ya takribani dola milioni 8 hadi 9 za Marekani kila mwezi, licha ya kuwa na watumiaji hai wapatao milioni 12.
Gharama za kompyuta zenye uwezo mkubwa wa kuchakata taarifa pamoja na gharama za kuajiri wataalamu wa teknolojia zilikuwa zikifanya uendeshaji wake kuwa mzigo mkubwa wa kifedha.
Sasa kampuni hiyo imeingia katika mchakato wa kisheria wa kutafuta namna ya kuuza baadhi ya mali zake.
Hapa ndipo suala la faragha linapokuwa zito.
Kampuni inapofilisika, mali zake zinaweza kuuzwa au kuhamishiwa kwa wamiliki wengine ili kutatua madeni na majukumu yake ya kifedha.
Mali hizo zinaweza kujumuisha teknolojia, haki za umiliki wa bunifu, mifumo ya kompyuta, taarifa za wateja na kumbukumbu nyingine za kibiashara.
Swali kubwa ni hili: Je, taarifa za siri ambazo watumiaji wamekuwa wakizishirikisha mifumo hiyo zinaweza kuhusishwa na mchakato huo?
Mazungumzo yako yanaweza kuwa na thamani ya kibiashara
Matatizo ya Character.AI yameibua mjadala kuhusu thamani ya taarifa ambazo watu wanazishirikisha majukwaa ya akili mnemba.
Fikiria aina ya mazungumzo yanayofanyika kila siku:
Mtu anamweleza mfumo wa akili mnemba kwamba ndoa yake inakabiliwa na matatizo.
Kijana anazungumzia unyanyasaji, upweke au msongo wa mawazo.
Mtu mwingine anashirikisha changamoto za madeni na hali yake ya kifedha.
Mtumiaji anaomba ushauri kuhusu tatizo la kiafya.
Mwingine anafichua mgogoro wa kifamilia au siri ya rafiki yake.
Mazungumzo hayo yanaweza kufichua mengi zaidi ya jina na anwani ya barua pepe.
Yanaweza kuonyesha udhaifu wa kihisia, mahusiano ya kifamilia, hali ya afya, mitazamo binafsi na mienendo ya mtu.
Katika nyaraka za mahakama zilizowasilishwa Oktoba 2026, muungano wa maafisa wakuu wa sheria kutoka majimbo mbalimbali ya Marekani ulieleza wasiwasi kuhusu aina ya taarifa nyeti zinazoweza kuhifadhiwa na Character.AI.
Taarifa hizo zinajumuisha mazungumzo ya maandishi na sauti, umri wa watumiaji, taarifa za kihisia na kiafya, mienendo ya watumiaji, vitambulisho vya vifaa vya kielektroniki na taarifa za malipo kwa baadhi ya wateja wanaolipia huduma.
Wasiwasi mwingine unahusu uwezekano wa taarifa hizo kutumiwa kutengeneza mifumo mipya, kufundisha akili mnemba, kuchambua mienendo ya watumiaji na kuwalenga kwa matangazo.
Kwa maneno mengine, taarifa unazoshirikisha mfumo wa akili mnemba zinaweza kuwa na thamani kubwa zaidi kuliko unavyodhani.
Disney imeingia kwenye picha, lakini kuna jambo muhimu la kuelewa
Mojawapo ya maendeleo yaliyovutia katika sakata hili ni kuhusika kwa kampuni kubwa ya burudani ya Disney.
Character.AI ilikubaliana na pendekezo la mkataba wa dola milioni 20 za Marekani, unaohusu leseni isiyo ya kipekee ya kutumia baadhi ya haki za umiliki wa bunifu.
Disney pia imewaajiri baadhi ya wafanyakazi wa Character.AI.
Hata hivyo, kuna tofauti muhimu ambayo watumiaji wanapaswa kuielewa: Pendekezo hilo la Disney halijumuishi historia za mazungumzo ya watumiaji na taarifa zao binafsi.
Kwa hiyo, si sahihi kusema kwamba Disney imenunua siri za watumiaji wa Character.AI.
Lakini kwa nini basi wataalamu wa faragha bado wana wasiwasi?
Ni kwa sababu mchakato wa kufilisika unahusisha mali nyingine ambazo zinaweza kuuzwa kwa wanunuzi tofauti.
Hapo ndipo jambo jingine muhimu zaidi linapoibuka.
Mnunuzi mwingine ajitokeza kwa ofa ya dola milioni 10
Tarehe 14 Novemba 2026, kampuni inayojulikana kama Smirks and Pangs Acquisition LLC ilitajwa kuwa mnunuzi mwingine anayependekezwa kwa baadhi ya mali ambazo hazijajumuishwa katika makubaliano ya Disney.
Pendekezo lake ni kulipa dola milioni 10 za Marekani taslimu pamoja na kuchukua baadhi ya madeni maalumu yaliyotajwa katika makubaliano hayo.
