DRC na M23 zakubaliana kuendeleza mazungumzo ya amani
Makubaliano hayo yamefikiwa baada ya pande hizo kufanya mazungumzo ya siku tano nchini Uswisi.
Muhtasari
- Syria: Milango ya diplomasia iko wazi, lakini hatuiamini Israel
- Mashambulizi ya kupangwa yaripotiwa kusini mwa Thailand
- DRC na M23 zakubaliana kuendeleza mazungumzo ya amani
- Zelensky ana 'maswali ya kujibu' - Waziri wa Ulinzi wa aliyefukuzwa kazi aiambia BBC
- Bin Salman jijini Paris: Ushirikiano unaovuka mipaka ya uhusiano wa nchi mbili
- Uingereza yapinga madai ya kushambuliwa mtandaoni na Iran
- Chile yafunga ubalozi wake nchini Iran
- Botswana yahaha kuhusu raia wake kujiunga na jeshi la Urusi
- Iran yatishia kushambulia nchi itakayoisaidia Marekani
Moja kwa moja
Na Ambia Hirsi
Syria: Milango ya diplomasia iko wazi, lakini hatuiamini Israel

Chanzo cha picha, Anadolu via Getty Images
Waziri wa Mambo ya Nje wa Syria amesema kuwa Damascus inatarajia mazungumzo na Israel kuhusu makubaliano ya usalama kurejelewa hivi karibuni.
Siku chache baada ya shambulio la anga la Israel dhidi ya kambi ya kijeshi ya Syria, Asad Shaibani alisisitiza katika mahojiano na shirika la habari la Reuters kwamba kipaumbele cha Damascus kwa sasa ni kusitisha mashambulio ya Israel.
Kwa mujibu wake, ili kusonga mbele katika mwelekeo huo, pande zote mbili lazima zichukue hatua za kujenga hali ya kuaminiana.
Bw. Shaibani alisema kuwa mazungumzo kuhusu makubaliano ya usalama yalikuwa yamesitishwa tangu kuanza kwa vita vya Iran, lakini yanatarajiwa kurejelewa hivi karibuni.
Pia alisema kuwa mawasiliano kati ya pande hizo mbili yalikuwa yamevunjika baada ya Israel kushambulia kambi ya anga ya Syria.
Serikali ya Syria ina matumai kuwa kufikiwa kwa makubaliano kutashinikiza Israel kuondoa majeshi yake kutoka katika ardhi yake.
Bw. Sheibani aliitaka Israel kutumia fursa hii ya "kihistoria" kwa kuwa "milango ya diplomasia" bado iko wazi, lakini pia alionyesha kuwepo kwa ukosefu wa imani: "Tunaamini kwamba tunapaswa kuwa na mawasiliano, hasa na upande ambao mara kwa mara unatishia usalama wa Syria; lakini ikiwa mawasiliano hayo hayataleta matokeo chanya, hatuyahitaji. Kwa sasa hatuiamini Israel."
Marekani imekuwa ikijaribu kwa zaidi ya mwaka mmoja kuwa mpatanishi kati ya Israel na serikali ya Syria Ahmed al-Sharaa—ambaye ni mshirika mpya wa Washington katika Mashariki ya Kati—lakini juhudi hizo hazijafua dafu.
Katika kipindi hiki, Israel imetuma majeshi yake katika ardhi ya Syria na kushambulia ngome na vifaa vya serikali, ikitaja masuala ya usalama kama sababu ya hatua hizo.
Ofisi ya Waziri Mkuu wa Israel haikujibu ombi la shirika la habari la Reuters la kutaka maoni kuhusu kauli hizo.
Maelezo zaidi:
Mashambulizi ya kupangwa yaripotiwa kusini mwa Thailand

Chanzo cha picha, AFP via Getty Images
Jeshi la Thailand limesema kuwa zaidi ya mashambulizi 50 ya makusudi ya kuchoma moto, yaliyopangwa kwa lengo la "kuchochea machafuko," yamefanyika katika eneo la kusini mwa nchi hiyo linalokabiliwa na uasi.
Watu wawili walijeruhiwa, huku jengo la ofisi ya serikali ya eneo hilo, duka la bidhaa mbalimbali, na gari lililoibwa vikiwa miongoni mwa maeneo na vitu vilivyochomwa moto.
Matukio hayo yalitokea katika majimbo ya mpakani kusini mwa nchi hiyo kati ya saa mbili usiku kwa saa za huko (saa saba mchana kwa saa za GMT) na usiku wa manane siku ya Jumamosi, kulingana na taarifa kutoka kwa Kamandi ya Operesheni za Usalama wa Ndani ya jeshi hilo.
Matukio mengi yaliripotiwa katika jimbo la Narathiwat, huku mengine yakitokea katika majimbo jirani ya Yala na Pattani. Kwa mujibu wa gazeti la Bangkok Post, wanawake wawili walijeruhiwa wakati bomu lilipolipuka katika wilaya ya Muang mkoani Narathiwat.
Minara ya mawasiliano ilichomwa moto katika maeneo kadhaa, na maafisa wa usalama waliwaonya wakazi kutogusa vitu vyovyote wanvyotilia shaka.
Mamlaka ziliweka amri ya kutotoka nje usiku katika jimbo la Narathiwat, hatua ambayo iliondolewa Jumapili asubuhi.
Hakuna mashambulizi mengine yaliyoripotiwa siku ya Jumapili.
DRC na M23 zakubaliana kuendeleza mazungumzo ya amani

