Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.

Bofya kuelekea tovuti kuu

Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data

Moja kwa moja, Rais wa Zambia ashinda muhula wa pili kwa asilimia 60 ya kura

Mpinzani wake mkuu, Brian Mundubile awali alijitangazia ushindi na kudai bila kutoa ushahidi kwamba kulikuwa na kasoro katika shughuli ya upigaji kura.

Moja kwa moja

Na Ambia Hirsi & Mariam Mjahid

  1. Ndugu wa Bashar al Assad ahukumiwa kifo nchini Syria

    Mahakama nchini Syria imemhukumu kifo Wassim al Assad, binamu wa Rais wa zamani wa Syria Bashar al Assad, aliyeondolewa madarakani.

    Wassim al Assad amepatikana na hatia ya makosa kadhaa, yakiwemo mauaji yaliyopangwa, yaliyotekelezwa wakati wa vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini Syria. Alikamatwa mwezi Juni.

    Uamuzi huo umetolewa wiki moja baada ya Bashar al Assad na kaka yake pia kuhukumiwa kifo bila kuwepo mahakamani, baada ya kutuhumiwa kufanya uhalifu dhidi ya ubinadamu.

    Bashar al Assad na familia yake walikimbilia nchini Urusi baada ya vikosi vya upinzani kuingia katika mji mkuu Damascus mwezi Desemba 2024, na kumaliza utawala wa familia yake uliodumu kwa zaidi ya miaka 50 nchini humo.

  2. Patrick Vieira ateuliwa kuwa kocha mkuu wa Senegal

    Senegal imemteua Patrick Vieira, mshindi wa Kombe la Dunia la 1998 akiwa na Ufaransa, kuwa kocha mkuu wa timu ya taifa, Shirikisho la Soka la Senegal limetangaza Jumanne.

    Vieira anachukua nafasi ya Pape Thiaw, aliyefutwa kazi baada ya Kombe la Dunia lililopita.

    Vieira, ambaye ni raia wa zamani wa Ufaransa, ameripotiwa kufikia makubaliano na Shirikisho la Soka la Senegal, FSF, ya kuiongoza timu hiyo kwa mkataba wa miaka minne.

    Mkataba huo unatarajiwa kujumuisha maandalizi ya Senegal kuelekea Kombe la Mataifa ya Afrika la 2027, AFCON, pamoja na mchakato wa kufuzu na maandalizi ya Kombe la Dunia la 2030.

    Lengo la haraka la Vieira linadaiwa kuwa kuiongoza Senegal kufika angalau fainali ya AFCON 2027, huku kwa muda mrefu akitarajiwa kuiwezesha timu hiyo kufuzu Kombe la Dunia la 2030 na kujenga kikosi kitakachoiweka Senegal miongoni mwa mataifa yanayoongoza kwa soka barani Afrika.

    Shirikisho hilo limesema uteuzi wa Vieira, aliyezaliwa Senegal, ni “hatua ya kimkakati” inayolenga “kuanzisha mfumo wa kiufundi wa kiwango cha juu, unaoendana na malengo ya michezo ya nchi”.

    Kwa mujibu wa taarifa ya BSN Sports, Vieira anatarajiwa kulipwa kati ya faranga milioni 35 na 45 za CFA kwa mwezi, sawa na takriban dola 61,600 hadi 79,200 za Marekani.

    Vieira alizaliwa mjini Dakar mwaka 1976 na akawa mmoja wa viungo mashuhuri zaidi wa kizazi chake. Alitumia sehemu kubwa ya maisha yake ya soka la klabu katika Arsenal, ambako alikuwa nahodha na alisaidia klabu hiyo kushinda mataji matatu ya Ligi Kuu ya England, ikiwemo msimu maarufu wa 2003 hadi 2004 ambao Arsenal haikupoteza mchezo wowote.

    Pia aliwahi kuchezea Juventus, Inter Milan na Manchester City kabla ya kustaafu soka la ushindani.

    Akiwa na timu ya taifa ya Ufaransa, Vieira alicheza mechi 107 na alikuwa sehemu ya kikosi kilichoshinda Kombe la Dunia la FIFA mwaka 1998 nchini Ufaransa. Pia alishinda Mashindano ya Ulaya mwaka 2000 akiwa na Ufaransa.

    Uhusiano wake na Senegal ni wa karibu, kwa kuwa alizaliwa Dakar na ameendelea kudumisha uhusiano na nchi hiyo.

    Vieira pia ana uhusiano na Diambars, akademi ya soka na mradi wa kukuza vipaji nchini Senegal ambao umetoa wachezaji kadhaa wenye vipaji.

