Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Bahari za barafu na mashimo ya ajabu: Fahamu siri ya viumbe wa angani
Iwapo maisha yapo mahali pengine katika ulimwengu, huenda yasiwe kwenye sayari zinazofanana na Dunia. Hizi ni baadhi ya sehemu za ajabu zaidi ambazo wanasayansi wanaamini zinaweza kuficha dalili za viumbe wa nje ya Dunia.
Kwa muda mrefu, juhudi za kutafuta uwepo wa viumbe vingine nje ya dunia zimejikita katika dunia zinazofanana na sayari yetu.
Wanasayansi walikuwa wakitafuta sayari zenye ardhi na maji, zilizoko umbali unaofaa kutoka kwa nyota zake kiasi cha kuwa na joto linaloruhusu maisha kama tunavyoyafahamu duniani.
Pia kulikuwa na uwezekano wa kuwepo kwa maisha kwenye baadhi ya miezi inayozunguka sayari za jirani kama Mars na Jupiter.
Lakini vipi ikiwa kuna viumbe hai katika maeneo ambayo hatukuwahi kuyatarajia?
Sasa wanasayansi wanazidi kupanua upeo wa utafiti wao na kuchunguza mazingira yasiyo ya kawaida ambayo huenda yakaruhusu maisha ya viumbe wa nje ya dunia kustawi.
Baadhi yao wanachunguza bahari kubwa zilizojificha chini ya maganda mazito ya barafu, huku wengine wakitafuta alama au mabaki yanayoweza kuwa yaliachwa na ustaarabu wa viumbe wenye uwezo wa kusafiri kati ya mifumo tofauti ya nyota.
Kadiri utafiti unavyoendelea, mbinu za kutafuta maisha nje ya dunia nazo zinakuwa za ubunifu zaidi na tofauti zaidi.
Hili linaonyesha kwamba iwapo maisha yapo mbali huko angani, huenda yakapatikana katika sehemu ambazo hapo awali zilionekana kuwa haziwezekani kabisa kuhimili uhai.
"Tunajaribu kufikiria aina mbalimbali za alama za kimaumbile ambazo tunaweza kuzitafuta," anaeleza Lisa Kaltenegger, mtaalamu wa astrobiolojia katika Chuo Kikuu cha Cornell nchini Marekani na mwandishi wa kitabu Alien Earths.
"Tunapanua wigo wa uwezekano ili tusikose ishara zozote zinazoweza kuashiria uwepo wa maisha."
Viumbe vyote vinavyojulikana duniani vina mambo fulani ya msingi yanayoyafanya yawepo. Kila kiumbe hai tunachokijua kinahitaji maji katika hali ya kimiminika pamoja na chanzo cha nishati. Mimea hutegemea mwanga wa jua, huku wanyama wakitegemea chakula.
Aidha, viumbe vyote duniani vimejengwa kwa msingi wa elementi ya kaboni. Bila kaboni, hakuna aina ya maisha, iwe rahisi au changamani, ambayo ingeweza kuwepo kwenye sayari yetu.
Lakini je, hali hiyo ni lazima iwe hivyo kila mahali katika ulimwengu?
Wanasayansi wanaamini huenda si lazima. Inawezekana maisha katika sehemu nyingine za anga yakawa yamejipanga kwa njia tofauti kabisa na tuliyoizoea duniani. Ndiyo maana watafiti sasa wanalazimika kuangalia uwezekano mpana zaidi, badala ya kutafuta tu maisha yanayofanana na yale tunayoyajua hapa duniani.
Joto kali na mazingira yenye msongamano mkubwa
Sayari ya Venus ni mfano wa sehemu ambayo huenda ikawa na uwezo wa kushangaza wa kuhifadhi viumbe.
Mwaka 2020, wanaanga walitangaza kuwa walikuwa wamegundua dalili za uwepo wa gesi ya fosfini (phosphine) katika anga ya sayari hiyo.
Ingawa gesi hiyo inaweza kuzalishwa na matukio ya kiasili kama vile milipuko ya volkano, na bado kuna mjadala wa kisayansi kuhusu ikiwa kweli iligunduliwa katika sayari ya Zuhura, fosfini pia inaweza kuzalishwa na viumbe hai.
Uvumbuzi huo uliamsha msisimko mkubwa miongoni mwa wanasayansi kwa sababu Zuhura kwa muda mrefu imechukuliwa kuwa mojawapo ya sehemu zisizofaa kabisa kwa viumbe hai.