Chanzo cha picha, Getty Images
Serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) na waasi wa M23 wamekubaliana kuendelea na mazungumzo ya kutafuta amani, lakini bado hawajakubaliana kuhusu baadhi ya mambo muhimu.
Makubaliano hayo yamefikiwa baada ya pande hizo kufanya mazungumzo ya siku tano nchini Uswisi.
Zimekubaliana mpango unaoonyesha hatua na muda wa kuendelea na mazungumzo yaliyokuwa yakifanyika chini ya makubaliano ya amani ya Doha, Qatar.
Pia wamekubaliana kuanza kutumia mfumo maalum wa kufuatilia kama kuna ukiukaji wa usitishaji mapigano.
Ukaguzi wa kwanza unatarajiwa kufanyika Jumatatu katika eneo la Minembwe, Kivu Kusini, ambalo limeathiriwa na mapigano.
Hata hivyo, bado hawajakubaliana kuhusu baadhi ya masuala, yakiwemo vikwazo dhidi ya M23 na kuachiwa kwa baadhi ya watu waliokamatwa.
Wakati mazungumzo yakiendelea, mapigano bado yanaendelea katika maeneo ya Kisu Kaskazini na Kivu Kusini, huku serikali na M23 zikituhumiana kuvunja makubaliano ya kusitisha mapigano.
Mzozo huo pia umeendelea kuongeza mvutano kati ya DRC na Rwanda. Rwanda inasema serikali ya DRC inashindwa kuliondoa kundi la FDLR, ambalo Kigali inaliona kuwa tishio kwa usalama wake.
DRC, kwa upande wake, inaituhumu Rwanda kuiunga mkono M23 kwa wanajeshi na silaha.
Rwanda inakanusha madai hayo. Mapigano hayo yamesababisha mamilioni ya watu kuondoka katika makazi yao.
Soma pia:
Zelensky ana 'maswali ya kujibu' - Waziri wa Ulinzi wa aliyefukuzwa kazi aiambia BBC

Chanzo cha picha, Reuters
Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky ana "maswali ya kujibu" kuhusu ufisadi serikalini mwake, kulingana na kauli ya aliyekuwa Waziri wa Ulinzi, Mykhailo Fedorov, alipozungumza na BBC.
Fedorov, waziri maarufu aliyeleta mageuzi ya kisasa katika jeshi na kuanzisha matumizi ya ndege zisizo na rubani vitani, alifutwa kazi mwezi uliopita baada ya kudaiwa kutofautiana na mkuu wa jeshi la Ukraine.
Aliiambia BBC kuwa uchunguzi kuhusu utakatishaji fedha uliotangazwa wiki iliyopita umezua maswali iwapo Zelensky alikuwa na taarifa za ufisadi miongoni mwa wandani wake.
Pia Fedorov alisisitiza kuwa "demokrasia haipaswi kuwa mateka wa Putin" - lakini hakuweka wazi azma yake ya kisiasa, siku chache baada ya kuweka mtandaoni video inayotoa wito wa kutaka uchaguzi ufanywe nchini Ukraine.
Maandamano ya yalizuka nchini Ukraine kupinga kuftwa kwake lakini uungwaji mkono wake ulipungua na maandamano yalikommeshwa Jumatano, baada ya kuthibitishwa kwa nafasi ya Fedorov.
Wito wake wa uchaguzi ya wakati wa vita umepingwa kwa kiasi kikubwa.
Ukraine imekuwa chini ya sheria za kijeshi tangu uvamizi kamili wa Urusi mwaka 2022, ikimaanisha uchaguzi umesitishwa.
Fedorov ndiye mwanasiasa wa kwanza kigogo kuitisha uchaguzi mkuu ambapo kulingana na sheria za Ukraine,ni marufuku kuandaa uchaguzi wakati wa vita.
Pia unaweza kusoma:
Mohammed bin Salman kutua jijini Paris kwa ziara ya siku mbili

