Moja kwa moja , Israel yaishutumu Iran kwa kutengeneza silaha za kemikali, yataka Marekani kuanzisha mashambulizi mapya
Waziri wa Ulinzi wa Israel, Israel Katz, ameishutumu Iran kwa kuendeleza mpango wa kutengeneza silaha za kemikali, lakini akasisitiza kuwa Tehran bado haijafikia uwezo wa kuzitumia kuishambulia Israel.
Rais wa zamani wa Ufaransa na mkewe washtakiwa kwa kuifadhili Libya
Chanzo cha picha, Getty Images
Maelezo ya picha, Rais wa zamani wa Ufaransa, Nicolas Sarkozy, na mkewe Carla Bruni-Sarkozy
Rais
wa zamani wa Ufaransa, Nicolas Sarkozy, na mkewe Carla Bruni-Sarkozy,
watafikishwa mahakamani mwaka ujao, ili kujibu tuhuma za kutoa ufadhili wa kifedha kinyume cha sheria kufadhili kampeni ya uchaguzi wa mwaka 2007
ya aliyekuwa kiongozi wa Libya, Muammar Gaddafi.
Sarkozy
na mkewe Bruni wamekanusha madai hayo.
Mwezi Septemba 2025, Sarkozy alihukumiwa
kifungo cha miaka mitano jela katika kesi hiyo hiyo, na kuwa rais wa kwanza wa
zamani wa Ufaransa kufungwa gerezani.
Hata
hivyo, alikaa gerezani kwa siku 20 pekee kabla ya kuachiliwa.
Uamuzi
kuhusu rufaa yake pia unatarajiwa kutolewa wiki ijayo.
Tetesi za Soka: Arteta asema Arsenal inahitaji bahati zaidi ili kumaliza mechi zake kwa ushindi
Chanzo cha picha, Getty Images
Katika wiki za hivi karibuni
Arsenal imekuwa ikishindwa kumaliza mechi kwa ushindi hata pale inapokuwa na
udhibiti wa mchezo huo.
Katika
mechi zake tisa zilizopita katika mashindano yote, ni mara moja pekee ambapo
The Gunners wamefanikiwa kushinda kwa tofauti ya zaidi ya bao moja.
Changamoto
hiyo imejitokeza tena hapo jana
baada ya Arsenal kutoka sare ya bao 1-1 dhidi ya Borussia Dortmund.
Licha ya kutawala na kudhibiti sehemu kubwa ya michezo yao,
Arsenal imekuwa na vipindi ambavyo kiwango chake cha kucheza hushuka na kuruhusu wapinzani wao kuwatawala
Katika
mechi ya ugenini dhidi ya Slavia Prague kwenye Ligi ya Mabingwa, baada ya
kufunga mabao mawili katika kipindi cha kwanza, kiwango cha Arsenal kilishuka.
Hali
kama hiyo ilijitokeza pia katika mechi dhidi ya Newcastle kwenye Ligi Kuu ya
England mwishoni mwa wiki iliyopita. Arsenal iliongoza wakati wa mapumziko,
lakini ikajikuta ikifungwa mabao 2-1 katika kipindi cha pili kabla ya kupata sare ya mabao 2-2.
Baada ya kukamilika kwa mechi ya Borussia
Dortmund ,Kocha Mikel Arteta aligusia
kushindwa kwa timu yake kutumia vyema nafasi ilizopata, ingawa alisifu kiwango
kizuri cha wachezaji wake.
Arteta
alisema, "Kuna kipengele cha bahati,
lakini pia kuna umuhimu wa sisi kumalizia vyema zaidi katika nafasi tunazopata. Tunapaswa
kuendelea kujitahidi kwa sababu naamini kile ambacho timu imeonesha leo ni
mwelekeo sahihi."
Bajeti ya kuendeleza vita dhidi ya Iran ipo - Trump
Chanzo cha picha, Getty Images
Rais
wa Marekani Donald Trump,
amesema kuwa bajeti ya kuendesha vita dhidi ya Iran inajitosheleza hadi mwisho wa Januari 2027.
Katika
mahojiano na gazeti la New York Post, Trump alisema kuwa wanachama wa Democrat katika bunge la Congress,wanaweza kugeuza ‘ushindi’ wao kuwa ‘kushindwa’ iwapo
watajaribu kusitisha vita dhidi ya Iran.
Trump aliongezea kuwa wameliharibu jeshi
la wanamaji la Iran Pamoja na mifumo yake ya ulinzi wa anga.
"Tunaweza
kumaliza vita hivi wakati wowote tunapotaka,"alisema Trump.
Wiki
iliyopita, Seneti ya Marekani ilipinga mswada uliolenga kuweka mipaka kwa
mamlaka ya Trump ya kuendeleza vita dhidi ya Iran.
Mswada
huo ungehitaji Rais wa Marekani ama kusitisha vita dhidi ya Iran au kupata
idhini ya Congress ili kuendelea na operesheni za kijeshi.
Thomas Markle akabiliwa na mashtaka ya kumiliki picha za unyanyasaji wa kingono dhidi ya watoto
Chanzo cha picha, Pinellas County Sheriff's Office
Thomas
Markle, babake Meghan Markle, amefunguliwa mashtaka na baraza
kuu la mahakama mjini Los Angeles, Marekani, kwa tuhuma za kumiliki picha na
video za unyanyasaji wa kingono dhidi ya watoto.
