Moja kwa moja, Mbunge wa Marekani: Trump na washirika wake wananufaika na vita dhidi ya Iran

Hakuna ushahidi unaothibitisha moja kwa moja madai ya Warren kuhusu uhusiano kati ya michango ya kampeni na faida zinazodaiwa kupatikana kutokana na vita hivyo.

Ruka Video uendelee
  • xx
  • Besigye
  • .
  • xx
  • xx
  • xx
  • Lungu
  • xx
  • xx
  • d
  • s
  • a
  • Sonko
  • xx
  • xx
  • xx
  • xx
  • xx
  • Dangote

Moja kwa moja

Na Ambia Hirsi

  1. Na kufikia hapo tunakamilisha matangazo ya moja kwa moja. Kwaheri.

  2. Niger yadhibiti kambi muhimu ya anga baada ya uasi

    .

    Chanzo cha picha, AFP via Getty Images

    Jeshi la Niger linasema kuwafanikiwa kurejesha udhibiti wa Kambi ya Anga 101, moja ya vituo muhimu vya kijeshi katika mji mkuu wa Niamey, baada ya wanajeshi waasi kushambulia kambi hiyo pamoja na maeneo mengine nyeti ya serikali.

    Mapigano hayo, yaliyoanza mapema Jumamosi, ni changamoto mpya kwa kiongozi wa kijeshi wa Niger, Jenerali Abdourahamane Tiani, ambaye serikali yake imekuwa ikikabiliana na uasi wa makundi ya wanajihadi unaoendelea kwa miaka kadhaa.

    Mamlaka za Niger zilisema jaribio hilo la uasi limedhibitiwa na kwamba vikosi vinavyoiunga mkono serikali vimerejesha hali ya utulivu.

    Shirikisho la Nchi za Sahel (AES), ambalo linajumuisha Niger, Mali na Burkina Faso, lilieleza tukio hilo kuwa ni "usaliti uliofanywa na kundi la wanajeshi waliokuwa wakijaribu kuvuruga utulivu kupitia mashambulizi yaliyolenga Kambi ya Anga 101 na maeneo mengine nyeti jijini Niamey" usiku wa tarehe 28 hadi 29 Agosti 2026.

    Katika taarifa yake, AES ilisema: "Kutokana na ushujaa na weledi wa vikosi vya ulinzi vilivyo waaminifu kwa serikali, jaribio hili jipya lilizimwa na kushindwa."

    Shirikisho hilo pia lilisisitiza kuwa linaendelea kuiunga mkono Niger katika juhudi zake za kulinda mamlaka ya nchi na kurejesha amani.

    Runinga ya taifa ya Niger ilirusha picha zikionyesha watu wanaodaiwa kuwa wanajeshi waasi wakikamatwa na Kikosi cha Walinzi wa Rais. Hata hivyo, hadi sasa hakuna taarifa rasmi iliyotolewa kuhusu idadi ya waliofariki au kujeruhiwa.

    Jenerali Tiani hajatoa kauli yoyote hadharani kuhusu tukio hilo.

    Urusi nayo ilisema ilishiriki kusaidia Niger kukabiliana na uasi huo. Katika taarifa iliyotolewa Jumapili, Wizara ya Mambo ya Nje ya Urusi ilisema Moscow inaonesha mshikamano wake na wananchi wa Niger kufuatia mashambulizi dhidi ya taasisi za serikali mjini Niamey yaliyofanywa na vikosi vinavyopinga serikali.

    Wizara hiyo iliongeza kuwa mashambulizi hayo yalizimwa na vikosi vya taifa la Niger kwa msaada wa wanajeshi wa African Corps, kikosi kinachosimamiwa na Wizara ya Ulinzi ya Urusi.

    Urusi pia iliahidi kuendelea kuisaidia Niger katika mapambano dhidi ya makundi yenye itikadi kali na kuunga mkono uhuru pamoja na maendeleo ya nchi hiyo.

    Kambi ya Anga 101, ambayo ni sehemu ya uwanja wa ndege wa kimataifa wa Diori Hamani, hutumiwa na jeshi la Niger kwa ndege na droni za kijeshi. Pia ni makao ya kikosi cha pamoja cha kupambana na ugaidi cha AES. Kwa mujibu wa Reuters, wanajeshi wa Urusi na Italia pia wana uwepo katika kambi hiyo.

