Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.

Bofya kuelekea tovuti kuu

Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data

Moja kwa moja, Trump atangaza kuiwekea Iran vikwazo vikali vya kiuchumi

Shinikizo hili jipya la kulenga zaidi uchumi wa Iran linakuja wakati vita vya Iran vikielekea kutimiza miezi sita bila ya juhudi zozote madhubuti za kidiplomasia wala kijeshi.

Muhtasari

Moja kwa moja

Na Ambia Hirsi

  1. Israel yatangaza zabuni ya mradi 'tata' wa makazi katika Ukingo wa Magharibi

    Israel imetangaza zabuni ya kujenga takriban nyumba 1,200 kwa ajili ya walowezi katika eneo lenye umuhimu wa kimkakati katika Ukingo wa Magharibi unaokaliwa kwa mabavu, huku ikijaribu kuondoa kabisa uwezekano wa kuwepo kwa taifa la Palestina.

    Mipango ya ujenzi katika eneo linalojulikana kama "E1" huko Jerusalem Mashariki imekuwa ikikosolewa vikali na jumuiya ya kimataifa kwa muda mrefu, na makazi hayo yanachukuliwa kuwa haramu kwa mujibu wa sheria za kimataifa.

    Kupitia mpango huu, Ukingo wa Magharibi utagawanywa katika sehemu mbili, na Jerusalem Mashariki itatenganishwa na maeneo mengine.

    Waziri wa Mambo ya Nje wa Uingereza, Ed Miliband, alikemea kutangazwa kwa zabuni hiyo akiitaja kuwa "kitendo kisichokubalika na kilicho na madhara" na kuitaka Israel "kusitisha mara moja mipango ya E1, kuondoa zabuni hiyo na kukomesha upanuzi wa makazi ya walowezi."

    Tangu Israel ilipokalia kwa mabavu Ukingo wa Magharibi na Jerusalem Mashariki wakati wa Vita vya Mashariki ya Kati vya mwaka 1967, imejenga takriban makazi 160, ambayo ni makazi ya Wayahudi wapatao 700,000.

    Wapalestina wanataka maeneo haya, pamoja na Ukanda wa Gaza, kwa ajili ya taifa lao la baadaye.

    Hivi sasa, takriban Wapalestina milioni 3.3 wanaishi sambamba na walowezi hao.

    Licha ya upinzani mkali kutoka kwa jumuiya ya kimataifa, serikali mfululizo za Israel zimeendelea kuruhusu upanuzi wa makazi hayo.

    Maelezo zaidi:

  2. Mkuu wa Ujasusi Ecuador, Wamarekani 5 wafariki ajali ya helikopta Kenya

    Serikali ya Ecuador imesema mkuu wake wa Idara ya Ujasusi na mke wake wamefariki dunia katika ajali ya helikopta iliyoanguka jana Jumatano katika kaunti ya Samburu nchini Kenya.

    Raia watano wa Marekani pia walifariki dunia katika ajali hiyo, Msemaji wa Idara ya Mambo ya Nje ya Marekani alisema.

    Mamlaka ya Usafiri wa Anga ya Kenya (KCAA) ilisema kuwa helikopta hiyo ilikuwa katika safari ya kutalii mandhari ikitoka kwenye hifadhi ya wanyamapori ya Loisaba kuelekea Ewaso Nyiro, mto unaopita kando ya hifadhi kadhaa za taifa.

    Kaunti ya Samburu ni mojawapo ya maeneo maarufu ya utalii nchini Kenya, ikiwa na hifadhi nyingi za wanyamapori zinazomilikiwa na sekta binafsi, na inajulikana kwa mandhari yake ya kuvutia na ya kipekee.

    Picha kutoka eneo la tukio zinaonesha moshi ukifuka katika eneo lenye miti ambapo helikopta hiyo ilianguka kwenye Mlima Ololokwe, huku wahudumu wa Shirika la Msalaba Mwekundu Kenya wakikaribia mabaki ya helikopta ambayo bado yalikuwa yakiteketea kwa moto.

    Ecuador haijatoa maelezo kuhusu kifo cha Sensi-Contugi, mwenye umri wa miaka 44, ambaye aliteuliwa kuwa Mkurugenzi Mkuu wa Kituo cha Ujasusi wa Kimkakati mwaka 2024.

  3. Jeshi la Israel lakiri kumuua msichana wa Kipalestina

    Jeshi la Israel limethibitisha kwa mara ya kwanza kuwa wanajeshi wake walilifyatulia risasi gari alimokuwa Hind Rajab,msichana wa Kipalestina wa umri wa miaka mitano aliyeuawa pamoja na jamaa zake sita wakisafiri Gaza mnamo mwaka 2024.

