Moja kwa moja, Siku ya mwisho ya usajili Ulaya: Enzo anakaribia kutua Man City

Dirisha la usajili wa wachezaji linafungwa saa 7 usiku wa kuamkia kesho Jumatano Septemba 2, huku vilabu vikiharakisha kukamilisha dili zao kabla ya muda wa mwisho.

Moja kwa moja

Yusuph Mazimu & Mariam Mjahid

  1. Enzo Fernández akaribia kutua Manchester City kutoka Chelsea

    D

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Manchester City inakaribia kumsajili kiungo wa Chelsea Enzo Fernández, huku mchezaji huyo akiwa ameweka wazi kuwa anataka kuhamia Etihad.

    Fernández, 25, alijiunga na Chelsea akitokea Benfica kwa £107m mwaka 2023.

    Alianza katika mchezo wa kwanza wa Chelsea msimu huu dhidi ya Fulham, lakini hakucheza dhidi ya Luton katika Kombe la Carabao na pia aliachwa nje ya kikosi kilichokutana na Brighton.

    Kutokuwepo kwake katika michezo hiyo kumeongeza dalili kwamba huenda akaondoka Stamford Bridge kabla ya dirisha la usajili kufungwa.

    City tayari imetumia fedha nyingi katika dirisha hili, ikiwa ni pamoja na £116m kumsajili Elliot Anderson kutoka Nottingham Forest na £81.4m kwa Ayyoub Bouaddi kutoka Lille.

    Fernández anaweza kuwa mchezaji mwingine mkubwa kujiunga na Man City kabla ya dirisha la usajili kufungwa.

  2. Gabriel Jesus ajiunga rasmi Barcelona kwa pauni milioni 8.6

    d

    Chanzo cha picha, Skysport

    Mshambuliaji wa Arsenal, Gabriel Jesus, amejiunga rasmi na Barcelona kwa uhamisho wa pauni milioni 8.6, leo katika siku ya mwisho ya dirisha la usajili.

    Mchezaji huyo wa Brazil amesaini mkataba utakaomuweka Barcelona hadi Juni 2029 na amesema kutimiza uhamisho huo ni kutimia kwa "ndoto" yake.

    Uhamisho wa Jesus haujafunga uwezekano wa Barcelona kumsajili mshambuliaji wa Atletico Madrid, Julián Álvarez, huku taarifa zikisema dili hizo mbili hazihusiani.

    Jesus, mwenye umri wa miaka 29, alijiunga na Arsenal akitokea Manchester City kwa pauni milioni 45 mwaka 2022.

    Amefunga mabao 32 katika mechi 123 alizoichezea Arsenal, lakini msimu uliopita alianza mechi tatu pekee za Ligi kuu ya England.

    Alikosa sehemu kubwa ya msimu uliopita baada ya kupata jeraha la goti katika mchezo wa Kombe la FA dhidi ya Manchester United Januari 2025.

    Kabla ya kujiunga na Barcelona, Jesus pia alikuwa akisakwa na Napoli.

  3. Newcastle yamsajili Fernandez-Pardo kwa pauni milioni 51

    d

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Newcastle United imekamilisha usajili wa mshambuliaji Matias Fernandez-Pardo kutoka Lille kwa ada ya awali ya pauni milioni 51.4.

    Fernandez-Pardo, mwenye umri wa miaka 21, aliwasili Tyneside Jumatatu usiku kwa ajili ya vipimo vya afya kabla ya kusaini mkataba wa muda mrefu na Newcastle.

    Mchezaji huyo wa kimataifa wa Ubelgiji amesema amefurahishwa kujiunga na klabu hiyo kubwa na kwamba mazungumzo yake na kocha Matthias Jaissle yalimsukuma kufanya uamuzi huo.

    Fernandez-Pardo alikuwa akifuatiliwa kwa muda mrefu na Newcastle, tangu kipindi ambacho Eddie Howe alikuwa kocha wa klabu hiyo.

    Uwezo wake wa kucheza nafasi mbalimbali katika safu ya ushambuliaji pia ulimfanya kuwa chaguo muhimu kwa Jaissle.

    Msimu uliopita, Fernandez-Pardo alikuwa miongoni mwa wachezaji bora wenye umri wa miaka 21 au chini katika ligi tano kubwa za Ulaya.

    Alishika nafasi ya pili kwa kutengeneza nafasi kubwa za kufunga, na nafasi ya saba kwa jumla ya mabao na pasi za mabao, akiwa na 13.

    Jaissle amemtaja Fernandez-Pardo kuwa mchezaji mwenye kiwango cha juu cha ufundi, kasi na uwezo wa kuwatoka mabeki, akisema ana uwezo wa kufunga na kutengeneza mabao.

