Je, Tanzania imeilenga Kenya kuzuia wafanyabiashara wadogo?

    • Author, Alfred Lastek
    • Akiripoti kutoka, BBC Dar es Salaam
  • Iliyochapishwa
  • Muda wa kusoma: Dakika 7

Katika kile kinachoonekana kama mwendelezo wa sera za kulinda uchumi wa ndani, Serikali ya Tanzania imetangaza rasmi marufuku dhidi ya shughuli 15 za kibiashara kwa raia wa kigeni.

Amri hii imezua hisia kali ndani na nje ya mipaka ya taifa hilo hasa kwenye mitandao ya kijamii, huku maswali mengi yakiibuka kuhusu malengo yake halisi. Ingawa waraka wa serikali haukutaja nchi yoyote, mjadala mkubwa umezuka nchini Kenya, ambako hisia za "kulengwa" na hatua hiyo zimeibuka.

Kwa upande wa Tanzania, serikali inasema hatua hiyo imelenga kulinda fursa za ajira, kipato na uwekezaji kwa wananchi wake hasa wale wanaojihusisha na biashara ndogondogo.

Agizo hilo, linakataza wageni kushiriki katika sekta 15 zikiwemo uhamishaji wa pesa kwa njia ya simu, uongozaji wa watalii, uchimbaji mdogo wa madini, ununuzi wa mazao shambani, saluni za urembo, maduka ya bidhaa za kiutamaduni, pamoja na kuanzisha redio na televisheni.

Waziri wa Viwanda na Biashara nchini Tanzania, Dkt Selemani Jafo alieleza kuwa wageni wamekuwa wakijihusisha kwa kasi na sekta isiyo rasmi na maeneo ambayo yanafaa zaidi kuachiwa Watanzania.

Kwa upande mwingine, baadhi ya wanasiasa na wadau wa biashara wa Kenya wanasema kuwa wameguswa moja kwa moja, wakiona kama huo ni mwendelezo wa kile wanachokiita "mtazamo wa kisiasa usio rafiki" kutoka kwa jirani yao wa kusini.

Kwa mujibu wa Benki ya Dunia, Tanzania na Kenya ni nchi zenye uchumi mkubwa zaidi katika Jumuiya ya Afrika Mashariki na ndio nchi zenye idadi kubwa ya watu na pia zenye kutengeneza fursa nyingi zaidi kwa watu wake hivyo sera za mataifa hayo zinalenga kulinda biashara na kutoa fursa zaidi kwa wazawa haswa kwenye biashara ndogo ndogo.

Ushindani wa kibiashara umekuwa ukitajwa kila mara, lakini sera na vikwazo vya kibiashara wanavyoendelea kuvitatua vinalenga kulinda maslahi ya mataifa yote.

Kwanini Serikali ya Tanzania imekuja na uamuzi huu?

Kwa muda mrefu, wafanyabiashara wa kitanzania wamekuwa wakitoa malalamiko kuhusu kuongezeka kwa raia wa kigeni, hususani kutoka China, Kenya na India, wanaoingia kwenye biashara ndogondogo ambazo awali zilikuwa zikifanywa na Watanzania wenyewe.

Katika masoko kama Kariakoo, Mbagala na Karume yaliyopo jijini Dar es Salaam kumekuwa na ongezeko kubwa la maduka yanayoendeshwa na wageni, hasa Wachina, wanaouza bidhaa moja kwa moja kwa wateja kwa bei ya chini. Hali hiyo imewasukuma wazawa wengi kufunga biashara au kufanya kazi kwa hasara.

Mwaka jana, wafanyabiashara wa Kariakoo waligoma wakishinikiza serikali kushughulikia changamoto mbili kuu, moja ikiwa ni kodi kubwa wanazotozwa na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), na ya pili ikiwa ni ongezeko la wafanyabiashara wa kigeni waliovamia sekta ya rejareja na biashara za mtaani.

Malalamiko haya yamekuwa yakijirudia katika maeneo mengi nchini, ambapo wageni wanadaiwa kuanzisha biashara bila kufuata taratibu, kuendesha shughuli zao kama familia bila kutoa ajira kwa wazawa, na kuuza kwa bei kandamizi ambayo inaleta ushindani usio wa haki.

Katika kukabiliana na hali hiyo, serikali iliunda kamati ya watu 15 kuchunguza mazingira ya wafanyabiashara wa kigeni na hasa athari zao kwa wafanyabiashara wa ndani katika maeneo ya jiji la Dar es Salaam. Ripoti ya kamati hiyo, na vikao mbalimbali kati ya wafanyabiashara na Serikali, kwa mujibu wa vyanzo vya ndani, ndiyo msingi wa uamuzi huu wa sasa.

Biashara zilizopigwa marufuku kwa raia wa kigeni

Amri mpya inayojulikana kama Amri ya Leseni za Biashara (Marufuku ya Shughuli za Biashara kwa Wasio Raia), 2025, inabainisha wazi aina za biashara ambazo kuanzia sasa hazitafanywa tena na raia wa kigeni.

