Mabeki wa siku hizi sio wazuri kama ilivyokuwa wakati wangu - Rooney

Iliyochapishwa
Muda wa kusoma: Dakika 5

Mshambulizi wa zamani wa Manchester United na Uingereza Wayne Rooney amecheza dhidi ya mabeki wa viwango vya juu wakati wake.

Akiwa amekaa kwa miaka 13 kwenye kikosi cha United ambacho kilikuwa na mafanikio ndani ya Ulaya, Rooney alikutana na mabeki bora wa kati barani humo.

Lakini katika toleo la hivi punde la podikasti ya BBC The Wayne Rooney Show, fowadi huyo anasema mabeki wa leo hawalingani na wale aliokumbana nao katika maisha yake ya soka ya miaka 19.

"Katika miaka hii ya sasa , mabeki wa kati hawako sawa na wale niliocheza nao," mchezaji huyo wa miaka 39 alisema.

Kati ya kizazi cha wachezaji wa sasa wa Premier League, anawataja William Saliba wa Arsenal na Gabriel kama mabeki bora.

"Saliba na Gabriel wanashirikiana vizuri sana," alisema.

"Unaweza kuwaona wanaongoza na kuzungumza, ndivyo unachohitaji, unahitaji wazungumzaji na viongozi kama mabeki wa kati.

"Je, ningewaweka katika kiwango sawa na wachezaji ambao nimecheza dhidi yao? Hapana singefanya. Lakini wanaweza kuwa wachezaji bora zaidi wakati huu."

Saliba alisaini mkataba mpya na The Gunners wiki hii na Rooney anasema ni hatua "kubwa" kwamba meneja Mikel Arteta ameweza kumbakisha Mfaransa huyo.

"Hiyo inasaidia na labda wachezaji wengine watafuata nyayo na wachezaji wataingia Januari na msimu ujao wa joto," alisema.

"Unapojua kuna utulivu, hiyo inasaidia kila mtu."

Katika kipindi cha hivi punde zaidi cha podikasti hiyo, Rooney anaorodhesha mabeki watano bora ambao amekutana nao.

Hakuwa na haraka ya kuwasifu wachezaji wawili wa Manchester United Rio Ferdinand na Nemanja Vidic na kusema wote wawili wangejumuishwa kwenye orodha yake ya jumla ya mabeki watano bora.

Lakini orodha hii inajumuisha wachezaji watano bora aliocheza dhidi yao kwenye Ligi ya Mabingwa.

5. Alessandro Nesta

Rooney alisema: "Tulicheza dhidi yake mwaka wa 2007 kwenye Ligi ya Mabingwa. Alikuwa mwerevu sana, kila mara alikuwa akiangalia anachokifanya, anaweza kuwa mbaya pia.

"Tulicheza na AC Milan pale Old Trafford katika mechi ya mkondo wa kwanza. Baada ya dakika 10 nilimsikia akipumua kwa nguvu nyuma yangu na 'nilidhani nimempata, hajamaliza dakika 90'. Alifanikiwa kupita dakika hizo - lakini nilifunga dakika ya mwisho [ United ikishinda 3-2].

"Lakini katika mechi ya mkondo wa pili - na sababu kubwa iliyonifanya nimuorodheshe - alikuwa mchezaji tofauti kabisa, asiyepumua sana, na kuhema.

"Tulipoteza 3-0... Nilihisi tumepiga hatua kubwa kama timu lakini [AC Milan] ilikuwa timu ya ajabu - na hilo lilikuwa funzo la kweli kwetu."

4. Ricardo Carvalho

Alichokisema Rooney: "Ni vigumu kucheza dhidi ya, kiongozi mwenye uzoefu, mwenye akili katika namna alivyonifanya nipewe kadi nyekundu kwenye Kombe la Dunia [mwaka 2006].

"Alikuwa amejipanga, alikuwa anaweza kuruka juu kwa kichwa na alikuwa mzuri katika kukaba. Labda alisahaulika kwa sababu ya John Terry pale Chelsea.

"Lakini Carvalho alikuwa sehemu kubwa ya mafanikio ya Chelsea. Alikuwa 'mchafu' pia. Kulikuwa na kiungo muhimukati ya wachezaji niliowachagua. Wote walikuwa wajanja na werevu."

3. Paolo Maldini

Alichokisema Rooney: "Nilikuwa nikimwangalia ana alikuwa mchezaji mashuhuri. Nilipokuja dhidi yake pengine ilikuwa mara moja pekee ambayo nilishangaa uwanjani. Alikuwa na akili sana.

"Nilichopenda sana alikuwa anaelewa jinsi mchezo ulivyokuwa ukiendelea, alipokuwa anazungumza na wachezaji wenzake unaona wanamsikiliza, alikuwa na kipaji hicho juu yake.

"Ulinzi wake, usomaji wake wa mchezo, unafikiri umempita, lakini angejiweka katika nafasi nzuri zaidi."

2. Gerard Pique

Alichokisema Rooney: "Mchezaji niliyecheza naye na dhidi yake. Alikuwa kijana mdogo huko Manchester United lakini hakupewa heshima aliyostahili. Hakuwa mwepesi zaidi lakini alijiweka kwenye nafasi nzuri sana kukabiliana na hilo.

"Uwezo wake wa kucheza mpira ulikuwa mzuri kama beki yeyote utakayemuona katika suala la kupiga pasi na kuanza mashambulizi.

"Alikuwa mshindi, mhusika mkuu, mwenye furaha kuwa karibu naye wakati tunacheza. Shida yake United ilikuwa wakati alipopitia, kiufundi alikuwa mzuri lakini swali lilikuwa je, ana nguvu ya kimwili kucheza katika ligi ya Uingereza

"Alikuwa akilinganishwa na Jonny Evans, sote tulihisi wakati huo Jonny alikuwa mchezaji bora na alikuwa anafaa zaidi kwa Ligi ya Premia. Meneja alimzuia Jonny na kumruhusu Gerard kurejea Barcelona. Sidhani yeyote kati yetu angeweza kufikiria kiwango cha mchezo alichoonesha alipoondoka ."

1. John Terry

Alichosema Rooney: "Bila shaka ni bora. Alikuwa imara kucheza dhidi yake. Akizungumzia viongozi, alikuwa nahodha mzuri wa England nilipocheza naye.

"Jinsi alivyojilinda, alikuwa hodari, mzuri angani, alicheza rafu, alikuwa tishio kwa wachezaji.

"Alikuwa ni mmoja wa mabeki ambao ukimsogelea alikuwa anakuumiza tu, hakukusudia ila alikuwa anakuachia kitu kila mara.

"Sidhani kama watu wanampa sifa anayostahili, alikuwa mzuri kwa miguu yote miwili."

Imetafsiriwa na Seif Abdalla