Kifurushi cha mali kinachohusishwa na pendekezo hilo kinaripotiwa kujumuisha tovuti na programu za Character.AI, mifumo ya akili mnemba, taarifa za matumizi ya bidhaa na kumbukumbu za uzingatiaji wa sheria.
Jambo linalostahili kuangaliwa zaidi ni kwamba taarifa za matumizi ya bidhaa ni miongoni mwa mali zinazotajwa katika mchakato huo.
Hata hivyo, hili halimaanishi kwamba mazungumzo yote ya siri ya watumiaji tayari yameuzwa. Wala halithibitishi ni taarifa zipi hasa zitakazohamishwa kwa mnunuzi atakayepatikana.
Lakini linazidisha umuhimu wa swali moja: Nani atakuwa na mamlaka ya kusimamia taarifa hizo baada ya mchakato wa mauzo kukamilika?
Kwa mujibu wa ratiba iliyotangazwa, mwisho wa kupokea zabuni nyingine ni tarehe 24 Novemba, mnada umepangwa kufanyika tarehe 1 Desemba, huku kikao cha mahakama kuhusu uuzaji wa mali hizo kikipangwa kufanyika tarehe 3 na 4 Desemba 2026.
Mchakato huo bado unaendelea.
Kesi za watoto zinazotia wasiwasi
Mjadala kuhusu Character.AI hauishii kwenye matatizo ya kifedha na faragha ya taarifa.
Pia unahusishwa na madai mazito kuhusu usalama wa watoto.
Mojawapo ya kesi zilizoripotiwa sana ni ile ya kijana wa miaka 14, Sewell Setzer III, ambaye mama yake, Megan Garcia, alidai kwamba mwanawe alianzisha uhusiano wa kihisia na kingono usiofaa na mfumo wa Character.AI uliotengenezwa kwa mfano wa mhusika wa kipindi cha televisheni.
Kijana huyo alifariki kwa kujitoa uhai mwaka 2024.
Mama yake alidai kwamba mazungumzo yake na mfumo huo wa akili mnemba yalichangia kifo chake.
Mwezi Januari 2026, Google na Character.AI zilikubaliana kumaliza kesi ya familia hiyo kwa makubaliano ya nje ya mahakama. Masharti ya kifedha ya makubaliano hayo hayakuwekwa wazi kwa umma.
Familia nyingine pia zimefungua kesi zikidai kwamba mifumo hiyo iliwachochea watoto kujidhuru, kuimarisha mawazo hatari au kuwahusisha katika mazungumzo ya kingono yasiyofaa.
Kesi nyingine ilihusisha madai kwamba mfumo wa mazungumzo ulimhimiza kijana kufikiria kuwaua wazazi wake baada ya kutokubaliana kuhusu muda wa matumizi ya simu.
Ni muhimu kusisitiza kwamba haya ni madai yaliyowasilishwa katika kesi za kisheria, si uthibitisho kwamba kila mfumo wa akili mnemba una tabia hizo.
Hata hivyo, matukio hayo yanaonyesha hatari zinazoweza kujitokeza pale watoto walio katika mazingira magumu wanapojenga uhusiano mkubwa wa kihisia na mifumo ambayo si binadamu na haiwezi kutoa huduma halisi za kitaalamu.
Hali inakuwa ya kutisha zaidi tunapofikiria kwamba mazungumzo yanayohusishwa na kesi hizo yanaweza kuwa na taarifa nyeti sana kuhusu watoto.
Hata usipotumia akili mnemba, unaweza kuathirika
Hili ni jambo ambalo watu wengi huenda hawajalifikiria.
Si lazima uwe mtumiaji wa Character.AI au mfumo mwingine wowote wa akili mnemba ili taarifa zinazokuhusu ziweze kuingia katika kumbukumbu zake.
Fikiria mtu anayeuliza mfumo wa akili mnemba:
"Dada yangu amekuwa akisumbuliwa na msongo wa mawazo. Ninawezaje kumsaidia?"
Au:
"Rafiki yangu amenieleza siri nzito kuhusu maisha yake. Nifanye nini?"
Bila kujua, unaweza kuwa umeshirikisha mfumo huo taarifa binafsi za mtu mwingine ambaye hakukubali taarifa zake zitumike kwa namna hiyo.
Mtu huyo huenda hajawahi hata kufungua akaunti kwenye jukwaa hilo, lakini taarifa zinazomhusu zinaweza kuwa sehemu ya mazungumzo yanayohifadhiwa na kampuni ya teknolojia.
Hii inaonyesha kwamba suala la faragha katika akili mnemba halimhusu mtumiaji mmoja pekee.
Linaweza kuathiri familia, marafiki, wafanyakazi wenzako na jamii kwa ujumla.
Je, huu ni mwanzo wa mgogoro mkubwa katika sekta ya akili mnemba?
Character.AI inaweza kuwa kampuni moja tu, lakini changamoto zake zinaibua maswali kuhusu mustakabali wa sekta nzima ya akili mnemba.
