Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.

Bofya kuelekea tovuti kuu

Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data

Moja kwa moja, Mjumbe wa Trump akutana na kiongozi wa Hamas kushinikiza mpango wa amani Gaza

Afisa mmoja wa Palestina ameiambia BBC kuwa mkwe wa Trump alikutana na ujumbe ulioongozwa na kiongozi mpya wa Hamas, Khalil al-Hayya, nchini Misri siku ya Jumapili.

Moja kwa moja

Na Ambia Hirsi & Mariam Mjahid

  1. Hatua zetu za kujilinda zinaweza kugeuka kuwa mashambulizi - Iran

    Naibu Mkuu wa Masuala ya Kisiasa wa Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu nchini Iran, Yadollah Javani, amesema hatua zinazochukuliwa na Iran katika vita vinavyoendelea kwa sasa ni za kujilinda, lakini zinaweza kubadilika na kuwa mashambulizi siku zijazo.

    Akizungumza katika mahojiano na televisheni na redio ya taifa ya Iran, Javani amesema maadui wa Iran ndio walioanzisha vita hivyo, na kwamba hatua za Iran ni sehemu ya kujilinda.

    Iran pia imesema itachukua hatua zote muhimu kulinda nchi na kuzuia vitisho vya maadui, huku ikisema inaweza kubadilisha namna inavyojibu endapo hali itahitaji.

    Javani amesema majeshi ya Iran yatachukua hatua mpya kwa kuzingatia maelekezo yatakayotolewa, na kwamba yatachukua hatua zote muhimu kulinda nchi, kuhakikisha usalama na kuzuia vitisho kutoka kwa maadui kwa wakati unaofaa.

    Kauli ya Javani imekuja baada ya mshauri wa Kamanda Mkuu wa Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu, Mohammad Reza Naqdi, kusema Iran imeamua kubadili mkakati wake wa kijeshi kutoka unaolenga zaidi kujilinda hadi unaoruhusu pia kushambulia pale itakapoonekana kuwa ni lazima.

    Soma zaidi:

  2. Mamlaka ya Mapato Kenya KRA yapewa mamlaka ya kuwajibisha wanaokosa kulipa ushuru wa nyumba za bei nafuu

    Mamlaka ya Mapato Kenya, KRA, imepewa mamlaka makubwa zaidi ya kuchukua hatua dhidi ya wanaokiuka sheria kwa kutolipa Ushuru wa Nyumba, ikiwemo kusitisha akaunti za benki na kutaifisha mali za wadaiwa.

    Hatua hiyo imefuatia mabadiliko ya sheria yaliyoanza kutekelezwa Julai 1, na kuipa KRA uwezo wa kulazimisha ulipaji wa madeni ya Ushuru wa Nyumba kupitia hatua kali zinazotumiwa dhidi ya wakwepa kodi na wadaiwa wa kodi.

    KRA imekuwa ikikusanya ushuru huo, unaotozwa kwa kiwango cha asilimia 1.5 ya mshahara au mapato ghafi, tangu Julai 2024. Hata hivyo, mamlaka hiyo haikuwa na mamlaka ya kisheria ya moja kwa moja ya kuchukua hatua kali dhidi ya wadaiwa, hali iliyowawezesha maelfu ya wafanyakazi na kampuni kukwepa malipo.

    Sheria ya Fedha ya mwaka 2026 imeziba pengo hilo na pia kuipa KRA mgao mkubwa zaidi wa mapato inayokusanya kutokana na Ushuru wa Nyumba. Katika mwaka uliomalizika Juni, ukusanyaji wa ushuru huo ulifikia shilingi bilioni 79.9.

    Katibu Mkuu wa Wizara ya Nyumba, Charles Hinga, amesema Serikali sasa inatarajia KRA kuchukua hatua madhubuti zaidi dhidi ya wadaiwa, baada ya mamlaka hiyo kusisitiza kwamba ilihitaji mamlaka ya wazi ya kisheria kabla ya kuwachukulia hatua waajiri waliowakata wafanyakazi wao ushuru huo lakini wakashindwa kuuwasilisha serikalini.

