Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Makosa 10 ya kushangaza yaliyowagharimu wanaanga
Sayansi ya roketi ni ngumu.Imekuwa ikifahamika kwa ugumu wake. Vyombo vya anga vina mamilioni ya vipengele, na kila kimoja hutekeleza maelfu ya hatua na michakato. Hitilafu moja tu inaweza kuhatarisha mafanikio ya safari nzima.
Wataalamu wanaosimamia safari za anga hawawezi tu kumtuma fundi kwenda Mars au katika kina cha anga za mbali kurekebisha tatizo endapo kitu kitaenda vibaya.
Badala yake, hutumia muda mrefu kukagua, kujaribu na kuthibitisha kila sehemu ya ili kuhakikisha kila kitu kinafanya kazi kama ilivyopangwa.
Lakini hata wataalamu wa sayansi ya roketi ni binadamu kama wengine. Nao hupitia siku mbaya kazini na wakati mwingine hufanya makosa ya kustaajabisha.
Kuanzia kusahau kuwasha redio hadi matukio ya wanaanga kutoa gesi tumboni, haya ni baadhi ya mambo 10 yaliyowahi kutokea katika historia ya uchunguzi wa anga za juu.
Uchunguzi wa NASA uliharibika kwa kosa la mahesabu
Mnamo tarehe 23 Septemba 1999, chombo cha uchunguzi cha Mars Climate Orbiter (MCO) cha NASA kilifika kwenye sayari ya Mars, kikiwa tayari kufuatilia mabadiliko ya hali ya hewa.
Hata hivyo, kabla ya kuanza kazi hiyo, kilihitaji kwanza kuingia kwenye mzunguko wa sayari hiyo. Badala ya kutumia injini zake kupunguza kasi, NASA ilipanga kukipitisha kwenye tabaka la juu la anga nyembamba la Mars ili msuguano wa hewa usaidie kukipunguzia mwendo.
Dakika chache kabla ya hatua hiyo muhimu kufanyika, mawasiliano kati ya chombo hicho na kituo cha udhibiti yalikatika ghafla. Tangu wakati huo, hakikusikika tena.
Baadaye ilibainika kuwa chanzo cha tatizo hilo kilikuwa namba moja tu iliyotumika kuonyesha kiwango cha nguvu kilichokuwa kinazalishwa na injini za chombo hicho.
Programu ya kompyuta iliyotolewa na kampuni ya Marekani ya Lockheed Martin ilikuwa ikitoa thamani hiyo kwa kutumia mfumo wa vipimo wa Marekani wa pound-force seconds, badala ya mfumo wa metri uliotarajiwa na NASA.
Hilo lilipelekea mahesabu yasiyolingana na hatimaye kuisababisha safari hiyo kushindwa.
Hata hivyo, NASA hutumia mfumo wa kimataifa wa vipimo vya metri, ambapo nguvu hupimwa kwa Newton seconds. Tofauti hiyo ilisababisha thamani iliyokuwa ikitumwa kuwa na hitilafu ya takribani mara 4.45.
Mkanganyiko huo ulifanya Mars Climate Orbiter ikaribie Mars katika kimo cha chini zaidi kuliko ilivyokusudiwa. Katika eneo hilo la chini, anga la sayari hiyo huwa zito zaidi, na hivyo kuongeza msuguano uliolikumba chombo hicho.
Kutokana na hali hiyo, chombo hicho dhaifu kilishindwa kuhimili nguvu hizo na kuvunjika, na kusababisha kupotea kwa safari hiyo yote.
Kisa hicho kimebaki kuwa moja ya makosa ya gharama kubwa na ya kuaibisha zaidi katika historia ya uchunguzi wa anga za juu, kikionyesha jinsi tofauti ndogo tu katika mfumo wa vipimo inaweza kuharibu mradi wa mamilioni ya dola.
Juisi ya machungwa iliwaponza wanaanga wakapata gesi nyingi tumboni
NASA hufuatilia mara kwa mara viashiria muhimu vya afya za wanaanga wake na huwa tayari kuchukua hatua mara moja pindi dalili zozote za matatizo ya kiafya zinapoonekana.
Hivyo, pale wanaanga wa safari ya Apollo 15 walipoonyesha dalili za mapigo ya moyo yasiyo ya kawaida, madaktari walihofia kuwa mazingira ya kutokuwa na uzito yalikuwa yanavuruga uwiano wa madini muhimu mwilini, hususan elektrolaiti.
