Je, Urusi inaficha mlipuko wa ugonjwa wa tauni?

Iliyochapishwa
Muda wa kusoma: Dakika 5

Hospitali kadhaa katika eneo la Irkutsk nchini Urusi zimeripotiwa kuwekwa chini ya karantini baada ya mfanyakazi wa maabara kufariki dunia kutokana na ugonjwa unaoshukiwa kuwa tauni ya mapafu (pneumonic plague).

Mamlaka za Urusi bado hazijathibitisha rasmi kuwa kifo hicho kilisababishwa na tauni. Hata hivyo, inasadikiwa kuwa taarifa kuhusu tukio hilo zinadhibitiwa kwa karibu, jambo ambalo limezua maswali kuhusu hali halisi ilivyo.

Licha ya ukosefu wa taarifa rasmi, ripoti zinazoashiria ugonjwa huo zimeendelea kusambaa kwenye mitandao ya kijamii na vyombo huru vya habari, na kuongeza hofu ya uwezekano wa mlipuko mkubwa zaidi.

Tauni ya mapafu ni aina hatari ya tauni ambayo huathiri mfumo wa kupumua na inaweza kusambaa kutoka mtu mmoja kwenda mwingine kupitia matone ya mate kwenye hewa, endapo hatua za haraka za kudhibiti maambukizi hazitachukuliwa.

Ni nini kilitokea Irkutsk?

Mnamo tarehe 2 Oktoba 2026, chaneli za Telegram za Urusi—ikiwemo baadhi ya zile zinazohusishwa na vyombo vya usalama—ziliripoti kuwa mfanyakazi wa taasisi inayoshughulika na mapambano dhidi ya ugonjwa wa tauni katika jiji la Irkutsk, Siberia, alifariki dunia kutokana na tauni ya mapafu.

Kwa mujibu wa ripoti hizo, Daria Shipilova, mwenye umri wa miaka 28, alihamishiwa katika hospitali iliyoko jijini Shelekhov, katika eneo la Irkutsk, mnamo Septemba 29 2026 lakini akafariki dunia siku mbili baadaye.

Baada ya kifo chake, hospitali hiyo iliwekwa chini ya karantini. Takriban watu 200 waliokuwa wametangamana na Shipilova nao pia waliwekwa karantini.

Vyombo vya habari mbalimbali vimetoa maelezo yanayokinzanai kuhusu jinsi mhudumu huyo wa maabara alivyoweza kuambukizwa ugonjwa huo.

Kwa mujibu wa taarifa moja, alilazwa hospitalini akiwa na dalili za tauni ya mapafu (pneumonic plague) muda mfupi baada ya kurejea kutoka safari nchini Thailand.

Ripoti nyingine zinadai kuwa aliambukizwa baada ya kuvunja kwa bahati mbaya vijitupa vya maabara (test tubes) vyenye kimelea cha tauni alipokuwa akitekeleza majukumu yake ya kikazi.

Taarifa zingine pia zimeeleza kuwa hivi karibuni alikuwa amesafiri kikazi kwenda Buryatia, eneo la Urusi lililo karibu na mpaka wa Mongolia, ambako vyanzo vya asili vya tauni vilikuwa vimeripotiwa kugunduliwa.

Mamlaka za Urusi mpaka sasa hazijathibitisha rasmi ni maelezo yapi kati ya hayo ni sahihi. Kutokana na ukosefu wa taarifa za wazi, kumekuwa na uvumi na maswali mengi kuhusu chanzo halisi cha maambukizi hayo na hatari ya uwezekano wa kuenea kwa ugonjwa huo.

Tauni ya mapafu ni aina hatari zaidi ya ugonjwa wa tauni kwa sababu inaweza kuambukizwa kutoka mtu mmoja hadi mwingine kupitia matone ya mate yanayotoka mdomoni wakati mtu anapokukohoa au kupiga chafya, hivyo kuhitaji hatua za haraka za kudhibiti maambukizi.

