Vita vya DRC vitamalizikaje?

Chanzo cha picha, Getty Images
Mkataba wa amani uliotiwa saini na Rais wa Rwanda Paul Kagame na Rais wa DRC Félix Tshisekedi mjini Washington chini ya usimamizi wa Rais wa Marekani Donald Trump tarehe 4 Desemba 2025, bado haujaweza kumaliza vita hivyo.
Miongoni mwa masharti ya mkataba huo ni kwamba Rwanda iondoe "mara moja" wanajeshi wake, wanaokadiriwa kufikia maelfu, kutoka mashariki mwa DRC. Mkataba huo pia unaitaka serikali ya DRC kudhoofisha uwezo wa kundi la waasi la FDLR.

Chanzo cha picha, Richard Moncrieff
Dkt. Richard Moncrieff, anayesimamia eneo la Maziwa Makuu katika taasisi huru ya utafiti wa migogoro ya International Crisis Group, aliiambia BBC Gahuza kuwa ingawa kunaonekana kuwa na utulivu katika mapigano, hali hiyo haimaanishi kwamba vita vimekwisha. Badala yake, anasema, pande zinazopigana zimebadilisha mbinu zao.
"Mabadiliko makubwa yaliyotokea mwaka wa 2026 ni kuongezeka kwa matumizi ya ndege zisizo na rubani na jeshi la Rwanda, M23 pamoja na jeshi la DRC."
Vita mashariki mwa DRC vilianza tena kwa nguvu takriban miaka mitano iliyopita kati ya jeshi la serikali ya nchi hiyo FARDC na waasi wa M23, ingawa mzozo huo umedumu kwa karibu miaka 30, ukikatizwa mara kadhaa na vipindi vya utulivu kabla ya kuanza tena.
Kwa sasa, M23 inadhibiti maeneo makubwa katika majimbo ya Kivu Kaskazini na Kivu Kusini, pamoja na miji ya Goma na Bukavu, ambayo ni miji mikuu ya majimbo hayo.
Mwezi Disemba mwaka wa 2025, siku chache baada ya Rwanda na DRC kutia saini mkataba wa amani, M23 pia iliteka mji wa Uvira, Kivu Kusini, kabla ya baadaye kuondoka kutokana na shinikizo la kimataifa lililoongozwa na Marekani.

Chanzo cha picha, Getty Images
Kinshasa na wataalamu wa Umoja wa Mataifa wanaishutumu Rwanda kwa kuunga mkono kundi la waasi la M23 kwa kuwapatia mafunzo ya kijeshi na silaha.
Rwanda imekanusha madai hayo. Kinshasa na Marekani zinaendelea kuitaka Rwanda kuondoa wanajeshi wake katika ardhi ya DRC.
Kwa upande mwingine, Kigali na ripoti za UN zinaishutumu serikali ya DRC kwa kushirikiana na FDLR, kundi la waasi linalopinga serikali ya Rwanda na linalofanya shughuli zake mashariki mwa DRC. Kinshasa inakanusha madai hayo, ikisema hakuna mpango wa serikali wa kushirikiana na FDLR.
Mwezi Julai mwaka huu, Kinshasa iliafikia makubaliano na FDLR, ambapo kundi hilo lilisema limekubali kuweka silaha chini kwa hiari kupitia kampeni za uhamasishaji badala ya kutumia nguvu
Makubaliano ya Kinshasa na FDLR
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Serikali ya Rwanda imelaani makubaliano hayo kati ya serikali ya DRC na FDLR. Katika ujumbe aliouchapisha kwenye mtandao wa X, Waziri wa Mambo ya Kigeni wa Rwanda Olivier Nduhungirehe alisema makubaliano hayo ni ya kuchochea mvutano na Kinshasa inawatumia kuchelewesha makubaliano.
Rwanda inalishutumu kundi hilo kwa kuhusika katika mauaji ya kimbari dhidi ya Watutsi mwaka 1994.
Msemaji wa FDLR Cure Ngoma aliiambia BBC kwamba, chini ya makubaliano yaliyoafikiwa na Kinshasa, kundi hilo liko tayari kurejea Rwanda. Alisema kundi hilo linakubali kwamba "uwajibikaji wa uhalifu ni wa mtu binafsi," na liko tayari kwa wanachama wake wanaotuhumiwa kushiriki katika mauaji ya kimbari kufikishwa mahakamani.
Baada ya hapo, alisema, kundi hilo litapigania masuala yake kupitia njia za kisiasa.
Dkt. Moncrieff anakubaliana kwamba "FDLR ina uhusiano wa wazi na wale waliohusika katika mauaji ya kimbari nchini Rwanda mwaka 1994," lakini anaongezea kuwa
"Uwezo wake wa kuidhuru na kuivuruga Rwanda ni mdogo sana. Ningesema pia kwamba Jenerali James Kabarebe alisema mwaka 2019 kwamba FDLR si tishio tena kwa Rwanda. Na kwa kiasi kikubwa nakubaliana naye."
"FDLR ina itikadi kali sana ya chuki dhidi ya Watutsi, lakini tishio lake ndani ya Rwanda ni mdogo sana."
"Rais wa Rwanda Paul Kagame alisema kwamba FDLR inashirikiana na jeshi la Congo, na hilo ni kweli. Lakini ushirikiano huo uliongezeka kuanzia mwaka 2021, ambao pia ndio mwaka Rwanda ilipopeleka M23 mashariki mwa DRC. Na nadhani jambo hili linaonyesha kwamba kupeleka makundi yenye silaha mashariki mwa DRC na kuyatumia kama njia ya kudhibiti eneo hilo kunaweza kunachochea changamoto zaidi badala ya kupata suluhisho."
Katika miaka iliyotangulia kabla kuzuka tena kwa vita, FARDC na Jeshi la Ulinzi la Rwanda (RDF) zilikuwa zikifanya operesheni za pamoja za kijeshi dhidi ya FDLR. Mwaka wa 2019, walimuua kiongozi wa wakati huo wa FDLR, Sylvestre Mudacumura.
Vita hivi vitamalizikaje?