  4. Álvarez kutua Arsenal?

    b

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Uhamisho wa mshambuliaji wa Atletico Madrid, Julián Álvarez, unaweza kuwa miongoni mwa dili kubwa zaidi za siku ya mwisho ya usajili leo, huku hatima yake ikiwa bado haijajulikana.

    Mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 26 anataka kuondoka Atletico, lakini klabu hiyo imekataa kumuuza kwenda Barcelona.

    Hata hivyo, Atletico iko tayari kufanya biashara na Arsenal, ambayo imekuwa ikimfuatilia Álvarez kwa muda mrefu.

    Arsenal imekuwa ikifuatilia kwa karibu hali hiyo huku Atletico ikitaka kumuuza mchezaji huyo kuwa euro milioni 150, sawa na takriban pauni milioni 128.

    Álvarez hakufanya mazoezi siku kadhaa na hakusafiri na kikosi cha Atletico kilichoikabili Sevilla Jumamosi.

    Kocha Diego Simeone alisema mchezaji huyo hakuwa katika hali nzuri ya kutosha kusafiri.

    Hata hivyo, Simeone amejaribu kutuliza hali hiyo, akisema atafanya kila awezalo kumfanya Álvarez ajisikie kuwa sehemu muhimu ya kikosi atakaporejea mazoezini.

  5. Vieira ajiunga Hamburg kwa uhamisho wa kudumu

    S

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Kiungo wa Arsenal, Fabio Vieira, amejiunga na klabu ya Bundesliga ya Hamburg kwa uhamisho wa kudumu.

    Mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 26 alikuwa Hamburg kwa mkopo msimu wa 2025-26, baada ya awali pia kucheza kwa mkopo katika klabu yake ya zamani, Porto.

    Vieira alicheza mechi 49 akiwa na Arsenal katika mashindano yote na kufunga mabao saba pamoja na kutoa pasi tano za mabao.

    Akiwa Hamburg, alisaidia klabu hiyo kurejea Bundesliga baada ya miaka saba na sasa ameondoka Arsenal moja kwa moja kujiunga na klabu hiyo.

    Miongoni mwa kumbukumbu zake kubwa akiwa Arsenal ni kufunga penati ya ushindi katika mikwaju ya penali dhidi ya Manchester City, iliyoiwezesha Arsenal kutwaa Ngao ya Jamii ya 2023 katika Uwanja wa Wembley.

  6. Aston Villa yamsajili Mbaye kwa pauni milioni 47

    d

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Aston Villa imekamilisha usajili wa winga wa Senegal mwenye umri wa miaka 18, Ibrahim Mbaye, kutoka Paris St-Germain kwa ada ya euro milioni 55, sawa na takriban pauni milioni 47.

    Mbaye alifunga mabao matatu na kutoa pasi mbili za mabao katika mechi 31 za mashindano yote msimu uliopita, wakati PSG ikitetea mataji yake ya Ligue 1 na Ligi ya Mabingwa Ulaya.

    Mchezaji huyo alicheza mechi zote nne za Senegal kwenye Kombe la Dunia 2026 na kufunga bao katika kichapo cha 3-1 dhidi ya Ufaransa.

    Kwa bao hilo, Mbaye alikua mchezaji mwenye umri mdogo zaidi kutoka Afrika kufunga katika Kombe la Dunia la wanaume.

    Mbaye alijiunga na PSG mwaka 2018 kutoka FC Versailles 78 na kupitia akademia ya klabu hiyo kabla ya kucheza mechi yake ya kwanza katika kikosi cha wakubwa Agosti 2024, akiwa na umri wa miaka 16.

    Alizaliwa Ufaransa na kuchezea timu za vijana za nchi hiyo, lakini mwaka 2025 aliamua kuichezea Senegal baada ya kustahili kufanya hivyo kupitia baba yake.

    Mbaye ni mshambuliaji wa hivi karibuni kujiunga na kikosi cha Unai Emery, baada ya Alejandro Garnacho, Johan Manzambi na Nicolas Jackson. Villa imepoteza Nyota wake kadhaa katika dirisha hili.

    Morgan Rogers alijiunga na Chelsea kwa pauni milioni 117, kabla ya beki Ezri Konsa kuhamia Arsenal kwa pauni milioni 55. Mshambuliaji Ollie Watkins naye alihamia klabu ya Al-Hilal ya Saudi Arabia kwa pauni milioni 51.

    Soma Zaidi;

  7. Nani anaweza kuhama leo?

    Kama ilivyo kawaida siku ya mwisho ya dirisha la usajili, bado kuna uwezekano wa kuona mabadiliko ya ghafla kabla ya muda wa mwisho, huku baadhi ya wachezaji wakisubiri hatima zao hadi dakika za mwisho.

