Myanmar yakabiliwa na hukumu ya kihistoria ya mauaji ya kimbari katika Mahakama ya Umoja wa Mataifa
Mahakama ya Kimataifa ya Haki (ICJ) inatarajiwa kutoa uamuzi wake leo, Alhamisi katika kesi ya mauaji ya kimbari dhidi ya Myanmar, iliyofunguliwa na Gambia miaka saba iliyopita, kuhusu mauaji na mateso yaliyowakumba Waislamu wa jamii ya Rohingya.
Uamuzi huo unaweza kuwa wa kihistoria, kwani tangu kusainiwa kwa Mkataba wa Kuzuia na Kuadhibu Uhalifu wa Mauaji ya Kimbari mwaka 1948, baada ya mauaji ya Holocaust yaliyofanywa na Wanazi, watu kadhaa wamewahi kufunguliwa mashtaka na kutiwa hatiani kwa uhalifu huo katika migogoro kama ile ya Rwanda na Yugoslavia ya zamani.
Hata hivyo, hakuna nchi iliyowahi kupatikana na hatia ya kutekeleza mauaji ya kimbari na mahakama ya kimataifa.
Wakili Arsalan Suleman, anayeongoza kesi dhidi ya Myanmar katika mahakama hiyo, amesema ushindi wa Gambia utakuwa na umuhimu mkubwa katika historia ya sheria za kimataifa.
Amesema uamuzi huo ungeimarisha upya Mkataba wa Mauaji ya Kimbari wa mwaka 1948 pamoja na dhana ya uwajibikaji wa kisheria wa kimataifa kwa uhalifu unaofanywa na mataifa.
Mnamo Agosti na Septemba 2017, operesheni ya kijeshi dhidi ya jamii ya Rohingya katika jimbo la Rakhine ilisababisha maelfu ya watu kuuawa na mamia ya maelfu wengine kukimbilia nchi jirani ya Bangladesh.
Operesheni hiyo ilihusisha kuchomwa kwa makazi ya Warohingya, huku manusura wakieleza mauaji, mateso na ubakaji wa watu wengi uliofanywa na wanajeshi wa Myanmar.
Mashirika ya kutetea haki za binadamu pamoja na ujumbe wa uchunguzi wa Umoja wa Mataifa yalifanya uchunguzi na kuweka kumbukumbu za kina kuhusu ukiukaji huo wa haki za binadamu.
Aidha, serikali ya Myanmar imehusishwa na uharibifu wa kimfumo wa vijiji vya Warohingya, hali iliyozidisha wasiwasi kuhusu hatima ya jamii hiyo.
Hata hivyo, swali kuu linalotarajiwa kuamuliwa na Mahakama ya Kimataifa ya Haki ni iwapo vitendo hivyo vilifikia kiwango cha uhalifu wa mauaji ya kimbari.
Ripoti ya Umoja wa Mataifa ya mwaka 2018, iliyotokana na mahojiano na mamia ya watu, ilieleza kuwa mbinu zilizotumiwa na jeshi la Myanmar zilikuwa zisizo na uwiano kabisa ikilinganishwa na vitisho halisi vya kiusalama.
Ripoti hiyo pia ilipendekeza kuwa viongozi wakuu wa jeshi la Myanmar wachunguzwe kwa tuhuma za mauaji ya kimbari katika jimbo la Rakhine na uhalifu dhidi ya ubinadamu katika maeneo mengine.
Hata hivyo, Myanmar ilikataa matokeo ya ripoti hiyo.
Unaweza pia kusoma: