Rubio asema Marekani haikabiliwi na mashambulizi ya kimfumo
Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Marco Rubio, amekanusha madai na hofu zilizoenea mitandaoni kuwa mfululizo wa hitilafu za mifumo ya teknolojia zilizotokea katika wiki iliyopita zina uhusiano, akisema hakuna ushahidi wowote unaoonyesha kuwa matukio hayo yanahusiana.
Rubio amekiri kuwa watu wana hofu kutokana na mfululizo wa hitilafu hizo, zilizojumuisha kusimamishwa kwa safari zote za ndege nchini Marekani na kuvurugika kwa huduma za benki pamoja na mifumo ya kampuni za Apple na Microsoft.
Hata hivyo, amewaambia waandishi wa habari kuwa: "Marekani haikabiliwi na mashambulizi ya kimfumo. Matukio haya hayahusiani kwa namna yoyote, kila moja lina chanzo chake."
Wataalamu wa usalama wa kimtandao wamesema hakuna ushahidi unaounganisha hitilafu hizo, huku matatizo mengi yakionekana kusababishwa na masasisho ya mifumo ya zamani ya teknolojia.
Katika wiki iliyopita, kumekuwa na hitilafu kubwa katika mifumo ya Microsoft, tatizo la kiufundi lililosababisha safari zote za ndege nchini Marekani kusimamishwa kwa saa kadhaa, pamoja na matatizo katika mifumo ya Shirika la Ujasusi la Marekani (NSA), benki kadhaa na kampuni ya Apple.
Kila kampuni na taasisi iliyoathirika imesema kuwa tukio lililoikumba halikuhusiana na shambulizi la kimtandao.
Kauli ya Rubio imekuja saa chache baada ya Mkurugenzi wa Ujasusi wa Taifa wa Marekani, Jay Clayton, pia kuzungumzia suala hilo katika mahojiano na kituo cha Fox News, akisema hitilafu hizo hazikusababishwa na mashambulizi ya kimtandao.
Alieleza kuwa taasisi nyingi zinafanya marekebisho na kuboresha mifumo yao, jambo ambalo limesababisha baadhi ya huduma kuvurugika.
Rubio aliulizwa iwapo utawala wa Rais Donald Trump una wasiwasi kuwa hofu ya umma inaweza kusababisha watu kuhifadhi bidhaa kwa wingi au kukimbilia kutoa fedha zao benki kwa kuhofia usalama wa fedha zao.
Akikiri kuwepo kwa hofu hizo, Rubio amesema njia bora ya kukabiliana nazo ni serikali ya Marekani kuwaeleza wananchi kile inachokifahamu kuhusu matukio hayo.
"Viashiria vyote tulivyonavyo vinaonyesha kuwa kila moja ya matukio haya lina maelezo au chanzo chake ambacho hakihusiani na wahalifu wa kimtandao, mtu mwenye nia ya uhasama au nchi nyingine," amesema.
Hitilafu za mifumo ya teknolojia zimekuwa zikiripotiwa kila siku tangu Alhamisi, wakati hitilafu ya Microsoft ilipovuruga huduma zake mbalimbali, ikiwemo barua pepe.
Unaweza pia kusoma: