Moja kwa moja, Iran yaahidi kusitisha mashambulizi iwapo Marekani itatekeleza makubaliano ya amani
Akizungumza katika mkutano wa Shirika la Ushirikiano la Shanghai, SCO, mjini Bishkek, Kyrgyzstan, Rais wa iran Masoud Pezeshkian amesema ''Iran itachukua hatua mara moja iwapo Marekani itarejea kwenye ahadi hizo za Islamabad.
Mwanaharakati Godlisten Malisa aachiwa baada ya kukamatwa kwa tuhuma za jinai
Chanzo cha picha, SOCIALS
Mwanaharakati nchini Tanzania Godlisten Elisante Malisa amesema ameachiwa huru na Jeshi la Polisi leo asubuhi bila kudhaminiwa, akikanusha taarifa kwamba aliachiwa kwa dhamana baada ya kuhojiwa kuhusu tuhuma za jinai.
Malisa amesema hajahojiwa wala kuandikiwa maelezo kuhusu tuhuma zozote za jinai, na kwamba mali zake zote, ikiwemo simu, fedha na mabegi, zimerudishwa kwake.
Amesema baada ya kukamatwa, Polisi walimtaka kuandika maelezo kuhusu namna alivyokamatwa eneo la Namanga hadi kufikishwa Arusha.
“Hawajanituhumu kwa chochote. Hawajanihoji kwa chochote, wala hawajanitajia tuhuma ambazo nimekuwa nikikabili zamani au tuhuma mpya,” amesema Malisa.
Amesema yeye pamoja na watu wengine waliokamatwa walikuwa katika Kituo cha Diplomasia na Utalii Arusha, licha ya kwamba kila mmoja alikuwa amesafiri kivyake.
Malisa amesema tukio hilo limemsikitisha, hasa kutokana na mazingira ya sasa nchini, akisema mawakili wake walilazimika kutumia muda mwingi kufuatilia suala hilo katika vituo vya Polisi.
Iran: Marekani na walioisaidia katika shambulio Larak watashambuliwa vikali
Chanzo cha picha, IRNA
Iran imeonya kwamba nchi au taasisi yoyote iliyosaidia kupanga, kuwezesha au kushiriki katika shambulio la Marekani dhidi ya Kisiwa cha Larak italazimika kubeba gharama na kuwajibika kwa madhara yatakayofuata.
Tehran imesema wahusika hao watakabiliwa pia na jibu kali kutokana na hatua zao.
Katika barua yake kwa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa na Baraza la Usalama, balozi wa Iran katika Umoja wa Mataifa amelaani shambulio hilo na kuitaka Marekani kusitisha kile Tehran inachokiita ukiukaji wa Mkataba wa Umoja wa Mataifa, pamoja na hatua zinazotishia usafiri wa meli katika Ghuba ya Uajemi na Mlango wa Bahari wa Hormuz.
Jeshi la Iran pia limeonya kwamba litajibu dhidi ya nchi yoyote ambayo eneo lake litatumiwa kuanzisha mashambulizi dhidi ya Iran.
Pezeshkian: Iran iko tayari kusitisha uhasama iwapo Marekani itatekeleza makubaliano
Chanzo cha picha, Getty Images
Rais wa Iran Masoud Pezeshkian amesema nchi yake iko tayari kuchukua hatua za kusitisha uhasama iwapo Marekani itarejea kutekeleza ahadi zake chini ya makubaliano yaliyofikiwa Juni.
Akizungumza katika mkutano wa Shirika la Ushirikiano la Shanghai, SCO, mjini Bishkek, Kyrgyzstan, Pezeshkian amesema ''Iran itachukua hatua mara moja iwapo Marekani itarejea kwenye ahadi hizo.
Kauli hiyo inakuja wakati mvutano kati ya Marekani na Iran ukizidi, baada ya pande hizo kushambuliana na kila upande ukisema ulijibu kile ulichokitaja kuwa uchokozi wa upande mwingine.
Pezeshkian amesema Iran inaamini makubaliano hayo bado yanaweza kuwa njia ya kumaliza uhasama, lakini ameituhumu Marekani kwa kushindwa kutekeleza ahadi zake.
Makubaliano ya Juni ya Islamabad yalilenga kusitisha mapigano na kurejesha mazungumzo kati ya Washington na Tehran, huku juhudi za kidiplomasia zikihusisha pia Pakistan na nchi nyingine za eneo hilo.
Iran yaikosoa Ulaya kwa kufuata msimamo wa Washington
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran, Esmaeil Baghaei, ameikosoa Ulaya kwa kile alichosema ni kufuata maagizo ya Washington badala ya kufanya maamuzi yake yenyewe.
Baghaei amesema Ulaya haiwezi kujidai kuwa ina uhuru wa kimkakati huku ikitekeleza matakwa ya Marekani.
''Uwezo wa kuwa na uhuru wa kimkakati haupatikani kupitia matamko makubwa, bali kupitia uwezo wa kufanya maamuzi kwa kujitegemea na kwa uwajibikaji, hata pale maamuzi hayo yanapotofautiana na msimamo wa taifa lenye nguvu zaidi'', amesema Baghaei.
Kauli yake imekuja baada ya Umoja wa Ulaya kuunga mkono hatua za Marekani dhidi ya Iran, jambo ambalo Tehran imelielezea kama dalili ya Ulaya kupoteza uwezo wake wa kufanya maamuzi huru.
Baghaei amesema Ulaya inapaswa kuchagua kati ya kutenda kama mshirika huru wa kimataifa au kuendelea kuakisi sera za Washington na kuuchukulia mwangwi huo kama uhuru wa kimkakati.
Urusi imesema vikosi vyake vya Africa Corps vilisaidia vikosi vya Niger kukabiliana na jaribio la mapinduzi katika mji mkuu Niamey Jumamosi.
Milio ya risasi na milipuko ilisikika katika maeneo kadhaa ya Niamey, yakiwemo karibu na ikulu ya rais na kambi ya kijeshi iliyoko katika uwanja wa ndege wa kimataifa wa Diori Hamani.
Mamlaka za Niger zilisema baadaye kuwa ziliweza kurejesha udhibiti wa maeneo yaliyokuwa yametekwa na wanajeshi walioasi.
Kwa mujibu wa Urusi, vikosi vya Niger kwa msaada wa wanajeshi wa Africa Corps vilifanikiwa kuwadhibiti waasi na kurejesha udhibiti wa kambi hiyo ya kijeshi.
Urusi imesema itaendelea kuisaidia Niger katika kukabiliana na vitisho vya usalama.
Hata hivyo, hali katika mji mkuu imeanza kurejea katika utulivu, huku serikali ya kijeshi ikisema bado inadhibiti nchi chini ya uongozi wa Rais Abdourahamane Tiani.
Idadi ya
watu waliofariki nchini Nepal kutokana na mafuriko makubwa katika eneo la mpaka
na Tibet imevuka 1,000, kulingana na shirika la taifa hilo linaloshughulikia
majanga.
Zaidi ya
watu 3,900 bado hawajulikani walipo; kati yao, zaidi ya 600 ni wafanyakazi
wanaoaminika kunaswa ndani ya mtandao mpana wa mahandaki yaliyojaa matope
katika maeneo ya miradi ya umeme wa maji kando ya Mto Trishuli.
Wahandisi
wamekuwa wakisukuma hewa ndani ya mahandaki hayo, na ingawa timu moja
ilifanikiwa kuingia katika mojawapo, iliondoka baada ya kukuta hakuna mtu
ndani.
"Natamani
tungempata. Natamani angerudi nyumbani," alisema Anushila Bhandari, mke wa
Aurus Bhandari, mhandisi mwenye umri wa miaka 33 ambaye ametoweka katika eneo
la mradi, akizungumza na BBC Nepali.
Waziri Mkuu
wa Nepal, Balendra Shah, alisema siku ya Jumatatu kuwa watu 279 wameokolewa
kutoka maeneo hayo.
Operesheni
ya uokoaji inaongozwa na timu ya kimataifa inayojumuisha wanajeshi kutoka China
na Nepal, huku wataalamu kutoka India, Korea na Australia pia wakishiriki.
Je, kuna uhaba wa maziwa nchini Kenya?
Chanzo cha picha, Getty Images
Unakumbwa na ugumu wa kupata maziwa kwenye maduka makuu nchini Kenya ?
Hasa katika mji mkuu Nairobi. Kumekuwa na malalmaishi kadha akwenye mitandao ya kijami kwamba kuna uhaba wa maziwa nchini kenya wengiw akisema kwamba aina kadhaa ya maziwa inayouzwa nchini hayapo madukani.
Sasa, bodi ya maziwa yaani Kenya Dairy Borad {KDB} imesema kwamba hali sio mbaya kama inavyotajwa ikifafanua kwamba ; ‘Maziwa bado yanapatikana kote nchini Kenya, lakini upatikanaji wake unakabiliwa na changamoto kubwa katika maeneo mengi ya nchi.’
Kwa mujibu wa taarifa ya bodi hiyo utafiti wa haraka wa soko uliofanywa tarehe 31 Agosti ulibaini shinikizo kubwa katika upatikanaji wa bidhaa hiyo katika masoko 11 kati ya 19 yaliyochunguzwa, yakiwemo Nakuru, Kisii, Embu, Kirinyaga, Kakamega, Narok, Busia, Kapsabet na Mombasa.
Mamlaka hiyo ilisema kuwa hali hiyo inadhihirika kupitia akiba ndogo kwenye rafu, chaguo pungufu la chapa za maziwa, ucheleweshaji wa usambazaji na maziwa kuuzwa haraka zaidi kuliko kawaida, badala ya uhaba mkubwa wa jumla.
Maziwa mabichi yaliyosafishwa kwa njia ya joto (pasteurised) yanaonekana kuathirika zaidi, huku bidhaa zinazodumu kwa muda mrefu kama vile maziwa ya UHT na yale ya aina ya ESL (Extended Shelf-Life) yakipatikana kwa urahisi zaidi.
Pakiti nyingi za mililita 500 zilikuwa zikiuzwa kwa bei ya kati ya Shilingi 55 na 65 za Kenya{ sawia na shilingi 1,229 za Tanzania na senti 46 za dola ya Marekani } ingawa bei za juu zaidi ziliripotiwa katika baadhi ya maeneo. Jijini Mombasa, baadhi ya bidhaa ziliuzwa kwa bei ya hadi Shilingi 80, huku bei pia zikiwa juu ya wastani wa kitaifa katika maeneo ya Kabarnet, Kapsabet na Thika.
Bodi ya Maziwa ilisema itaongeza juhudi za kufuatilia hali ya soko na imependekeza kuongezwa kwa uingizaji wa maziwa ya UHT kutoka nchi nyingine za Jumuiya ya Afrika Mashariki, ikibidi, ili kusaidia kukidhi mahitaji ya ndani.
Matokeo hayo yanaashiria kuwa Kenya inakabiliwa na hali ya kupungua kwa upatikanaji wa maziwa badala ya uhaba kamili, huku hali ya upatikanaji na bei zikitofautiana katika maeneo mbalimbali ya nchi.
Hasara ya mgomo wa wafanyakazi wa sekta ya usafiri wa anga nchini Kenya
Baada ya zaidi ya
saa 18 za mazungumzo, wadau katika sekta ya usafiri wa anga nchini Kenya
wamekubaliana kusitisha mgomo uliodumu kwa siku mbili.
Katika taarifa
iliyochapishwa mapema Jumanne, Waziri wa Uchukuzi wa Umma nchini Kenya, Davis
Chirchir, amesema: "Kufuatia makubaliano yaliyofikiwa, KAWU inatangaza
kusitisha mgomo huo mara moja na kuwaelekeza wafanyakazi walioathirika kurejea
katika majukumu yao ya kawaida."
Kwa sasa, pande zote zimeahidi kujitolea kurejesha haraka
shughuli za kawaida za usafiri wa anga, kudumisha amani ya viwanda na kutatua
malalamiko yoyote yaliyosalia au yatakayojitokeza baadaye kupitia mazungumzo,
upatanishi na mifumo iliyoanzishwa kisheria.
Hata hivyo, baadhi ya watu tuliozungumza nao wameeleza hofu
ya kukumbwa na ucheleweshaji wa safari kutokana na safari nyingi kuahirishwa
awali. Wengi wana hofu kuwa itachukua muda kabla ya hali ya kawaida kurejea.
Taarifa hii imekuja kama afueni kwa maelfu ya wasafiri
waliokwama katika viwanja vya ndege si tu nchini Kenya bali pia katika maeneo
mengine duniani. Maelfu ya wasafiri walikwama katika miji kama Doha, London na
Johannesburg wakisubiri safari ambazo zilitarajiwa kutua Nairobi au
kuunganishwa kupitia Nairobi, baada ya kuahirishwa kwa zaidi ya saa sita.
Kwa mujibu wa Chama cha Wahudumu wa Usafiri wa Anga nchini
Kenya (KAAO), Shirika la Mashirika ya Ndege Afrika (AFRAA) na Shirikisho la
Utalii nchini Kenya (KTF), hasara iliyopatikana katika siku mbili za mgomo
huenda ikafikia dola bilioni moja za Marekani, sawa na ilivyoshuhudiwa mwezi
Februari mwaka huu wakati Chama cha Wafanyakazi wa Viwanja vya Ndege nchini
Kenya (KAWU) kilipoitisha mgomo mwingine.
Kulingana na mwandishi huru na mtaalamu wa masuala ya
uchumi, Julian Amboko, Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Jomo Kenyatta (JKIA) una
umuhimu mkubwa kwa wasafiri wengi, hasa kutoka Afrika Magharibi ambao hutegemea
Kenya Airways kwa usafiri wao. Kwa sababu hiyo, safari nyingi kutoka eneo hilo
hupitia Nairobi, huku wengi wakitumia uwanja huo kuunganisha safari kuelekea
Ulaya, Mashariki ya Kati, Asia na mataifa ya Kusini mwa Afrika.
Wengi wameulizia iwapo viwanja vingine vya ndege katika
ukanda wa Afrika Mashariki vinaweza kuziba pengo linaloachwa wazi wakati wa
matatizo kama yale yaliyoshuhudiwa nchini Kenya katika siku mbili zilizopita.
Kulingana na Amboko, ikiwa Kenya haitafanya juhudi za
kupanua JKIA au kujenga uwanja mpya wa ndege, upanuzi wa viwanja vya ndege na
ujenzi wa viwanja vipya katika mataifa jirani unaweza kuiondoa JKIA katika
nafasi yake ya sasa kama kitovu kikuu cha usafiri wa anga katika ukanda huo kwa
kuzingatia idadi ya wasafiri wanaopita katika uwanja huo kila siku.
Baada ya mazungumzo ya siku nzima, Waziri wa Uchukuzi wa
Umma nchini Kenya, Davis Chirchir, alitangaza kwamba pande hizo zilikubaliana
kuwa ada za wakala zinazoshikiliwa na Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Kenya (KAA)
zitarejeshwa kwa KAWU mara moja.
Kuhusu masuala ya Mkataba wa Majadiliano ya Pamoja (CBA) wa
KCAA, Tume ya Mishahara na Marupurupu (SRC) imejitolea kuwashirikisha wahusika
ndani ya mfumo husika wa kisheria na kiudhibiti, kwa kuzingatia uwezo wa
mashirika ya serikali yanayohusika kulipa.
Suala la mkataba wa utambuzi kati ya KAWU na Jambojet
linasubiri maelekezo ya mahakama. Pande hizo zimesema zinaheshimu mchakato
unaoendelea wa kimahakama na zitaendelea kuongozwa na matakwa yote ya kisheria
na kiutaratibu yanayohusiana na suala hilo.
Huku mgomo ukisitishwa kwa sasa, pande husika zinatarajiwa
kuendelea kufanya vikao vya kutatua malalamiko yaliyosalia ya wafanyakazi hao
katika wiki chache zijazo.
Kwa sasa, kampuni kama Kenya Airways na Jambojet zimetangaza
kurejelewa kwa safari za ndege, huku wasafiri wengi wakielekea viwanjani
kuthibitisha iwapo wataweza kusafiri kwa muda uliopangwa.
Axios: Trump anafikiria mashambulizi madogo dhidi ya Iran ili kukabiliana na tishio kwa usafiri wa meli
Chanzo cha picha, Getty Images
Axios,
ikinukuu maafisa wa Marekani, iliripoti kuwa Donald Trump anafikiria kufanya
mashambulizi madogo dhidi ya mifumo ya makombora na rada ya Iran ili kuzuia
mashambulizi dhidi ya meli katika Lango la Hormuz.
Rais wa
Marekani Donald Trump na wasaidizi wake wakuu wanatafakari uwezekano wa kufanya
mashambulizi madogo katika Lango la Hormuz, kulingana na maafisa watatu wa
Marekani.
Inasemekana
kuwa wanataka kuzuia "kujengwa upya kwa uwezo wa rada na makombora wa
Iran."
Usiku wa
kuamkia leo, shambulio la Marekani dhidi ya maeneo fulani nchini Iran
lilisababisha vifo vya watu watatu na majeraha kwa wengine kadhaa. Mara baada
ya shambulio hilo, Iran ililenga kambi za Marekani nchini Jordan.
Waziri wa Jeshi la Marekani ajiuzulu baada ya miezi kadhaa ya kutoelewana na Hegsett
Chanzo cha picha, Reuters
Kwa mujibu
wa gazeti la Wall Street Journal, Katibu wa Jeshi la Marekani Daniel Driscoll
amewasilisha barua yake ya kujiuzulu kwa Rais Donald Trump kufuatia miezi
kadhaa ya mvutano na kutoelewana na Waziri wa Ulinzi wa Marekani Pete Hegsett,
na anatarajiwa kuondoka Pentagon katika siku zijazo.
Gazeti la
Wall Street Journal liliripoti siku ya Jumatatu kuwa kutoelewana huko kati ya
Driscoll na Hegsett kulikuwa kukiongezeka kuhusiana na mwelekeo wa baadaye wa
vikosi vya ardhini vya Jeshi la Marekani na uondoaji wa makamanda kadhaa wa
ngazi ya juu wa jeshi hilo.
Ikulu ya
Marekani imesifu utendaji kazi wa Bw. Driscoll, ikisema alitekeleza vyema
mpango wa ulinzi wa Trump, akisaidia kuongeza utayari na uwezo wa kivita wa
jeshi, pamoja na kushiriki katika mazungumzo kati ya Urusi na Ukraine.
Hatua ya
Driscoll kujiuzulu pia inachanganya hali ya usimamizi ndani ya jeshi la
Marekani.
Kwa mujibu
wa Wall Street Journal, baada ya kuondoka kwake, jeshi la Marekani halitakuwa
na afisa yeyote, iwe raia au mwanajeshi, aliyethibitishwa na Seneti kuongoza
jeshi hilo.
Iran yaliandikia barua Baraza la Usalama kufuatia shambulio la Marekani mjini Lark
Siku ya
Jumatatu, balozi wa kudumu wa Iran katika Umoja wa Mataifa, kupitia barua rasmi
kwa Katibu Mkuu wa umoja huo, alilaani shambulio jipya la Marekani dhidi ya
Kisiwa cha Lark na kuonya kwamba: "Marekani na pande zote zinazosaidia,
kuwezesha, kuunga mkono, au kushiriki kwa namna yoyote ile katika maandalizi,
utekelezaji, au kufanyika kwa vitendo vya uchokozi na vitendo vingine haramu
vya Marekani, zitawajibika kikamilifu kwa matokeo mabaya ya vitendo hivyo
haramu, ikiwa ni pamoja na uharibifu na hasara zote zinazotokana navyo, hasa
madhara makubwa yaliyowapata wananchi wa Iran."
Makao Makuu
ya Jeshi la Iran pia yaliyaonya mataifa ya eneo hilo siku ya Jumatatu kwamba,
iwapo mashambulio ya Marekani dhidi ya nchi hiyo yangeanzishwa au kufanywa
kutokea katika ardhi yao, Jeshi la Iran lingejibu kwa kulenga "chanzo cha
mashambulio hayo" kupitia operesheni za kijeshi.
