Tundu Lissu awauliza maswali mashahidi waliofichwa
Kesi ya kiongozi wa chama cha CHADEMA nchini Tanzania Tundu Lissu imeendelea leo kwa ushahidi kutolewa. Baadhi ya wafuasi wake walikuwepo mahakamani kufuatilia kesi hiyo.
Muhtasari
- Wanajeshi wa Marekani wawasili Nigeria
- Arsenal yamtangaza Saka kuwa mchezaji anayelipwa zaidi
- Mazungumzo ya nyuklia kati ya Marekani na Iran yamalizika Geneva
- Duru ya tatu ya mazungumzo kati ya Urusi na Ukraine yaanza Geneva
- Kesi ya uhaini ya Tundu Lissu yaahirishwa hadi kesho
- Kwa nini unatoa ushahidi ukiwa umejificha kwenye mbao?
- Waeleze majaji kama unafahamu maana ya neno kunuka - Tundu Lissu
- Tundu Lissu aanza kumuhoji Shahidi P4
- Wakili wa serikali Renatus Mkude anaendelea kumhoji shahidi PW9
- Wakili wa serikali Renatus Mkude anaanza kumhoji shahidi PW9
- Kesi ya Kiongozi wa chama cha CHADEMA Tundu Lissu imeanza
- Wanajeshi wa zamani Zimbabwe wapinga ubadilishaji katiba kuongeza muhula wa urais
- Urusi yajibu ripoti za kurekodi video za ngono za wanawake wa Ghana na Kenya
- Nigeria yasema imepokea wanajeshi 100 zaidi wa Marekani kukabiliana na waasi wa Kiislamu
- Mwaka Mpya wa Kichina: Mwaka wa Farasi wa Moto
- Trump anaamini Iran inataka kufanya makubaliano kuhusu mpango wake wa nyuklia
- Ukraine inagandisha mbegu za kiume za wanajeshi
- Hillary Clinton aishutumu serikali ya Trump kwa kuficha ukweli juu ya faili za Epstein
Moja kwa moja
Asha Juma & Rashid Abdallah
Wanajeshi wa zamani Zimbabwe wapinga ubadilishaji katiba kuongeza muhula wa urais

Chanzo cha picha, Getty Images
Rais wa Zimbabwe anakabiliwa na pingamizi la kisheria kutokana na azma yake ya kuongeza muda wake madarakani.
Kundi la wanajeshi wa vita vya ukombozi wa nchi hiyo wamefungua shauri mahakamani kuzuia serikali kufanya marekebisho ya katiba ili kuongeza ukomo wa mihula ya urais na bunge kutoka miaka mitano hadi saba.
Haya ni baada ya serikali ya Zimbabwe kutoa taarifa rasmi kuthibitisha mpango wake wa kubadili katiba ya nchi ili kuongeza muda wa uongozi wa Rais wa sasa Emmerson Mnangagwa, jambo linalochukuliwa kama lenye nia ya kusambaratisha uchaguzi unaotarajiwa kufanyika mwaka wa 2028.
Mapendezo hayo ambayo yaliwasilishwa na kuidhinishwa na bunge wiki iliyopita yananuia kuongeza muda wa urais na ubunge hadi mwaka wa 2030.
Bwana Mnangagwa alishinda muhula wake wa pili na wa mwisho wa urais mwaka 2023 katika uchaguzi ambao waangalizi wa kimataifa walisema ulikuwa na mapungufu makubwa.
Rais pia kwenye mabadiliko hayo atachaguliwa na wabunge kinyume na awali ambapo rais anafaa kuchaguliwa na raia.
Hii inapingana na mfumo wa kidemokrasia unaohitaji wananchi kushiriki moja kwa moja katika uchaguzi, jambo ambalo limeibua wasiwasi mkubwa wa kisiasa.
Kwa mujibu wa sheria ni kwamba mapendekezo hayo lazima yapigiwe kura ya maoni - hata hivyo serikali inasema umma watapata siku 90 kutoa maoni yao.
Urusi yajibu ripoti za kurekodi video za ngono za wanawake wa Ghana na Kenya

