'Nilivuta usukani': Abiria asimulia Jinsi alivyoinusuru ndege rubani alipochomwa kisu

Chanzo cha picha, Reuters
Abiria mmoja raia wa Israel aliyekuwa kwenye ndege ya kutoka Dubai kuelekea Tel Aviv amesimulia jinsi alivyomdhibiti rubani anayeshukiwa kumchoma kisu rubani mwenzake katika jaribio la kuiangusha ndege hiyo aina ya Boeing 737 Max 8. Abiria wengine walisimulia nyakati za hofu kubwa walizokumbana nazo baada ya kunusurika ajali hiyo.
Yaniv Hayun, aliyekuwa miongoni mwa abiria wa ndege ya Flydubai FZ1073, alikutana na Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu baada ya kuwasili Tel Aviv kwa ndege nyingine. Wakati wa mkutano huo, Hayun alikuwa bado amevaa fulana iliyokuwa na madoa ya damu.
Mamlaka husika zinaendelea na uchunguzi wa tukio hilo, huku sababu au nia ya mshukiwa ikiwa bado haijafahamika rasmi.
Wakati huohuo, shirika la ndege la Flydubai limetangaza kusitisha safari zake kuelekea Tel Aviv hadi uchunguzi wa tukio hilo utakapokamilika.
Baada ya Hayun kumdhibiti mshukiwa, ndege hiyo ilitulia na marubani wawili waliokuwemo ndani kama abiria walichukua udhibiti wake na kufanikisha kutua kwa dharura katika mji wa Tabuk, kaskazini-magharibi mwa Saudi Arabia.
"Hakukuwa na mtu yeyote kwenye chumba cha marubani"
Kwa mujibu wa Khayun, alimtaarifu Waziri Mkuu kuwa alihisi kuna hali isiyo ya kawaida baada ya ndege kuanza kushuka kwa kasi bila kutarajiwa, ikipoteza takribani mita 5,200 za urefu ndani ya muda wa chini ya dakika mbili.
"Ghafla mtu alianza kupiga mayowe, kisha taa zikazimika," Yaniv Hayun alisema katika video iliyochapishwa na Waziri Mkuu wa Israel.

Chanzo cha picha, Benjamin Netanyahu/X
"Rubani huyo aliyekuwa amejeruhiwa kwa kuchomwa kisu alikuwa ameanguka karibu na mlango wa chumba cha marubani, jambo lililofanya iwe vigumu kuufungua mlango huo," Khayun alisema.
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Hata hivyo, kwa mujibu wa Yaniv, rubani aliyejeruhiwa bado aliweza kufungua mlango wa chumba cha marubani kabla ya kupoteza fahamu.
"Nilipoingia ndani, nilimkuta mshambuliaji karibu na paneli ya uongozaji, kati ya viti vya marubani. Viti hivyo vilikuwa vitupu. Rubani mmoja alikuwa amelala sakafuni, huku mwingine akiwa ameanguka karibu na paneli ya vifaa. Mtu mwingine aliingia chumba cha marubani pamoja nami. Kisha nilimkamata mshambuliaji shingoni na kumvuta nje ya chumba hicho," alisema.
Kwa mujibu wa Yaniv, mshukiwa huyo alikuwa akijaribu kuharibu vifaa vya uongozaji wa ndege ili kuifanya ishindwe kudhibitiwa.
Yaniv alisema aliwaomba raia wengine wa Israel waliokuwa ndani ya ndege wamsaidie, na kwa pamoja walimdhibiti mshambuliaji huyo na kumwangusha chini ili asiweze kuendelea na mashambulizi.
Pia alieleza kuwa alilazimika kushika usukani wa ndege katika juhudi za kurejesha utulivu wake.
"Ulivuta usukani wa ndege?" Netanyahu alimuuliza.
"Nimekuwa nikifuatilia kipindi cha Air Accident Investigation, Mheshimiwa Waziri Mkuu," Yaniv alijibu. "Ndege ilianza kutulia, kisha mmoja wa marubani akaniambia anawezakuchukua udhibiti."
Hata hivyo, kwa mujibu wa ripoti za vyombo vya habari, Yaniv si rubani kitaaluma bali ni fundi bomba.
Netanyahu alimwelezea Hayun kuwa "shujaa" na kumuuliza alifanikiwa vipi kufanya jambo hilo.
"Sisi ni taifa la simba, sivyo?" Yaniv alijibu.
Netanyahu alisema alikuwa akimwona "shujaa wa kipekee", kabla ya kuonyesha doa la damu lililokuwa kwenye fulana ya Yaniv na kuuliza:
"Damu hiyo ni yake?"
"Ndiyo, ni yake," Yaniv alijibu.
"Ulichokifanya ni jambo la ajabu kabisa," Netanyahu alisema.
"Nimepitia tukio la kutisha sana"
"Nahisi kana kwamba nimepitia tukio la kutisha sana," alisema abiria mwingine, Zvika Meness, akisimulia yaliyotokea wakati wa mkasa huo angani.
Meness aliliambia shirika la utangazaji la umma la Israel, Kan, kwamba alishiriki katika juhudi za kumdhibiti mshambuliaji huyo. Alisema abiria wengine walisaidia kumfunga kwa kutumia vifungo vya plastiki na nyaya za vipokea-sauti ili kumzuia kuendelea na mashambulizi yake.
Kwa mujibu wa Meness, ushirikiano wa haraka wa abiria hao ulikuwa muhimu katika kumweka mshukiwa chini ya udhibiti na kuzuia hali hiyo kugeuka kuwa janga kubwa zaidi

