Iran: Hakuna hatua iliyopigwa kufufua makubaliano ya muda ya amani na Marekani
Chanzo hicho kimesema hakuna hatua iliyofikiwa katika mazungumzo ya kufufua makubaliano ya muda ya mwezi Juni.
Muhtasari
- Wanajeshi 82 wa Mali waliokuwa wakishikiliwa mateka waachiliwa huru
- Mwanamume,102, ashambuliwa baa na kufariki dunia
- Uingereza yatetea kukamata meli ya mafuta ya Urusi kufuatia tishio la Putin
- Wazambia waendelea kupiga kura katika uchaguzi mkuu wenye ushindani mkubwa
- Nigeria na Marekani zajadili namna ya kupambana na ugaidi
- Ziara ya Putin katika visiwa vinavyozozaniwa 'haikubaliki' - Japan
- Balozi wa Ufaransa nchini CAR akabiliwa na hatua za kinidhamu
- Iran: Hakuna hatua iliyopigwa kufufua makubaliano ya muda ya amani na Marekani
- Israel yashambulia Ukingo wa Magharibi
- Sura ya Haaland yatumika kuuza kokeini huko Ecuador
- Rais Ruto asema katiba mpya iwe msingi wa Dira ya Kenya 2060
- Askari watatu washikiliwa kufuatia kifo cha mtu mmoja katika hifadhi ya Ngorongoro
- Madaktari Uganda waipa serikali siku 14 kushughulikia maslahi ya madaktari wanafunzi
- Inspekta Jenerali aagiza polisi wasimamishwe kazi kila mtuhumiwa akifariki kizuizini Kenya
- Israel yapeleka wanajeshi zaidi katika kijiji ambako familia za Palestina zimezingirwa
- Mamlaka ya ICE yapanga kuwapatia maafisa glovu zinazoweza kutoa mshtuko wa umeme
- Caroline Levitt kujiuzulu kama msemaji wa Ikulu ya Marekani - Trump
- Serikali ya Uingereza yaonya kuhusu athari za kufungwa kwa Mlango wa Hormuz kwa uchumi
- Marekani na Iran zatoa madai kinzani kuhusu udhibiti wa Mlango wa Hormuz
Moja kwa moja
Na Mariam Mjahid, Asha Juma na Sarafina Robi
Wanajeshi 82 wa Mali waliokuwa wakishikiliwa mateka waachiliwa huru

Chanzo cha picha, AFP via Getty Images
Mali imesema kuwa wanajeshi wake 82 waliokuwa wakishikiliwa mateka tangu mwezi Aprili wameachiwa huru.
Washirika wa al-Qaeda katika eneo hilo, Jama'at Nusrat al-Islam wal-Muslimin (JNIM), na kundi la waasi linaloongozwa na kabila la Tuareg, Azawad Liberation Front (FLA), vilidai kuhusika na mashambulizi ya tarehe 25 Aprili, ambayo yalilenga uwanja mkuu wa ndege na kusababisha kifo cha waziri wa ulinzi.
Jeshi lilisema katika taarifa yake kuwa wanajeshi hao walikuwa "wakishikiliwa mateka" na "makundi ya kigaidi yaliyojihami yanayoshirikiana na muungano wa JNIM-FLA".
"Kuachiwa huru huku... ni matokeo ya mipango madhubuti na uhamasishaji ulioratibiwa wa rasilimali na uwezo unaohitajika kutekeleza operesheni ya aina hii," taarifa hiyo ilisema.
Makundi hayo mawili pia yalidai kuhusika na mashambulizi dhidi ya ngome za jeshi kote nchini Mali mnamo tarehe 4 Julai.
Mali imekuwa ikikabiliana na uasi tangu mwaka 2012. Kundi la JNIM, ambalo lilianzishwa mwaka 2017, limezidi kuimarika tangu wanajeshi wa Mali waliochukua madaraka katika mapinduzi ya mwaka 2020 na 2021 walipofukuza takriban wanajeshi 15,000 wa Ufaransa na Umoja wa Mataifa na kugeukia mamluki wa Urusi kwa ajili ya msaada wa kiulinzi.
Pia unaweza kusoma:
Mwanamume,102, afariki dunia kwa madai ya kushambuliwa katika baa

Mwanamume mwenye umri wa miaka 102 amefariki dunia baada ya kudaiwa kushambuliwa katika baa moja kusini mwa Wales.
Phillip Ormerod, kutoka Cwmbran, Torfaen, alipelekwa hospitalini akiwa katika hali mbaya kufuatia tukio hilo lililotokea tarehe mosi Agosti.
Polisi wa Gwent walithibitisha siku ya Alhamisi kwamba alikuwa amefariki dunia.
Mwanamume mwenye umri wa miaka 56 kutoka Llanelli, Carmarthenshire, alikamatwa kwa tuhuma za kusababisha jeraha kubwa la mwili, na anaendelea kuchunguzwa.
Huduma za dharura ziliitwa katika baa hiyo majira ya saa 22:25 BST kufuatia ripoti ya shambulio.
Mkaguzi Mkuu wa Upelelezi Shelley Comley, afisa mkuu wa upelelezi wa Polisi wa Gwent, alisema, "Tunaelewa kuwa umma wana shauku kubwa kuhusu tukio hili, lakini tunataka kuwakumbusha watu kwamba si tu uchunguzi huu wa jinai bado unaendelea, bali pia kuna familia inayokabiliana na maumivu ya kumpoteza mpendwa wao."
Jeshi la polisi linatoa wito kwa yeyote aliyekuwepo katika baa hiyo kati ya saa 22:00 na 23:00 usiku wa tukio hilo kuwasiliana nao.
Uingereza yatetea kukamata meli ya mafuta ya Urusi kufuatia tishio la Putin