Chanzo cha picha, Getty Images
Serikali ya Urusi imekiri ripoti kwamba mwanamume mmoja raia wa Urusi anadaiwa kurekodi matukio ya mapenzi ya wanawake aliokuwa amewarubuni katika nchi nyingi za Afrika na kuweka video zao mtandaoni bila ridhaa yao.
Ghana inasema inataka mshukiwa arejeshwe nchini humo ili haki ipatikane - lakini Moscow bado haijasema kama itatoa ushirikiano katika hilo.
Katika taarifa fupi, Ubalozi wa Urusi mjini Accra ulithibitisha tu kwamba "unazingatia" madai hayo.
Haikutoa dalili yoyote kama Urusi ingeunga mkono ombi la Ghana la kurejeshwa nchini humo - hatua inayochukuliwa kuwa isiyowezekana, kwani ni nadra Moscow kuwakabidhi raia wake.
Kenya imeanzisha uchunguzi wa mashirika mbalimbali na inashirikiana na washirika wa kimataifa, ikielezea kisa hicho kama uhalifu wa kuvuka mpaka unahitaji kuchukuliwa kwa hatua za haraka.
Mamlaka zote za Ghana na Kenya zimeshutumu rekodi hizo, na kuzitaja kuwa za kutatanisha, za ukatili na ukiukaji mkubwa wa haki za wanawake.
Soma zaidi:
Nigeria yapokea wanajeshi 100 zaidi wa Marekani kukabiliana wanamgambo wa kijihadi

Chanzo cha picha, Reuters
Nigeria inasema takriban wanajeshi 100 wa Marekani wamewasili nchini humo kusaidia kutoa mafunzo kwa wanajeshi wake.
Nigeria iliomba usaidizi wa mafunzo, kiufundi na ushirikiano wa kijasusi baada ya Rais wa Marekani Donald Trump kuishutumu kwa kushindwa kuwalinda Wakristo dhidi ya mashambulizi kijihadi.
Msemaji wa ulinzi wa Nigeria amesema takriban wanajeshi 100 wa Marekani wamewasili nchini Nigeria huku Marekani ikiimarisha operesheni ya kuwalenga waasi wa Kiislamu.
Rais Trump ameishutumu Nigeria kwa kushindwa kuwalinda Wakristo dhidi ya wanamgambo wenye itikadi kali za kidini kaskazini magharibi mwa nchi hiyo.
Hata hivyo, Nigeria imekanusha kubagua dini yoyote ikisema vikosi vyake vya usalama vinalenga makundi yenye silaha ambayo yanashambulia waumini wa pande zote mbili - Wakristo na Waislamu.
Soma zaidi:
Mwaka Mpya wa Kichina: Mwaka wa Farasi wa Moto

Chanzo cha picha, Tran Dinh Duc Hieu
Sherehe za mwaka mpya maarufu Lunar year zimeanza kuadhimishwa nchini China, Vietnam, Korea kusini na maeneo mengine bara Asia.
Katika maadhimisho hayo, huu unatajwa kuwa mwaka wa ‘Farasi wa Moto’ kuashiria uhai, matumaini na imani.
Picha za nyoka zikionyesha farasi angani zimeonekana katika mataifa mengi bara Asia huku sherehe hizi zikiadhimishwa na familia na marafiki.
Mwaka mpya wa China unaoandamana na mwezi mpya, katika kalenda ya Lunar, huadhimishwa kati ya tarehe 21 Januari hadi tarehe 20 Februari kila mwaka, na sherehe hizo hudumu kwa siku 15.