Ili kukabiliana na tatizo hilo, waliwaagiza wanaanga wa misheni iliyofuata, Apollo 16, kutumia kiasi kikubwa cha matunda ya jamii ya machungwa pamoja na juisi ya machungwa iliyoimarishwa kwa virutubisho, vyote vikiwa na kiwango kikubwa cha potasiamu.
Ingawa hatua hiyo huenda ilisaidia kulinda afya ya moyo wao, kulikuwa na tatizo moja: juisi hiyo ilikuwa na ladha mbaya sana. Zaidi ya hayo, asidi iliyomo kwenye matunda hayo ilisababisha athari zisizotarajiwa na za kuaibisha.
"Nimepata gesi tumboni tena," mwanaanga John Young alimwambia mwenzake Charles Duke walipokuwa wamepumzika ndani ya moduli ndogo na iliyofungwa kabisa ya kutua Mwezini kati ya matembezi yao ya kuukagua Mwezi.
"Nimezipata tena, Charlie. Sijui kabisa ni nini kinachonisababishia hali hii... Sijawahi kula matunda ya machungwa kwa kiasi hiki katika miaka 20 iliyopita. Na jambo moja ninalojua ni kwamba baada ya siku nyingine 12, sitaki tena kula matunda haya ya machungwa maishani mwangu," alisema kwa utani na kufadhaika.
Katika mazingira ya chombo cha anga kilichofungwa kabisa na chenye nafasi ndogo, tatizo hilo la gesi tumboni lilikuwa la kusumbua zaidi kuliko ambavyo lingeonekana hapa duniani, na limebaki kuwa moja ya visa vya kuchekesha zaidi katika historia ya safari za anga.
Gazeti la Uingereza liliizidi ujanja programu ya anga ya Umoja wa Kisovieti
Mwaka 1966, Umoja wa Kisovieti ulikuwa unaongoza kwa mbali mbio za anga za juu kati yake na Marekani. Kufikia wakati huo, tayari ulikuwa umeweka rekodi kadhaa za kihistoria, ikiwemo kurusha satelaiti ya kwanza angani, kumpeleka binadamu wa kwanza angani na kutuma picha za kwanza za upande wa mbali wa Mwezi.
Mnamo tarehe 3 Februari mwaka huo, misheni ya Luna 9 iliongeza mafanikio hayo ilipofanikiwa kutua kwa mara ya kwanza kwa usalama kwenye mwezi, katika eneo linalojulikana kama Ocean of Storms.
Mara tu baada ya kutua, chombo hicho kisicho na rubani kilianza kupiga picha za mandhari ya mbele ya mwezi ili Umoja wa Kisovieti uzitumie kuonyesha mafanikio yake. Hata hivyo, hakukuwa na mpango wowote wa kushirikisha picha hizo na vyombo vya habari vya Magharibi.
Wakati huo huo, wanaanga katika kituo cha Jodrell Bank karibu na mji wa Manchester nchini Uingereza walikuwa wakifuatilia misheni hiyo kwa kutumia darubini yao kubwa ya redio, mojawapo ya vifaa vichache duniani vilivyoweza kupokea mawimbi kutoka kwa Luna 9.
Mwandishi wa habari aliyekuwa akifuatilia tukio hilo, Terry Pattinson, aligundua kuwa Warusi walikuwa wakituma picha hizo kwa kutumia mfumo wa Radiofax, teknolojia ileile iliyokuwa ikitumiwa na magazeti wakati huo kutuma picha kwa njia ya mawimbi ya redio.
Akitambua kwamba angeweza kupata habari ya kipekee ambayo hakuna mwingine aliyokuwa nayo, Pattinson alipiga simu katika ofisi moja iliyokuwa umbali wa takribani kilomita 24. Wenzake walilazimika hata kubomoa ukuta wa chumba cha kuandalia picha ili kutoa mashine nzito iliyohitajika kwa kazi hiyo.
Hatimaye walifanikiwa kufikisha vifaa hivyo Jodrell Bank kwa wakati na kuanza kunasa picha zilizokuwa zinatumwa kutoka mwezini, kabla hata Umoja wa Kisovieti haujazitoa rasmi kwa ulimwengu. Hilo liliifanya mojawapo ya siri kubwa za programu ya anga ya Sovieti kufichuliwa na gazeti la Uingereza.
Siku iliyofuata, gazeti la Daily Express lilichapisha kwenye ukurasa wake wa mbele picha ya kwanza kabisa kuwahi kupigwa kutoka mwezini, likitangulia hata magazeti ya Umoja wa Kisovieti.