Chanzo cha picha, Ministry of Defence
Serikali ya Uingereza imetetea hatua yake ya kukamata meli ya mafuta ya Urusi iliyokuwa ikiendeshwa kisiri katika Mfereji wa Uingereza, baada ya Rais wa Urusi Vladimir Putin kutishia "kuchukua hatua sawia na hiyo".
Meli ya Smyrtos imetia nanga karibu na Weymouth baada ya vikosi vya Royal Marines kuizuia na kuingia kwenye meli hiyo katika operesheni ya kwanza ya aina yake ya kuzuia meli hiyo iliyowekewa vikwazo mnamo mwezi Juni.
Nahodha wa meli hiyo, Ajay Pant, amefunguliwa mashtaka kwa kukiuka vikwazo dhidi ya Urusi, akituhumiwa kupeleka au kuwasilisha moja kwa moja au kwa njia isiyo ya moja kwa moja mafuta ya Urusi yaliyopigwa marufuku.
Akisimamia mazoezi ya jeshi la majini la Urusi katika Bahari ya Pasifiki, Putin alizikemea nchi za Magharibi kwa "kukamata meli zetu", akiitaja hatua hiyo kuwa "si kitu kingine isipokuwa uharamia na ujambazi".
Mataifa ya Magharibi yanadai Urusi imekuwa ikiendesha "meli kwa njia ya siri" ili kukwepa vikwazo vya kimataifa vilivyowekwa kwa usafirishaji wake wa mafuta.
Meli hizi zinashutumiwa kutumia miundo tata ya umiliki na mbinu mbalimbali kuficha asili ya shehena yao, na kuficha uhusiano wao na Urusi.
Wizara ya Ulinzi ya Uingereza inasema Urusi ina meli zaidi ya 700, zinazohusika na kubeba 75% ya mafuta yaliyoidhinishwa nchini humo.
Pia unaweza kusoma:
Wazambia waendelea kupiga kura katika uchaguzi mkuu wenye ushindani mkubwa

Uchaguzi mkuu wa Zambia unaendelea, huku zaidi ya wapiga kura milioni 8.8 waliojiandikisha wakichagua rais, wabunge na viongozi wa serikali za mitaa.
Ingawa kuna wagombea 14 kwenye karatasi ya kupiga kura, ushindani mkubwa unaonekana kuwa kati ya Rais aliye madarakani Hakainde Hichilema na mgombea wa upinzani Brian Mundubile.
Je, Hichilema atapata muhula wa pili, au Mundubile ataibuka na ushindi wa kushtukiza?
Nigeria na Marekani zajadili namna ya kupambana na ugaidi

Chanzo cha picha, Getty Images
Nigeria na Marekani zimeanza mazungumzo huku masuala ya kupambana na ugaidi, kubadilishana taarifa za kijasusi, na ushirikiano wa kijeshi yakipewa kipaumbele kutokana na ukubwa na utata wa hali ilivyo nchini Nigeria.
Mazungumzo hayo yalianza siku ya Jumatano yakiongozwa kwa pamoja na Kikosi Kazi cha Pamoja cha Nigeria na Marekani kuhusu Ushirikiano wa Usalama, kikiongozwa na Mshauri wa Usalama wa Taifa wa Nigeria, Nuhu Ribadu, na Naibu Katibu wa Mambo ya Nje wa Marekani anayeshughulikia Masuala ya Kisiasa, Allison Hooker.
Mbali na Ribadu, wajumbe wengine wa ujumbe wa Nigeria ni pamoja na Waziri wa Mambo ya Nje Bianca Odumegwu-Ojukwu, Waziri wa Ulinzi Christopher Musa, na Waziri wa Mambo ya Ndani Olubunmi Tunji-Ojo. Pia, mashauriano ya nchi hizo mbili kuhusu sera ya ulinzi yamepangwa kufanyika leo.
Hali ya usalama nchini Nigeria inaonekana kuwa jambo la wasiwasi mkubwa kwa mataifa yote mawili kutokana na changamoto zinazoikabili nchi hiyo, zikiwemo vitendo vya uhalifu wa kutumia silaha, utekaji nyara, na uporaji unaoendelea katika maeneo ya kaskazini magharibi na katikati mwa nchi.
Aidha, kuna hali tete kaskazini mashariki mwa Nigeria, ambapo makundi ya Boko Haram na ISWAP (tawi la ISIS) yanatishia usalama wa raia na sekta ya usalama ya Nigeria. Hali hii inachochewa zaidi na changamoto za usalama katika eneo la Sahel, ambazo nazo zinatishia hali ya utulivu Nigeria.
Changamoto za usalama nchini Nigeria zinaonekana kuchangia ukosefu wa utulivu katika eneo hilo, huku wapiganaji wenye itikadi kali na wahalifu wakitumia fursa ya udhaifu wa utawala katika maeneo ya kaskazini mashariki na kaskazini magharibi mwa nchi hiyo.
Hata hivyo, operesheni za kijeshi zilizofanikiwa hivi karibuni zilizopelekea kuokolewa kwa mateka zaidi ya 300 na kuachiwa huru kwa watu 33 waliotekwa nyara katika Jimbo la Zamfara, zinaweza kuashiria juhudi na uzito unaowekwa na serikali ya Nigeria katika kudhibiti hali hiyo.
Marekani na Nigeria zinaelewa umuhimu wa kuongeza ushirikiano katika kubadilishana taarifa za kijasusi na kupambana na ugaidi pamoja na uasi nchini Nigeria, kabla hali hiyo haijazidi kuwa mbaya na kutishia utulivu wa eneo zima.
Ziara ya Putin katika visiwa vinavyozozaniwa 'haikubaliki’ - Japan