    Niger, Mali na Burkina Faso, ambazo zote zinaongozwa na tawala za kijeshi, zimepunguza ushirikiano na mataifa ya Magharibi katika miaka ya hivi karibuni na kuimarisha uhusiano wake na Urusi.

    Hata hivyo, mashambulizi ya wanajihadi yameendelea kushuhudiwa katika nchi zote tatu licha ya mabadiliko hayo ya ushirikiano wa kimataifa.

    Kwa serikali ya Niger, uasi wa Jumamosi unaongeza changamoto mpya, kwani jeshi sasa linakabiliwa si tu na vitisho kutoka kwa makundi ya waasi, bali pia dalili za kutoridhika kutoka ndani ya safu zake lenyewe.

    Mamlaka zimesema ulinzi umeimarishwa katika maeneo muhimu ya Niamey, yakiwemo lango kuu la uwanja wa ndege, eneo la Ikulu ya Rais na vituo vingine vya kijeshi.

    Wakala wa Habari wa Niger (ANP) umeeleza kuwa shughuli za kawaida za biashara zimeanza kurejea, huku vituo vya mafuta, maduka na biashara nyingine zikifunguliwa tena.

    Wakati huo huo, wafuasi wa serikali ya kijeshi walikusanyika katika Uwanja wa Concertation mjini Niamey kuonesha uungaji mkono wao kwa vikosi vya ulinzi na serikali ya Jenerali Tiani.

    Mpaka sasa, mamlaka hazijathibitisha ikiwa operesheni ya kuwatafuta wahusika imekamilika wala kutangaza idadi ya wanajeshi waliohusika katika jaribio hilo la uasi.

    Soma zaidi:

  3. NASA yarusha Darubini ya Roman kuunda ramani mpya ya ulimwengu

    .

    Chanzo cha picha, NASA

    Shirika la Anga la Marekani (NASA) limeirusha Darubini ya Anga ya Roman, ambayo inatarajiwa kusaidia wanasayansi kuchora ramani ya ulimwengu na kuchunguza baadhi ya mafumbo makubwa ya fizikia, yakiwemo asili ya maada nyeusi (dark matter) na nishati nyeusi (dark energy).

    Darubini hiyo ilirushwa siku ya Jumapili saa 07:26 kwa saa za eneo husika (11:26 GMT) ikiwa ndani ya roketi ya SpaceX Falcon Heavy kutoka Kituo cha Anga za Juu cha Kennedy, Florida.

    NASA imesema hatua ya kwanza ya misheni hiyo itadumu kwa miaka mitano, huku mradi mzima ukikadiriwa kugharimu takriban dola bilioni 4.3 za Marekani. Hata hivyo, maafisa wanaamini darubini hiyo inaweza kuendelea kufanya kazi kwa muda mrefu zaidi ya kipindi kilichopangwa.

    Kwa mujibu wa NASA, Darubini ya Roman imeundwa kuwa na uwezo mkubwa wa kutazama sehemu kubwa ya anga kwa wakati mmoja, jambo litakalowezesha ukusanyaji wa taarifa nyingi kuhusu ulimwengu.

    Darubini hiyo ina kioo chenye upana wa mita 2.4, sawa na kile kinachotumiwa na Darubini ya Anga ya Hubble, lakini ina uwezo wa kuchunguza eneo kubwa zaidi la anga kwa haraka zaidi.

    Wanasayansi wanatumai itasaidia kuongeza uelewa kuhusu jinsi ulimwengu ulivyoundwa na jinsi unavyoendelea kupanuka.

    Soma zaidi:

  4. Khamenei atoa wito wa umoja wa Waislamu, aishutumu Marekani na Israel

    Mojtaba Khamenei

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Maelezo ya picha, Mojtaba Khamenei

    Mojtaba Khamenei, Kiongozi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, ametoa ujumbe maalum kuadhimisha Wiki ya Umoja wa Kiislamu, akizitaja Marekani na Israel kuwa maadui wa ulimwengu wa Kiislamu.

    Katika ujumbe huo, Khamenei amesema viongozi wa Marekani na Israel "sio maadui wa Iran pekee, bali pia ni maadui wa Umma mzima wa Kiislamu", akiongeza kuwa hata baadhi ya viongozi wa nchi za Mashariki ya Kati na Afrika Kaskazini wanaoshirikiana nao hawajasazwa.

