Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Jinsi ya kuepuka tabia zilizojificha zinazoongeza hofu na sonona?
Katika kipindi cha ujana wake, Marie alianza kuhisi hofu na wasiwasi alipokuwa katika mazingira ya kuchangamana na watu kijamii. Hali hiyo ilizidi kuwa mbaya hadi akapatwa na msongo wa Mawazo mkali na kuamua kusitisha masomo kwa muda.
Alipoanza chuo kikuu, alianza kuepuka kabisa sherehe na mikusanyiko ya kijamii.
"Nilishindwa kujiunga na mitandao ya kijamii kama watu wengine," anasema Marie, ambaye si jina lake halisi. "Nilifikiri hakuna mtu aliyekuwa na hamu ya kunifahamu. Sikuwa na rafiki hata mmoja katika chuo kizima."
Wasiwasi wa Marie kuhusu kushirikiana na watu ulikuwa mkubwa kiasi kwamba aligundulika kuwa na tatizo la wasiwasi wa kuchangamana na watu kijamii, hali ambayo huathiri hadi asilimia 12 ya watu wakati fulani katika maisha yao.
Hata hivyo, watu wengi zaidi wanasema wanakabiliwa na wasiwasi huo. Wanafunzi wanaporejea vyuoni, tuliwauliza wataalamu jinsi ya kukabiliana na hisia hizi, iwe ni kwa wanaoanza mwaka wa kwanza au walio katika mwaka wao wa mwisho.
Utafiti uliofanywa na Chuo Kikuu cha Chichester umeonyesha kuwa zaidi ya mwanafunzi mmoja kati ya watano wa vyuo vikuu hupata aina fulani ya wasiwasi wa kijamii wakati wa masomo yao. Hali hiyo imehusishwa na matokeo duni ya kitaaluma, mahusiano yasiyoridhisha na upweke.
Kwa watu wengi, chuo kikuu huwa ni mara ya kwanza kuondoka nyumbani na kuishi peke yao. Pia huwa kipindi ambacho wengi hutamani kupata marafiki haraka.
Marie, aliyesoma katika Chuo Kikuu cha Exeter, anasema alijitahidi sana.
"Nilipofika mara ya kwanza, nilijiunga na kikundi fulani, lakini kila mtu alikuwa akizungumza na mwenzake, na ghafla nikaingiwa na hofu. Nilihisi kwamba nisingeweza kuendana nao, hivyo nikarudi nyumbani," anasema.
Dalili zinazoonyesha kuwa una wasiwasi wa kuchangamana na watu katika jamii
Marie anaelezea wasiwasi wake wa kijamii kama hali ya kujihisi kana kwamba yuko nje ya mwili wake.
Alipozungumza na watu wapya, alihisi uso wake ukipata joto na mikono yake ikihisi kana kwamba imejaa mchwa.
"Karibu nilihisi kama ninajitenga na mwili wangu," anasema Marie, ambaye sasa ana umri wa miaka 25. "Nilisahau jinsi ya kutengeneza maneno, nilisahau nilichotaka kusema."
"Baada ya kukutana na watu, nilihisi kana kwamba nilikuwa nimefanya jambo baya sana. Nilihisi aibu kubwa. Na kila mara nilifikiri kwamba kuna tatizo kubwa ndani yangu."
Neil Greening, mkurugenzi wa British Social Anxiety Foundation, anasema hiyo ni hali inayowakabili watu wengi wenye tatizo la wasiwasi wa kuchangamana na watu kwenye jamii.
"Watu hufikiri kwamba kuna tatizo katika haiba yao. Kwa hiyo, badala ya kuona tatizo hilo kama jambo linaloweza kutambuliwa na kutafutiwa msaada, hulificha ndani yao," anasema.
Jambo kuu la kuzingatia ni hili:
Ni kawaida kuhisi aibu au wasiwasi kidogo unapokutana na watu wapya, unapokuwa katika mazingira mapya au unapoenda kwenye usaili wa kazi. Lakini wasiwasi wa kijamii huwa tatizo pale unapomzuia mtu kushiriki kikamilifu katika shughuli za maisha yake.
Kwa watu ambao wamegundulika kitaalamu kuwa na tatizo hilo, madhara yanaweza kuwa makubwa, kama ilivyokuwa kwa Marie.
"Katika dunia ambayo uwazi katika kushirikiana na watu na kujiamini vinathaminiwa, inaweza kuwa vigumu kukubali kuwa una aina yoyote ya wasiwasi wa kijamii," anasema.
"Watu wengi hujaribu kuficha wasiwasi wao wa kijamii au kutumia tabia za kujilinda."