Chanzo cha picha, Getty Images
Sherehe hii hutajwa kuwa muhimu kwa jamii za mataifa ya bara Asia, siku za kwanza mbili za sherehe hizi, familia huja pamoja kula, kupeana zawadi na bahasha nyekundu zilizojaa pesa.
Pia unaweza kusoma:
Trump anaamini Iran inataka kufanya makubaliano kuhusu mpango wake wa nyuklia

Chanzo cha picha, EPA
Rais wa Marekani Donald Trump amesema kwamba atahusika kwa njia isiyo ya moja kwa moja katika mazungumzo ya hali ya juu kati ya Iran na Marekani kuhusu mpango wa nyuklia wa Tehran uliopangwa kufanyika leo siku ya Jumanne huko Geneva, akiongeza kuwa anaamini Iran inataka kufanya makubaliano.
"Nitahusika katika mazungumzo hayo, kwa njia isiyo ya moja kwa moja. Na yatakuwa yenye umuhimu sana," Trump aliwaambia waandishi wa habari ndani ya Air Force One.
Mvutano unaongezeka kabla ya mazungumzo, huku Marekani ikiendelea kupeleka meli na ndege za kivita Mashariki ya Kati.
Maafisa wa Marekani wameiambia Reuters kuwa wanajeshi wa Marekani wanafanya maandalizi ya iwapo mazungumzo hayatafanikiwa.
Alipoulizwa kuhusu matarajio ya makubaliano, Trump alisema Iran kwa muda mrefu imekuwa na msimamo mgumu katika mazungumzo ila imepata funzo kutokana na matokeo msimu uliopita wa kiangazi wakati Marekani iliposhambulia na kulipua maeneo ya nyuklia ya Iran.
Trump alisema Iran ilihamasishwa wakati huu kufanya mazungumzo.
"Sidhani kama wanataka matokeo ya kutofanya makubaliano," Trump aliongeza.
Kabla ya mashambulizi ya Marekani mnamo mwezi Juni, mazungumzo ya nyuklia ya Marekani na Iran yalikuwa yamekwama kwa madai ya Marekani kwamba Iran iachane na mpango wa urutubishaji madini, ambayo Marekani inaiona kama njia ya Iran kufikia kutengeneza silaha ya nyuklia.
"Tungeweza kuwa na makubaliano badala ya kutuma ndege ya kivita ya B-2s kuharibu uwezo wao wa nyuklia. Na tulilazimika kutuma B-2s,"
Trump alisema, akimaanisha ndege za kivita za Marekani zenye mabawa
Kwa upande wake, wizara ya mambo ya nje ya Iran ilisema Marekani imeelekea kwenye "msimamo wa kweli zaidi" kuhusu mazungumzo ya mpango wa nyuklia wa Tehran.
Soma zaidi:
Ukraine inagandisha mbegu za kiume za wanajeshi