  3. AU yaonya mataifa ya kigeni dhidi ya kuchochea vita Sudan

    Umoja wa Afrika, AU, umeonya kuwa kuingiliwa kwa mzozo wa Sudan na mataifa ya kigeni, pamoja na juhudi za kuunda serikali pinzani, kunahatarisha kurefusha vita na kuvuruga umoja wa nchi hiyo.

    Onyo hilo limetolewa wakati wa ziara ya siku mbili ya ujumbe wa Baraza la Amani na Usalama la AU nchini Sudan, unaolenga kuhimiza usitishaji wa mapigano, kurahisisha upatikanaji wa misaada ya kibinadamu na kufufua mazungumzo ya amani.

    Katika mazungumzo na Mkuu wa Jeshi la Sudan, Abdel Fattah al Burhan, mjini Khartoum, ujumbe huo umesisitiza kuwa mazungumzo na suluhisho la kisiasa linaloongozwa na Wasudan ndiyo njia pekee ya kufikia amani ya kudumu.

    Sudan imekuwa katika vita tangu mwaka 2023. Jeshi linadhibiti sehemu kubwa ya Khartoum na maeneo ya kati ya nchi, huku Kikosi cha Msaada wa Haraka, RSF, kikidhibiti maeneo makubwa ya Darfur.

    RSF na washirika wake pia wameunda muungano wa kisiasa unaolenga kuanzisha serikali pinzani.

    AU inataka mpito wa kisiasa unaowashirikisha wadau wote na unaoongozwa na Wasudan, ambao hatimaye utawezesha kuundwa kwa serikali ya kikatiba kupitia uchaguzi.

    Vile vile wanalenga kuzishinikiza Jeshi la Sudan, SAF, na Kikosi cha Msaada wa Haraka, RSF, kukubali usitishaji wa mapigano, kuhakikisha misaada inawafikia wanaohitaji na kulinda mchakato wa kisiasa utakaowawezesha Wasudan kuamua mustakabali wa nchi yao bila kutawaliwa na makundi hayo mawili yenye silaha.

    Ingawa upatanishi unaoongozwa na Waafrika umefanikiwa katika migogoro mingine, mzozo wa Sudan unaendelea kuwa changamoto kubwa. Tofauti na mgogoro wa kisiasa uliotokea Kenya baada ya uchaguzi wa mwaka 2007, ambapo upatanishi ulioungwa mkono na AU uliwezesha kufikiwa kwa makubaliano ya kugawana madaraka, mzozo wa Sudan unahusisha majeshi mawili yenye silaha nzito yanayodhibiti maeneo tofauti na ambayo bado yanaamini kuwa yanaweza kuimarisha nafasi zao kupitia matumizi ya nguvu.

    Ujumbe huo umefika Sudan wakati vita vikiwa katika hatua muhimu. Jeshi la Sudan, SAF, limerejesha udhibiti wa sehemu kubwa ya mji mkuu Khartoum, huku RSF ikiendelea kushikilia maeneo mengi ya Darfur, magharibi mwa nchi.

    Kordofan, eneo linalounganisha sehemu za kati, magharibi na kusini mwa Sudan, pia limekuwa kitovu kingine cha mapigano.

  4. Vijana wawili wamuua kiongozi wa wanamgambo hatari Somalia

    Serikali ya Somalia imesema vijana wawili wafugaji wamemuua mmoja wa viongozi hatari zaidi wa wanamgambo wanaofanya shughuli katika eneo hilo, jana Agosti 17, 2026, katika wilaya ya Ruunirgood, mkoani Middle Shabelle.

    Katika taarifa iliyotolewa na Wizara ya Ulinzi ya Somalia, wizara hiyo imesema kiongozi aliyeuawa ni Hassan Alasow Raage, anayefahamika pia kama Hassan Xusuleey. Alikuwa na umri wa miaka 50 na alizaliwa katika wilaya ya Ruunirgood.

    Kwa mujibu wa wizara hiyo, Hassan Alasow Raage alikuwa miongoni mwa viongozi wa wanamgambo wanaofanya shughuli katika mkoa wa Middle Shabelle, pamoja na kuwa kiongozi wa usafirishaji wa eneo hilo. Pia aliwahi kuwa mkuu wa kundi linaloitwa Sakawad katika wilaya ya Ruunirgood, na alikuwa akifahamika katika wilaya hiyo na maeneo ya jirani.

    Taarifa hiyo imesema, “Vijana hao wawili walimuua kiongozi huyo, kisha wakachukua bunduki yake aina ya AK 47 pamoja na risasi.”