Chanzo cha picha, Reuters
"Rubani mwingine aliyekuwa miongoni mwa abiria alichukua nafasi ya rubani msaidizi, na hatimaye wakafanikiwa kuitua ndege hiyo salama," aliongeza.
Baadaye, abiria wa ndege hiyo ya Flydubai walisafirishwa hadi Tel Aviv kwa ndege nyingike. Walipowasili katika Uwanja wa Ndege wa Ben Gurion, walipokelewa na umati wa watu waliokuwa wakipeperusha bendera za Israel, huku muziki, nyimbo na dansi vikishuhudia furaha ya kunusurika kwao.
"Namshukuru Mungu kwamba bado niko hai," alisema mmoja wa abiria, Haim Lazarovich, alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari. "Sehemu ya kutisha zaidi ya safari hiyo ilikuwa pale rubani alipopoteza udhibiti wa ndege."
Abiria mwingine, Oran Cohen, mwenye umri wa miaka 18, alielezea tukio hilo kuwa moja ya nyakati ngumu zaidi maishani mwake.
"Huenda yote yalidumu kwa dakika tano tu, lakini kwangu yalionekana kama mateso yasiyoisha. Nilimsikia kaka yangu, aliyekuwa ameketi nyuma yangu, akipiga kelele kwamba sote tutakufa," alisema.
Mfanyakazi mmoja wa huduma za dharura nchini Israel baadaye aliiambia BBC kuwa baadhi ya abiria walishindwa kuyazuia hisia zao waliposhuka kutoka kwenye ndege.
"Wengi walikuwa wamelemewa na hisia, huku wengine wakilia walipokuwa wakiondoka ndani ya ndege," alisema.
Wakati huohuo, kamanda wa ndege hiyo, Smith Macchhar, raia wa India aliyedungwa kisu katika tukio hilo, anaendelea kupata nafuu hospitalini, kwa mujibu wa Ubalozi wa India nchini Saudi Arabia.
Mshukiwa wa shambulio hilo amekamatwa na kwa sasa anahojiwa na mamlaka za Saudi Arabia huku uchunguzi wa tukio hilo ukiendelea.
Imetafsiriwa na Ambia Hirsi