Barua ya
Iran ya siku ya Jumatatu kwa Baraza la Usalama ilisema: "Iran pia inatoa
wito kwa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa na Baraza la Usalama kuitaka Marekani
kusitisha na kukomesha mara moja ukiukaji wake wa Mkataba wa Umoja wa Mataifa
pamoja na vitendo vyake vya uchokozi vinavyotishia uhuru wa usafiri wa majini
na usalama wa baharini katika Ghuba ya Uajemi na Lango la Hormuz."
Kampuni yatoa zawadi kumtafuta aliyeiba lori zima la bia
Chanzo cha picha, Getty Images
Kampuni ya
kutengeneza bia ya Pabst Brewing Company imegeukia mitandao ya kijamii kuomba
msaada wa kutafuta maelfu ya makopo ya bia yake ya Pabst Blue Ribbon (PBR)
yaliyoibwa kutoka kituo cha usambazaji huko California.
"TUMEIBIWA,"
kampuni hiyo ilitangaza. "Kwa mwizi huyo: hatukulaumu kwa kutaka kujivunia
kwa marafiki zako kuhusu kiasi kikubwa cha bia ya PBR ulicho nacho, tunatamani
tu ungeipata kwa njia halali na ya heshima."
Kwa mujibu
wa polisi, mtuhumiwa aliwasilisha nyaraka bandia katika kituo cha usambazaji
cha Anheuser-Busch mjini Montclair na kufanikiwa kuondoka na mzigo wa bia wenye
thamani ya dola za Marekani 25,000 (takriban pauni 18,500), ambao ulikuwa
umepangwa kupelekwa San Diego.
Pabst
imesema "inafuatilia kwa karibu sana" tukio hilo ambalo imeeleza kuwa
ni "la kushangaza na la kipuuzi", na sasa inatoa zawadi kwa yeyote
atakayesaidia kupatikana kwa bia hiyo yenye uzito wa pauni 40,000 (sawa na kilo
18,144).
Polisi wa
Montclair walisema kuwa huo ulikuwa wizi wa pili kutokea siku hiyo hiyo katika
kituo hicho hicho cha usambazaji. Wapelelezi wanachunguza iwapo matukio hayo
mawili yalikuwa sehemu ya operesheni moja ya uporaji wa mizigo kwa kutumia
nyaraka za udanganyifu.
Katika tukio
la kwanza, mzigo wenye thamani ya dola 45,000 (takriban pauni 33,000) uliokuwa
ukielekea Tucson, Arizona, ulichukuliwa tarehe 17 Agosti lakini haukuwahi
kufika ulipokusudiwa hata baada ya wiki mbili.
Saa moja
baadaye, polisi wanasema kuwa wezi walitumia nyaraka bandia kuchukua mzigo wa
bia ya Pabst Blue Ribbon.
"Wachunguzi
wamebaini kufanana kwa matukio haya mawili," polisi walisema. "Taarifa
zilizotolewa kuhusu kampuni ya usafirishaji, dereva na magari yaliyohusika zina
dosari na tofauti zinazoshukiwa, na kwa sasa zinaendelea kuchunguzwa."
Mgomo wa wafanyakazi katika uwanja wa JKIA Nairobi wasitishwa
Maelezo ya picha, Wasafiri walikwama katika uwanja wa JKIA kufuatia mgomo uliotatiza safari za ndege
Wadau wa
sekta ya uchukuzi, wakiongozwa na Waziri wa Uchukuzi Davis Chirchir, wanasema
wafanyakazi wa sekta ya anga wamekubali kusitisha mgomo baada ya kufikia
mwafaka wa kurejea kazini, hatua inayofungua njia kwa shughuli kurejea katika
hali ya kawaida.
Mgomo huo,
ulioanza tarehe 30 Agosti 2026, ulisababisha ucheleweshaji wa zaidi ya saa sita
na kufutwa kwa safari nyingi za ndege, na kuwaacha maelfu ya wasafiri wakiwa
wamekwama.
Wafanyakazi
walilalamikia masuala ikiwemo makubaliano ya pamoja yaliyokwama, wasiwasi wa
kuajiri wafanyakazi, na mapendekezo ya mabadiliko ya usimamizi wa uwanja wa
ndege.