    Wizara hiyo imeongeza kuwa kiongozi huyo alikuwa chanzo cha matatizo kwa wakazi wa wilaya hiyo na maeneo jirani, ikiwa ni pamoja na uporaji wa mali na mifugo, kuweka vikwazo na kuvuruga usafiri, hali iliyowalazimu watu wengi kuikimbia wilaya hiyo.

    Wizara ya Ulinzi imepongeza juhudi za wakazi wa eneo hilo katika kupambana na wanamgambo wa Khawarij, ikisema hatua hiyo inaonyesha kuwa wananchi wa Somalia wameamua kushiriki kikamilifu katika mapambano dhidi ya ugaidi.

  5. Rais Samia na Tshisekedi wajadili biashara, uwekezaji na usalama wa kikanda

    Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, amempokea Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, Felix Tshisekedi, katika Ikulu Ndogo ya Zanzibar, kwa ziara ya kikazi ya siku mbili nchini Tanzania.

    Mazungumzo ya viongozi hao yamejikita katika kuimarisha biashara na uwekezaji, sekta za madini na nishati, pamoja na masuala ya usalama wa kikanda.

    Rais Samia amesema wamejadili pia hali ya usalama nchini DRC, huku akimpongeza Tshisekedi kwa juhudi zake za kuleta amani na utulivu nchini humo.

    “Pamoja na kujadili hali ya usalama nchini DRC, nimempongeza Mheshimiwa Rais Tshisekedi kwa juhudi zake za kuleta amani na utulivu, pamoja na kutafuta suluhisho la kudumu la changamoto za kiusalama,” amesema Rais Samia.

    Hii ni mara ya tatu kwa Tshisekedi kutembelea Tanzania tangu alipoingia madarakani mwaka 2019.

    Ziara hiyo inafanyika wakati hali ya usalama mashariki mwa DRC ikiendelea kuwa changamoto, huku juhudi za kidiplomasia zikilenga kupata suluhisho la kudumu la mzozo huo.

  6. Iran yasema haitafungua Mlango wa Hormuz hadi Marekani itekeleze masharti ya makubaliano

    Spika wa Bunge la Iran, Mohammad Baqer Qalibaf, amesisitiza kuwa Iran haitafungua Mlango wa Hormuz hadi Marekani itekeleze masharti yote ya makubaliano yaliyofikiwa kati ya nchi hizo mbili.

    Qalibaf amesema Iran inataka vikwazo ilivyowekewa viondolewe, mali zake zilizotaifishwa ziwasilishwe, vikwazo dhidi ya mauzo ya mafuta viondolewe na vitisho vyote vya kijeshi dhidi yake vikomeshwe kabla ya njia hiyo kufunguliwa.

    Pia ameonya kuwa Iran iko tayari kujibu vikali iwapo itashambuliwa tena.

    Kauli yake imekuja baada ya maafisa wa Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu la Iran kutoa msimamo kama huo, wakati muda wa siku 60 uliowekwa na makubaliano hayo ukimalizika bila kufikiwa kwa makubaliano ya kina.

    Kwa upande wake, Rais wa Marekani Donald Trump amesema hana nia ya kuongeza muda wa makubaliano ya muda na Iran.

    Soma zaidi:

  7. 'Umaarufu wa Trump uko katika kiwango cha chini kabisa kuwahi kurekodiwa kutokana na vita vya Iran'

    Utafiti mpya wa maoni uliofanywa na Reuters na Ipsos unaonyesha kuwa kiwango cha kukubalika kwa Rais wa Marekani Donald Trump kimeshuka hadi asilimia 33, kiwango cha chini zaidi tangu alipoingia madarakani.

    Utafiti huo pia umeonyesha kuwa vita dhidi ya Iran ni miongoni mwa masuala yanayowatia wasiwasi mkubwa Wamarekani, huku asilimia 80 wakisema wana hofu kuhusu uwezekano wa vita vya muda mrefu kati ya Marekani na Iran.

    Hata hivyo, ni asilimia 33 pekee walioidhinisha namna Trump anavyoendesha utawala wake, huku asilimia 64 wakisema hawaridhishwi na mtindo wake wa uongozi.

    Kiwango cha kukubalika kwa Trump kimeshuka kutoka asilimia 35 mwezi uliopita, hali inayokaribia kiwango chake cha chini zaidi cha umaarufu katika muhula wake wa kwanza, kilichorekodiwa Desemba 2017.

    Tangu Trump alipoamuru mashambulizi ya pamoja ya Marekani na Israel dhidi ya Iran, umaarufu wake umeendelea kushuka kwa kiasi kikubwa mwaka huu.