Markle,
ambaye bado anazuiliwa katika jimbo la Florida, anadaiwa kumiliki kanda hizo zilizojumuisha angalau picha
moja ya mtoto ambaye hajafikia umri wa kubaleghe na mwingine mwenye umri wa
chini ya miaka 12, kwa mujibu wa nyaraka za mahakama zilizowasilishwa
California.
Markle
mwenye umri wa miaka 82 amekanusha kumiliki picha za unyanyasaji wa kingono
dhidi ya watoto. Anatarajiwa kufikishwa mahakamani mjini Los Angeles katika
wiki zijazo ili kujibu mashtaka hayo.
Wiki
iliyopita, mahakama ya Florida ilitangaza kuwa baba mkwe wa Prince
Harry ana uwezo wa kiakili wa kuelewa mashtaka yanayomkabili na kushiriki
katika kesi yake.
Shirika
la Upelelezi la Marekani (FBI) lilimkamata Markle tarehe 6 Novemba, katika makazi ya wazee katika jimbo la Florida.
Wakili
wa serikali ya Marekani, Bill Essayli, alisema kuwa iwapo atapatikana na hatia,
Markle anaweza kuhukumiwa kifungo cha hadi miaka 20 jela kwa kila shtaka.
Takriban wanajeshi laki tano wa Urusi wameuawa vitani Ukraine
Chanzo cha picha, Afp via Getty
Takriban wanajeshi 490,334 wa Urusi wamefariki tangu kuanza kwa vita nchini Ukraine
mwaka wa 2022, hii ni kulingana na takwimu za serikali ya Urusi
zilizochambuliwa na BBC.
Takwimu
zilizovuja kutoka shirika la takwimu la Urusi, Rosstat, zinaonesha jinsi
uvamizi wa Ukraine ulivyobadilisha kwa kiasi kikubwa mwenendo wa vifo
nchini humo, na kufichua gharama kubwa ya maisha ya binadamu katika vita
ambavyo Rais Vladimir Putin alidhani vingedumu kwa siku chache, lakini sasa
vinakaribia kutimiza miaka mitano.
BBC
Russian imepata zaidi ya rekodi milioni 11 za vifo kuanzia mwaka 2021 hadi
Septemba 2026, baada ya
udukuzi wa mtandao uliofanywa na makundi ya Belarus ya Cyber Partisans BY na
Silent Crow ya Ukraine.
Shirika
la takwimu la Urusi lilikiri kuwa lilidukuliwa, lakini likakanusha madai kwamba taarifa zozote zilivuja.
Kwa
kushirikiana na chombo huru cha habari cha Urusi, Mediazona, BBC Russian
ililinganisha takwimu za Rosstat na orodha yake ya wanajeshi waliothibitishwa
kufariki, ambayo imekuwa ikiandaliwa kwa kutumia taarifa kutoka vyanzo vya wazi
tangu kuanza kwa uvamizi huo.
Ulinganisho
huo umebaini kuwa asilimia 90 ya rekodi hizo zinaendana na taarifa za vifo vya
wanajeshi zilizokusanywa na BBC na Mediazona.
Israel yaishutumu Iran kwa kutengeneza silaha za kemikali
Chanzo cha picha, Getty Images
Maelezo ya picha, icha ya Israel Katz
Waziri wa Ulinzi wa Israel, Israel Katz, ameishutumu Iran kwa kuendeleza mpango wa
kutengeneza silaha za kemikali, lakini akasisitiza kuwa Tehran bado haijafikia
uwezo wa kuzitumia kuishambulia
Israel.
Katika
taarifa iliyochapishwa na chama cha Likud kupitia mtandao wa Telegram, Katz amesema Iran imeanza kutengeneza
silaha za kemikali lakini bado haina uwezo wa kuzitumia kuishambulia Israel.
"Hatupaswi
kuruhusu hali hii kuendelea,"alisema Katz.
Matamshi
ya Katz yanajiri siku chache baada ya kituo cha televisheni cha CNN kuripoti,
kikirejelea taarifa za kijasusi za Marekani, kwamba Iran imekuwa ikiandaa mipango ya kuwalenga
maafisa katika utawala wa Rais wa Marekani Donald Trump kwa kulipua kile
kinachojulikana kama “bomu chafu” au dirty
bomb, mjini Washington DC.
CNN
ilinukuu vyanzo ambavyo
hawakuvitaja majina,
vikisema mipango hiyo ya Iran ni ya
tahadhari, lakini haimaanishi kwamba shambulio linakaribia kutekelezwa.
Waziri huyo wa Ulinzi alidokeza uwezekano
wa Israel kuishambulia Iran akisema hawatasubiri kushambuliwa kwanza.
“Jeshi linaweza kuamrishwa kuchukua hatua mapema ili
kuzuia tishio hilo iwapo itabainika kuwa Iran inapanga kuishambulia Israel.”
Kauli
hizo zinajiri wakati Israel inakabiliwa
na changamoto za kisiasa, baada ya Waziri Mkuu wa mpito Benjamin Netanyahu na
mpinzani wake mkuu Gadi Eisenkot kushindwa kupata wingi wa viti katika uchaguzi mkuu uliofanyika
mwezi uliopita.
Rais
wa Israel Isaac Herzog alimpa Eisenkot jukumu la kujaribu kuunda serikali, huku
Netanyahu akizidisha matamshi yake kuhusu tishio la Iran na kusisitiza umuhimu
wa kuunda serikali ya umoja wa kitaifa itakayojumuisha chama chake cha Likud.
Ripoti
zingine zimeelezea kuwa Netanyahu amekuwa akimhimiza Rais wa Marekani Donald Trump, kuanzisha tena vita dhidi ya Iran.