Chanzo cha picha, AFP via Getty Images
Ziara ya Putin katika visiwa vinavyozozaniwa 'haikubaliki’ - Japan
Waziri Mkuu wa Japan, Sanae Takaichi, amekosoa ziara ya kwanza kabisa ya Vladimir Putin katika visiwa vyenye utata vya Kuril siku ya Alhamisi, akiitaja ziara huyo kuwa "isiyokubalika kabisa".
Vyombo vya habari vya serikali ya Urusi viliripoti kuwa Putin alitembelea Iturup, inayojulikana nchini Japan kama Etorofu, ambacho ni mojawapo ya visiwa vinne katika mnyororo wa visiwa vya Kuril vinavyodaiwa na Urusi na Japan.
Safari ya Putin "imezidisha hisia hasi za Wajapani dhidi ya Urusi," Takaichi aliwaambia waandishi wa habari, akisisitiza kuwa visiwa hivyo ni "eneo la kipekee la Japan la kihistoria na kwa mujibu wa sheria za kimataifa".
Nchi hizo zimekuwa katika mzozo kuhusu visiwa vya Kuril kwa miongo kadhaa, na hiyo ndiyo sababu kuu iliyofanya Urusi na Tokyo kutotia saini mkataba wa amani baada ya Vita vya Pili vya Dunia.
Visiwa vya Kuril viko kati ya Hokkaido kaskazini mwa Japan na Rasi ya Kamchatka ya Urusi. Visiwa vinne vilivyo kusini kabisa Japan inadai ni vyake ambayo huviita "Maeneo ya Kaskazini".
Visiwa hivyo vinasimamiwa na Urusi. Mwishoni mwa Vita vya Pili vya Dunia, Umoja wa Kisovieti uliunganisha visiwa hivyo na kuwafukuza takriban wakazi 17,000 wa Kijapani.
Wakati wa ziara yake, Putin alionja mayai ya samaki na kuzungumza na wenyeji wa visiwa hivyo, kulingana na ripoti za vyombo vya habari vya serikali ya Urusi.
Akizungumza kutoka ofisi ya waziri mkuu siku ya Alhamisi, Takaichi alisema safari ya Putin "inaumiza hisia za watu wa Japan" na "haiendani na msimamo thabiti wa Japan kuhusu Maeneo ya Kaskazini".
"Natumai kuwa upande wa Urusi utachukulia suala hili kwa uzito mkubwa," alisema.
Mapema siku hiyo, Waziri wa Mambo ya Nje wa Japan, Toshimitsu Motegi, alisema visiwa hivyo ni "eneo la Japan kiasili, kihistoria na kwa mujibu wa sheria za kimataifa, na Serikali ya Japan inapinga vikali ziara hii".
Kwa miaka mingi, jitihada za kutatua mzozo huo hazijapata ufumbuzi. Uhusiano wa nchi hizo mbili pia haujakuwa mzuri, huku Japan ikiweka vikwazo dhidi ya Urusi kutokana na uvamizi wake nchini Ukraine mwaka 2022.
Soma Zaidi:
Balozi wa Ufaransa nchini CAR akabiliwa na hatua za kinidhamu

Chanzo cha picha, AFP via Getty Images
Ufaransa imeanzisha mchakato wa kinidhamu dhidi ya balozi wake mkuu nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati (CAR) kufuatia madai ya utovu wa nidhamu, ikiwemo tuhuma kuwa aliwakaribisha wanawake kadhaa katika makazi yake rasmi na kufanya nao ngono.
Madai hayo dhidi ya Balozi Bruno Foucher, yanayohusu matukio yanayodaiwa kutokea kati ya Januari 2024 na Machi mwaka huu, yalisababisha Wizara ya Mambo ya Nje ya Ufaransa kuanzisha uchunguzi kuhusu uwezekano wa kukiuka hatua za usalama.
Balozi mmoja wa Ufaransa aliambia BBC kuwa wizara hiyo imeanzisha taratibu za kiutawala dhidi ya balozi huyo, ambazo bado "zinaendelea".
BBC imewasiliana na ubalozi wa Ufaransa mjini Bangui ili kupata maoni yao.
Haijulikani wazi ni nini hasa kinachohusishwa na taratibu hizo za kinidhamu dhidi ya Foucher au zitachukua muda gani.
Kwa mujibu wa ripoti za vyombo vya habari vya Ufaransa, Foucher anadaiwa kuwaalika takriban wanawake 30 katika makazi yake jijini Bangui.
Baadhi ya wanawake hao wanadaiwa kulala hapo usiku kucha, jambo lililoibua hofu kuhusu usalama.
Foucher, mwenye umri wa miaka 65, amekuwa akihudumu kama balozi mkuu wa nchi yake mjini Bangui tangu mwaka 2023.
Madai hayo ya utovu wa nidhamu yanajiri wakati Ufaransa na CAR zikifanya juhudi za kuboresha uhusiano wao wa pande mbili ambao hapo awali ulikuwa umetetereka.
Wakati wa ziara yake mjini Bangui mwezi Machi, Waziri wa Mambo ya Nje wa Ufaransa, Jean-Noël Barrot, alipongeza "kurejeshwa kikamilifu kwa uhusiano" kati ya nchi hizo mbili.
Iran: Hakuna hatua iliyopigwa kufufua makubaliano ya muda ya amani na Marekani

Chanzo cha picha, EPA
Iran na Marekani bado wako katika mkwamo kuhusu juhudi za kufikia makubaliano ya kudumu ya kumaliza vita katika eneo la Ghuba, kulingana na chanzo cha ngazi ya juu cha Iran.
Chanzo hicho kimesema hakuna hatua iliyofikiwa katika mazungumzo ya kufufua makubaliano ya muda ya mwezi Juni.
Kauli hizo zilitolewa wakati Rais wa Marekani Donald Trump alipotoa tena shutuma kali dhidi ya viongozi wa Iran, jambo lililopunguza zaidi matumaini ya kutatuliwa kwa mgogoro huo, kufuatia mashambulizi mapya dhidi ya meli katika eneo hilo siku ya Jumanne.
Makubaliano yaliyofikiwa mwezi Juni yalitangaza “kusitishwa mara moja na kwa kudumu kwa operesheni za kijeshi katika pande zote.” Hata hivyo, makubaliano hayo yalianza kupata pigo muda mfupi baadaye.
Marekani inaishutumu Iran kwa kushindwa kutekeleza makubaliano yaliyowekwa chini ya mkataba huo ya kufungua tena njia muhimu ya usafirishaji ya Mlango wa Hormuz. Tehran, kwa upande wake, inasema Washington imekiuka ahadi zake, ikiwa ni pamoja na kuondoa zuio dhidi ya bandari za Iran na kuachilia mali za Iran zilizozuiliwa.
“Moja ya masuala yanayojadiliwa kupitia wapatanishi ni Marekani kurejea katika makubaliano ya muda na kuweka muda maalumu wa kutekeleza ahadi hizo. Hakujawa na maendeleo yoyote kabisa kuhusu suala hili,” chanzo cha Iran kilisema.
Trump alisema siku ya Jumatano kwamba Marekani ina “udhibiti kamili” wa Mlango wa Hormuz.
Hata hivyo, Mamlaka ya Mlango wa Ghuba ya Uajemi, chombo ambacho Iran ilianzisha kusimamia njia hiyo ya majini, ilisema kuwa bado imefungwa na haitafunguliwa tena hadi masharti ya Iran yatakapokubaliwa.
Katika kipindi chote cha mzozo huo, Trump amekuwa akibadilika badilika, mara anasema maneno ya vitisho vya kuongeza mzozo na madai kwamba makubaliano ya amani yako karibu kufikiwa.
Soma Zaidi Hapa:
Israel yashambulia Ukingo wa Magharibi

Chanzo cha picha, EPA
Shirika la habari la Palestina la Wafa limeripoti kuwa vikosi vya Israel vilianzisha operesheni katika miji na vijiji vitatu katika jimbo la Nablus mapema leo asubuhi.
Ripoti hiyo inaonyesha kuwa wakati wa operesheni, magari ya kijeshi yaliingia katika vijiji vya Burqa vilivyo kaskazini magharibi mwa Nablus, Qasra upande wa kusini, na Salem vilivyoko mashariki.
Kwa mujibu wa shirika hilo la habari, vikosi vya Israel huko Burqa vilivamia nyumba kadhaa na kuwakamata wakazi kadhaa wa Kipalestina.
Huko Qasra, magari makubwa ya kijeshi yalipelekwa Salem, doria za kijeshi zilifanya ukaguzi katika vitongoji na barabara kuu kadhaa.
Shirika la Habari la Wafa pia liliripoti kuwa vikosi vya Israel viliwakamata Wapalestina watano katika miji ya Allar, Sidon, na Qafeen, kaskazini mwa Tulkarm.
Soma Zaidi:
Zambia yafanya uchaguzi wa Rais na wabunge leo

Chanzo cha picha, Getty Images
Wananchi wa Zambia wanapiga kura kumchagua Rais na wabunge katika uchaguzi unaotajwa kuwa mtihani muhimu kwa demokrasia ya nchi hiyo, ambayo ina historia ya uchaguzi wa ushindani barani Afrika.
Rais Hakainde Hichilema anawania muhula wa pili, huku umaarufu wake ukihusishwa kwa kiasi kikubwa na namna serikali yake ilivyoshughulikia kipindi cha changamoto za kiuchumi.
Hata hivyo, ukosefu wa ajira unaoongezeka ni miongoni mwa masuala yanayowatia wasiwasi wapiga kura.
Uchaguzi huo unatarajiwa kuwa ushindani mkali kati ya Hichilema na kiongozi wa upinzani, Brian Mundubile, anayepata uungwaji mkono kutoka kwa wafuasi wa rais wa zamani, Edgar Lungu.
Ili kushinda urais, mgombea anapaswa kupata zaidi ya asilimia 50 ya kura.
Marekani yakosoa Israel kwa kuendelea kuwa na wanajeshi Lebanon