    Pia ametoa wito kwa viongozi wa mataifa ya Kiislamu, hususan za Mashariki ya Kati na Ghuba, kutambua adui wao wa kweli, kuelewa mikakati yake na kukabiliana nayo.

    Akisisitiza umuhimu wa umoja wa Waislamu, Khamenei amesema mtu yeyote anayechochea migawanyiko au mivutano miongoni mwa Waislamu, kwa makusudi au bila kukusudia, anatekeleza malengo ya maadui wa Uislamu.

    Wiki ya Umoja wa Kiislamu huadhimishwa kila mwaka kati ya tarehe 12 na 17 Rabiul Awwal, katika Kalenda ya Kiislamu kutokana na tofauti ya tarehe ya kuzaliwa kwa Mtume Muhammad kati ya madhehebu ya Sunni na Shia. Maadhimisho hayo yalianzishwa mwaka 1981 kwa pendekezo la Ayatollah Hossein Ali Montazeri.

    Ujumbe huo umetolewa wakati Mkutano wa 40 wa Kimataifa wa Umoja wa Kiislamu ukihitimishwa mjini Tehran.

    Tofauti na viongozi wengi wa Iran waliotangulia, Mojtaba Khamenei hajawahi kuonekana hadharani tangu achukue uongozi wa nchi hiyo, huku ujumbe wa maandishi ukiwa njia kuu ya mawasiliano yake kwa umma.

    Soma pia:

  5. Guinea-Bissau yapiga kura ya maoni kuhusu katiba mpya

    .

    Wananchi wa Guinea-Bissau wanapiga kura katika kura ya maoni ya kuidhinisha katiba mpya inayopendekezwa, ambayo itapanua mamlaka ya rais na kubadilisha mfumo wa kisiasa kabla ya uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika mwezi Desemba.

    Kura hiyo inafanyika miezi kadhaa baada ya jeshi kuchukuwa madaraka kufuatia uchaguzi wa urais uliokumbwa na utata mwezi Novemba, ambapo rais wa zamani Umaro Sissoco Embaló na mgombea wa upinzani Fernando Dias walitangazia ushindi.

    Vyama vya upinzani na makundi ya kiraia vimetoa wito kwa wananchi kususia kura hiyo, vikidai kuwa inalenga kuhalalisha utawala wa kijeshi na kuongeza mamlaka ya rais.

    Wakazi waliozungumza na BBC walisema ushiriki wa wapiga kura ulionekana kuwa mdogo, huku mwandishi mmoja wa habari mjini Bissau akieleza kuwa watu wengi walijiepusha kufika katika vituo vya kupigia kura kutokana na kukosa imani na mchakato huo.

    Guinea-Bissau imekabiliwa na misukosuko ya kisiasa tangu ilipopata uhuru kutoka Ureno mwaka 1974, ikishuhudia mapinduzi na majaribio kadhaa ya mapinduzi.

    Mhadhiri wa somo la sheria na mwanaharakati wa haki za binadamu, Fodé Mané, alisema hali ya usalama siku ya kura ilikuwa ya tahadhari kubwa. Alidai kuwa wafuasi wa viongozi wa kijeshi ndio walioonekana kuwa huru zaidi kusafiri na kufanya shughuli zao, madai ambayo BBC haikuweza kuyathibitisha kwa njia huru.

    Takriban watu 915,000 wamejiandikisha kupiga kura.

    Endapo katiba hiyo mpya itaidhinishwa, mamlaka ya rais itaimarishwa na kupunguza idadi ya wabunge kutoka 102 hadi 65.

    Serikali ya mpito inasema mabadiliko hayo yataboresha utawala na kupunguza migogoro ya kiuongozi kati ya rais na waziri mkuu, lakini wakosoaji wanaonya kuwa yataidhoofisha demokrasia na kuongeza mkusanyiko wa madaraka mikononi mwa rais.

  6. Kiongozi wa upinzani wa Zambia ashtakiwa kwa uhaini

    Brian Mundubile

    Chanzo cha picha, AFP via Getty Images

    Kiongozi wa upinzani nchini Zambia, Brian Mundubile, ameshtakiwa kwa uhaini, kwa mujibu wa wakili wake, katika hatua inayokuja wakati wa mvutano wa kisiasa kufuatia uchaguzi wa urais uliopita.

    Mundubile alikamatwa Alhamisi baada ya operesheni ya usalama iliyomlazimu kujificha kwa muda. Mwanasiasa huyo alikuwa amepinga matokeo ya uchaguzi uliompa Rais Hakainde Hichilema ushindi wa muhula wa pili.

    Mamlaka zilidai kuwa chama cha Mundubile, NRPUP, kilikuwa kinapanga uasi wa kutumia silaha, madai ambayo chama hicho kimeyakanusha.

    Akizungumza Jumamosi usiku, wakili wake Milner Katolo alisema mteja wake atafikishwa mahakamani kujibu shtaka la uhaini. Aliongeza kuwa watu wengine 17, wakiwemo mgombea mwenza wa Mundubile, Makebi Zulu, pia wanakabiliwa na mashtaka hayo.

    Kwa mujibu wa matokeo rasmi, Mundubile alipata asilimia 38 ya kura katika uchaguzi wa Agosti 13, huku Hichilema akishinda kwa asilimia 60.

    Siku moja baada ya uchaguzi, vikosi vya usalama vilivamia jengo lililohusishwa na kiongozi huyo wa upinzani mjini Lusaka. Operesheni hiyo iliripotiwa kusababisha kifo cha waziri wa zamani na kuwakamata wanasiasa kadhaa.

    Baadaye Mundubile na Zulu walikimbilia katika jengo la Umoja wa Mataifa mjini Lusaka kabla ya kutiwa mbaroni na mamlaka za Zambia.

    Wakati huo huo, upinzani unasema haukuweza kuwasilisha pingamizi mahakamani dhidi ya matokeo ya uchaguzi kwa sababu mahakama zilikuwa zimefungwa siku ya mwisho wa muda wa kisheria wa kufungua kesi.

    Rais Hichilema anatarajiwa kuapishwa kwa muhula wake wa pili tarehe 1 Septemba.

    Waangalizi wa uchaguzi walisema upigaji kura ulikuwa wa amani kwa kiasi kikubwa, ingawa Tume ya Haki za Kibinadamu ya Zambia imetoa wito wa uchunguzi kuhusu watu wanaodaiwa kutoweka baada ya operesheni za usalama zilizofanyika wakati wa uchaguzi.

    Soma zaidi:

  7. Messi afunga mabao manne Inter Miami ikiifunga Montreal 7-1

    Lionel Messi amefikisha mabao 18 katika msimu huu wa Ligi Kuu ya Marekani (MLS).

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Lionel Messi amefunga mabao manne na kutoa pasi moja ya bao huku Inter Miami ikiichapa Montreal mabao 7-1 katika mechi ya Major League Soccer (MLS), na kurejea kwenye njia ya ushindi baada ya kipindi kigumu cha matokeo.

    Nyota huyo wa Argentina mwenye umri wa miaka 39 aliifungia Miami mabao manne, likiwemo bao la mpira wa adhabu na hat-trick yake katika kipindi cha pili, huku pia akimsaidia Luis Suarez kufunga.

    Ushindi huo ulikuwa wa kwanza kwa Miami baada ya kushinda mechi moja pekee katika michezo saba tangu kurejea kwa Messi kutoka Kombe la Dunia la Klabu mapema mwezi huu.

    Hii ilikuwa mara ya kwanza kwa Messi kufunga mabao manne katika mechi ya MLS na kumfikisha mabao 18 msimu huu, hivyo kuwa kinara wa ufungaji wa ligi hiyo.

    Kocha wa muda wa Inter Miami, Guillermo Hoyos, alimsifu Messi akisema: “Hakuna maneno ya kuelezea uzuri wa soka kama huo.”

  8. Mgomo JKIA: Baadhi ya safari za ndege nchini Kenya zacheleweshwa

    Wasafiri katika Uwanja wa Kimataifa wa JKIA

    Chanzo cha picha, Reuters

    Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Kenya (KAA) imetangaza kuwa baadhi ya ndege zinazoondoka katika viwanja vya ndege nchini humo zitachelewa.

    Kupitia taarifa iliyotolewa Jumapili, KAA imesema inashirikiana kwa karibu na mashirika ya usafiri wa anga, kampuni za ndege na wadau wengine katika sekta hiyo ili kudhibiti hali hiyo, kupunguza usumbufu kwa wasafiri na kuhakikisha shughuli za viwanja vya ndege zinaendelea kwa ufanisi.