    Vita kati ya Marekani na Israel dhidi ya Iran pia vilisababisha kufungwa kwa Mlango wa Hormuz, njia muhimu inayotumika kusafirisha takriban moja ya tano ya mafuta ghafi yanayouzwa duniani. Hatua hiyo imesababisha bei ya mafuta kupanda nchini Marekani.

  8. Afisa wa FIFA afutwa kazi baada ya kukosoa mpango wa Infantino

    Alikuwa mmoja wa wakosoaji wakubwa wa mipango ambayo baadae ilifutiliwa mbali ya rais wa FIFA Gianni Infantino, ya kuuza hisa za Kombe la Dunia na michuano mingine kwa wawekezaji binafsi.

    Katika taarifa, msemaji wa FIFA alithibitisha tu kwamba “ushirikiano wa kikazi kati ya FIFA na Kevin Lamour katika nafasi ya Afisa Mkuu wa Uendeshaji umekamilika tarehe 17 Agosti 2026.”

    “FIFA inamshukuru Kevin kwa miaka yake miwili ya huduma na inamtakia kila la heri katika maisha yake ya baadaye.”

    Mwezi uliopita, Bwana Lamour alisema kuwa mipango ya kuuzia wawekezaji binafsi hisa iliwahadaa wafanyakazi wa FIFA na kuutaja mradi huo kama "mradi wa mtu mmoja."

    Soma zaidi:

  9. Rais wa Zambia ashinda muhula wa pili kwa asilimia 60 ya kura

    Rais wa Zambia Hakainde Hichilema amechaguliwa tena kwa muhula wa pili wa miaka mitano baada ya kupata asilimia 60 ya kura zilizopigwa, Tume ya Uchaguzi imetangaza.

    Ushindi wa Hichilema ulitarajiwa sana, huku mpinzani wake mkuu Brian Mundubile akipata asilimia 38 ya kura.

    Wagombea wengine 12 waliachwa nyuma kwa kiasi kikubwa.

    Chini ya mfumo wa uchaguzi wa Zambia, mgombea anahitaji zaidi ya asilimia 50 ya kura ili kushinda katika duru ya kwanza na kuepuka duru ya pili.

    Matokeo hayo yalitolewa baada ya mchakato uliokumbwa na mvutano, huku Mundubile, mwenye umri wa miaka 55, awali akidai ushindi na kudai—bila kutoa ushahidi—kwamba kulikuwa na kasoro katika upigaji kura.

    Katika taarifa yake baada ya kutangazwa mshindi, Hichilema, mwenye umri wa miaka 64, alisema: "Tumeguswa sana na imani mliyoiweka mikononi mwetu."

    Alisema uchaguzi huo ulionyesha kuwa Zambia ni taifa la amani, sheria na utulivu, na "taifa la kidemokrasia linalotatua tofauti zake kupitia sanduku la kura, na si mahali pengine popote."

    "Kwa wananchi waliopendelea mawazo yaliyowasilishwa na wapinzani wetu, tunawasikia, na tutaendelea kuwatumikia," aliongeza.

    Mamia ya wafuasi wa Hichilema, waliovalia rangi nyekundu za chama chake cha UPND, walifurika mitaani katika mji mkuu, Lusaka, kusherehekea baada ya kutangazwa kwa matokeo hayo.

    Zambia ina historia ya makabidhiano ya madaraka kwa amani.

    Tangu kurejea kwa mfumo wa demokrasia ya vyama vingi mwaka 1991, mabadiliko ya uongozi wa urais yamefanyika kupitia uchaguzi.

    Haijabainika kama upinzani utapinga matokeo ya uchaguzi.

    Maelezo zaidi:

  10. Meli 'yashambuliwa' katika Mlango wa Bahari wa Hormuz

    Shirika la Uendeshaji Biashara ya Baharini la Uingereza linasema limepokea ripoti kwamba meli moja imelengwa na kifaa kisichojulikanakilichorushwa kutoka angani wakati ilipokuwa ikipita kwenye Mlango-Bahari wa Hormuz.

    Shirika hilo liliongeza kuwa tukio hilo lilisababisha uharibifu wa chumba cha injini na kifo cha mfanyakazi mmoja.

    Kulingana na ripoti hiyo, Walinzi wa Pwani wa Oman kwa sasa wako mbioni kuwaokoa wafanyakazi wengine wa meli hiyo.

    Kwa mujibu wa Shirika la Uendeshaji Biashara ya Baharini la Uingereza, hakuna uharibifu wa mazingira ulioripotiwa kutokana na tukio hilo na mamlaka zinachunguza.

