Polisi
nchini Nigeria wanasema wamewakamata washukiwa wanne wa utekaji nyara wa watoto
tisa katika kanisa moja katikati mwa jimbo la Benue wiki moja iliyopita.
Watoto hao
waliachiliwa huru siku ya Jumamosi lakini haijafahamika iwapo waliachiwa na
watekaji wao, au waliachiwa wakati wa operesheni ya polisi.
Baadhi ya
ripoti zinasema, waliokolewa na maafisa wa usalama wa eneo hilo vikiwemo
vikundi vya ulinzi.
Waumini hao walitekwa nyara mnamo Februari 8 walipokuwa
wakisali katika Kanisa Katoliki la St John katika eneo la serikali ya mtaa ya
Ado katika jimbo la Benue.
Kumekuwa na matukio mengi ya utekaji nyara nchini Nigeria
na kusababisha uchunguzi wa kimataifa, hasa kutoka Marekani, juu ya hali mbaya
ya usalama katika nchi hiyo yenye watu wengi zaidi barani Afrika.
"Watoto waliookolewa, wanaojumuisha wasichana sita
na wavulana watatu, wanapokea matibabu na usaidizi," Solomon Iorpev,
mshauri wa gavana wa jimbo la Benue, alisema katika taarifa yake siku ya Jumamosi.
Benue ni sehemu ya eneo linaloitwa Ukanda wa Kati nchini
Nigeria, ambalo limeshuhudia mapigano kati ya wakulima na wafugaji kuhusu ardhi
na maliasili, pamoja na utekaji nyara unaofanywa na wahalifu wenye silaha.
Wakati tabia ya kulipa fidia kwa wateka nyara ni kinyume
cha sheria nchini Nigeria, serikali inashukiwa kulipa pesa taslimu mara kwa
mara.
Polisi hawakujibu mara moja ombi la AFP la kutoa maoni
yao.
Utekaji nyara huo uliibua hasira ya Marekani na Rais
Donald Trump alisema Wakristo wa Nigeria wanakabiliwa na mateso.
Serikali ya Nigeria na wataalamu walikanusha shutuma
hizo, wakisema kwamba migogoro mingi nchini humo inakumba Wakristo na Waislamu,
mara nyingi bila ubaguzi.
Kufuatia utekaji nyara huo, Rais wa Nigeria Bola Tinubu
alitangaza hali ya hatari mnamo mwezi Novemba na kuanzisha zoezi la kuwaajiri
wanajeshi na polisi zaidi.