Tukio hilo lilikuwa la kuaibisha kwa programu ya anga ya Sovieti. Licha ya kuwa walikuwa wamefanikiwa kutua kwa mara ya kwanza kwa usalama kwenye Mwezi, walijikuta wakipitwa na gazeti la kigeni katika kuonyesha mafanikio hayo kwa ulimwengu.
Baada ya tukio hilo, mamlaka za Sovieti zilichukua hatua za kuimarisha usiri wa mawasiliano yao ya anga kwa kuanza (encrypt) mawimbi yao ya redio, ili kuzuia watu wengine kuyasoma au kuyachukua bila kibali.
Kisa hicho kimebaki kuwa moja ya matukio ya kushangaza zaidi katika historia ya uchunguzi wa anga, ambapo uchunguzi makini wa mwandishi wa habari na matumizi ya teknolojia iliyokuwepo wakati huo yaliwezesha gazeti la Uingereza kuipiku moja ya programu za anga zilizokuwa za siri zaidi duniani.
Gundi iliyowekwa vibaya karibu iharibu safari ya Mars
Misheni ya rover ya NASA, Opportunity, ilikaribia kuahirishwa baada ya mafundi kugundua kuwa sehemu ya tabaka la nje la roketi ilikuwa inaanza kung'oka kufuatia dhoruba ya mvua kabla ya uzinduzi.
Tatizo lilisababishwa na namna gundi ilivyowekwa kwenye vipande vya korki vinavyolinda roketi dhidi ya joto kali. Badala ya kupakwa kwa usawa ili kuzuia maji kupenya, gundi ilipakwa kwa njia iliyoyaruhusu maji kutiririka kati ya vipande hivyo na kuvifanya vitengane.
Baada ya juhudi kubwa na ushauri wa dharura kutoka kwa watengenezaji wa gundi, NASA ilifanikiwa kuvishikiza tena vipande hivyo, na kuiruhusu Opportunity kuanza safari yake kuelekea Mirihi mnamo Julai 7, 2003.
Picha za kutembea mwezini zilipigwa upya
NASA ilifahamu kuwa hatua ya kwanza ya Neil Armstrong kutua Mwezini mwaka 1969 ingekuwa tukio la kihistoria ambalo dunia nzima ingetaka kushuhudia. Hata hivyo, kamera iliyorekodi tukio hilo ilikuwa na uwezo mdogo na ilichukua picha nyeusi na nyeupe kwa kasi ya fremu 10 kwa sekunde, chini ya kiwango cha televisheni za wakati huo.
Ili kuruhusu matangazo yaonyeshwe duniani kote, wahandisi walilazimika kutumia njia rahisi lakini ya kipekee: walionyesha video hiyo kwenye skrini ndogo kisha wakairekodi tena kwa kamera iliyokuwa na kasi inayokubalika kwa matangazo ya televisheni.
Miaka kadhaa baadaye, watafiti walijaribu kutafuta kanda za awali za video hiyo ili kupata ubora wa juu zaidi, lakini kanda hizo hazikuweza kupatikana, jambo lililosababisha dunia kuendelea kutegemea nakala zilizorekodiwa upya.
Bahati mbaya ya mwanaanga wa Apollo ilivyoharibu kamera
NASA ilikuwa na matumaini makubwa kwamba safari ya Apollo 12 ingeleta picha za rangi zenye ubora wa juu kutoka Mwezini baada ya picha hafifu za Apollo 11. Hata hivyo, matumaini hayo yalizimika mapema wakati mwanaanga Alan Bean alipogeuza kamera kwa bahati mbaya kuelekea jua wakati wa kuisakinisha kwenye uso wa Mwezi.
Mwanga mkali wa jua uliharibu mara moja sehemu muhimu ya kamera iliyokuwa ikipokea picha, na kuifanya ishindwe kufanya kazi. Matokeo yake, dunia ilikosa picha za moja kwa moja za matembezi ya wanaanga hao Mwezini.
Bahati mbaya ya Bean haikuishia hapo. Wakati wa maandalizi ya kurejea duniani, aliacha kwa bahati mbaya filamu kadhaa za picha za rangi kwenye uso wa Mwezi, ambako zinakadiriwa kuwa bado zipo hadi leo.
Walifika mwezini wakasau kuwasha radio
Baada ya kusafiri pamoja kwa miaka saba kuelekea sayari ya Saturni, chombo cha Cassini na kifaa cha kutua cha Huygens vilitengana mwishoni mwa mwaka 2004. Huygens, kilichosimamiwa na Shirika la Anga la Ulaya (ESA), kilitua kwa mafanikio kwenye Titan, mwezi mkubwa wa Saturni, mnamo Januari 2005 na kukusanya mamia ya picha za uso wake wa ajabu.