    Tukio hili linajiri wakati ambapo usafirishaji katika Mlango-Bahari wa Hormuz unaendelea kukabiliwa na usumbufu mkubwa na idadi ya meli zinazosafiri kupitia njia hiyo imepungua sana; zaidi ya meli 130 zilikuwa zikipita hapita hapo kwa siku kabla ya kuanza kwa vita kati ya Marekani na Israeli dhidi ya Iran.

    Awali Rais Donald Trump aliwaambia waandishi wa habari katika Ikulu ya White House kwamba hana mpango wa kurefusha makubaliano ya muda na Iran, na kwamba aliamini Tehran haiko tayari kufikia makubaliano ambayo yeye anayaona kuwa muhimu.

    Soma Zaidi:

  11. Afisa wa Polisi na raia wawili wafariki dunia katika vurugu za Linda Mwananchi, Kenya

    Afisa mmoja na raia wawili wamefariki dunia, huku wengine wkijeruhiwa kutokana na ghasia za zilizokumba mkutano wa kisiasa wa Linda Mwananchi katika eneo la Homa Bay, nchini Kenya.

    Afisa huyo ambaye alipigwa jiwe kichwani alikimbizwa katika hospitali moja katika Kaunti ya Kisumu, ambako alifariki dunia alipokuwa akipokea matibabu.

    Polisi imetoa taarifa na kusema kuwa washukiwa 37 wamekamatwa baada ya kupatikana na silaha mbalimbali za kienyeji, zikiwemo mapanga, kamba, vyuma, visu, marungu, fimbo za polisi na tochi.

    Kukamatwa kwao ni sehemu ya operesheni inayoendelea dhidi ya wahalifu na makundi ya vijana wanaosababisha vurugu nchini humo, wakiwemo wale wanaoshukiwa kuhusika na ghasia zilizoshuhudiwa Homa Bay siku ya Jumapili.

    Katika taarifa iliyotiwa saini na Msemaji wa Huduma ya Kitaifa ya Polisi (NPS), Muchiri Nyagah, alisema washukiwa hao watachukuliwa hatua za kisheria na kufikishwa mahakamani ili kujibu mashtaka yanayowakabili.

    Aliongeza kuwa polisi wanamsaka Oliver Jaoko, anayejulikana kwa jina la “Olivetti,” ambaye ameelezwa kujisalimisha katika kituo cha polisi kilicho karibu ili kusaidia katika uchunguzi unaoendelea. Wakati huo huo, operesheni ya kumkamata yeye pamoja na watu wengine wote wanaoshukiwa kuhusika na vurugu hizo inaendelea.

    Vurugu hizo zimezua taharuki kubwa kisiasa huku waandaaji wa vuguvugu la Linda Mwananchi wakiwatuhumu baadhi ya watu wasiotajwa majina katika siasa na usalama kwa kuhusika na kile wanachodai kuwa ni shambulio lililoratibiwa. Hata hivyo, madai hayo hayajathibitishwa kwa njia huru.

    Katika taarifa iliyotolewa Jumatatu, vuguvugu hilo lilisema msafara wake ulikumbana na vizuizi barabarani kuanzia mpaka wa Kisumu na Homa Bay, kupitia barabara za Homa Bay–Migori na Migori–Kisii.

    Vuguvugu hilo lilidai kuwa makundi yaliyokuwa yakishambulia msafara huo yalionekana kushirikiana na maafisa wa polisi.

    Soma Zaidi:

  12. Mzozo wa Ukraine: Urusi yaionya Uingereza - kunani?

    Urusi imeishutumu Uingereza kwa "kuchochea mzozo wa Ukraine" kufuatia uthibitisho kwamba ndege zisizo na rubani zilizotengenezwa Uingereza zilitumika kushambulizi maeneo yaliyolengwa nchini Urusi.

    "Kwa kufanya hivyo, Uingereza inashiriki kama msaidizi na mhusika mwenza katika uhalifu wa umwagaji damu na mashambulizi ya kigaidi," ilisema taarifa kutoka Ubalozi wa Urusi nchini Uingereza.

    "London bila shaka italazimika kuwajibikia hatua yake," ilisema taarifa hiyo, huku ikiongeza kuwa kadiri inavyozidi kujihusisha na mgogoro huo, "ndivyo gharama itakayolipa itakavyokuwa kubwa zaidi."

    Msemaji wa Wizara ya Ulinzi (MoD) amembia BBC kuwa Uingereza inasimama "bega kwa bega" na Ukraine.

    "Urusi haipaswi kuwa na shaka yoyote kuhusu azimio la Serikali hii la kupinga uchokozi wa wake, iwe ni nchini Ukraine au dhidi ya Uingereza na washirika wetu," alisema msemaji huyo katika taarifa.

    Uingereza iliongeza kuwa "imejitolea kutoa vifaa ambavyo Ukraine inahitaji ili kujilinda dhidi ya uvamizi haramu wa [Rais wa Urusi Vladimir] Putin".

    Ndege hizo zisizo na rubani zilizotengenezwa na kampuni mbili tofauti za Uingereza zimetumika kushambulia kwa mafanikio vituo vya kijeshi na viwandandani ya Urusi, ikiwemo mitambo ya kusafisha mafuta na maghala ya kampuni ya mauzo ya mtandaoni ya Wildberries.

    Ukraine imekuwa ikilenga mara kwa mara kampuni hiyo —ambayo inajulikana kama toleo la Urusi la Amazon—na kusema kuwa vituo saba kati ya 10 vikubwa zaidi vya usafirishaji na uhifadhi bidhaa vya Wildberries "vimesambaratishwa".

    Pia unaweza kusoma:

  13. Wazee wako kwenye hatari kubwa zaidi ya joto kali kuliko ilivyodhaniwa — Utafiti

    Wanasayansi wanaonya kwamba athari za ongezeko la joto duniani kwa afya ya wazee hazijapewa uzingativu unaostahili.

    Watafiti katika Chuo Kikuu cha Stanford nchini Marekani wanasema tafiti zilizopita zililenga zaidi watu wenye umri mdogo ambao wana uwezo mkubwa wa kutoa jasho na wana mioyo yenye nguvu zaidi.

    Wanasema nchi zilizo katika hatari kubwa zaidi ni pamoja na India, Pakistan, Bangladesh na Niger, ambako umaskini na upatikanaji mdogo wa mifumo ya kupoza joto huongeza hatari ya kuathirika.

    Wanasayansi hao wanaonya kuwa joto kali na kuongezeka kwa idadi ya wazee duniani kunaweza kuleta changamoto mpya za kibinadamu, kuongeza shinikizo kwenye sekta ya kilimo, na kuchochea uhamiaji wa kutoka nchi moja hadi nyingine.

    Pia unaweza kusoma:

  14. Mzozo wa Ethiopia waporomosha mfumo wa afya

    Mzozo wa wenyewe kwa wenyewe ulioikabili Ethiopia kwa muda mrefu umesababisha kuporomoka kwa mfumo wa afya kutokana na kulengwa kwake na mashambulizi.

    Ripoti mpya ya utafiti iliyotolewa na Makundi mawili ya Haki za binadamu Physicians for Human Rights -PHR- na lile linalohusiana na masuala ya Haki na Uwajibikaji katika eneo la pembe ya Afrika -OJAH imesema makundi yenye silaha mara kwa mara yamekuwa yakilenga sekta hiyo ya afya katika maeneo yaliyokumbwa ya Tigray, Amhara na Afar.

    Ripoti hiyo inaangazia jinsi makundi yenye silaha yalivyolenga mara kwa mara hospitali, kliniki, na wahudumu wa afya, na hivyo kufanya mashambulizi dhidi ya sekta ya afya kuwa mbinu ya kawaida ya kivita.

    Hiyo ni kwa mujibu wa tathmini iliyofanywa kati ya mwaka wa 2024 na 2026 katika maeneo ya Tigray, Amhara, na Afar.

    Utafiti pia umeonesha kuwa Jeshi la Ethiopia, Jeshi la Ulinzi la Eritrea, Wapiganaji wa Tigray, wanamgambo wa Amhara Fano na polisi wa maeneo hayo walihusishwa katika mashambulizi hayo yaliyodhoofisha huduma za afya.

    Lindsey Green, Naibu Mkurugenzi wa kitengo cha Utafiti katika shirika linalohusika na haki za binadamu la Physicians for Human Rights amesema vitendo vya uporaji au kuuawa kwa mfanyakazi wa afya ni matukio ya mara kwa mara.

    Hali hiyo pia imesababisha eneo la Tigray kuwa na uhaba wa dawa, mafuta, vifaa, pamoja na wafanyakazi wa afya wasiolipwa wakati Amhara migogoro inayoendelea imepunguza upatikanaji wa huduma muhimu.

    Mbali na mashambulizi hayo ripoti hiyo pia imeelezea ukatili wa kingono.

    Ripoti hiyo ya mashirika ya haki za binadamu inaeleza pia kuwa wakati mapigano kwa kutumia silaha yakianza tena katika eneo la Tigray nchini Ethiopia, na kuendelea katika maeneo ya Amhara na Afar, ni lazima vikosi vyote vyenye silaha visitishe mashambulizi ya makusudi dhidi ya hospitali na wahudumu wa afya.