Chanzo cha picha, Getty Images
Ufaransa inajiandaa kumpokea Mrithi wa Kiti cha Ufalme na Waziri Mkuu wa Saudi Arabia, Mohammed bin Salman, kwa ziara rasmi ya siku mbili itakayoanza leo Jumapili, katika kipindi ambacho hali ya mambo katika Mashariki ya Kati ni inaendelea kuwa tete.
Kwa mujibu wa Ikulu ya Élysée, ziara hiyo inaakisi kile ilichokitaja kuwa ni "uhai wa mazungumzo" kati ya Saudi Arabia na Ufaransa, na ni fursa ya kuimarisha ushirikiano wa kimkakati kati ya nchi hizo mbili.
Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron na Mrithi wa Kiti cha Ufalme Mohammed bin Salman wanatarajiwa kufanya mkutano wa kwanza wa Baraza la Ushirikiano wa Kimkakati la Ufaransa na Saudi Arabia, ambapo watajadili masuala ya kiuchumi na kimkakati, pamoja na masuala ya kikanda.
Paris inachukulia uratibu na washirika wake wa Ghuba kuwa muhimu kwa uimarishaji wa utulivu na amani katika eneo hilo.
Macron na Mrithi wa Kiti cha Ufalme wa Saudi Arabia pia watashiriki katika hafla ya kufunga mashindano ya Kombe la Dunia la Michezo ya Kielektroniki (Esports World Cup), ambayo yanafanyika Paris kwa mara ya kwanza nje ya Saudi Arabia tangu mashindano hayo yalipoanzishwa.
Uingereza yapinga madai ya kushambuliwa mtandaoni na Iran

Chanzo cha picha, Getty Images
Serikali ya Uingereza imekanusha taarifa ya gazeti la Telegraph kuhusu shambulio la mtandaoni la Iran dhidi ya kiwanda cha kufua umeme nchini humo, ikisema tukio hilo liliathiri jenereta ndogo ya nishati, wala sio kiwanda cha umeme.
Gazeti la Telegraph liliripoti kwamba Iran ilikuwa imedukua mtandao wa kiwanda cha umeme cha Uingereza kwa siku nne katika shambulio la mtandaoni "lisilo na kifani ".
Lakini msemaji wa serikali ya Uingereza alisema mfumo wa nishati wa nchi hiyo ulikuwa imara sana na "hakukua na tishio lolote dhidi ya mfumo mkuu wa nishati."
Vyanzo vya serikali ya Uingereza pia vilielezea ripoti ya Telegraph kama iliyotiwa chumvi na kusema tukio hilo halikuhusisha mitambo yoyote ya umeme.
Uingereza inasema kwamba kufuatia tukio hilo, Idara ya Usalama wa Nishati imewafahamisha watendaji wakuu katika makampuni ya nishati na kuwatumia mapendekezo na mwongozo kuhusu hatua zinazofuata.
Kituo cha Kitaifa cha Usalama wa Mtandaoni cha Uingereza pia kina jukumu katika kushughulikia matukio makubwa ya mtandao na kuratibu majibu ya serikali na mashirika yaliyoathiriwa.
Pia unaweza kusoma:
Chile yafunga ubalozi wake nchini Iran
Serikali ya Chile imetangaza kuwa itafunga ubalozi wake nchini Iran mwisho wa mwezi huu wa Agosti, lakini inasisitiza kuwa uamuzi huo hautavuja uhusiano wa kidiplomasia kati ya nchi hizo mbili.
Wizara ya Mambo ya Nje ya Chile imesema kuwa baada ya kufungwa kwa ubalozi huo mjini Tehran, masuala ya kibalozi ya nchi hiyo yatasimamiwa kupitia ubalozi mdogo wa Chile mjini Ankara, mji mkuu wa Uturuki.
Wizara hiyo ilitaja sababu za uamuzi huo kuwa ni marekebisho ya kiutendaji na kuweka vipaumbele katika rasilimali ili kufanikisha malengo ya sera ya kigeni ya serikali, pamoja na hatua za tahadhari zinazohusiana na hali ya usalama katika eneo la Mashariki ya Kati.
Uamuzi huo ulitangazwa wakati Waziri wa Mambo ya Nje wa Chile, Francisco Pérez Macena, akihitimisha ziara rasmi nchini China, ambayo ni mshirika mkuu wa kibiashara wa Chile.
Rais wa Chile mwenye msimamo wa mrengo wa kulia, José Antonio Caste, ambaye amekuwa madarakani tangu mwezi Machi, amedumisha misimamo inayolingana na ile ya utawala wa Trump.
Hata hivyo, baadhi ya maafisa wa utawala wake wametilia shaka mbinu inayotumiwa na Marekani katika uhusiano wake na Amerika ya Kusini katika wiki za hivi karibuni.
Soma pia:
Botswana yahaha kuhusu raia wake kujiunga na jeshi la Urusi