    “KRA ilisema ilihitaji mamlaka ya wazi ya kisheria ili kurejesha fedha ambazo hazikuwasilishwa au ambazo hazikulipwa,” Hinga alisema Ijumaa.

    Kauli hiyo inaashiria kuwa Wizara ya Nyumba sasa inatarajia utekelezaji mkali zaidi wa sheria, kufuatia kupewa kwa KRA mamlaka ya moja kwa moja ya kushughulikia madeni ya Ushuru wa Nyumba.

    Soma pia:

  3. UAE ya kwanza duniani kuidhinisha dawa ya kumeza ya kutibu vitiligo

    Falme za Kiarabu UAE zimekuwa nchi ya kwanza duniani kuidhinisha matumizi mapya ya dawa ya RINVOQ, inayojulikana pia kama upadacitinib, katika kutibu vitiligo isiyo ya segmenti, ugonjwa wa ngozi unaosababisha baadhi ya maeneo ya ngozi kupoteza rangi.

    Mamlaka ya Dawa ya Falme za Kiarabu, Emirates Drug Establishment EDE, ilitangaza Jumatatu kuwa imeidhinisha matumizi ya RINVOQ kutibu vitiligo isiyo ya segmenti kwa watu wazima na vijana wenye umri wa miaka 12 na zaidi ambao hali yao inahitaji matibabu ya kimfumo, yaani dawa zinazosambazwa mwilini kupitia mfumo wa damu.

    Kwa mujibu wa EDE, hatua hiyo inaifanya RINVOQ kuwa dawa ya kwanza ya kumeza iliyoidhinishwa kwa kundi hilo la wagonjwa.

    Dawa hiyo hutumiwa kwa kumeza mara moja kwa siku, na hivyo kuongeza chaguo la matibabu kwa wagonjwa wanaokidhi vigezo vya matumizi kwa mujibu wa miongozo ya kitabibu.

    Vitiligo ni ugonjwa wa ngozi unaotokea pale seli zinazozalisha rangi ya ngozi zinapoharibika au kuacha kufanya kazi, na kusababisha mabaka meupe au yenye rangi iliyopungua kwenye sehemu mbalimbali za mwili.

    Soma Pia;

  4. Katambi: Ajenda ya Katiba mpya si ya wapinzani

    Waziri wa Mambo ya ndani ya nchi Tanzania, Patrobas Katambi amesema ajenda ya Katiba mpya si ya wapinzani, bali ni mchakato unaotokana na hatua za kisheria zilizochukuliwa na Serikali ya Tanzania baada ya changamoto zilizojitokeza katika uchaguzi wa mwaka jana.

    Katambi amesema Rais wa Tanzania aliunda tume ya kuchunguza matukio yaliyotokea kabla, wakati na baada ya uchaguzi wa Oktoba, hatua ambayo amesema ililenga kubaini ukweli na kuweka msingi wa hatua zaidi.

    Amesema tume hiyo iliwahoji Watanzania na kukusanya taarifa kuhusu matukio hayo, huku hatua nyingine zikianza kuchukuliwa.

    "Watu wanaopinga wanafanya hivyo kwa sababu wanajua ukweli utajulikana", anasema Katambi.

    Waziri Katambi amesema hatua za kisheria zitachukuliwa dhidi ya yeyote atakayebainika kuhusika katika matukio hayo, bila kujali nafasi yake.

    "Kama ni Serikali, watendaji wa Serikali au mtu mmoja mmoja, kama ulishiriki kwa namna yoyote, kwa kufadhili au kuchochea, utawajibika kwa mujibu wa sheria",, anasema Katambi.

    Akizungumzia maandamano yaliyotokea baada ya uchaguzi, Katambi amepinga madai kwamba yalikuwa maandamano halali, akisema baadhi yalihusisha vurugu.

    "Wanaopinga wanafanya hivyo kwa sababu wanajua hakukuwa na maandamano halali. Kulikuwa na vurugu."

    Amesema sheria inataka maandamano kuwa na kiongozi anayejulikana na anayewajibika kwa matendo yanayotokea wakati wa maandamano.

    "Hakuna nchi yoyote duniani ambayo maandamano yanaweza kuanzishwa bila kuwa na kiongozi. Kama yalikuwa halali, ajitokeze kiongozi aseme, mimi nilikuwa kiongozi, kwa sababu sheria zetu zinataka maandamano yote yawe na kiongozi."