Kufuatia
makubaliano hayo Muungano wa wafanyakazi hao KAWU tayari umewataka kurudi
kazini mara moja .
"Tunasitisha mgomo wetu na kuwaomba wanachama wetu kuanza mchakato wa kurejesha shughuli na huduma katika hali ya kawaida," Ndiema aliambia mkutano na waandishi wa habari.
"Kwa wale walio kazini, tunawaomba waanze kushughulikia safari za ndege." alisema Mkuu wa chama cha wafanyakazi wa sekta ya anga.
Kwa sasa shughuli za
uwanja wa ndege zinaendelea kurejea katika hali ya kawaida, ingawa abiria
wanashauriwa kuthibitisha ratiba moja kwa moja na mashirika yao ya ndege.
Mgomo huo, uliohusisha hasa maafisa wa kudhibiti usafiri wa anga siku ya Jumapili na Jumatatu, ulivuruga safari kadhaa za ndege zinazoingia na kutoka katika Uwanja Mkuu wa Ndege wa Kimataifa wa Jomo Kenyatta, huku ucheleweshaji ukisambaa hadi kwenye viwanja vya ndege vya kanda hiyo katika Afrika Mashariki na maeneo mengine.
Aliyekuwa kiongozi wa genge la Crips apatikana na hatia ya mauaji ya Tupac Shakur
Chanzo cha picha, AFP via Getty
Aliyekuwa
kiongozi wa genge la uhalifu, Duane "Keffe D" Davis, amepatikana na
hatia ya kupanga mauaji ya Tupac Shakur – hii ikiwa ni hukumu ya kwanza katika
kesi ya muda mrefu ambayo haikutatuliwa na iliyowavutia mashabiki wa muziki wa
hip-hop kwa karibu miaka 30.
Baraza la
wazee wa mahakama lilimkuta Davis na hatia ya shtaka moja la mauaji kwa kutumia
silaha hatari kuhusiana na kifo cha nyota huyo wa rap, aliyeuawa kwa kupigwa
risasi kutoka kwenye gari linaloenda kasi jijini Las Vegas mnamo tarehe 7
Septemba 1996.
Akiwa amevaa
suti nyeusi, mwanamume huyo mwenye umri wa miaka 63 alisimama bila kuonyesha
hisia zozote mahakamani huko Las Vegas wakati hukumu ikisomwa, kabla ya kusema
kuwa atakata rufaa.
Jamaa wa
Shakur walishikana mikono, huku baadhi yao wakikumbatiana na kulia.
Shakur
alikuwa na umri wa miaka 25 alipouawa akiwa katika kilele cha taaluma yake kama
mmoja wa wasanii wenye ushawishi mkubwa katika muziki wa rap.
Amefanikiwa kuuza zaidi ya rekodi milioni 75
duniani kote.
Meli nyengine ya kubeba mafuta yashambuliwa katika mlango bahari wa Hormuz
Chanzo cha picha, Reuters
Shirika la
Uingereza la Operesheni za Biashara ya Baharini (UKMTO) limetangaza kuwa meli nyengine
ya kubeba mafuta katika Lango la Hormuz imeshambuliwa.
Kulingana na
ripoti hiyo, meli hiyo ililengwa "wakati ikipita na kutoka katika Lango la
Hormuz."
Shirika hilo
la Uingereza limesema tukio hilo lilitokea kilomita 31 mashariki mwa eneo la
Khasab nchini Oman, likihusisha "makombora matatu ambayo
hayakutambulika."
Hakuna
ripoti za majeruhi au vifo kutokana na shambulio hilo kufikia sasa.
Saa moja
kabla ya ripoti hiyo kutolewa, vyanzo vya habari visivyo rasmi nchini Iran
viliripoti kuwa makombora matatu yalikuwa yamerushwa kutoka pwani ya kusini mwa
Iran.
Kama
tulivyotangaza hapa muda mfupi uliopita, Mamlaka ya Uingereza ya Operesheni za
Meli za Biashara ilitangaza tukio jingine la baharini siku ya Jumatatu, lakini
ilibainisha kuwa tukio hilo katika Bahari ya Hindi lilitokea siku ya Jumapili,
tarehe 30 Agosti.