    Mamlaka hiyo imewashauri abiria kuwasiliana na kampuni zao za ndege ili kupata taarifa za hivi karibuni kuhusu ratiba za safari zao na kupanga safari zao ipasavyo.

    KAA pia imeomba radhi kwa usumbufu unaotokana na ucheleweshaji huo na kuwashukuru abiria kwa uvumilivu wao wakati juhudi za kurejesha hali ya kawaida zikiendelea.

    Mamlaka hiyo imesema itaendelea kutoa taarifa zaidi kadri hali itakavyoendelea kubadilika.

  9. Netanyahu alaani vurugu za walowezi Ukingo wa Magharibi

    Netanyahu

    Chanzo cha picha, Reuters

    Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu amelaani mashambulizi yaliyofanywa na walowezi wa Israel dhidi ya vijiji vya Wapalestina vya Qusra na Jalud katika Ukingo wa Magharibi unaokaliwa kwa mabavu.katika tukio la hivi punde la mivutano ambayo imedumu kwa karibu wiki tatu.

    Katika hatua isiyo ya kawaida, Netanyahu alilaani kile alichokiita "vitendo vya uhalifu na vurugu" vilivyofanyika katika vijiji viwili vya Wapalestina siku ya Jumamosi. Aliwataja walowezi hao kama "kundi dogo la wahuni wasioheshimu sheria."

    Katika taarifa, alisema, "Ninelaani vikali vitendo vya uhalifu na vurugu vilivyofanywa katika vijiji vya Qusra na Jalud na wahuni wachache wasioheshimu sheria; watu ambao wanaitendea dhuluma kubwa jamii ya Wayahudi wanaoheshimu sheria, wanazuia kazi ya jeshi la Israel katika kutekeleza majukumu yake, na kuharibu taswira ya Israel katika nyanja ya kimataifa."

    Rais wa Israel Isaac Herzog alilaani vurugu hizo, akizielezea kama "uvukaji wa mstari mwekundu uliofanywa na watu wanaokiuka sheria, ambao wanatenda kinyume kabisa na sheria na maadili ya Taifa la Israel," na kusema kuwa kilichotokea ni "doa kwa sifa ya Israel."

    Wakazi wa Qusra na jeshi la Israel walisema kuwa makumi ya walowezi walivamia kijiji hicho, wakawarushia mawe wakazi na kuwalazimisha baadhi yao kujifungia majumbani mwao.

    Ripoti zaidi zinasema walowezi wa Israel waliovaa barakoa waliwashambulia na kuwajeruhi wafanyakazi wa NBC News pamoja na mwanamke Mpalestina katika kijiji cha Jalud, karibu na Qusra, katika Ukingo wa Magharibi unaokaliwa.

    Wakati huo huo, raia mmoja Mpalestina mwenye uraia wa Marekani alikuwa akielekea Qusra akisema anataka kufika kwa familia yake iliyokuwa imezingirwa na walowezi.

    Jeshi la Israel limesema lilituma wanajeshi na polisi wa mpakani eneo hilo baada ya kupokea taarifa za makabiliano kati ya waandamanaji wa Israel na Wapalestina, yaliyojumuisha kurushiana mawe.

    Soma pia:

  10. Kim Jong Un amfuta kazi Waziri wake wa Ulinzi

    Gwaride la jeshi la Korea Kaskazini

    Chanzo cha picha, Reuters

    Rais wa Korea Kaskazini, Kim Jong Un, amemfuta kazi Waziri wa Ulinzi na kufanya mabadiliko kadhaa katika ngazi za juu za jeshi, kulingana na vyombo vya habari vya serikali.

    Shirika la habari la KCNA limesema uamuzi huo ulifikiwa katika mkutano ulioongozwa na Kim Jong Un, ambapo viongozi walijadili kile kilichoelezwa kuwa mpango wa marekebisho ya muundo wa jeshi.

    Kwa mujibu wa KCNA, Noh Kwang-chul ameondolewa katika wadhifa wa Waziri wa Ulinzi na kushushwa cheo kuwa naibu mkuu wa kwanza wa Idara ya Viwanda vya Silaha ndani ya chama tawala.

    Nafasi hiyo sasa itashikiliwa na Kim Song-gi, ambaye alikuwa mkuu wa Idara Kuu ya Siasa ya Jeshi la Watu wa Korea.