    Katambi amesema mchakato huo unapaswa kuangaliwa kwa kuzingatia sheria za kitaifa, kikanda na kimataifa, akisisitiza kuwa hatua zinazochukuliwa hazilengi kukandamiza upande wowote wa kisiasa.

    Sasa, karibu mwaka mmoja baadaye, Rais Samia Suluhu Hassan ameunda na kuzindua Tume ya Rais ya Uchunguzi wa Wahusika wa Ghasia na Ukiukwaji wa Sheria katika matukio hayo.

    Tume hiyo ina jukumu la kwenda hatua zaidi ya kuchunguza matukio yenyewe, ikiwemo kubaini waliohusika, waliochochea na, kwa mujibu wa Rais Samia, hata waliotoa fedha ili ghasia hizo zitokee.

    Soma Zaidi:

  5. Vigogo wa upinzani Zambia wakamatwa siku chache baada ya uchaguzi wa urais

    Vikosi vya usalama nchini Zambia vimesema vimekamata silaha na kuwakamata watu 11, wakiwemo viongozi waandamizi wa upinzani, kwa madai ya kuhusika katika njama ya uasi dhidi ya serikali.

    Kwa mujibu wa Katibu Mkuu wa Serikali, Patrick Kangwa, mgombea mkuu wa upinzani katika uchaguzi wa urais uliofanyika Alhamisi iliyopita, Brian Mundubile, pia alikuwapo eneo ambalo operesheni hiyo ilifanyika katika mji mkuu, Lusaka.

    Hata hivyo, Mundubile ameelezea uvamizi huo uliofanyika usiku wa Ijumaa kuwa "jaribio la kuniua", akidai kwamba "wenzangu walipigwa risasi" akitazama.

    Tukio hilo limeongeza mvutano wa kisiasa nchini Zambia siku chache baada ya uchaguzi wa urais, huku mamlaka zikisisitiza kuwa operesheni hiyo ililenga kuzuia tishio la usalama wa taifa na viongozi wa upinzani wakipinga madai hayo.

    Kwa matokeo kutoka zaidi ya nusu ya majimbo ya uchaguzi yaliyohesabiwa, anaonekana kuwa nyuma ya rais aliyepo madarakani, Hakainde Hichilema. Mundubile alikuwa ametangaza mapema kwamba ameshinda uchaguzi huo na kudai kuwa kulikuwa na dosari na ukiukwaji katika mchakato wa upigaji kura.

    Mamlaka nchini Zambia zimekanusha madai hayo, huku waangalizi wa uchaguzi katika taarifa zao za awali wakieleza kuwa siku ya upigaji kura ilikuwa kwa kiasi kikubwa ya amani na iliyoendeshwa kwa utaratibu.

    Hata hivyo, waangalizi hao walieleza wasiwasi wao kuhusu mabadiliko ya sheria za uchaguzi yaliyofanyika muda mfupi kabla ya uchaguzi, pamoja na masuala ya uhuru wa vyombo vya habari na upatikanaji sawa wa nafasi za vyombo vya habari kwa vyama na wagombea wakati wa kampeni kuelekea uchaguzi huo.

  6. Kaimu Gavana: Mashambulizi ya Ukraine yaua watu sita Urusi

    Watu sita wameuawa na wengine wanne kujeruhiwa katika mashambulizi ya makombora ya Ukraine yaliyolenga eneo la Belgorod nchini Urusi usiku kucha, kwa mujibu wa kaimu gavana wa eneo hilo.

    Mtoto mwenye umri wa miaka 14 alikuwa miongoni mwa waliojeruhiwa, Alexander Shuvaev aliandika kwenye mtandao wa Telegram siku ya Jumatatu.

    Maafisa wa Ukraine walisema watu wawili waliuawa katika mashambulizi ya ndege zisizo na rubani za Urusi yaliyotokea usiku katika eneo la Sumy, karibu na mpaka wa Urusi, ambalo limekuwa likikumbwa na mashambulizi ya mara kwa mara.