    Gari la wagonjwa lililotumwa kumfikia—katika hatua iliyoratibiwa na jeshi la Israel—lilishambuliwa kwa makombora, na kusababisha vifo vya wahudumu wawili wa afya.

    Mwili wa Hind ulipatikana siku kadhaa baadaye, pamoja na miili ya watu wengine waliouawa.

    Katika taarifa, Jeshi la Ulinzi la Israel (IDF) limesema linaanzisha uchunguzi kuhusu vifo hivyo pamoja na mauaji ya wahudumu wawili wa afya waliotumwa kuokoa maisha ya Hind.

    Uchunguzi pia utaanzishwa kuhusu mauaji ya maafisa 15 wa kutoa misaada ya dharura waliouawa na wanajeshi wa Israel mjini Rafah mwaka jana.

    Matukio yote mawili yalilaaniwa kimataifa.

    Awali, Jeshi la Israel (IDF) lilisema kuwa hakuna hata mmoja wa askari wake aliyekuwa katika eneo hilo wakati Hind alipouawa. Hata hivyo, kauli hiyo ilianza kutiliwa shaka.

    Baadaye, IDF ilisema kuwa ilikuwa "imefanya operesheni dhidi ya maeneo yanayotumiwa na magaidi" kwa kutumia vikosi vilivyokuwa vikifanya kazi katika vitongoji vya Jiji la Gaza, ikiwemo Tel al-Hawa, ambapo Hind alikuwepo.

  4. Trump atangaza kuiwekea Iran vikwazo vikali vya kiuchumi

    Rais wa Marekani Donald Trump amesema anaanzisha vikwazo vipya vya kiuchumi dhidi ya Iran na nchi yoyote ile itakayoisaidia au kufanya biashara nayo.

    Kupitia mtandao wake wa kijamii wa Truth Social,Bwana Trump amesema anachukua hatua hiyo kwasababu Iran imeshindwa kufikia makubaliano na Marekani.

    Rais Trump ambaye mara kwa mara ametishia kuichukulia hatua kali zaidi Iran kwa kutoridhia kufikia makubaliano ya kuumaliza mzozo wa Mashariki ya Kati amesema leo anatangaza operesheni kali zaidi ya kiuchumi kuwahi kuchukuliwa dhidi ya nchi yoyote ile na itakuwa vita vya kiuchumi na kubaguliwa kwa kiwango ambacho hakijawahi kushuhudiwa.

    Aidha ametangaza kuwa nchi yoyote itakayoruhusu asasi zake za kifedha,biashara,viwanja vya ndege au asasi zake za kiserikali kuisadia kivyovyote vile Iran nayo itaathirika vibaya kiuchumi.

    Hata hivyo,hajatoa maelezo zaidi kuhusu hatua hizo mpya dhidi ya Iran au kutaja ni nchi zipi nyingine zitakazolengwa na vikwazo hivyo vipya.

    Kauli ya Trump inakuja wiki moja baada ya waziri wake wa fedha Scott Bessent kusema Marekani itaiwekea vikwazo vya kiuchumi Iran kwa viwango ambavyo havijashuhudiwa katika kipindi cha nyuma.

    Makubaliano ya kusitisha vita vya Iran kwa siku sitini yalikamalika Jumatatu wiki hii huku kukiwa hakuna dalili za kukomeshwa kwa mzozo huo wa Mashariki ya Kati.

    Shinikizo hilo jipya la kuulenga zaidi uchumi wa Iran linakuja wakati vita vya Iran vikielekea kutimiza miezi sita bila ya juhudi zozote madhubuti za kidiplomasia wala kijeshi.

    Rais Trump aliyevianzisha vita hivyo mwishoni mwa mwezi Februari pamoja na Israel, anamulikwa darubini kali kisiasa nchini mwake wakati nchi hiyo ikijiandaa kwa uchaguzi wa katikati mwa muhula unaotarajiwa mwezi Novemba.

    Mshirika wake katika vita hivyo vya Iran,Waziri mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu naye anakabiliwa na shinikizo la kisiasa kuhusu anavyoshughulikia mzozo wa Iran na wa Gaza kuelekea uchaguzi mkuu wa Israel unaotarajiwa mwezi Oktoba mwaka huu.

    Licha ya mashambulizi ya makombora kupungua katika siku za hivi karibuni kati ya Iran na Marekani,Iran imeendelea kuzuia meli kupita katika Mlango Bahari wa Hormuz licha ya shinikizo kali kutoka kwa Marekani kutaka njia hiyo muhimu ya safari za meli za mizigo baharini kufunguliwa.

    Soma zaidi:

  5. Karibu kwa matangazo ya moja kwa moja leo Alhamisi 20.08.2026.