Mnamo 4 Oktoba 2026, chombo huru cha habari cha Lyudi Baikal kiliripoti kuwa hospitali tatu katika mji wa Irkutsk pamoja na kliniki moja ya uzazi ziliwekwa chini ya karantini kwa muda wa wiki tatu.

Chombo hicho kilinukuu chanzo kutoka sekta ya afya kikisema kuwa madaktari walikuwa wakijadili kwa uwazi uwezekano wa maambukizi ya ugonjwa wa tauni.

"Madaktari wanazungumzia waziwazi kuhusu ugonjwa wa tauni," chanzo hicho kilinukuliwa kikisema.

Siku moja kabla ya taarifa hiyo kuchapishwa, Kiwanda cha Alumini cha Irkutsk kilichopo Shelekhov kilitangaza kuwa wafanyakazi wake walitakiwa kuvaa barakoa kama hatua ya tahadhari.

Hatua hizo zimeibua maswali kuhusu hali halisi ya tukio hilo, huku mamlaka za Urusi zikiendelea kusalia kimya kuhusu madai ya kuzuka kwa maambukizi ya tauni katika eneo hilo.

Mamlaka zimetoa taarifa za wazi kwa kiwango gani?

Mamlaka za Urusi bado hazijathibitisha rasmi taarifa za kuwepo kwa kisa cha tauni katika mkoa wa Irkutsk.

Shirika la ulinzi wa afya na haki za watumiaji la Urusi, Rospotrebnadzor, limesema kuwa Shipilova alikuwa akiugua "nimonia ya chanzo kisichojulikana". Shirika hilo pia lilisisitiza kuwa hali ya afya ya umma katika mkoa wa Irkutsk pamoja na miji ya Irkutsk na Shelekhov ni "thabiti".

Akizungumza kwa mara ya kwanza kuhusu suala hilo tarehe 5 Oktoba 2026, msemaji wa Kremlin, Dmitry Peskov, aliwataka wananchi kutopuuzia taarifa rasmi kwa kusikiliza "uvumi mbalimbali".

Hata hivyo, baadhi ya viongozi wa eneo hilo walitaja ugonjwa wa tauni katika taarifa zao kabla ya kuyabadilisha au kuyaondoa maelezo hayo baadaye.

Mkuu wa mkoa wa Buryatia, Alexey Tsidenov, aliandika kwenye programu ya mawasiliano ya Max jioni ya tarehe 2 Oktoba kwamba Shipilova alikuwa amefariki kutokana na tauni. Baadaye alibadilisha kauli hiyo na kusema kuwa "huenda alifariki kutokana na tauni". Chombo cha habari cha Lyudi Baikal kiliripoti mabadiliko hayo.

Katika tukio lingine, mamlaka za mji wa Baikalsk ziliwashauri wakazi kuepuka safari za kwenda Shelekhov kutokana na "taarifa zisizo rasmi kuhusu kisa cha tauni katika mji huo". Taarifa hiyo iliondolewa baadaye.

Mnamo 2 Oktoba 2026, gavana wa Irkutsk, Igor Kobzev, alitangaza kupitia Telegram kwamba kikao cha dharura kilifanyika na mkuu wa afya wa Urusi, Anna Popova, kufuatia kisa kinachoshukiwa cha "maambukizi hatari sana". Tangu wakati huo hajatoa taarifa mpya kuhusu suala hilo.

Vyombo vya habari vya serikali vinasemaje?

Pia kuna dalili za juhudi za kupunguza uzito wa tukio hilo katika vyombo vya habari vya serikali.

Kwa mujibu wa Lyudi Baikal, kituo cha televisheni cha REN TV, kinachodhibitiwa na serikali, kilifuta machapisho matano ya Telegram yaliyohusu taarifa za kuenea kwa tauni.

Moja ya machapisho hayo yaliyofutwa lilidai kuwa baadhi ya watu waliowekwa karantini baada ya kukutana na mwanamke huyo walikuwa wameanza kuonyesha dalili za ugonjwa huo.