    Mashambulizi hayo yametokea siku moja baada ya kile ambacho maafisa wa Urusi walikielezea kuwa shambulizi "kubwa zaidi mwaka huu" lililofanywa na Ukraine, ambapo takriban watu saba waliuawa. Wakati huo huo, mashambulizi ya Urusi dhidi ya Ukraine pia yaliua takriban watu saba na kujeruhi zaidi ya 39 usiku wa Jumamosi.

    Urusi ilianzisha uvamizi wake dhidi ya Ukraine mnamo mwezi Februari 2022, na kwa sasa inadhibiti takriban asilimia 20 ya eneo la Ukraine.

    Kwa mujibu wa Shuvaev, mashambulizi ya hivi karibuni ya Ukraine yaliteketeza jengo na kuharibu gari katika kijiji cha Koloskovo katika wilaya ya Valuysky, karibu na mpaka wa Urusi na Ukraine.

    Mtoto aliyejeruhiwa alipelekwa hospitalini kwa matibabu, huku watu wengine wawili wakipatiwa huduma za afya, aliongeza.

    Katika wiki za hivi karibuni, Kyiv imeongeza mashambulizi ya ndege zisizo na rubani ndani kabisa ya eneo la Urusi.

    Soma Zaidi Hapa:

  7. Waziri wa Israel atoa wito wa kuwaua Wapalestina 30 hadi 40 huko Gaza kila usiku

    Waziri wa Usalama wa Taifa wa Israel mwenye misimamo mikali ya mrengo wa kulia, Itamar Ben-Gvir, amesema kuwa majeshi ya Israel yanapaswa "kuwaua watu 30 au 40" huko Gaza kila usiku akiashirikia kuwa "wale isiwe kwa wanaohatarisha usalama katika wakati huo maalum", kulingana na shirika la habari la Al-Jazeera.

    Ben-Gvir alitoa kauli hizo katika mazungumzo ya podikasti na Rom Braslavski, mateka wa zamani wa Israel aliyekuwa akishikiliwa Gaza wakati Israel ikiendesha vita katika eneo hilo baada ya mashambulizi yaliyoongozwa na Hamas mnamo Oktoba 2023. Kipande cha mazungumzo hayo kilisambaa mtandaoni siku ya Jumapili na kushirikishwa kwa kiasi kikubwa na vyombo vya habari vya Kipalestina.

    "Kuna watu huko ambao hawastahili kuishi. Hawapaswi kuendelea kuishi. Hata si watu," Ben-Gvir aliongeza, huku akihimiza mauaji yanayolenga Wapalestina huko Gaza.

    Kauli hizo ni miongoni mwa matamshi mengine mengi ya utata na yenye msimamo mkali ambayo Ben-Gvir amewahi kutoa. Waziri huyo ni sehemu ya serikali ya muungano ya Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu na anasimamia jeshi la polisi pamoja na huduma za magereza za Israel.

    Ben-Gvir ameendelea kupata ushawishi mkubwa zaidi kisiasa nchini Israel wakati taifa hilo likielekea kwenye uchaguzi uliopangwa kufanyika Oktoba 27.

  8. Mlipuko wa Ebola watajwa kuwa mbaya zaidi katika historia ya DR Congo

    Mlipuko wa 17 wa Ebola nchini Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo umetajwa rasmi kuwa mbaya zaidi katika historia ya nchi hiyo, miezi mitatu baada ya kugunduliwa kwa mara ya kwanza.

    Kulingana na takwimu za hivi karibuni iliyotolewa na Wizara ya Afya, aina adimu ya virusi vya Bundibugyo imesababisha vifo 2,325 kati ya vmaambukizi 4,945 yaliyothibitishwa kufikia tarehe 15 Agosti 2026.

    Takwimu zinaonyesha kiwango cha vifo kimefikia 47%, huku watu 1,040 wakinusurika na virusi hivyo kufuatia huduma ya usaidizi na udhibiti wa maambukizi.

    Kwa sasa hakuna chanjo zilizoidhinishwa au matibabu ya moja kwa moja iliyotolewa kukabiliana na aina ya Ebola ya Bundibugyo.