Ukraine iliyokumbwa na vita imeanzisha mpango unaofadhiliwa na serikali unaowaruhusu wanajeshi kugandisha mbegu zao za kiume, huku nchi hiyo ikikabiliwa na tatizo la idadi ndogo ya watu kutokana na uvamizi wa Urusi.
Chini ya mpango huo, wanajeshi wa Ukraine wanaweza kuhifadhi mbegu za kiume bila malipo, na kuwapa wenzi wao chaguo la kupata watoto katika siku zijazo ikiwa wanajeshi watafariki dunia au wakiwa na msongo wa mawazo ama pengine wanapopata jeraha la muda mrefu lenye kuathiri uzazi wao.
Maxim hana shida kujadili suala la mbegu zake za kiume. Ukweli ni kwamba, anatamani kama kuna mengi zaidi ambayo yangefanywa katika jeshi la Ukraine na kuzungumza kuhusu uwezo wao wa kuzaa.
"Wanaume wetu wanafariki dunia. Kikosi cha Ukraine kinakufa. Hili linahusu kunusuru taifa letu," mwanajeshi huyo amesema akizungumza kwa simu kutoka mahali fulani karibu na eneo la kivita la mashariki.
Mwanaume huyo mwenye umri wa miaka 35 anahudumu katika Jeshi la Walinzi wa Kitaifa la Ukraine na aliporudi likizoni hivi karibuni mkewe alimshawishi aende kliniki huko Kyiv na kuacha sampuli ya mbegu za kiume.
Yaligandishwa bila malipo kama sehemu ya mpango wa kuwasaidia wanajeshi walioko vitani.
Ikiwa Maxim atauawa, mkewe ataweza kutumia sampuli hiyo kujaribu kupata mtoto ambaye wamekuwa wakimtaka kila wakati.
Lakini anasema mbegu zake zilizogandishwa zinaweza kuwa muhimu katika kuwa na familia, kwa vyovyote vile.
"Iwe uko sahihi kwenye 'nukta sifuri' vitani, au kilomita 30 au hata 80 nyuma, hakuna uhakika kwamba uko salama," mwanajeshi huyo anasema, akielezea kwamba ndege zisizo na rubani za Urusi zinazoruka juu kidogo tu ni tishio la kila mara.
"Hiyo ina maana ya msongo wa mawazo, na hii [inaweza] kuwa na athari: uwezo wako wa kuzaliana ukapungua. Kwa hivyo tunapaswa kufikiria kuhusu mustakabali wa taifa letu la Ukraine."
Kliniki za uzazi za kibinafsi zilianza kutoa kile kinachojulikana kama uhifadhi wa mbegu za kiume kwa wanajeshi wanaume na wanawake mnamo mwaka 2022 mwanzoni mwa uvamizi wa Urusi.
Waliweza kugandisha mbegu au mayai yao bure iwapo wangejeruhiwa vitani au uwezo wao wa kuzaliana uwathirike.
Mwaka uliofuata bunge liliingilia kati kudhibiti utaratibu huo na kuondoa ufadhili wa serikali.
"Wanajeshi wetu wanatetea mustakabali wetu, lakini wanaweza kupoteza wao wenyewe, kwa hivyo tulitaka kuwapa nafasi hiyo," ndivyo Mbunge Oksana Dmitrieva anavyoelezea sheria aliyosaidia kuiandika.
"Ni kwa ajili ya kuwasaidia, ili waweze kutumia mbeguza kiume baadaye."
Soma zaidi:
Hillary Clinton aishutumu serikali ya Trump kwa kuficha ukweli juu ya faili za Epstein

Waziri wa zamani wa mambo ya nje wa Marekani, Hillary Clinton, ameishutumu serikali ya Rais Donald Trump kwa "kuficha ukweli" kuhusu jinsi ilivyoshughulikia faili zinazohusiana na marehemu Jeffrey Epstein, mhalifu wa ngono.
"Zitoe faili hizo. Wanapeleka jambo hili polepole," waziri huyo wa zamani wa mambo ya nje wa Marekani aliambia BBC huko Berlin, ambapo alihudhuria Kongamano la Dunia la kila mwaka.
Ikulu ya White House ilisisitiza kwamba kwa kutoa faili hizo walikuwa wamewafanya jambo kubwa "zaidi kwa waathiriwa kuliko kile ambacho Democrats imewahi kufanya".
Alipoulizwa ikiwa Andrew Mountbatten-Windsor anapaswa kuwasilisha kesi mbele ya kamati ya bunge, Hillary Clinton alisema: "Nadhani kila mtu anapaswa kutoa ushahidi kwa anayeombwa kutoa ushahidi."
Kuonekana kwenye faili si dalili ya kutenda makosa. Andrew amekuwa akikanusha kufanya makosa yoyote.
Mamilioni ya faili mpya zinazohusiana na Epstein ziliwekwa hadharani na idara ya sheria ya Marekani mapema mwezi huu baada ya Bunge kupitisha sheria inayoitaka Idara hiyo kutoa taarifa zinazohusiana na uchunguzi wa Epstein.
Bi Clinton na mumewe, rais wa zamani Bill Clinton, wamekubali kutoa ushahidi katika uchunguzi wa bunge kuhusu mhalifu wa kingono marehemu Epstein.
Bill Clinton atafika tarehe 27 Februari, na Hillary Clinton atafika siku iliyotangulia.
Rais Trump amekanusha mara kwa mara kufanya makosa na kusema aliachana na Epstein miaka mingi iliyopita.
Bill Clinton - ambaye ametajwa mara kadhaa katika faili za Epstein - alikuwa akimfahamu Epstein, ambaye alifariki gerezani mwaka wa 2019, lakini anasema alikata mawasiliano miongo miwili iliyopita.
Soma zaidi:
Hujambo. Karibu katika matangazo yetu mubashara ya 17/02/2026.