    Mashirika hayo yametoa wito kwa wanajeshi kusitisha mashambulizi ya makusudi dhidi ya hospitali na wafanyakazi wa afya na kuitaka serikali ya Ethiopia na jumuiya ya kimataifa kulinda vituo vya afya, kuwawajibisha wahusika na kutoa haki kwa walionusurika.

    Soma zaidi:

  15. Kushner asema Hamas kuachia silaha katika siku 30 zijazo

    Mjumbe wa Rais wa Marekani ambaye pia ni Mkwe wa Rais Donald Trump Jared Kushner amesema hatua za kuwapokonya sialaha wanamgambo wa Hamas zinasonga mbele na huenda zikaanza kutekelezeka katika kipindi cha mwezi mmoja ujao kuambatana na makubaliano ya amani kuhusu Gaza.

    Baada ya kufanya mazungumzo na Waziri mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu mjini Tel Aviv hapo jana Jumatatu, Bwana Kushner amesema huenda wakaanza kuona matokeo ya yaliyofikiwa katika siku thelathini zijazo na kuwa hilo litaanza kwa kuondolewa kwa silaha Gaza.

    'Ikiwa Hamas watasalimisha silaha na mahandaki yao kwa hiari yao katika muda wa siku 60 hadi 90 zijazo, bila shaka hilo litakuwa ni kuondolewa kwa tishio kubwa la kiusalama kwa Israel, mafanikio makubwa ambayo huenda hayakutarajiwa. Na iwapo hawatatimiza ahadi yao sasa, kila mtu ataona kwamba hawana nia ya dhati kuhusu amani, na kisha Israel itapata uungwaji mkono mkubwa zaidi kutoka Marekani na wengine kwenda na kumaliza kazi hiyo kwa njia inayofaa'.

    Kauli hiyo inakuja baada ya Kushner na Netanyahu kukubaliana kuwa Jenerali wa Jeshi la Marekani ndiye atakahakiki kuwa wanamgambo wa Hamas wanaweka chini silaha zote huku Bwana Netanyahu akisisitiza kuwa majeshi ya Israel hayataondoka katika ukanda wa Gaza hadi pale Hamas itakaposalimisha silaha zake zote.

    Waziri huyo Mkuu wa Israel amekuwa akisita kuridhia makubaliano yaliyosimamiwa na Marekani kuhusu kupatikana amani Gaza, akikabiliwa na shinikizo la kisiasa nchini mwake kutolegeza kamba dhidi ya Hamas.

    Siku ya Jumapili, Bwana Kushner ambaye pia ni rafiki wa muda mrefu wa Netanyahu, alifanya mazungumzo ya ana kwa ana na kiongozi mpya wa Hamas Khalil al-Hayya nchini Misri. Hamas imeahidi kukabidhi silaha zake kwa uongozi mpya wa Palestina utakaosimamia Gaza.

    Netanyahu, waziri mkuu wa Israeli aliyedumu kwa muda mrefu zaidi ambaye hatma yake kisiasa iko mashakani katika uchaguzi unaotarajiwa mwezi Oktoba mwaka huu, anaonekana kuzidi kupinga mitizamo ya mshirika wake wa karibu Rais Trump.

    Waziri mkuu huyo pia ameweka wazi kutoridhishwa kwake na uamuzi wa Trump wa kusitisha vita vya Marekani na Israeli dhidi ya Iran vilivyoanzishwa mwishoni mwa Februari na badala yake kufuata njia ya kutafuta makubaliano na viongozi wa wa Iran.

    Katika mahojiano yaliyoibua hisia kubwa miongoni mwa nchi za Kiarabu, Itamar Ben Gvir, waziri wa usalama wa taifa wa Israel mwenye msimamo mkali wa mrengo wa kulia hivi karibuni alisema kuwa Israeli inapaswa kuua watu 30 hadi 40 kila usiku huko Gaza.

    Kwa upande wake,Rais wa Israel Isaac Herzog, alipokutana na Kushner hapo jana, alisifu juhudi za Bodi ya Amani iliyoanzishwa na Rais Trump kwa kuhakikisha mustakabali mzuri na salama zaidi kwa Israel, Gaza na kanda ya Mashariki ya Kati kwa jumla.

    Operesheni za kijeshi za Israel zimewaua takriban Wapalestina 1,265 tangu makubaliano ya kusitisha vita yalipofikiwa mwezi Oktoba mwaka jana.

    Rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan amemueleza Rais Trump kuwa Israel inawashambulia Wapalestina wa Gaza wakati ambapo awamu ya pili ya makubaliano ya kusitisha vita inapaswa kuwa inatakelezwa.

