Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.

Bofya kuelekea tovuti kuu

Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data

Moja kwa moja , Trump aituhumu Iran kwa kuongeza mashambulizi ya droni na makombora

Rais wa Marekani Donald Trump amedai kuwa Iran imerusha ndege zisizo na rubani na makombora mengi zaidi, ndani ya wiki moja iliyopita kuliko wakati mwingine wowote

Muhtasari

Moja kwa moja

Na Beldeen Waliaula

  1. Trump aunga mkono kurejea kwa Jensen Huang katika kampuni ya Nvidia

    Rais wa Marekani Donald Trump ameunga mkono kurejea kwa Jensen Huang katika kampuni ya Marekani ya kutengeneza chipu za kompyuta, Nvidia.

    Katika ujumbe aliouchapisha kwenye mtandao wake wa kijamii wa Truth Social, Trump alisema: "Natumai bodi ya wakurugenzi ya Nvidia itamrejesha Jensen Huang. Huo utakuwa uamuzi bora kwa kampuni hiyo na Marekani."

    Matamshi hayo yanajiri baada ya Jensen Huang kujiuzulu kutoka wadhifa wake wa Afisa Mkuu Mtendaji wa Nvidia mapema mwezi huu.

    Kuondoka kwa Huang kulifuatia utata kuhusu maisha yake binafsi, uliohusisha madai ya kuwa na uhusiano wa kimapenzi nje ya ndoa na mwanamke anayedaiwa kuwa jasusi wa China.

    Nvidia ni mojawapo ya kampuni zinazoongoza duniani katika utengenezaji wa chipu za kisasa zinazotumika katika teknolojia ya akili unde (AI).

    Soma pia:

  2. AFCON 2027: Viwanja sita vyateuliwa kuandaa mechi Kenya, Tanzania na Uganda

    Viwanja sita vimeteuliwa kuandaa mechi za fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) mwaka ujao, ambazo zitaandaliwa kwa pamoja nchini Kenya, Tanzania na Uganda.

    Viwanja vitakavyotumika kwa mashindano hayo vilitangazwa wakati wa mkutano wa Shirikisho la Soka barani Afrika (CAF) uliofanyika mwishoni mwa wiki iliyopita nchini Nigeria.

    Mjini Nairobi, mechi zitachezwa katika Uwanja mpya wa Talanta wenye uwezo wa kuchukua watazamaji elfu 60,000, ambao unatarajiwa kufunguliwa mwezi Januari.

    Tanzania itakuwa na viwanja vitatu vitakavyotumika katika miji ya Arusha, Dar es Salaam na Zanzibar.

    Uganda itatumia Uwanja wa Taifa wa Mandela ulioko Kampala pamoja na Uwanja mpya wa Hoima City, ambao timu ya taifa ya Uganda imekuwa ikiutumia katika mechi zake za hivi karibuni za kimataifa.

    Uwanja utakaotumika kuandaa fainali ya mashindano hayo ya timu 24, yatakayofanyika kuanzia Juni 19 hadi Julai 17, bado haujaamuliwa.

    Fainali za mwisho za Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON), zilizofanyika Morocco kuanzia Desemba 2025 hadi Januari 2026, zilichezwa katika viwanja tisa vilivyoko katika miji sita.

    Soma pia:

  3. Mataifa yashindwa kufikia makubaliano katika mkutano wa COP31

    Nchi mbalimbali zimeshindwa kufikia makubaliano mapya muhimu ya kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi, kufuatia mivutano kuhusu matumizi ya nishati ya kisukuku na ufadhili katika mkutano wa Umoja wa Mataifa kuhusu tabianchi ya COP31 nchini Uturuki.

    Mazungumzo hayo yaliyopaswa kukamilika siku ya Ijumaa ila yaliendelea hadi Jumapili huku wanaoshiriki wakijaribu kufikia mwafaka, na hivyo kuwa mkutano wa Umoja wa Mataifa kuhusu tabianchi uliochukua muda mrefu zaidi katika historia.

    Hata hivyo, mapendekezo ya mwisho hayakukubalika na Umoja wa Ulaya, mataifa ya visiwa vya Pasifiki na nchi nyingine kwa sababu hayakutaja moja kwa moja matumizi ya nishati ya kisukuku, ambayo ndiyo chanzo kikuu cha ongezeko la joto duniani.

    Wakati huohuo, nchi nyingi maskini zilipinga kutokuwepo kwa ahadi zozote za wazi za kifedha kutoka kwa mataifa tajiri za kuzisaidia kukabiliana na athari za ongezeko la joto duniani.

    Mara ya mwisho makubaliano makuu ya kisiasa katika mkutano wa COP kushindwa kufikiwa kwa aina hii ilikuwa mwaka 2009 mjini Copenhagen, Denmark.

    Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, António Guterres, ambaye huu ulikuwa mkutano wake wa mwisho wa COP kabla ya kuondoka madarakani, alisema amesikitishwa sana na matokeo hayo.

