Watu 31 wafariki baada ya lori ya mafuta kupata ajali mjini Cairo

Chanzo cha picha, Getty Images
Watu 31 wamefariki na wengine 21 kujeruhiwa baada ya moto mkubwa kuzuka kwenye barabara moja kuu mjini Cairo, Misri.
Ajali hiyo ilitokea baada ya lori ya mafuta kupenduka na kusababisha ajali, kwa mujibu wa Wizara ya Afya ya nchi hiyo.
Hospitali zilizo karibu zilipokea majeruhi waliokuwa na majeraha ya kuungua na matatizo ya kupumua kutokana na kuvuta moshi baada ya tukio hilo lililotokea jana jioni, katika barabara iliyoko eneo la Warraq.
Video zilizosambazwa kwenye mitandao ya kijamii zilionyesha miale mikubwa ya moto na moshi mweusi ukipaa juu angani, huku magari kadhaa yaliyokuwa karibu yakiteketea.
Maafisa hawajatoa maelezo rasmi kuhusu chanzo cha moto huo. Hata hivyo, vyombo vya habari vinavyomilikiwa na serikali vimeripoti kuwa lori hilo la mafuta lilipinduka na kumwaga petroli kwenye magari yaliyokuwa karibu.
Mwendesha mashtaka mkuu wa eneo hilo ameanzisha uchunguzi kuhusu tukio hilo na kuagiza sampuli za vinasaba (DNA) zichukuliwe kutoka kwa miili ya waliofariki.
Gazeti la serikali la Al-Ahram limeripoti, likinukuu vyanzo vinavyofahamu uchunguzi huo, kuwa lori hilo lililokuwa likimilikiwa na kampuni binafsi lilikuwa likisafiri kwenye barabara hiyo, wakati nyaya za umeme zilianguka mbele yake na kumfanya dereva ashindwe kulidhibiti gari hilo.