Kwa kuwa Huygens haikuwa na redio yenye nguvu za kutosha kutuma taarifa moja kwa moja duniani kutoka umbali huo mkubwa, ilituma taarifa zake kwa Cassini, ambayo nayo ilizisafirisha kwenda duniani.
Baada ya miaka ya maandalizi, wanasayansi walisubiri kwa hamu kuona picha kutoka Titan.
Hata hivyo, walipokuwa wakipokea taarifa hizo waligundua kuwa karibu nusu ya picha zilikuwa zimepotea. Uchunguzi ulionyesha kuwa Huygens ilikuwa na njia mbili za mawasiliano ya redio, lakini moja ya njia hizo haikuwashwa ipasavyo na timu ya misheni. Kwa sababu picha tofauti zilikuwa zikitumwa kupitia kila njia, kosa hilo lilisababisha sehemu kubwa ya taarifa na picha za kihistoria kutoka Titan kupotea milele.
Wanaanga na tabia ya kupoteza mabegi ya vifaa
Mtu anapofanya matengenezo nyumbani, mara nyingi ana uhakika kuwa kisanduku chake cha zana hakitatoweka chenyewe.
Angani, hali ni tofauti kabisa. Mwaka 2023, wanaanga Jasmin Moghbeli na Loral O'Hara walipokuwa wakifanya matengenezo ya paneli za sola za kituo cha Kimataifa cha Anga (ISS), waligundua baadhi ya zana zao zimepotea.
Baada ya kuzitafuta, waliziona zikielea nyuma ya ISS. Ingawa wanaanga hufunga kwa kamba kila kifaa wanachotumia wakati wa matembezi ya angani ili kisipotee, wakati mwingine huweza kusahaulika, zisifungwe vizuri au kufunguka zenyewe.
Sio tukio la kwanza. Mwaka 2017, wanaanga Shane Kimbrough na Peggy Whitson walipoteza kinga ya uchafu yenye urefu wa takribani mita 1.5 wakati wakifunga sehemu mpya ya kuunganisha vyombo vya anga.
Walilazimika kuitazama ikielea polepole mbali nao, bila uwezo wa kuifikia tena.
Jaribio la kubana matumizi liliishia kugharimu Sovieti karibu safari zote nne za Mars
Katika miaka ya 1970, programu ya anga ya Umoja wa Kisovieti ilijaribu kupunguza gharama wakati wa kutengeneza misheni za Mars 4 hadi Mars 7, zilizolenga kuzunguka sayari na kutuma vyombo vya kutua kwenye uso wa sayari hiyo.
Ili kuokoa fedha, wahandisi walibadilisha viunganishi vya dhahabu kwenye baadhi ya vifaa vya kielektroniki na kutumia alumini, ambayo ilikuwa nafuu zaidi.
Hata hivyo, alumini iliharibika haraka kuliko dhahabu, na kusababisha hitilafu kuanza kujitokeza baada ya miaka michache.
Matokeo yake yalikuwa mabaya. Mars 6 iliharibika ikiwa njiani, Mars 4 ikakosa mwelekeo na kupita mbali na Mars, Mars 5 ikapata hitilafu ilipofika kwenye mzunguko wa sayari hiyo, na Mars 7 ikatoa chombo chake cha kutua lakini ikashindwa kukipeleka mahali sahihi. Jaribio la kubana matumizi liliishia kugharimu Sovieti karibu safari zote nne za Mars.
Eneo jipya la ISS liliwasababisha wanaanga kuzunguka bila kutarajia
Moduli ya Nauka, iliyojengwa na Urusi kwa ajili ya Kituo cha Kimataifa cha Anga (ISS), iliwasili kwenye kituo hicho mnamo Julai 2021 baada ya kuchelewa kwa takribani miaka 14.
Mambo yalionekana kwenda vizuri mwanzoni, lakini hitilafu ya kompyuta ilisababisha injini za Nauka kuwashwa ghafla.
Kwa kuwa wafanyakazi wa ISS hawakuweza kuzizima mara moja, kituo hicho kililazimika kutumia injini zake kupambana na nguvu hizo ili kudumisha mwelekeo wake.
Mvurugano huo uliendelea kwa takribani dakika 40 hadi mafuta ya Nauka yalipoisha.
Kufikia wakati huo, ISS ilikuwa imezunguka mara moja na nusu angani.
Jambo la kushangaza ni kwamba wanaanga waliokuwa ndani ya kituo hicho hawakuripoti kuhisi mzunguko huo mkubwa kabisa.