Chanzo cha picha, EPA
Marekani imeikosoa Israel, mshirika wake wa karibu, katika hatua nadra baada ya Waziri wa Ulinzi wa Israel, Israel Katz, kusisitiza kuwa wanajeshi wa nchi hiyo wataendelea kubaki kusini mwa Lebanon.
Idara ya Nchi ya Marekani imesema inatarajia Israel kuheshimu masharti ya makubaliano ya kusitisha mapigano na kujiondoa katika maeneo yaliyokubaliwa.
Katz alitoa kauli hiyo wakati wa ziara yake kusini mwa Lebanon, ambako alithibitisha kuwa vikosi vya Israel vinaendelea kubomoa nyumba zote katika eneo hilo.
Waziri Mkuu wa Lebanon, Nawaf Salam, amesema hatua ya Israel ya kubomoa nyumba hizo inakiuka sheria za kimataifa.
Makubaliano hayo yanataka wanajeshi wa Israel kuondoka katika maeneo ya kusini mwa Lebanon, huku jeshi la Lebanon likichukua jukumu la kudhibiti silaha za Hezbollah.
Wakati huo huo, mawaziri wa Israel wameendelea kutoa kauli kali kuhusu msimamo wao kisiasa, huku uchaguzi ukikaribia.
Dalili za ushirikiano wa Houthi na al Shabaab kudhibiti Mlango wa Bab al Mandab - Telegraph

Chanzo cha picha, Mohammed Hamoud/Getty Images
Gazeti la Uingereza la Telegraph limechapisha taarifa yenye kichwa, “Houthi wapanga kufungua uwanja mpya wa vita katika vita vya Iran na kufunga njia ya pili ya majini.” Taarifa hiyo imeandikwa na mwandishi wa masuala ya kimataifa, Akhtar Makoi.
Mwandishi amesema Houthi, wanaotajwa kwa sasa kuwa kundi lenye nguvu zaidi linaloungwa mkono na Iran katika eneo hilo, wanajiandaa kuufunga Mlango wa Bab al Mandab kwa niaba ya Iran, hatua inayolenga kuongeza shinikizo kwa Rais wa Marekani Donald Trump na kuathiri zaidi uchumi wa dunia.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, kuna ushirikiano kati ya Houthi na kundi la al Shabaab nchini Somalia, unaolenga kuyadhibiti maeneo yote mawili yanayozunguka Mlango wa Bab al Mandab na kuufunga pale Iran itakapoamua kufanya hivyo.
Taarifa hiyo imenukuu chanzo kikisema Houthi wanapeleka teknolojia ya ndege zisizo na rubani kutoka Iran kwa kundi la al Shabaab, kwa maelekezo kutoka Tehran. Lengo ni kuunda hali katika Mlango wa Bab al Mandab inayofanana na ile ya Mlango wa Hormuz.
Mwandishi amesema takriban asilimia 10 hadi 12 ya biashara ya dunia hupitia Mlango wa Bab al Mandab, ambao unaunganisha Bahari ya Shamu na Bahari ya Hindi kupitia Mfereji wa Suez.
Ameonya kuwa endapo njia hiyo ingefungwa, meli zingelazimika kutumia njia mbadala inayozunguka ncha ya kusini mwa Afrika, safari ambayo inaweza kuongeza muda wa usafirishaji kwa wiki kadhaa na hivyo kuongeza gharama za usafirishaji.
Taarifa hiyo pia imesema jeshi la Marekani limeanzisha wimbi jipya la mashambulizi ya anga dhidi ya Iran, huku kukiwa na taarifa kwamba Tehran imetishia kuufunga Mlango wa Bab al Mandab.
Mlango wa Hormuz na Mfereji wa Suez ni miongoni mwa njia muhimu zaidi za majini duniani kwa usafirishaji wa bidhaa na nishati.
Soma zaidi:
Sura ya Haaland yatumika kuuza kokeini huko Ecuador