    Kiungo wa Manchester City, Jack Grealish, anaonekana kuwa mbioni kurejea Everton kwa mkopo, huku winga wa Everton, Iliman Ndiaye, akitarajiwa kuhamia upande wa pili kwa ada ya pauni milioni 65.

    Kiungo wa Chelsea, Enzo Fernández, pia amehusishwa na uhamisho kwenda Manchester City, ambako angeungana tena na kocha wake wa zamani, Enzo Maresca.

    Wakati huo huo, Real Madrid inamtazama kiungo wa Monaco, Lamine Camara, katika jitihada za kuimarisha safu yake ya kiungo.

    Nchini Hispania, mshambuliaji wa Atletico Madrid, Julián Álvarez, anawindwa na Arsenal na Barcelona na huenda akaondoka Madrid kabla ya dirisha kufungwa.

    Liverpool pia inaweza kuhusika katika dili la dakika za mwisho. Winga wake, Cody Gakpo, amehusishwa na Tottenham na Manchester City, lakini kuondoka kwake kutategemea Liverpool kupata mbadala wake, jambo ambalo kwa sasa linaonekana kuzidi kuwa gumu.

    Kwa vilabu vya EPL, muda wa mwisho wa kukamilisha usajili ni saa 1:00 usiku kwa saa za Afrika Mashariki, hivyo saa za mwisho za dirisha zinaweza kuwa na shughuli nyingi huku vilabu vikikimbizana kukamilisha dili zao.

    Soma Zaidi;

  8. Usajili uliotikisa siku ya mwisho

    d

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Siku ya mwisho ya usajili imekuwa ikishuhudia baadhi ya uhamisho mkubwa na wa kushtukiza katika soka, huku vilabu vikisubiri hadi dakika za mwisho kukamilisha dili. Miongoni mwa zilizokumbukwa zaidi ni uhamisho wa Alexander Isak kutoka Newcastle United kwenda Liverpool katika siku ya mwisho ya dirisha la usajili la msimu wa 2025-26.

    Uhamisho huo pia uliweka rekodi mpya ya uhamisho wa mchezaji nchini Uingereza.

    Lakini Isak si wa kwanza kufanya siku ya mwisho kuwa ya kihistoria. Hizi ni baadhi ya dili zilizotikisa soka katika miaka iliyopita:

    • Claude Makélélé – Real Madrid kwenda Chelsea, 2003

    • Wayne Rooney – Everton kwenda Manchester United, 2004

    • Carlos Tévez na Javier Mascherano – Corinthians kwenda West Ham, 2006

    • Ashley Cole – Arsenal kwenda Chelsea, 2006

    • Hugo Lloris – Lyon kwenda Tottenham Hotspur, 2012

    • Mesut Özil – Real Madrid kwenda Arsenal, 2013

    • Cristiano Ronaldo – Juventus kwenda Manchester United, 2021

    • Cole Palmer – Manchester City kwenda Chelsea, 2023

    Soma Zaidi;

  9. Dirisha la usajili linafungwa leo

    D

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Dirisha la usajili wa wachezaji linafungwa usiku wa leo kuamkia Jumatano, huku vilabu vikiharakisha kukamilisha ‘dili’ zao kabla ya muda wa mwisho.

    Kwa vilabu vya Ligi kuu England, dirisha la usajili linafungwa saa 1:00 usiku kwa saa za Afrika Mashariki. Dirisha hilo limekuwa wazi tangu Juni 15.

    Ligi nyingine kubwa za Ulaya nazo zinafunga madirisha yao leo, lakini kwa nyakati tofauti.

    Ligi kuu ya Italia, Serie A dirisha litafungwa saa 21:00 usiku kwa saa za Afrika Mashariki, huku La Liga ya Hispania ikifunga saa 23:59 usiku.

    Kwa upande wa Ufaransa, Ligue 1 inafunga dirisha lake mapema 20:59, wakati Bundesliga ya Ujerumani tayari ilifunga usajili wake Agosti 31.

    Nchini Scotland na katika Women's Super League, vilabu vitakuwa na muda zaidi, huku madirisha yao yakifungwa Septemba 3. Hata baada ya muda wa mwisho kufika, baadhi ya dili zinaweza kutangazwa baadaye.

    Kwa EPL, vilabu vilivyowasilisha taarifa za uhamisho wao ‘deal sheet’ kabla ya dirisha kufungwa zinaweza kupewa hadi saa mbili za ziada kukamilisha taratibu za usajili.

    Soma Zaidi;

  10. Hujambo na karibu kwa matangazo ya moja kwa moja kuhusu fununu za uhamisho.