    Majaribio ya chanjo mbadala yalianza mwezi uliopita, na mamlaka za afya zinatumia Ervebovaccine—iliyotengenezwa awali kwa aina ya Zaire—chini ya itifaki za matumizi ya huruma kufuatia tafiti zinazopendekeza kuwa inaweza kutoa ulinzi mtambuka.

    Virusi hivyo vimesambaa kwa kasi katika majimbo sita, hasa kaskazini-mashariki mwa nchi.

    Idadi ya maeneo yaliyoathirika imeongezeka kutoka maeneo machache hadi 55 tangu mwezi Mei.

    Ijapokuwa hapo awali maambukizi yalijikita katika majimbo ya Ituri na Kivu Kaskazini, sasa maambukizi yamethibitishwa pia katika majimbo ya Kivu Kusini, Haut-Uélé, Tshopo, na hivi punde zaidi, Bas-Uélé.

    Jimbo la Ituri bado ndilo kitovu cha janga hili, likiwa na asilimia 84.8 ya maambukizi yote yaliyothibitishwa kufikia sasa kwa takribani asilimia 88.1 ya wagonjwa wapya walioripotiwa.

    Kwa sasa, jumla ya wagonjwa 730 wanapata matibabu katika vituo maalum vilivyotengwa na Vituo vya Matibabu ya Ebola (ETCs).

    Mlipuko huu wa sasa umepita ule wa janga la Ebola la DRC la miaka ya 2018–2020, ambalo lilidumu kwa miezi 23 na kusababisha vifo 2,299 kati ya visa 3,481 vilivyorekodiwa.

    Akionya kuhusu hatari inayozidi kuongezeka, Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Afya Duniani (WHO), Dkt. Tedros Adhanom Ghebreyesus, alisema: "Tayari hili ni janga la pili kwa ukubwa la Ebola kuwahi kushuhudiwa, na linaenea kwa kasi zaidi kuliko mlipuko wowote wa awali wa Ebola.

    Kwa kasi yake ya sasa, linaelekea kupita mlipuko wa Ebola uliotokea Afrika Magharibi kati ya mwaka 2014 na 2016."

    Soma zaidi:

  9. Iran yatangaza zawadi nono kwa atakayemua au kumkamata mwanajeshi wa Marekani

    Kamanda wa Jeshi la Iran, Amir Hatami, ametangaza kuwa yeyote atakayemuua au kumkamata mwanajeshi wa Marekani na kumkabidhi kwa mamlaka atapewa zawadi ya dola 30,000; lakini ikiwa mwanamke atafanya hivyo, zawadi hiyo itaongezwa maradufu.

    Kulingana na ripoti ya shirika la habari la serikali ya Iran (IRNA), Hatami alisema uamuzi huo umefikiwa kufuatia maombi mengi kutoka kwa wananchi waliotaka kuchangia fedha za zawadi hiyo.

    "Jeshi litatoa zawadi ya dola 30,000 kwa yeyote atakayemuua au kumkamata afis wa vikosi vya Marekani, na ikiwa mwanamke atafanya hivyo, zawadi hiyo itaongezwa maradufu," IRNA ilimnukuu Hatami akisema.

    Hakutaja muda au mahali maalum ambapo mashambulizi hayo yanayoweza kutokea.

    Hakuna ripoti rasmi iliyotolewa kuhusu uwepo wa vikosi vya ardhini vya Marekani ndani ya Iran tangu kuanza kwa vita, isipokuwa tukio moja la mwezi Aprili mwaka jana la kuokelewa rubani wa ndege ya Marekani iliyoanguka.

    Kamanda huyo wa jeshi la Iran aliongeza kusema, "Uwepo wa Marekani kimsingi 'umedhibitiwa' katika eneo hili na kwa mtazamo wa Tehran, vikosi vya Marekani havina tena haki ya kuingia katika Ghuba, Lango la Hormuz, na Bahari ya Oman."

    Soma zaidi:

  10. Korea Kusini yaanza mazoezi ya kijeshi na Marekani

    Kadhaa baada ya Rais wa Marekani Donald Trump kusema kuwa angepunguza kwa kiasi kikubwa kiwango cha mazoezi ya kijeshi ya nchi yake na Korea Kusini, Seoul imetangaza kuanza kwa mazoezi hayo.