Chanzo cha picha, Idara ya polisi ya Ecuador
Sura ya mshambuliaji nyota wa Norway, Erling Haaland, imewahi kuonekana kwenye mabango, kadi za michezo na skrini za televisheni baada ya kuwa gumzo mitandaoni kwa kufunga mabao saba katika mechi nne za Kombe la Dunia mwezi Julai.
Sasa polisi nchini Ecuador wamekuta picha yake katika eneo lisilotarajiwa, ikiwa imechapishwa kwenye vifurushi vya kijani vya mstatili vilivyokuwa sehemu ya mzigo mkubwa wa kokeini uliokamatwa kwenye lori karibu na mpaka wa Colombia.
Polisi wamesema dereva wa lori hilo alikamatwa baada ya kukamatwa kwa kilo 469 za kokeini Jumatano. Hata hivyo, hawakutoa maelezo kuhusu sababu ya picha za mshambuliaji huyo mwenye nywele za dhahabu kuwekwa kwenye vifurushi hivyo.
Ni jambo la kawaida kwa wasafirishaji wa dawa za kulevya kuweka majina au picha za wanamichezo maarufu na watu mashuhuri kwenye mizigo yao, kama njia ya kuashiria mtandao wa kihalifu uliotengeneza mzigo huo au mteja anayelengwa.
Taarifa ya polisi imesema maafisa wa kupambana na dawa za kulevya walianzisha operesheni baada ya kupokea taarifa kutoka kwa mtu asiyejulikana mapema Jumanne, kuhusu lori lililokuwa likisafiri katika barabara kuu ya Pan American.
Baada ya kulifanyia upekuzi, polisi waligundua vifurushi 370 vilivyofichwa katika sehemu iliyotengenezwa kwa siri chini ya lori hilo.
Polisi walitoa video ikionyesha vifurushi hivyo vikimwagika kutoka sehemu hiyo ya siri, huku picha za Haaland, ambaye mashabiki wake humuita kwa majina ya utani kama “pretty princess” na “babygirl”, zikionekana wazi.
Haaland alikuwa miongoni mwa wafungaji bora na wachezaji waliovutia zaidi katika Kombe la Dunia lililofanyika Mexico, Marekani na Canada. Urefu wake pamoja na ucheshi wake vimechochea video na vichekesho vingi kusambaa mitandaoni.
Haaland si mwanasoka pekee ambaye picha yake imeonekana kwenye mizigo ya dawa za kulevya. Picha ya nahodha wa timu ya taifa ya Argentina, Lionel Messi, pia imewahi kupatikana kwenye kifurushi kingine kilichokamatwa.
Rais Ruto asema katiba mpya iwe msingi wa Dira ya Kenya 2060

Chanzo cha picha, Ikulu Kenya/Facebook
Rais William Ruto amesisitiza umuhimu wa Katiba mpya katika kuandaa Dira ya Kenya 2060, akisema ushirikishwaji wa wananchi lazima uwe sehemu muhimu ya mchakato huo wa kupanga maendeleo ya muda mrefu ya nchi.
Ruto aliyasema hayo Jumatano, Agosti 12, 2026, katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Kenyatta, KICC, jijini Nairobi, wakati wa uzinduzi wa mjadala wa kitaifa kuhusu mpango mpya wa maendeleo wa Kenya, Beyond Vision 2030.
Zaidi ya wajumbe 5,000 kutoka kaunti zote 47 walishiriki katika uzinduzi huo, ulioashiria kuanza kwa mashauriano kuhusu Dira inayopendekezwa ya Kenya 2060.
Ruto amesema Dira ya 2030 iliandaliwa kabla ya Katiba mpya ya mwaka 2010, hivyo mchakato wa kuandaa Dira ya 2060 unapaswa kuzingatia matakwa ya Katiba kuhusu ushirikishwaji wa wananchi.
“Dira ya 2030 iliandaliwa kabla ya Katiba mpya. Katiba mpya imetupatia mfumo bora na ulio wazi zaidi wa kupanga mambo ya muda mrefu. Ni muhimu tufanye mchakato huu kwa kuzingatia Katiba mpya ambayo inatutaka kushauriana na wananchi. Hili si jambo la hiari, ni lazima,” amesema Ruto.
Rais amesema ushiriki mdogo wa wananchi katika kuandaa Dira ya 2030 uliathiri uelewa na uhusiano wao na mpango huo.
Amesema mchakato wa sasa unatoa fursa kwa Wakenya kushiriki moja kwa moja katika kuamua vipaumbele vya maendeleo ya nchi kwa muda mrefu.
Ruto ameahidi kuwa serikali itatoa rasilimali zinazohitajika kuhakikisha mashauriano hayo yanafanyika kwa kuzingatia wananchi na mahitaji yao.
“Kwa upande wa serikali, tuko tayari kutoa rasilimali zote zinazohitajika ili mchakato huu uwe wa wananchi, uongozwe na raia na uzingatie mustakabali wa nchi. Tuko tayari,” amesema.
Amezitaka taasisi za elimu, makundi ya kidini, wafanyabiashara, vyama vya kisiasa na mashirika ya kiraia kushiriki kikamilifu katika mchakato huo.
Askari watatu washikiliwa kufuatia kifo cha mtu mmoja katika hifadhi ya Ngorongoro