    Katika mabadiliko hayo, mshauri wa masuala ya ulinzi wa Kim Jong Un, Pak Jong-chun, ameteuliwa kuwa makamu mwenyekiti wa Tume Kuu ya Kijeshi pamoja na kuwa mjumbe wa Politburo ya Chama cha Wafanyakazi wa Korea.

    Vyombo vya habari vya serikali havikutoa sababu za mabadiliko hayo. Hata hivyo, hatua hiyo imekuja wakati Korea Kaskazini ikiendelea kuimarisha uwezo wake wa kijeshi na kuimarisha ushirikiano wa kiulinzi na Urusi, huku mvutano katika Rasi ya Korea ukiendelea.

    Pia unaweza kusoma:

  11. Tishio dhidi ya mwana wa Netanyahu lasababisha kuondolewa kwake Marekani - ripoti

    Netanyahu

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Vyombo kadhaa vya habari vya Israel vimeripoti kuwa shirika la usalama wa ndani la nchi hiyo, Shin Bet, limethibitisha kile lilichokitaja kuwa tishio kubwa dhidi ya Yair Netanyahu, mwana wa Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu.

    Kwa mujibu wa ripoti hizo, tathmini ya usalama ilisababisha uamuzi wa kumhamisha Yair Netanyahu kutoka Marekani kwenda Israel pamoja na kikosi chake cha ulinzi.

    Taarifa hizo zimekuja baada ya kuibuka kwa ripoti kuhusu safari yake ya dharura kutoka Florida kwenda Israel. Shin Bet haijatoa maelezo zaidi kuhusu asili ya tishio lililoripotiwa au waliotuhumiwa kuhusika.

    Hivi karibuni, Benjamin Netanyahu alidai kuwa Iran ilikuwa imejaribu kumuua mmoja wa wanawe, ingawa hakumtaja kwa jina wakati huo. Ripoti za sasa zinaeleza kuwa alikuwa akimuashiria Yair Netanyahu.

    Kwa upande wake, Iran imewahi kukanusha madai ya kuhusika katika njama za mauaji dhidi ya viongozi au watu mashuhuri wa kisiasa wa Marekani na Israel.

    Kufikia sasa, Tehran haijatoa tamko rasmi kuhusu taarifa hiyo ilizoripotiwa na vyombo vya habari vya Israel.

    Maelezo zaidi:

  12. Mbunge wa Marekani: Trump na washirika wake wamenufaika na vita dhidi ya Iran

    Donald Trump

    Chanzo cha picha, Reuters

    Maelezo ya picha, Rais wa Marekani Donald Trump

    Seneta wa chama cha Democratic, Elizabeth Warren, amemtaja Donald Trump kuwa "rais fisadi zaidi katika historia ya Marekani" wakati akimkosoa kuhusu sera zake kuhusiana na Iran na sekta ya mafuta.

    Akizungumza katika mkutano wa kampeni, Warren alidai kuwa baadhi ya makampuni makubwa ya mafuta yaliyounga mkono kampeni ya Trump yamenufaika pakubwa kutokana na vita dhidi ya Iran.

    "Donald Trump anapoanzisha vita na Iran na marafiki zake wa sekta ya mafuta, ambao walichangia kampeni yake, wakipata faida kubwa kutokana na vita hivi, ni wajibu wetu kufichua hali hiyo na kuipinga," alisema Warren.

    Warren hakutaja kampuni yoyote mahsusi kuhusiana na madai hayo. Wakati huo huo, ongezeko la bei ya mafuta na faida kubwa zilizoripotiwa katika baadhi ya kampuni za sekta ya nishati limekuwa likifuatiliwa kwa karibu na wachambuzi katika miezi ya hivi karibuni.

    Hata hivyo, hakuna ushahidi uliowasilishwa unaothibitisha moja kwa moja madai ya Warren kuhusu uhusiano kati ya michango ya kampeni na faida zinazodaiwa kupatikana kutokana na vita hivyo.

    Kwa upande wake, Trump amewahi kukosoa kupanda kwa bei ya mafuta na kuwataka wazalishaji kuongeza uzalishaji ili kusaidia kudhibiti bei.

    Soama zaidi:

  13. Natumai hujambo. Karibu kwa matangazo ya moja kwa moja.