    Bw. Trump alisema kuwa kiongozi wa Korea Kaskazini, Kim Jong-un, ndiye aliyemfanya kufikia uamuzi huo. Aliyataja mazoezi hayo kuwa ya gharama kubwa na ya kichokozi, huku akigusia hatua ya Korea Kusini kukataa kujiunga na mazungumzo kuhusu mpango wa nyuklia wa Iran.

    Mazoezi ya 'Ulchi Freedom Shield' hufanyika kila mwaka ili kujiandaa dhidi ya tisho la mashambulizi katika Rasi ya Korea.

    Korea Kaskazini inaendelea kuimarisha silaha zake za nyuklia na wiki iliyopita ilifanya majaribio kadhaa ya makombora ya masafa marefu (ballistic missiles). .

    Katika ujumbe wake wa mitandao ya kijamii siku ya Jumapili, Trump alisema ilikuwa "ni vigumu kuahirisha," mpango huo kwani Marekani na Korea Kusini zilikuwa zikitarajiwa kuanza mazoezi yao ya kila mwaka ya kijeshi Jumatatu.

  11. Matukio ya vurugu yagubika mkutano wa 'Linda Mwananchi' Homa Bay magharibi mwa Kenya

    Kaunti ya Homa Bay ilishuhudia hali ya wasiwasi mkubwa wa kisiasa na hofu kuhusu usalama siku ya Jumapili, tarehe 16 Agosti, wakati vuguvugu la 'Linda Mwananchi' - mrengo hasimu wa chama cha upinzani cha Orange Democratic Movement (ODM) lilipofanya mkutano mkubwa wa kisiasa huko Nyandiwa, huku kukiwa na ripoti za kufungwa kwa barabara, mapigano, uharibifu wa mali na mashambulizi dhidi ya waandishi wa habari.

    Kwa mujibu wa vyombo vya habari vya ndani hali ya wasiwasi ilianza mapema Jumapili, ambapo barabara kuu zinazoelekea maeneo ya Mji wa Homa Bay na Nyandiwa ziliripotiwa kufungwa kwa mawe makubwa na vizuizi vingine.

    Baadhi ya njia zilikuwa hazipitiki, jambo lililotatiza usafiri wakati wafuasi na viongozi wa kisiasa wakielekea kwenye mkutano huo uliopangwa.

    Msafara wa 'Linda Mwananchi' uliripotiwa kulazimika kutumia njia mbadala, ikiwemo barabara mbovu na njia za kutembea kwa miguu, ili kufika Nyandiwa baada ya sehemu za barabara kuu kufungwa.

    Maafisa wa usalama waliusindikiza msafara huo huku hali ya wasiwasi ikiongezeka katika maeneo kadhaa ya kaunti hiyo.

    Makabiliano yaliropotiwa baadaye ambapo gari moja lilichomwa moto, watu kadhaa wakiwemo waandishi wa habari kujeruhiwa, na washukiwa 17 kukamatwa.

    Kwa mujibu wa mashuhuda mashambulizi hayo yaliyodaiwa kuwalenga wafuasi wa Linda Mwananchi yalianza usiku wa Jumamosi wakati wahuni waliposhambulia hoteli moja Homa Bay; kuvunja madirisha, kuharibu mali na kuiba vitu kabla ya kuondoka kwa kutumia pikipiki.

    Walikuwa wamejihami kwa mawe na rungu walipokuwa wakipita eneo la Nyandiwa, Suba Kusini, ambapo kundi la 'Linda Mwananchi' ilikuwa imepanga kuhudhuria ibada kanisani.

    Shirika la kutetea haki za binadamu la Amnesty International Kenya, limelaani matukio hayo na kuelezea wasiwasi kuhusu vitendo vya vurugu dhidi ya waandishi wa habari, kuvurugwa kwa matangazo ya vyombo vya habari, uharibifu wa mali, uwekaji wa vizuizi visivyo halali barabarani na vitisho.

    Shirika hilo linataka uchunguzi ufanywe kubaini chanzo cha vurugu hizo na kutoa wito kwa mamlaka kulinda haki za kikatiba za raia pamoja na usalama wa umma.

