Unachopaswa kujua kuhusu malengelenge ya sehemu za siri

Chanzo cha picha, Julian Tse
Meliss Edwards alipokuwa na umri wa miaka ishirini, ni siku chache sana alizotoka nje ya nyumba bila miwani ya jua, si kwa sababu kulikuwa na jua kali, bali kwa sababu alihisi aibu.
"Sikutaka kabisa mtu yeyote anione," anasema mwanamke huyo mwenye umri wa miaka 29, akikumbuka jinsi alivyohisi baada ya kugundulika kuwa na maambukizi ya genital herpes (malengelenge ya sehemu za siri). "Na hivyo ndivyo hasa hali ya kuhisi aibu ilivyo."
Wataalamu wa afya wanasema kuwa kwa watu wengi, athari za kisaikolojia zinazotokana na kugundulika kuwa na ugonjwa huo zinaweza kuwa mbaya zaidi kuliko dalili za kimwili za ugonjwa wenyewe.
Kulingana na makadirio yaliyotolewa na Shirika la Afya Duniani (WHO) mwaka 2024, takriban watu milioni 846 wenye umri wa miaka 15 hadi 49 duniani kote wanaishi na maambukizi ya genital herpes, idadi inayozidi mtu mmoja kati ya watu watano katika kundi hili la umri.
Ugonjwa huu unaweza kudhibitiwa na kutibiwa, lakini hauna tiba ya kuuponyesha kabisa. Mara nyingi, maambukizi hayaleti dalili zozote au huleta dalili chache sana. Hata hivyo, kwa baadhi ya watu, husababisha vidonda na malengelenge yenye maumivu makali katika sehemu za siri, ambayo yanaweza kujirudia mara kwa mara katika maisha yao yote.
Kwa Meliss, anayetoka Wales nchini Uingereza, maumivu ya kimwili wakati ugonjwa huo ulipoanza kujitokeza kwa mara ya kwanza hayakuvumilika.
"Nilipoupata kwa mara ya kwanza, ilikuwa hali ya kutisha sana," anaiambia BBC.
Mtayarishaji huyo wa maudhui ya kidijitali anaamini kuwa aliambukizwa virusi hivyo kupitia tendo la ndoa lisilo salama na mwanaume ambaye alijua ana genital herpes lakini hakumwambia.
Anasema kuwa kugundulika kuwa na ugonjwa huo kulizua hisia mbalimbali, ikiwemo huzuni, hasira na hali ya kutokubali ukweli. Alisema alihisi kutengana na utu wake wa asili na hakuweza tena kuamini maamuzi yake mwenyewe.
Herpes ya sehemu za siri ni nini?
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Herpes ya sehemu za siri husababishwa na virusi vinavyoitwa herpes simplex. Virusi hivi vinapoingia mwilini, hubaki humo milele.
Virusi hivi havisambai kwenda sehemu nyingine za mwili wala kusababisha malengelenge katika maeneo mengine. Badala yake, hubaki vikiwa havifanyi kazi (katika hali ya kusinzia) kwenye neva moja katika eneo hilo hilo na, vinapoamshwa tena, husababisha vidonda katika eneo hilo hilo.
Kuna aina mbili za virusi vya herpes simplex: virusi vya herpes simplex aina ya 1 (HSV-1) na virusi vya herpes simplex aina ya 2 (HSV-2). Aina zote mbili zinaweza kusababisha herpes ya sehemu za siri. Inakadiriwa kuwa mwaka 2020, takriban watu milioni 520 duniani kote walikuwa wameambukizwa virusi vya herpes simplex aina ya 2.
Herpes ya sehemu za siri aina ya 2 inachukuliwa kuwa hatari zaidi kwa mtazamo wa afya ya jamii kwa sababu ina uwezekano mkubwa wa kujirudia na kuleta dalili tena. Pia, inachangia takriban asilimia 90 ya visa vyenye dalili za herpes ya sehemu za siri na inahusishwa na ongezeko la mara tatu la hatari ya kuambukizwa virusi vya UKIMWI.
Wanawake wana uwezekano mkubwa, karibu mara mbili, wa kupata herpes ya sehemu za siri aina ya 2 ikilinganishwa na wanaume, kwa sababu utando laini wa ute ndani na kuzunguka uke hurahisisha virusi hivyo kupenya.
Virusi vya herpes simplex aina ya 1 huambukizwa hasa wakati wa utotoni kupitia mate au kugusana kwa ngozi na ngozi karibu na mdomo, na husababisha herpes ya mdomoni. Vidonda vya mdomoni ndiyo dalili ya kawaida zaidi.

Chanzo cha picha, Getty Images
Marianne Nicholson, mkurugenzi wa shirika la hisani la Uingereza la *Herpes Virus Society*, anasema watu wengi hawajui kuwa vidonda vya baridi na *herpes* ya sehemu za siri husababishwa na virusi vilevile, akiongeza kuwa ngono ya mdomo ni njia ya kawaida ya maambukizi.
"Virusi havitambui eneo vilipo mwilini. Ikiwa mtu ana vidonda vya baridi na akafanya ngono ya mdomo, virusi vinaweza kuambukizwa kwenye sehemu za siri," anasema.
Dalili zinaweza kujumuisha malengelenge madogo, madoa, au vidonda katika eneo la sehemu za siri, hisia ya kuungua au kuchomachoma karibu na sehemu za siri, na maumivu au hisia ya kuungua wakati wa kukojoa.
Utambuzi wa ugonjwa huu hufanywa kwa kupima sampuli ya majimaji yaliyo ndani ya kidonda, na inawezekana tu wakati dalili zipo.
Ugonjwa huu unaweza kudhibitiwaje?
Melis anasema kuwa alipofanya utafiti mtandaoni kutafuta msaada, alikutana na vichwa vya habari vya kutisha.
"Nilisoma mambo kama, 'Maisha yako hayatakuwa sawa tena,' au 'Nani anajua kama utaweza kupata watoto?' Kauli zote hizi za kutisha nilizopaswa kukabiliana nazo," anasema.
Lakini Nicholson, ambaye ameishi na herpes kwa zaidi ya miongo mitatu, anasema ni tatizo la ngozi linaloweza kudhibitiwa kwa watu wengi.
"Kuna hofu nyingi zisizo za lazima," anasema. "Watu hufikiri ugonjwa huu ni aina fulani ya adhabu, lakini sivyo ilivyo."
Watu wengi hawapati dalili zozote. Wale wanaopata maambukizi ya mara kwa mara mara nyingi wanaweza kudhibiti hali hiyo kwa kutumia dawa za kupambana na virusi na mabadiliko ya mtindo wa maisha.
"Ni mtu mmoja tu kati ya watatu anayejua kuwa ana virusi hivi," anasema Nicholson. "Watu wawili kati ya watatu hupata maambukizi madogo kiasi kwamba hawayatambui hata kidogo."
Hata katika hatua za awali za maambukizi, matibabu ya dalili yanaweza yasiwe ya lazima kwa sababu malengelenge mara nyingi hupona yenyewe.
Hata hivyo, matibabu yanaweza kusaidia, hasa ikiwa dalili ni kali. Unaweza kuandikiwa dawa za kupambana na virusi ili kuzuia hali hiyo isizidi kuwa mbaya au kupewa mafuta ya kupaka ili kupunguza maumivu.

Chanzo cha picha, Emrah Zengin
Kurudia tena kwa ugonjwa huo mara nyingi huwa kidogo kuliko mara ya kwanza, na vipindi kati yake huongezeka baada ya muda.
Shirika la Afya Duniani linasema kutumia kondomu hupunguza hatari ya maambukizi ya herpes, na watu wenye dalili zinazoendelea wanapaswa kuepuka kuwasiliana kingono na wengine. Pia linapendekeza watu wenye dalili wapewe upimaji wa VVU.
Kulingana na Huduma ya Kitaifa ya Afya ya Uingereza, ugonjwa, msongo wa mawazo, na mzunguko wa hedhi vyote vinaweza kusababisha kuongezeka kwa herpes.
Shirika linapendekeza watu wajaribu kulinda eneo lililoathiriwa kutokana na mwanga wa urujuanimno na msuguano kutokana na ngono au kuvaa nguo za kubana, pamoja na kuepuka pombe na kuvuta sigara.
Melis anasema polepole aligundua kuwa utambuzi wake haukubainisha utambulisho wake, na sasa anatumia mitandao ya kijamii kuongeza uelewa na kuhamasisha watu.
"Nilipoanza kuugua, hakukuwa na kitu chochote kwenye mtandao isipokuwa matokeo ya kutisha ya utafutaji wa Google na machapisho ya Reddit," anasema.
"Kwa hivyo, ikiwa naweza kuwa mtu niliyetakiwa kuwa wakati huo, angalau kitu kizuri kimetokana na hali hii."