Kutengeneza na kuendesha mifumo mikubwa ya akili mnemba kunahitaji fedha nyingi kwa ajili ya miundombinu ya kompyuta, wataalamu na uwekezaji wa muda mrefu.
Baadhi ya kampuni zinaweza kushindwa kupata mapato yanayotosha kufidia gharama hizo.
Ikiwa kampuni nyingi zaidi zitakabiliwa na matatizo ya kifedha, taarifa za wateja zinaweza kuwa miongoni mwa mali muhimu katika mchakato wa kuungana kwa kampuni, kununuliwa au kufilisika.
Hatari si kwamba kila kampuni ya akili mnemba itafilisika.
Hatari ni kwamba watumiaji wanakabidhi taarifa zao nyeti kwa kampuni ambazo huenda hawajui hata kama zina uwezo wa kuendelea kufanya biashara kwa miaka mingi ijayo.
Pia tunapaswa kuelewa kwamba sera ya faragha si dhamana kwamba taarifa zako zitabaki chini ya umiliki uleule milele.
Sheria zinazohusu uhamishaji wa taarifa hutofautiana kulingana na nchi, mazingira ya mauzo na masharti ya kisheria yanayotumika.
Unaweza kufanya nini kulinda taarifa zako?
Somo hapa si kwamba kila mtu anapaswa kuacha kutumia akili mnemba.
Teknolojia hii inaweza kusaidia sana katika kufanya utafiti, kujifunza, kuandika, kupanga shughuli na kutatua changamoto mbalimbali za kila siku.
Lakini watumiaji wanapaswa kuelewa kwamba mfumo wa mazungumzo wa akili mnemba ni huduma inayoendeshwa na kampuni, si shajara binafsi iliyofungwa kwa ufunguo.
Haya ni baadhi ya mambo unayoweza kufanya:
1. Epuka kushirikisha taarifa nyeti kupita kiasi.
Usiweke nywila, taarifa za benki, namba za utambulisho, kumbukumbu binafsi za matibabu au siri za biashara katika mifumo ya kawaida ya mazungumzo ya akili mnemba.
2. Kagua mipangilio ya faragha.
Jua kama mazungumzo yako yanahifadhiwa, kama yanaweza kutumiwa kufundisha mifumo ya akili mnemba na kama unaweza kukataa matumizi fulani ya taarifa zako.
3. Futa akaunti ambazo huzitumii tena.
Ikiwa umeacha kutumia huduma fulani, tafuta utaratibu wa kufuta akaunti na taarifa zako. Kumbuka kwamba kuondoa programu kwenye simu hakumaanishi taarifa zilizohifadhiwa kwenye seva za kampuni zimefutika.
4. Heshimu siri za watu wengine.
Mazungumzo yako yanaweza kufichua taarifa binafsi za watu ambao hawakukubali kushirikisha taarifa zao na mfumo wa akili mnemba.
5. Hifadhi taarifa muhimu kabla ya kufunga akaunti.
Ikiwa ungependa kubaki na nakala za mazungumzo yako, angalia kama huduma husika inaruhusu kupakua taarifa zako kabla ya kuomba zifutwe.
6. Usichukulie akili mnemba kama mtaalamu mwenye leseni.
Mfumo unaweza kuzungumza kama daktari, wakili au mwanasaikolojia, lakini kuzungumza kwa ufasaha hakumaanishi una sifa za kitaaluma au uwajibikaji wa kisheria unaofanana na wa mtaalamu halisi.
Swali ambalo kila mtumiaji wa akili mnemba anapaswa kujiuliza
Tumeingia katika zama za teknolojia zinazovutia sana.
Mashine sasa zinaweza kuzungumza nasi, kutoa ushauri, kuandika taarifa, kuchambua nyaraka na hata kuiga mahusiano ya kihisia.
Lakini wakati tunajishughulisha na kugundua mambo ambayo akili mnemba inaweza kufanya, huenda tunasahau kujiuliza nini kinatokea kwa taarifa tunazozikabidhi.
Tumeanza kuwa huru kuzishirikisha mashine mambo ambayo hapo awali tuliyaficha hata kwa watu wa karibu.
Na pengine huo ndio changamoto mkubwa zaidi wa faragha katika zama hizi za akili mnemba.
Kabla hujamweleza mfumo wa akili mnemba siri yako ya ndani kabisa, jiulize: Je, nitakuwa tayari kampuni nyingine, mmiliki mpya au taasisi nisiyoijua kupata nafasi ya kuona mazungumzo haya siku zijazo?
Kwa sababu teknolojia inaweza kuendelea kuhifadhi kile ulichosema hata baada ya kampuni uliyokuwa ukiiamini kutoweka.
Na hilo ni suala la faragha ambalo hatuwezi tena kulipuuza.
End of Pia unaweza kusoma:
Imefasiriwa na Asha Juma