Chanzo cha picha, Getty Images
Dkt. Moncrieff anasema ili vita viishe, kuna mambo yanayopaswa kufanywa na Rwanda, DRC, FDLR na M23.
Anasema kwamba, "Kumalizika kwa vita kunahitaji mchanganyiko wa Rwanda kuondoka au kuwaondoa wanajeshi wake, Kinshasa kutoa uhakikisho wa usalama kwa Rwanda kuhusu FDLR na masuala mengine ya mashariki mwa DRC, pamoja na kuvunjwa kwa M23. Pia kunaweza kuhitajika makubaliano kuhusu viongozi wake, ambao baadhi yao kwa sasa wamewekewa vikwazo au wamehukumiwa vifungo virefu au adhabu ya kifo nchini DRC. Haya yanaonekana kuwa vikwazo kwa amani. Kwa hiyo, mambo haya yanapaswa kujadiliwa."
Mchambuzi huyo anasema vikwazo vikali ambavyo Marekani imeiwekea jeshi la Rwanda na baadhi ya maafisa wake wa ngazi za juu, "kwa sasa havijaonekana kuwa na athari yoyote kwenye uuzaji wa silaha kwa RDF au programu za mafunzo."
Hata hivyo, anaongeza kwamba "kuiwekea vikwazo jeshi zima ni jambo ambalo, kwa muda mrefu, linaweza kuwa na athari."
"Kwa hiyo, kwa sasa athari si kubwa sana, lakini lazima tukubali kwamba kuiwekea vikwazo jeshi zima ni jambo la kipekee kabisa."
Mazungumzo ya Doha yamefikia wapi?
Ingawa Jacques Kongolo Bigirumwami, mshauri wa Rais Felix Tshisekedi, aliiambia BBC kwamba M23 haipaswi kuwa sehemu ya mazungumzo ya kitaifa ambayo rais alikubali kushiriki mwezi uliopita, Dkt. Moncrieff anasema "M23 inapaswa kuwa sehemu ya mazungumzo ya kitaifa kwa kiwango ambacho inawasilisha madai ya masuala ya kitaifa."
"Lakini mapigano mashariki mwa DRC yanaweza kutatuliwa tu kati ya Kinshasa na Kigali, kwa sababu Kigali ina udhibiti kamili wa M23 na ndiyo inayoipa maagizo."
Mazungumzo ya hivi karibuni ya amani kati ya serikali ya DRC na M23 yalifanyika Montreux, Uswizi, kuanzia tarehe 17 hadi 21 Agosti mwaka huu, yakifuatia mazungumzo yaliyofanyika mwezi Aprili.
Katika mazungumzo hayo ya hivi karibuni, pande hizo mbili zilikubaliana kwamba zingechukua hatua ya kwanza ya kufuatilia utekelezaji wa makubaliano ya kusitisha mapigano huko Minembwe, katika jimbo la Kivu Kusini.
Pande zote mbili zimeshutumiwa kutumia ndege zisizo na rubani katika eneo linalokaliwa na jamii ya Wanyamulenge, madai ambayo wamekanusha
Dkt. Moncrieff anasema kuwa "Kinachowatokea Wanyamulenge kwa kweli kinatia wasiwasi mkubwa."
"Itakuwa vigumu sana kutatua masuala kama haya ambayo suluhisho lake la muda mrefu na endelevu linategemea mahusiano mazuri kati ya jamii mbalimbali za Wakongo "
"Kwa hiyo, nadhani Kigali na Kinshasa zote zinafanya kosa kubwa sana kwa kutumia silaha za kivita kujaribu kutatua matatizo ya jamii."
Dkt. Moncrieff anasema anaona mchakato wa upatanishi unaoongozwa na Qatar unakaribia kufikia mwisho, kwa sababu "Doha haijaweza kuzifanya pande muhimu zinazohusika katika vita kusonga mbele kutoka kwenye misimamo yao mikali"
Qatar inatafuta kukabidhi mchakato huo wa upatanishi kwa Uswizi.