Sayari hiyo ina joto kali sana, shinikizo kubwa la angahewa na mawingu yenye tindikali kali.
Hata hivyo, baadhi ya watafiti wanaamini kwamba kama kuna maisha huko, huenda yasiishi kwenye uso wa sayari, bali katika tabaka za juu za anga lake ambako mazingira yanaweza kuwa ya wastani zaidi.
Wazo hilo limewafanya wanasayansi kujiuliza swali muhimu: je, maisha nje ya dunia lazima yafanane na yale tunayoyajua, au yanaweza kustawi katika mazingira ambayo kwa binadamu yanaonekana kuwa magumu na yasiyowezekana kabisa?
Mazingira magumu lakini yenye uwezekano wa kuwepo uhai.
"Kwa hakika hatukutarajia kwamba sayari ya Zuhura (Venus) inaweza kuwa na mazingira yanayoweza kuhimili uhai," anaeleza Dave Clements, mwanaanga wa Chuo cha Imperial College London. Hata hivyo, wazo hilo lilikuwa limependekezwa tangu miaka ya 1960 na mwandishi na mwanasayansi maarufu Carl Sagan.
Kwa mtazamo wa kwanza, Zuhura inaonekana kuwa mahali pasipofaa kabisa kwa maisha. Joto lake linaweza kuzidi nyuzi joto 400°C, na mgandamizo wa hewa yake zito ni sawa na lile linalopatikana chini kabisa ya bahari.
Lakini kuna jambo la kushangaza. Katika urefu wa kilomita 55 hadi 65 kutoka kwenye uso wa sayari hiyo, hali ya joto na shinikizo ndiyo inayofanana zaidi na ya dunia kuliko sehemu nyingine yoyote katika mfumo wa jua nje ya sayari yetu.
Baadhi ya wanasayansi wanaamini maisha yanaweza kuwepo, huenda katika mfumo wa vijidudu vinavyoelea ndani ya matone ya mawingu na kuzalisha gesi ya fosfini.
Ili kuchunguza nadharia hiyo kwa kina, miradi kadhaa ya safari za utafiti kuelekea Zuhura inaandaliwa.
Dave Clements anashiriki katika mradi wa Uingereza unaoitwa Verve (Venus Explorer for Reduced Vapours in the Environment).
Hiki ni kifaa kidogo cha utafiti chenye ukubwa unaokaribiana na boksi la viatu. Timu yake inatumaini kifaa hicho kitajumuishwa kwenye ujumbe wa Envision, mradi wa Shirika la Anga la Ulaya (ESA) unaotarajiwa kuzinduliwa mwaka 2031.
Kitakapofika karibu na sayari hiyo Venus, kifaa hicho kitapangiwa mzunguko maalum utakaokiruhusu kusogea karibu na anga ya sayari hiyo na kuichunguza kwa undani.
Lengo kuu litakuwa kutafuta dalili za gesi ya fosfini pamoja na gesi nyingine kama amonia na haidrojeni, ambazo zinaweza kutoa vidokezo kuhusu uwepo au kutokuwepo kwa viumbe hai katika sayari hiyo.
Hata hivyo, Clements anasisitiza kuwa:
"Huu si utafiti unaotarajia kutukutanisha na viumbe wa kijani kutoka sayari nyingine."
Badala yake, anasema lengo ni kukusanya ushahidi wa kisayansi ambao unaweza kuunga mkono au kupinga nadharia kwamba kuna aina fulani ya maisha katika anga la sayari hii ya Venus.
Timu ya Verve bado inasubiri uamuzi wa mwisho kutoka ESA kuhusu kama mradi huo utajumuishwa kwenye ujumbe wa Envision.
Wakati huo huo, kuna mradi mwingine unaoitwa Morning Star, ushirikiano kati ya kampuni ya Marekani ya Rocket Lab na Taasisi ya Teknolojia ya Massachusetts (MIT).
Mradi huo unakusudia kutuma kifaa cha utafiti kwenye sayari hiyo ili kuchunguza anga kwa kutumia mbinu inayojulikana kama fluorescence, kwa lengo la kutafuta alama zinazoweza kuashiria uwepo wa maisha.
Sayari ndogo isiyoashiria kuwa na uhai
Mahali pengine katika mfumo wa jua, Ceres, sayari ndogo (dwarf planet), ni miongoni mwa maeneo yasiyotarajiwa ambayo sasa yanachunguzwa kutafuta dalili za viume hai.