    Maelezo zaidi:

  12. Trump: Ninapunguza kiwango cha mazoezi ya kijeshi ya Marekani na Korea Kusini

    Rais Donald Trump amesema Marekani itapunguza kwa kiasi kikubwa mazoezi ya kijeshi ya pamoja na Korea Kusini, akitaja "uhusiano wake mzuri sana" na kiongozi wa Korea Kaskazini, Kim Jong Un.

    Pia aliangazia kwenye mtandao wa kijamii wa Truth Social hivi karibuni kwamba Korea Kusini ilikataa kuungana na Marekani katika mchakato wa kuiondolea Iran uwezo wa kumiliki silaha za nyuklia.

    "Mazoezi haya sio ya gharama kubwa tu—ambapo sehemu kubwa ya gharama hizo hulipwa na Marekani (kama kawaida!)—bali pia yanatoa ishara isiyofaa kabisa na ya uhasama," Trump aliandika.

    Seoul ilisema mazoezi hayo na Marekani yataendelea "kama ilivyopangwa". Pyongyang bado haijatoa tamko lolote. Haya yanajiri baada ya Korea Kaskazini kufanya majaribio ya makombora yake ya balistiki mwezi huu, hatua ambayo imepigwa marufuku na Umoja wa Mataifa.

    Katika ujumbe wake wa mitandao ya kijamii siku ya Jumapili, Trump alisema ilikuwa "ni vigumu kuahirisha," mpango huo kwani Marekani na Korea Kusini zilikuwa zikitarajiwa kuanza mazoezi yao ya kila mwaka ya kijeshi Jumatatu.

    Walieleza kuwa zoezi hilo la siku 11 litakuwa na ukubwa sawa na lile ya miaka iliyopita, itahusisha takriban wanajeshi 18,000 wa Korea Kusini.

    Katika mkutano na waandishi wa habari, viongozi wa kijeshi pia walizungumzia hatua ya Korea Kaskazini kupeleka wanajeshi kusaidia vita vya Urusi dhidi ya Ukraine.

    Msemaji wa jeshi la Marekani, Ryan Donald, alisema "mafunzo yetu yanazingatia tishio hilo," akiashiria suala la wanajeshi wa Korea Kaskazini kurejea kutoka uwanja wa vita. Takriban wanajeshi 28,500 wa Marekani wamepelekwa nchini Korea Kusini.

    Soma zaidi:

  13. Mjumbe wa Trump akutana na kiongozi wa Hamas kushinikiza mpango wa amani Gaza

    Mjumbe wa Rais wa Marekani Donald Trump katika Mashariki ya Kati, Jared Kushner, amefanya mazungumzo nadra na Hamas kujadili utekelezaji wa mpango wa amani wa Gaza unaoungwa mkono na Marekani.

    Afisa mmoja wa Palestina ameiambia BBC kuwa mkwe wa Trump alikutana na ujumbe ulioongozwa na kiongozi mpya wa Hamas, Khalil al-Hayya, nchini Misri siku ya Jumapili.

    "Mwezi uliopita, Bodi ya Amani ya Trump ilisema kulikuwa na makubaliano ya Hamas na makundi mengine yenye silaha huko Gaza kuvuliwa silaha kabisa."

    Wiki iliyopita, Israel ilikataa mpango wa Trump wa vipengele 15 unaotaka jeshi la Israel kujiondoa Gaza na eneo hilo kujengwa upya chini ya uongozi mpya wa kiraia wa Wapalestina.

    Nchi nane za Kiislamu zilitoa taarifa siku ya Jumapili zikilaani uamuzi wa Israel wa kukataa mpango huo.

    Trump anaongoza Bodi ya Amani, shirika la kimataifa lililoanzishwa awali kwa lengo la kuleta amani Gaza, lakini baadaye likaongezewa jukumu la kushughulikia migogoro mbalimbali duniani.

    Inadaiwa kuwa mkutano kati ya Kushner na Hayya ni wa kwanza wa ngazi hiyo kufanyika tangu makubaliano ya usitishaji mapigano katika Ukanda wa Gaza yalipofikiwa mwaka jana.

    Soma Zaidi:

  14. Hujambo na karibu katika matangazo yetu mubashara 17/08/2026.