    Unaweza kusoma Zaidi:

  16. Uturuki iko tayari kuwa mpatanishi kati ya Marekani na Iran - Erdogan

    Rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan amesema ipo haja ya kuendeleza mazungumzo ya kidiplomasia na Iran na Uturuki iko tayari kushiriki katika juhudi hizo.

    Haya yanajiri baada ya Ofisi ya Rais wa Uturuki kutangaza kwamba kiongozi huyo amefanya mazungumzao kwa njia ya simu na mwenzake wa Marekani Donald Trump na kukariri utayari wa Ankara wa kuunga mkono juhudi za amani.

    Awali, mjumbe wa Rais Trump, Jared Kushner,alisema kuwa mazungumzo kati ya Iran na Marekani yalikuwa mazito na ya kina, lakini pande hizo mbili bado hazijafikia mwafaka.

    Bw. Kushner, ambaye pia ni mkwe wa Donald Trump, aliambia kituo cha habari cha Fox News kuwa mazungumzo kati ya Marekani na taasisi mbalimbali za serikali ya Iran.

    Siku ya Jumatatu Waziri wa Mambo ya Nje wa Uturuki, Hakan Fidan, alizungumza kwa simu na mwenzake wa Iran, Abbas Araqchi, kuhusu juhudi za kufungua Mlango-bahari wa Hormuz na kuhakikisha kuwa usitishaji wa uhasama kati ya Iran na Marekani unaendelea.

    Chanzo cha kidiplomasia cha Uturuki kilikataa kutoa maelezo zaidi kuhusu mazungumzo kati ya viongozi hao wawili.

    Soma zaidi:

  17. Hichilema atangazwa mshindi wa uchaguzi wa urais Zambia

    Rais Hakainde Hichilema ametangazwa kuwa mshindi wa uchaguzi wa urais wa Zambia wa mwaka 2026 baada ya kupata zaidi ya asilimia 60 ya kura zilizopigwa.

    Tume ya Uchaguzi ya Zambia (ECZ) ilitangaza matokeo ya mwisho yaliyojumuishwa kutoka majimbo yote 226, yakionyesha kuwa Hichilema, wa chama cha United Party for National Development, alipata kura 2,965,326 (asilimia 60.49). Mpinzani wake mkuu, Brian Mundubile wa chama cha National Reconciliation Party for Unity and Prosperity, alipata kura 1,856,217 (asilimia 37.87). Tofauti ya kura kati ya Hichilema na mpinzani wake ni kura 1,109,109.

    Jumla ya wapiga kura 8,786,300 walisajiliwa kushiriki uchaguzi huo. Wagombea wengine walikuwa nyuma sana, wakiongozwa na Harry Kalaba (Citizens First) aliyepata kura 19,070 na Kelvin Fube Bwalya (Zambia Must Prosper) aliyepata kura 17,078.

    Ushindi wa Hichilema unampa muhula wa pili wa miaka mitano. Chini ya mfumo wa uchaguzi wa Zambia, mgombea anahitaji zaidi ya asilimia 50 ya kura hili kushinda katika duru ya kwanza na kuepuka duru ya pili.

    Matokeo haya yanakuja baada ya mchakato uliokabiliwa na changamoto na malalamiko. Mundubile alikuwa amedai ushindi akiegemea kwenye hesabu huru za kura zilizofanywa na timu yake ya kampeni na kudai kuwepo kwa kasoro nyingi, ikiwemo tofauti kati ya matokeo ya vituo vya kupigia kura na yale yaliyotangazwa na ECZ, pamoja na madai ya kuhusika kwa jeshi katika vituo vya kujumlisha kura.

    Pia aliishutumu Tanzania kwa kutuma watu kuingilia kati uchaguzi huo, madai ambayo serikali ya Tanzania iliyakanusha na kuyataja kuwa ya uongo.

    Bado haijabainika ikiwa upinzani utapinga matokeo hayo ya uchaguzi.

    Siku moja baada ya upigaji kura, ECZ ilisitisha kwa muda zoezi la kuhesabu na kutangaza matokeo, ikitaja ripoti za vurugu dhidi ya wafanyakazi wa uchaguzi na wizi wa karatasi za kura zilizopigwa katika baadhi ya maeneo. Kusitishwa huko kuliondolewa siku hiyo hiyo.

    Waangalizi wa uchaguzi wa kikanda na kimataifa walielezea Siku ya Uchaguzi kuwa ya amani kwa kiasi kikubwa katika vituo walivyofuatilia na kuzitaka pande zote kuwa watulivu na kuheshimu mchakato rasmi. Hichilema sasa anatarajiwa kuanza muhula wake wa pili kama rais wa Zambia.

    Maelezo zaidi:

  18. Karibu kwa matangazo ya moja kwa moja.