Ikiwa katika ukanda wa vimondo (asteroid belt) kati ya (Mars) na (Jupiter), Ceres ni ndogo sana, ikiwa karibu mara nne ndogo kuliko dunia. Kwa mwonekano wa kwanza, ni ya kijivu, baridi na isiyoonyesha dalili zozote za uhai.
Hata hivyo, wakati chombo cha anga cha NASA cha Dawn kilipoizunguka Ceres kati ya mwaka 2015 na 2018, wanasayansi waligundua jambo la kushangaza kwenye uso wake.
Waliona madoa yanayong'aa yaliyokuwa yakionekana kama yameundwa na aina fulani ya chumvi yenye madini mengi, inayofanana na maji yenye chumvi nyingi (brine).
Ugunduzi huo uliwavutia watafiti kwa sababu maji yenye chumvi ni miongoni mwa viambato muhimu vinavyoweza kuunda mazingira yanayofaa kwa viumbe hai.
Ingawa Ceres inaonekana kuwa dunia kame na isiyo na uhai, madoa hayo ya ajabu yanaashiria kuwa huenda kuna shughuli za kijiolojia au hata mabaki ya maji yaliyokuwa au yanayoweza kuwa bado yapo chini ya uso wake.
Kwa hiyo, kile kilichoonekana awali kuwa mwamba mkubwa usio na uhai sasa kimekuwa moja ya maeneo yanayowavutia wanasayansi katika harakati za kutafuta dalili za uhai.
Wanasayansi wanaamini kuwa Ceres, sayari ndogo iliyoko kati ya Mars na Jupiter, huenda ilikuwa na mazingira yanayoweza kuhimili maisha mabilioni ya miaka iliyopita.
Mtafiti Sam Courville anasema huenda kulikuwa na bahari iliyojificha chini ya uso wake, iliyopata joto kutokana na mionzi ya elementi za asili, hali ambayo ingeweza kutoa nishati muhimu kwa maisha.
Madoa meupe yanayoonekana leo kwenye uso wa Ceres yanaweza kuwa mabaki ya bahari hiyo ya zamani.
Ili kuthibitisha nadharia hiyo, wanasayansi wanaliona kuwa muhimu kutuma chombo cha anga kuchukua sampuli kutoka kwenye uso wa Ceres na kuzileta duniani kwa uchunguzi wa kina.
Wakati huohuo, macho ya watafiti yanaelekezwa kwenye miezi ya sayari ya Jupiter, hasa mwezi na Ganymede, ambako kunaaminika kuwepo bahari zilizojificha chini ya tabaka nene la barafu.
Mwezi unaonekana kuwa moja ya sehemu zenye matumaini makubwa ya kugundua maisha kwa sababu bahari yake inaweza kuwa na virutubisho vinavyohitajika na viumbe hai.
Wanasayansi sasa wanapanua mbinu za kutafuta maisha ya viumbe wa nje ya dunia kwa kuangalia jambo ambalo hapo awali lilionekana la ajabu au lisilowezekana.
Mtafiti Vidal amebaini mfumo wa nyota unaoitwa "spider pulsar", ambao unaonekana kuelekea karibu na nyota nyingine katika kipindi cha miaka 420 ijayo.
Anaona hili kuwa jambo lisilo la kawaida kiasi kwamba linaweza kuwa ishara ya Dyson sphere, muundo mkubwa wa kiteknolojia unaodhaniwa kujengwa na ustaarabu wa hali ya juu ili kuvuna nishati ya nyota.
Wakati huo huo, miradi ya kutafuta ishara za redio kutoka kwa viumbe wa anga, kama Breakthrough Listen, bado haijapata ushahidi wa moja kwa moja wa maisha ya nje ya Dunia.
Hali hiyo imewafanya wanaanga kuanza kuchunguza mawazo mapya, yakiwemo uwezekano wa kuwepo kwa miundo mikubwa ya kiteknolojia karibu na mashimo meusi au vitu vinavyotoka katika mifumo mingine ya nyota.
Darubini mpya kama Vera C. Rubin Observatory inaweza kusaidia kugundua dalili za teknolojia hiyo kwa kuchunguza mienendo isiyo ya kawaida ya vitu hivyo.
Kwa ujumla, wanasayansi wanaamini kwamba kama maisha yapo mahali pengine katika ulimwengu, huenda yakagunduliwa kupitia ishara mbalimbali, kama gesi za kipekee kwenye sayari zisizoonekana kuwa na uhai, bahari zilizofichika chini ya barafu, au hata alama za teknolojia ya juu.