Dalili za mtu mwenye tatizo la wasiwasi wa kijamii ni pamoja na:
- Kukaa kimya
- Kutoa majibu mafupi
- Kujishughulisha na simu ili kuepuka mawasiliano na wengine
- Kukaa kila mara na mtu au kundi fulani
- Kuzingatia mada salama katika mazungumzo, kama vile kazi
Greening anasema kuna baadhi ya ushahidi unaoonyesha kuwa wasiwasi wa kijamii unaongezeka, huku matumizi yanayoongezeka ya simu janja na kufanya kazi kwa njia ya mbali yakichangia kupungua kwa mwingiliano wa kijamii na kuongezeka kwa wasiwasi.
Unawezaje kujikwamua?
Marie, ambaye sasa anasomea shahada ya uzamivu, ameanza kudhibiti vizuri wasiwasi wake wa kijamii.
Baada ya kumaliza shahada yake ya kwanza, alipata msaada kutoka Huduma ya Taifa ya Afya ya Uingereza (NHS), kupitia tiba ya mazungumzo inayojulikana kama tiba ya utambuzi na tabia (CBT).
Tiba hiyo inachukuliwa kuwa mojawapo ya njia zinazotumika zaidi kutibu wasiwasi wa kijamii kwa sababu humsaidia mtu kubadili namna anavyofikiri na pia kubadili tabia zake.
Profesa David Clarke, mwanasaikolojia katika Chuo Kikuu cha Oxford, anasema angependa watu wengi zaidi kujitokeza na kutafuta matibabu. Hata hivyo, anasisitiza kuwa watu wanaweza pia kuchukua hatua za kujisaidia.
Hatua ya kwanza, anasema, ni kuacha kujichunguza kupita kiasi.
"Watu wenye wasiwasi wa kijamii huendelea kujichunguza wanapokuwa katika mazingira ya kijamii. Je, uso wangu umekuwa mwekundu? Je, ninaonekana mjinga? Je, ninaonekana mwenye wasiwasi?"
Anashauri: "Elekeza umakini wako nje yako, fikiria kinachoendelea, mtu mwingine au mambo yanayotokea yanayokuzunguka."
Pia anasema mtu anapaswa kujaribu kupima hofu zake kupitia majaribio ya kitabia. Kwa mfano, kuuliza swali katika mkutano au kuzungumza katika kundi, kisha kuangalia kile kinachotokea.
"Watu wenye wasiwasi wa kijamii huwa wanatarajia matokeo mabaya, kama vile kudhani kwamba watafedheheshwa, wengine watawadharau au wataonekana kuwa watu wa kuchosha," anasema.
"Kujaribu mawazo hayo na kuona kama kweli yanatokea kunaweza kuwasaidia kuvunja tabia hizo. Inaweza kutisha, lakini inaweza kuwa na manufaa makubwa."
Pia anasema watu wanapaswa kuacha tabia za kujilinda, kama vile kuandaa kila mazungumzo kichwani kabla hayajatokea, kuepuka kutazamana machoni au kukaa na mtu mmoja maalumu muda wote.
Na mwisho, Clarke anashauri watu waepuke kujitesa kwa mawazo baada ya mikusanyiko au mazungumzo kuisha.
"Ni rahisi sana kupotosha na kutafsiri vibaya kile kilichotokea," anasema.
Hilo ni jambo ambalo Marie analifahamu vizuri.
"Nilikuwa narudia matukio hayo kichwani tena na tena," anasema. "Nilichojifunza ni kwamba kukabiliana na wasiwasi wa kijamii ni mchakato wa hatua kwa hatua."
"Tiba ilinisaidia sana, lakini pia nilisaidiwa na jambo ambalo rafiki yangu aliniambia miaka kadhaa iliyopita."
Anakumbuka: "Nilipomwambia kwamba sikuweza kwenda naye kukutana na baadhi ya marafiki zake kwa sababu nilikuwa na ujuzi duni wa kushirikiana na watu, aliniambia kwamba hakuwahi kuniona hivyo na kwamba nilipaswa kuacha kujikosoa sana."
"Hapo ndipo hisia zote ziliponijia kwa nguvu."
"Sasa najilazimisha kushirikiana zaidi na watu," anasema. "Inanisaidia pia kwa sababu watu wachache wamesoma kozi yangu ya sasa ya elimu ya juu."
"Pia nimejiunga na kikundi cha wanaastronomia. Bado si rahisi, na mambo hayaendi kila mara kama ninavyotaka, lakini najifunza namna ya kukabiliana nayo."