    Aliyashutumu makundi yenye ushawishi mkubwa katika sekta ya nishati ya kisukuku, akisema yanatumia mbinu zinazofanana na zile za kampuni kubwa za tumbaku.

    Alisema makundi hayo yanapotosha sayansi, kuchelewesha sera, kuzuia hatua za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi na kujikusanyia faida kubwa huku watu kote duniani wakilipa gharama.

  4. Trump aituhumu Iran kwa kuongeza mashambulizi ya droni

    Rais wa Marekani Donald Trump amedai kuwa Iran imerusha ndege zisizo na rubani na makombora mengi zaidi, ndani ya wiki moja iliyopita kuliko wakati mwingine wowote katika kipindi cha zaidi ya mwaka mmoja tangu vita kuanza.

    Trump hakutaja ripoti wala chanzo chochote cha takwimu kuthibitisha madai yake, lakini alihusisha kuongezeka kwa mashambulizi hayo na ushindi wa chama cha Democratic katika uchaguzi wa katikati ya muhula Marekani.

    "Kwanza, nilisema kuwa iwapo chama cha Democratic kingeshinda, masoko ya hisa yangeshuka, jambo ambalo limetokea. Pili, nilisema kuwa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, ambayo hadi sasa imewaua waandamanaji 81,000, ingeongeza mashambulizi yake, jambo ambalo pia limetokea."

    Rais huyo wa Marekani aliongezea kuwa,

    "Iran imefyatua ndege zisizo na rubani na makombora mengi zaidi katika wiki moja iliyopita kuliko wakati mwingine wowote katika kipindi cha zaidi ya mwaka mmoja. Msijali, yote yamenaswa na kudunguliwa, bila kusababisha uharibifu wowote."

    Soma pia:

  5. Mvulana wa miaka saba aokolewa baada ya saa 14 chini ya vifusi Ukraine

    Mvulana mwenye umri wa miaka saba ameokolewa kutoka kwenye vifusi vya jengo la makazi lililoporomoka katika mji wa Dymer, baada ya kunaswa humo kwa saa 14 kufuatia mashambulizi ya usiku ya Urusi katika eneo la Kyiv, yaliyosababisha vifo vya watu tisa, kwa mujibu wa maafisa wa Ukraine.

    Shambulizi hilo lilitokea mapema Jumapili. Mkuu wa utawala wa eneo la Kyiv, Tymur Tkachenko, alisema pia mwanamke mwenye umri wa miaka 79 aliokolewa akiwa hai kutoka kwenye jengo hilo lililoporomoka.

    Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky pia amesema watu watatu waliuawa na wengine 13 kujeruhiwa katika shambulizi tofauti lililotokea katika mji wa Vyshneve, pia katika eneo la Kyiv,hapo jana. Shambulizi hilo lililenga duka la bidhaa za vyakula.

    Mamlaka za Ukraine zimesema mvulana aliyeokolewa katika mji wa Dymer anaendelea vizuri kiafya na alikimbizwa hospitalini.

    Soma pia:

  6. Meli ya Urusi yashambuliwa kwa droni katika bandari ya Libya

    Serikali ya Libya imesema mlipuko uliotokea ndani ya meli ya Urusi iliyokuwa imetia nanga katika kituo cha wanamaji kilichoko Benghazi,ulisababishwa na shambulizi linaloshukiwa kutekelezwa na ndege isiyo na rubani.

    Mlipuko huo ulitokea mapema Jumapili wakati meli hiyo ilipowasili bandarini kwa ajili ya kuongeza mafuta na kupokea bidhaa kabla ya kuendelea na safari yake ya kurejea Urusi.

    Taarifa ya serikali hiyo imesema hakuna mtu aliyejeruhiwa katika tukio hilo. Hadi kufikia sasa, Moscow haijatoa tamko lolote kuhusu shambulizi hilo.

    Baadaye hapo jana, Wizara ya Afya ya Libya ilisema kuwa imepokea watu waliojeruhiwa kutoka katika meli nyingine ya kibiashara ambayo pia ililengwa katika shambulizi lililotokea karibu na pwani ya Benghazi.

    Wizara hiyo ilisema majeraha ya waliojeruhiwa yalikuwa madogo na hali zao za afya zilikuwa imara.

    Ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini Libya ulieleza wasiwasi mkubwa kuhusu mashambulizi hayo, huku ukitaka uchunguzi wa haraka, huru na wa wazi kufanyika.

    "Libya haiwezi kumudu, wala hairuhusiwi kuwa uwanja wa mapambano ya migogoro ya kigeni," Umoja wa Mataifa uliandika kwenye mtandao wa X

    Video zilizochapishwa kwenye mitandao ya kijamii na kuthibitishwa kijiografia na kitengo cha BBC Verify zinaonyesha meli iliyoshambuliwa ikiwa imezingirwa na moto na moshi.