Chanzo cha picha, Getty Images
Na Alfred Lasteck
Mwandishi, BBC Swahili
Askari watatu wa uhifadhi wanashikiliwa na Jeshi la Polisi mkoani Arusha kwa mahojiano, baada ya mmoja kati ya watu watatu waliokuwa wamekamatwa katika Hifadhi ya Ngorongoro kufariki dunia na mwingine kupelekwa hospitalini.
Kwa mujibu wa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, SACP Justine Masejo, polisi ilipokea taarifa kuhusu watu wawili waliofikishwa katika Hospitali ya Lutheran Wilayani Karatu, mmoja akiwa amefariki na mwingine akiendelea kupatiwa matibabu.
Polisi ilisema uchunguzi wa awali ulibaini kuwa aliyefariki ni Sefu Mussa, mwenye umri wa miaka 25, fundi gereji na mkazi wa Matejo, Arusha.
Mwingine aliyefikishwa hospitali akipatiwa matibabu ametambuliwa kuwa Salimu Haji, maarufu Chambega, fundi gereji na mkazi wa Makao Mapya, Arusha.
Uchunguzi wa polisi pia umebaini kuwa watu hao walikuwa pamoja na Abdallah Nuru, maarufu Ngandana, ambaye inadaiwa ndiye aliyekuwa akiendesha pikipiki iliyowabeba wote.
Kwa mujibu wa Jeshi la Polisi, wanaume hao watatu walikamatwa na askari wa uhifadhi wa Ngorongoro Agosti 12, majira ya saa nne asubuhi, baada ya kuingia katika eneo la hifadhi bila kufuata utaratibu na wakiwa na pikipiki ambazo haziruhusiwi kuingia katika hifadhi hiyo.
Polisi imesema katika maelezo ya awali, watu hao walidai walikuwa wakisafiri kutoka Arusha kuelekea Babati kuhudhuria msiba, lakini walipotea njia na kujikuta ndani ya Hifadhi ya Ngorongoro.
Jeshi la Polisi limesema linaendelea kuchunguza maelezo hayo pamoja na kilichotokea baada ya kukamatwa na askari wa uhifadhi.
Kamanda Masejo amesema uchunguzi unalenga kubaini chanzo cha kifo cha Sefu Mussa na mazingira yaliyosababisha kifo hicho, pamoja na hali ya Salimu Haji ambaye anaendelea kupata matibabu.
Jeshi la Polisi limesema tayari limewahoji baadhi ya watu ili kusaidia kuthibitisha taarifa za awali na kubaini kilichotokea tangu watu hao walipokamatwa na askari wa uhifadhi hadi mmoja wao kufariki na mwingine kuendelea kupata matibabu hospitalini na mwingine, Ngandana alifikaje Arusha.
Tukio hilo linajiri huku kukiwa na wasiwasi wa muda mrefu kuhusu madai ya ukiukaji wa haki za binadamu unaohusishwa na operesheni za vyombo vya sheria na shughuli za uhifadhi katika eneo la Ngorongoro.
Mashirika ya kutetea haki za binadamu pamoja na jamii za eneo hilo zimewahi kutoa madai ya matumizi ya nguvu kupita kiasi, kukamatwa kiholela na vitendo vya kuwanyanyasa wananchi wakati wa operesheni za utekelezaji wa sheria.
Miongoni mwa malalamiko hayo ni kuhamishwa kwa lazima kwa jamii ya Wamasai, ambao wameishi pamoja na wanyamapori katika eneo hilo kwa muda mrefu.
Kwa upande wao, mamlaka zimekuwa zikisisitiza kuwa hatua hizo zinalenga kulinda eneo la hifadhi na kuhakikisha sheria na kanuni za uhifadhi zinafuatwa.
Kukamatwa kwa watu katika tukio la hivi karibuni kunatarajiwa kuchunguzwa ili kubaini iwapo taratibu zilizowekwa zilifuatwa ipasavyo.
Soma Zaidi:
Madaktari Uganda waipa serikali siku 14 kushughulikia maslahi ya madaktari wanafunzi

Chanzo cha picha, Getty Images
Maelezo ya picha, Ni picha ya mgomo wa madaktari Kenya Chama cha Madaktari Uganda, UMA, kimeipa Serikali siku 14 kutatua mzozo kuhusu ajira, upangaji wa vituo vya kazi na maslahi ya madaktari wanafunzi.
Chama cha UMA kimeonya kuwa iwapo Wizara ya Afya haitatoa majibu ya maandishi na ya kuridhisha ndani ya muda huo, madaktari nchini kote watafanya mgomo nchini kote.
Rais wa UMA, Daktari Frank Asiimwe, amesema: “Ili kulinda heshima ya taaluma ya udaktari pamoja na ubora na usalama wa utoaji wa huduma za afya, madaktari kote Uganda wataanza mgomo baada ya siku 14 kumalizika iwapo Wizara ya Afya itashindwa kutoa mawasiliano ya wazi, ya maandishi na ya kuridhisha kuhusu upangaji na uwezeshaji wa madaktari wanafunzi.”
Daktari Asiimwe amesema madaktari wataondoa huduma zao baada ya muda huo kumalizika, ingawa huduma za dharura na zile muhimu kwa kuokoa maisha zitaendelea kutolewa.
UMA pia inataka Serikali kuongeza ufadhili katika sekta ya afya, kuondoa zuio la kuajiri wahudumu wa afya, kushughulikia tofauti za mishahara kwa madaktari wasaidizi na kuwapandisha vyeo madaktari ambao wamebaki katika nafasi zao kwa zaidi ya muongo mmoja licha ya kupata tajriba ya juu.
Hatua hiyo inakuja baada ya wanachama wa UMA kupiga kura kuunga mkono madaktari wanafunzi na kuidhinisha kufanya mgomo iwapo Serikali itashindwa kushughulikia malalamiko yao.
Soma Zaidi hapa:
Inspekta Jenerali aagiza polisi wasimamishwe kazi kila mtuhumiwa akifariki kizuizini Kenya