Tarehe 2 Oktoba 2026, shirika la habari la serikali la TASS lilichapisha maoni ya aliyekuwa mkuu wa Rospotrebnadzor, Gennady Onishchenko, aliyesema:

"Haiwezekani sana kuwa ni tauni."

Tangu habari hizo zianze kujitokeza hadharani tarehe 2 Oktoba, vituo vikuu vya televisheni vya serikali nchini Urusi havijataja tena neno "tauni" katika taarifa zao za habari.

Wakati huo huo, takwimu za huduma ya uchambuzi wa Telegram, TJStat, zinaonyesha kuwa neno "tauni" lilitajwa mara 4,437 kwenye vituo vya habari vya Telegram tarehe 2 Oktoba, idadi iliyopanda hadi mara 5,993 kufikia tarehe 5 Oktoba.

Je, wananchi wameamini maelezo?

Taarifa zinazokinzana kutoka kwa mamlaka na vyombo vya habari zimezua hofu na sintofahamu miongoni mwa wananchi.

Mnamo 3 Oktoba 2026, Lyudi Baikal iliripoti kuwa wakazi wa Irkutsk na Shelekhov walikimbilia maduka ya dawa kutafuta antibiotiki zinazotumika kutibu tauni.

Chapisho la gavana Kobzev kuhusu "maambukizi hatari sana" lilipokea maoni 180 kutoka kwa watumiaji wa Telegram, idadi kubwa ikilinganishwa na machapisho yake mengine ambayo kwa kawaida hupokea maoni machache.

Watumiaji wengi walitaka mamlaka kutaja wazi aina ya ugonjwa unaoshukiwa, huku wengine wakiweka mmitandaoni taarifa kuhusu dalili za tauni na kuikosoa serikali kwa "kutosema ukweli".

Baadhi ya wachambuzi pia walitilia shaka kutolewa kwa maelezo rasmi.

Mchambuzi wa siasa Georgi Bouvet aliandika kwa kejeli:

"Sio tauni, mamlaka zinawahakikishia wananchi. Mhudumu wa maabara ya tauni amefariki tu kutokana na sababu isiyojulikana, aina fulani ya maambukizi ya mapafu. Mambo kama hayo hutokea."

Naye mwandishi wa habari Dmitry Kolesov aliandika kwenye Telegram:

"Lakini ni nani atakayeamini hilo kirahisi? Ikiwa mamlaka zinaweza kusema hatuko vitani bali tunaendesha 'operesheni maalum ya kijeshi', kwa nini pia zisiseme kwamba hatuna tauni bali tunashughulikia tu 'nimonia ambayo chanzo chake hakijachojulikana'?"

Kuna uwezekano wa mlipuko mkubwa?

Uwezekano wa ugonjwa huo kuenea kwa kiwango kikubwa unategemea mambo mawili: Ikiwa ni kweli mhudumu wa maabara Shipilova aliyefariki alikuwa kweli na tauni ya mapafu, na iwapo aliwaambukiza watu wengine.

Mtaalamu wa magonjwa ya mlipuko Mikhail Favorov aliiambia televisheni ya Dozhd tarehe 4 Oktoba 2026 kwamba kulikuwa na "hatari kubwa ya maambukizi" ndani ya hospitali ambako Shipilova alitibiwa, lakini hatari kwa watu waliowahi kukutana naye kabla ya kulazwa ilikuwa ndogo zaidi.

Hata hivyo, alisisitiza kuwa uwezekano wa mlipuko mkubwa katika kiwango cha mji mzima ulikuwa mdogo sana.

"Nafasi ya kutokea kwa mlipuko mkubwa ni ndogo sana kwa sababu watu wote waliokutana naye wanapaswa kuwa tayari wamewekwa karantini," alisema.

Favorov aliongeza kuwa, licha ya ukosefu wa taarifa za kina kwa umma, mamlaka zinaelewa uzito wa hali hiyo na zina miongozo maalumu ya jinsi ya kukabiliana na matukio ya aina hiyo.

Imetafsiriwa na Ambia Hirsi