    Picha za setilaiti kutoka kampuni ya Planet Labs PBC pia zinaonyesha meli ikiwa inawaka moto katika bandari ya Benghazi.

    Serikali ya Umoja wa Kitaifa (GNS) inayotawala mashariki mwa Libya ilisema meli hiyo ya Urusi, ambayo haikutajwa jina wala kutambuliwa rasmi, ilikuwa ikitumia bandari ya Benghazi chini ya makubaliano yaliyopo ya usafiri wa baharini.

    Soma pia:

  7. Tetesi za usajili Ulaya: Manchester United yamtaka Ivan Toney

    Manchester United inajiandaa kumsajili mshambuliaji wa Al-Ahli na timu ya taifa ya England, Ivan Toney, katika dirisha dogo la usajili la Januari.

    Hata hivyo, klabu nyingine za Ligi Kuu England pia zinamfuatilia mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 30. (

    Teamtalk) Arsenal na Chelsea zinaendelea kumfuatilia kwa muda mrefu kocha wa Como, Cesc Fabregas, kama mmoja wa warithi wa kiti cha ukocha wa timu zao katika siku zijazo. Fabregas aliwahi kuzichezea klabu zote mbili za London.

    (Football Insider) Beki wa Nigeria, Calvin Bassey, anahusishwa na uwezekano wa kujiunga na Manchester United. Hata hivyo, mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 26 amesema yuko kwenye mazungumzo na Fulham kuhusu kuongeza mkataba wake.

    (Standard) Kiungo wa Liverpool na timu ya taifa ya Argentina, Alexis Mac Allister, mwenye umri wa miaka 27, anatamani kusaini mkataba mpya wa kuendelea kubaki Anfield. Mazungumzo kati yake na klabu hiyo yameripotiwa kushika kasi.

    (Football Insider) Arsenal na Liverpool zina nia ya muda mrefu ya kumsajili kiungo wa Bayern Munich na timu ya taifa ya Ujerumani, Jamal Musiala, mwenye umri wa miaka 23.

    Klabu hizo zinaweza kujaribu kumnasa kutokana na kutokuwa na uhakika kuhusu mustakabali wake Bayern Munich. (Talksport) Paris Saint-Germain inaweza kuongeza kasi ya jitihada za kumsajili mshambuliaji wa Bournemouth, Eli Junior Kroupi, mwenye umri wa miaka 20, baada ya mshambuliaji mwenzake wa timu ya taifa ya Ufaransa, Desire Doue, 21, kupata jeraha kubwa la goti.

    (Teamtalk) Kipa wa Schalke 04, Loris Karius, amehusishwa na uwezekano wa kujiunga na Bayern Munich.

    Hata hivyo, kipa huyo wa Ujerumani mwenye umri wa miaka 33 amesema hajafanya mazungumzo na mtu yeyote kuhusu uwezekano wa kuhamia klabu nyingine.

    (Sky Sports Germany) AC Milan inaelekea kumpa kipaumbele mshambuliaji wa Real Madrid na timu ya taifa ya Brazil, Endrick, mwenye umri wa miaka 20, badala ya kujaribu kumsajili Nicolo Tresoldi, mshambuliaji wa Club Brugge mwenye umri wa miaka 22 ambaye pia ni mchezaji wa timu za vijana za Ujerumani. (Gazzetta dello Sport)

  8. Rais William Ruto na Tshisekedi wakubaliana kuimarisha uhusiano wa kikanda

    Rais William Ruto na mwenzake wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), Félix Tshisekedi, wamekubaliana kushirikiana kurejesha uhusiano wa kidiplomasia na kuimarisha ushirikiano kati ya nchi hizo mbili.

    Makubaliano hayo yalifikiwa hapo jana wakati wa Mkutano wa Kisiasa wa Ngazi ya Juu wa Nchi Nne uliofanyika mjini Oyo, Congo.

    Mkutano huo uliongozwa na Rais Denis Sassou N’Guesso wa Jamhuri ya Congo, huku Rais wa Baraza la Mawaziri la Togo, Faure Essozimna Gnassingbé, ambaye pia ni mpatanishi wa Umoja wa Afrika katika mzozo wa mashariki mwa DRC, akihudumu kama mpatanishi.

    Kuhusu uhusiano wa kidiplomasia, viongozi hao walikubaliana kushirikiana kurejesha uwakilishi wa kidiplomasia katika ngazi ya mabalozi, kuanzisha tena mashauriano ya mara kwa mara ya kisiasa na kuendeleza shughuli za Tume ya Pamoja ya Ushirikiano kati ya Kenya na DRC.

    Viongozi hao wawili pia waliahidi kuimarisha ushirikiano katika masuala ya amani na usalama wa kikanda, pamoja na kuimarisha muungano wa kikanda kupitia Mkutano wa Kimataifa wa Ukanda wa Maziwa Makuu (ICGLR) na Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC).

  9. Hujambo na karibu katika matangazo yetu ya moja kwa moja Jumatatu ya leo