Chanzo cha picha, NPS
Inspekta Jenerali wa Polisi nchini Kenya, Douglas Kanja, ameamuru maafisa wanaokuwa kazini wakati mtuhumiwa anafariki akiwa kizuizini kusimamishwa kazi mara moja, wakisubiri uchunguzi wa mazingira ya kifo hicho.
Kanja amesema agizo hilo linawahusu afisa anayesimamia Kitabu cha Matukio ya Polisi, O.B., askari anayelinda seli na afisa wa zamu.
Akizungumza na makamanda wa polisi wa mikoa, Kanja amesema maafisa hao wanapaswa kuwajibishwa katika kila kisa cha kifo kinachotokea ndani ya seli za polisi, huku uchunguzi ukiendelea kubaini kilichotokea.
“Kifo chochote kinachotokea katika seli za polisi, afisa anayerekodi O.B., askari anayelinda seli na afisa wa zamu lazima wasimamishwe kazi mara moja, huku uchunguzi ukiendelea. Hilo ni jambo ambalo nyinyi kama makamanda lazima mhakikishe linafanyika,” amesema Kanja.
Kanja pia amewakosoa makamanda wa polisi kwa kushindwa kudhibiti utovu wa nidhamu miongoni mwa maafisa walio chini yao, akisema watakaoshindwa kuchukua hatua watachukuliwa hatua za kinidhamu.
Naye Naibu Inspekta Jenerali wa Polisi anayesimamia Huduma ya Polisi ya Utawala, Gilbert Masengeli, amesema makamanda watawajibishwa iwapo uhalifu utaongezeka katika maeneo yao ya kiutawala.
“Uhalifu ukiongezeka katika maeneo yenu ya uwajibikaji, nyinyi kama makamanda mtakuwa wa kwanza kuulizwa maswali. Hili ni onyo dhidi ya uzembe katika uongozi,” amesema Masengeli.
Kanja pia ameonya kuwa makamanda watakaoshindwa kudhibiti magenge ya uhalifu katika maeneo yao watakabiliwa na hatua za kinidhamu, ikiwemo kushushwa cheo.
Onyo hilo linakuja huku kuongezeka kwa shughuli za magenge ya uhalifu kukizua wasiwasi kuhusu usalama nchini Kenya kuelekea Uchaguzi Mkuu wa 2027.
Soma pia:
Israel yapeleka wanajeshi zaidi katika kijiji ambako familia za Palestina zimezingirwa

Chanzo cha picha, Reuters
Israel imesema itapeleka wanajeshi zaidi katika kijiji kimoja cha Ukingo wa Magharibi, ambako walowezi wa Kiyahudi wamezizingira familia mbili za Wapalestina ndani ya nyumba zao tangu Jumapili.
Video iliyotolewa inaonyesha kundi la kwanza la wanajeshi wa Israel likiingia katika eneo hilo, huku baadhi yao wakionekana kusali pamoja na wakazi wa Kiyahudi wenye misimamo mikali.
Maafisa zaidi wa usalama walipelekwa katika eneo hilo na kuondoa hema lililokuwa limewekwa hapo. Hata hivyo, waliondoka baada ya mapigano kuzuka, na wakazi kurejea katika eneo hilo.
Familia za Wapalestina zinazoishi katika kijiji cha Qasra, kusini mwa Nablus, zimesema zimekatiliwa huduma za maji na umeme, huku akiba yao ya chakula ikizidi kupungua.
Kwa mujibu wa sheria za kimataifa, makazi yote ya Wayahudi katika Ukingo wa Magharibi unaokaliwa na Israel ni kinyume cha sheria.
Soma Zaidi:
Mamlaka ya ICE yapanga kuwapatia maafisa glovu zinazoweza kutoa mshtuko wa umeme

Chanzo cha picha, Getty Images
Maafisa wa Uhamiaji na Utekelezaji wa Forodha nchini Marekani, ICE, wanaweza kuanza kutumia glovu zinazoweza kutoa mshtuko wa umeme wanapotekeleza majukumu yao ya kiusalama.
ICE imepanga kutumia hadi dola milioni 20 kununua glovu hizo zinazojulikana kama Generated Low Output Voltage Emitter, GLOVE, kwa mujibu wa taarifa iliyochapishwa Jumatatu na Idara ya Usalama wa Taifa, DHS.
Glovu hizo zina uwezo wa kutoa mshtuko wa umeme wa hadi volti 380, karibu mara tatu ya kiwango cha umeme kinachotolewa na soketi ya kawaida nchini Marekani.
Mashirika ya kutetea haki za kiraia, likiwemo American Civil Liberties Union, ACLU, yameeleza wasiwasi kuhusu matumizi ya glovu hizo.
ICE imekuwa ikikabiliwa na uchunguzi kuhusu mbinu zake wakati wa operesheni za utekelezaji wa sheria, ambazo zimesababisha maafisa wake kuhusishwa katika matukio kadhaa ya watu kuuawa kwa kupigwa risasi.
DHS imeiambia BBC kuwa ICE inaendelea kutathmini mahitaji ya maafisa wake walio katika maeneo ya utekelezaji wa sheria, ili kuhakikisha wanapata vifaa vinavyohitajika kuwakamata na kuwaondoa nchini wahamiaji wanaokiuka sheria za uhamiaji.
Kampuni ya Compliant Technologies LLC, inayotengeneza glovu hizo, imeiambia BBC kuwa haiwezi kutoa maoni kuhusu mauzo hayo.
DHS imesema mkataba wa ununuzi wa glovu hizo bila mchakato wa zabuni unaweza kuchapishwa mapema Ijumaa.
Glovu hizo huwashwa kwa kubonyeza kitufe na zinaweza kutoa hadi mishtuko 30 ya umeme kwa sekunde. Pia zina vichakataji vidogo vinavyorekodi kila matumizi ya kifaa.
Compliant Technologies inasema kwenye tovuti yake kuwa glovu hizo hazisababishi majeraha na zinatumiwa na taasisi mbalimbali za utekelezaji wa sheria.
Soma Zaidi:




















