Hitilafu ya kiufundi yaathiri huduma za benki kadhaa Marekani

Chanzo cha picha, Getty Images
Wateja wa benki na taasisi kadhaa za kifedha nchini Marekani, zikiwemo Bank of America, JPMorgan Chase, Wells Fargo na benki nyingine kubwa, wameripoti kukumbwa na hitilafu katika upatikanaji wa baadhi ya huduma za kibenki.
Kwa mujibu wa tovuti ya Downdetector, inayofuatilia taarifa za watumiaji kuhusu kukatika au kuvurugika kwa huduma za mtandaoni, takribani watu 4,500 wameripoti kukumbwa na hitilafu katika huduma za benki mtandaoni za JPMorgan Chase.
BBC imeelezwa kuwa benki hiyo ilikumbwa na hitilafu ya kiufundi, na kwamba tukio hilo halionekani kuhusiana na mashambulizi ya kimtandao au masuala ya usalama wa mifumo ya kompyuta.
Hata hivyo, benki nyingine kadhaa, zikiwemo Capital One na PNC, zimesema mifumo yao ya kibenki haijaathiriwa na hitilafu hizo.
Chase Bank ilitangaza kupitia taarifa kwenye mitandao ya kijamii kuwa hitilafu katika programu za kompyuta huenda ilisababisha kukwama kwa huduma katika baadhi ya benki nyingine.
"JPMorgan Chase Bank inakabiliwa na hitilafu ya muda iliyosababishwa na tatizo la programu katika mifumo yake ya vifaa vya kompyuta vilivyopo ndani ya benki. Hakuna ushahidi unaoashiria kuwa hitilafu hii inahusiana na shambulizi la kimtandao. Baadhi ya maombi ya wateja yanachukua muda mrefu zaidi kushughulikiwa kuliko kawaida," ilisema taarifa hiyo.
Taarifa hiyo iliongeza: "Katika baadhi ya miamala ambayo benki yetu imehusika pamoja na benki nyingine, huenda benki hizo pia zimeathirika. Hata hivyo, hili si tatizo lililoenea kwa upana wala linaloathiri mfumo mzima wa huduma za kibenki."
Chase Bank imesema wateja bado wanaweza kufikia akaunti zao na fedha zao, huku benki hiyo ikiendelea na juhudi za kutatua tatizo hilo.
Unaweza pia kusoma:




