Chanzo cha picha, Anadolu via Getty
Maelezo ya picha, Waziri wa Mambo ya Nje wa Botswana, Fenyo Butal. Botswana inasema kuwa takribani raia wake wanane waliokuwa wakijaribu kujiunga na jeshi la Urusi wamezuiwa.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Botswana, Fenyo Butal, aliambia bunge mnamo Agosti 21 kuwa alizuia raia wanane wa nchi hiyo waliokuwa na mpango wa kujiunga na jeshi la Urusi ili kushiriki katika vita dhidi ya Ukraine.
"Serikali ina wasiwasi mkubwa kuhusu visa vinavyoongezeka vya raia wa Botswana kusajiliwa kuipigania Urusi katika vita vya Ukraine," alisema Bw. Butal.
Aliongeza kuwa serikali ina "ripoti za kutia wasiwasi" kuhusu "ahadi za ajira, mafunzo au kazi za usalama nchini Urusi" zinazotolewa katika ngazi ya jamii, kwa lengo la kuwahadaa raia na kuwapeleka kwenye mstari wa mbele wa vita vya nchi nyingine.
"Kufikia sasa raia 22 wa Botswana wamedanganywa na mipango hii ya uajiri," alisema waziri wa mambo ya nje wa Botswana.
Aliongeza: "Tulifanikiwa kuwazuia raia wetu wanane katika viwanja vya ndege vya Siretse Khama, O.R. Tambo, na Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Addis Ababa, muda mfupi kabla ya safari yao kwenda Urusi na kuwarejesha nyumbani.
"Ripoti za maelfu ya Waafrika kusajiliwa katika jeshi la Urusi kwa njia za udanganyifu na zisizo halali katika miaka ya hivi karibuni zimeibua mivutano ya kidiplomasia.''
Maelezo zaidi:
Iran yatishia kushambulia nchi itakayoisaidia Marekani

Chanzo cha picha, Reuters
Katibu wa Baraza Kuu la Usalama la Iran, Mohsen Rezaei, amesema kwamba "nchi yoyote itakayoisaidia Marekani kutekeleza vikwazo vya kiuchumi dhidi ya nchi yetu inachukuliwa kuwa adui."
Rezaei aliongeza katika taarifa kwa televisheni ya taifa: "Tunaziarifu nchi jirani na nchi zingine duniani: Msijiunge na vita vya kiuchumi vinavyoendeshwa na Marekani."
"Maslahi ya nchi zinazosaidia Marekani kuendesha vita vya kiuchumi dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu italengwa," alisema Rezaei, na kuongeza: "Kwa nchi jirani zitashirikiana na Wamarekani katika vita hivyo vya kiuchumi, hakuna tone hata moja la mafuta litakalotoka..." Ghuba na Lango la Hormuz.
Kauli ya Rezaei inakuja baada ya Washington kutangaza kuwa itaimarisha vikwazo vya kiuchumi ili kuishinikiza Tehran kurejea kwenye meza ya mazungumzo.
Rezaei aliendelea kusema: "Bado hatujashambulia maslahi yoyote ya kiuchumi ya Marekani, mpaka sasa tumelenga kambi za kijeshi tu; lakini iwapo wanataka kutuwekea vikwazo vya kiuchumi, basi kampuni za mafuta na za kiuchumi za Marekani zilizo karibu na Iran na maeneo mengine, zijiandae kwa mapigo yetu ."
Alisisitiza kuwa endapo Rais wa Marekani Donald Trump atachukua "hatua yoyote (dhidi yetu), majibu yetu yatakuwa kama tetemeko la ardhi."
Siku ya Jumamosi, Iran ililaani mipango ya Marekani ya kutangaza vikwazo vipya ambavyo vinaweza kuongeza shinikizo kwa uchumi wa Iran na kuleta madhara kwa washirika wake wakuu wa kibiashara, akiwemo China.
Takriban miezi sita tangu kuzuka kwa uhasama kufuatia mashambulizi ya anga ya Marekani na Israel dhidi ya Iran mnamo tarehe 28 Februari, pande hizo mbili zimesitisha mapigano, lakini hakuna dalili za kurejea kwenye mazungumzo ya amani.
Soma pia:
Karibu kwa matangazo ya moja kwa moja.




