Kati ya shughuli hizo ni uuzaji wa bidhaa kwa rejareja, huduma za saluni, uhamishaji wa fedha kwa njia ya simu, na uanzishaji au uendeshaji wa vituo vya redio na televisheni.

Aidha, huduma za uongozaji watalii, uendeshaji wa mashine za kamari nje ya kasino rasmi, na kumiliki viwanda vidogo pia zimewekwa kwenye orodha hiyo.

Shughuli nyingine zilizozuiwa ni biashara ya uwakala wa fedha, udalali katika sekta ya ardhi na biashara, matengenezo ya simu na vifaa vya kielektroniki, huduma za usafi wa majumbani na maofisini, huduma za forodha na usafirishaji, pamoja na uchimbaji mdogo wa madini. Pia, wageni hawataruhusiwa kununua mazao moja kwa moja kutoka shambani.

Kwa mujibu wa amri hiyo, mamlaka zote za utoaji wa leseni nchini zimetakiwa kusitisha mara moja utoaji au upyaishaji wa leseni kwa wageni katika maeneo hayo. Wale ambao tayari walikuwa na leseni halali, wameruhusiwa kuendelea hadi leseni zao zitakapomalizika muda wake.

Adhabu kwa watakaokiuka ni kali: faini ya hadi shilingi milioni 10, kufutiwa visa na vibali vya ukaazi, au kifungo cha hadi miezi sita. Kwa Watanzania watakaobainika kuwasaidia wageni kuendesha biashara hizi kwa mgongo wa mbele, adhabu ni faini ya hadi milioni tano au kifungo cha miezi mitatu.

Kwa upande wa wafanyabiashara wa watanzania, wamefarijika kwa hatua hii. Mfaume Fadhili Mfaume, Makamu Mwenyekiti Jumuiya ya Wafanyabiashara Kariakoo anasema, "Sisi tumepokea vizuri, tunaishukuru serikali na kuipongeza, kabla ya hapo kulikuwa na vikao vingi na serikali na baadaye serikali iligundua kwamba zipo biashara zinazofaa kufanywa na wazawa, zimeingiliwa na wageni kwa kiwango kikubwa."

Nini mtazamo wafanyabiashara na wanasiasa wa Kenya ?

Tangazo hili limepokelewa kwa hisia tofauti nchini Kenya, ambapo maelfu ya raia wake wamewekeza au wanafanya kazi katika sekta zilizolengwa na amri hiyo. Wapo wanaounga mkono na wapo wanaoona kama ni hatua isiyostahili. Viongozi wa kisiasa na wadau wa biashara nchini humo wamelalamikia uamuzi huo wakisema ni wa kulenga moja kwa moja maslahi ya Wakenya walioko Tanzania.

Mmoja wa waliotoa kauli ya moja kwa moja kupitia runinga ya TV47 ya nchini humo ni Seneta Joe Nyutu, ambaye alisema, "Marufuku hii, ingawa inawagusa wageni wote, inaelekezwa kwa Wakenya. Lakini hatupaswi kulipiza kisasi kwa sababu makosa mawili hayaleti haki." Kauli yake inaonesha hisia ya maumivu lakini pia wito wa kuhimiza uvumilivu na kutafuta njia ya mazungumzo ya kidiplomasia.

Kwa upande mwingine, Seneta wa zamani, Ngunjiri Wambugu alichukua msimamo wa kuelewa hatua ya Tanzania, akisema, "Kwa mtazamo wa Kenya, tunahisi Tanzania wamekuwa haitendi haki. Lakini ukiwa Mtanzania, unashindana kwenye biashara ndogo na wageni nafikiri wanajaribu kulinda watu wao."

Katika tasnia ya utalii, Victor Shitakha, Mwenyekiti wa Kenya Coast Tourism Association, alielezea masikitiko yake kwa uamuzi huo kwa kusema, "Ingawa naelewa lengo ni kulinda wananchi wake, lakini nimesikitika nchi kuchukua uamuzi wa aina hii. Nasikitika kwa uamuzi huu ambao unasababisha nchi zetu kutengana."

Msimamo mwingine umetolewa na Sam Ikwaye, Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya wahudumu wa hotel na wapishi Kenya, ambaye alionya kuwa kujilinda ni haki, lakini lazima pawe na mipaka. Alisema, "Ni jukumu la kila nchi kulinda wananchi wake na ajira zao, lakini lazima wazingatie kuwa hakuna nchi inayoweza kusimama peke yake. Ushirikiano wa kikanda ni nguzo muhimu kwa ustawi wa Afrika Mashariki."

Kuhusu la kulengwa wafanyabiashara fulani, Mfaume Mfaume anasema,"Hakuna wanaolengwa zaidi, isipokuwa wote wanaofanya biashara, kwa kulinda maslahi ya pande zote, sio biashara zote zimekatazwa ni biashara 15 pekee, zipo biashara ambazo wageni wanaendelea kufanya…

"…ikiwa biashara anafanya mfanyabiashara fulani haikingiliwi na mgeni maana yake mtaji (wa mtanzania) utakuwa, ataajiri na serikali itapata kodi," anasema kiongozi huyo wa Chama cha Wafanyabiashara wa Kariakoo.

Serikali ya Kenya imesikitishwa na hatua ya Tanzania

Wizara ya Uwekezaji, biashara na viwanda nchini Kenya inasema kwamba kuna idadi kubwa ya Wakenya ambao wanaishi na kufanya kazi na biashara katika mataifa jirani kwenye ukanda wa Afrika ya Mashariki na kwamba kuna haja ya vijana hao kupewa fursa ya kufanya kazi hizo popote ambapo kazi hizo zinajitokeza kwenye ukanda huu.

Waziri wa Biashara, Lee Kinyajui amezungumza haya katika kikao cha wanahabari huku akitaja pia kwamba kama taifa Kenya imesikitiishwa na hatua ya Tanzania kuwazuia raia wa mataifa ya kigeni kutofanya biashara kadhaa ndani ya taifa hilo.

"Kenya ina tambua na kuheshimu uhuru wa utaifa wa mataifa wanachama wa jumuiya ya Afrika Mashariki kuweka sheria zinazodhibiti biashara katika mataifa hayo. Lakini Kenya inaamini pia kwamba kuna umuhimu wa kufanya majadiliano, kushirikiana kwa karibu mara kwa mara katika kutekeleza sera hizo ambazo zinaathrii biashara kati ya mataifa majirani," alisema Waziri Kinyanjui.

Aidha Kenya inahisi kwamba hatua hii ya Tanzania kuwazuia raia wa kigeni kutomiliki au kunedesha aina 15 za biashara ndani ya nchi hiyo kuwa jambo linalo kudhohofisha lengo kuu la uwiano na utangamano wa kanuni za kibiashara za pamoja za Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC common market protocol).

Waziri Kinyanjui sasa anasema kwamba Kenya na Tanzania zinatarajiwa kufanya vikao vya kuangazia suala la kuingiza na kusafirisha nje bidhaa kama vile Tumbaku katika mkutano utakao andaliwa jijini Arusha kati ya Agosti 11 na 12 mwaka 2025.

"Kwa msingi wa Jumuiya moja, watu moja, tumejitolea kuhakikisha kwamba kanuni za kutotenganisha, uwazi na usawa ndizo zinazoongoza maamuzi ya siku za usoni kuhusus biashara," alisema waziri huyo.

Aidha mwezi Mei mwaka huu, Waziri wa Mambo ya Nje wa Kenya, Musalia Mudavadi, alisema kuwa takribani Wakenya 250,000 wanaishi, kufanya kazi au kuendesha biashara nchini Tanzania, jambo alilolisisitiza kuwa linalenga kuendeleza uhusiano mwema.

Ni vipi Tanzania inalinda wafanyabiashara wake ?

Kufuatia suala hilo na kuendelea kutekeleza wajibu wake, Julai 2024 Serikali ilizindua Sera ya Taifa ya Biashara ya mwaka 2023 inayolenga kuondoa vikwazo vilivyokuwapo awali na kuboresha mazingira, ili kuchochea ufanyaji biashara ndani na nje ya nchi.

Sera hiyo ililenga kuongeza mchango wa sekta ya biashara katika pato la Taifa, kuchochea ajira na uwezo wa bidhaa za Tanzania kuyafikia masoko yaliyopo ya Bara la Afrika.

Hata hivyo, Serikali imeeleza kuwa inaendelea kutatua changamoto mbalimbali kwa kuhakikisha hatua mbalimbali zinachukuliwazinalinda biashara ndogo kwa ajili ya kuchochea ukuaji wa biashara hizo.

Julai 5, mwaka jana akiwa katika kongamano la wajasiriamali wadogo, wa chini na wa kati (MSMEs), Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara wa Tanzania, Exhaud Kigahe alisema licha ya biashara ndogo na kati nchini kutoa ajira nyingi na kuchangia katika pato la Taifa lakini bado wanakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo masoko na kukosa mikopo.

Kigahe alisema katika asilimia 95 ya biashara nchini, sekta ya biashara ndogo na za kati ni ya pili baada ya sekta ya kilima katika kutoa ajira. Pia amesema sekta hiyo inachangia asilimia 40 ya ajira zote nchini na asilimia 35 ya pato la taifa.

Pamoja na ufanisi huo lakini bado sekta hiyo inayokabiliwa na changamoto nyingi ikiwemo ukosefu wa dhamana kwa ajili ya kupata mikopo, miundombinu duni ya shughuli na matumizi ya teknolojia duni za uchakataji malighafi.

"Pia watu wanakosa elimu na ujuzi juu ya usimamizi wa biashara, ukosefu soko la uhakika za bidhaa zinazozalishwa," alisema Kigahe.