Kwa nini kufikiria kifo chako kunaweza kuwa na faida?

.

Chanzo cha picha, Getty Images

Iliyochapishwa
Muda wa kusoma: Dakika 2

Kila aliye hai leo wewe, marafiki zako na familia yako siku moja hatutakuwepo.

Ni ukweli usioepukika, lakini mara nyingi tunajitahidi sana kuupuuza au kutokubali ukweli huo. Jules Howard anaeleza kwa nini huenda kufanya hivyo si jambo zuri.

Kulingana na data kutoka kampuni ya Statista, ni asilimia 11 pekee ya watu wanaofikiria kuhusu kifo katika maisha yao ya kila siku. Wengi wetu tumejikita zaidi katika mambo ya maisha, kiasi kwamba huenda tukafikiria kuhusu kifo mara tatu au nne tu kwa mwaka.

Lakini hilo linaeleweka, sivyo? Kifo ni jambo la kutisha. Tunaishi. Tunakufa. Na hapo ndipo kila kitu kinaishia. Kwa hiyo, kuna sababu gani ya kufikiria zaidi kuhusu kifo?

Kwa mujibu wa baadhi ya wanasayansi, kuna faida za kufikiria zaidi kuhusu kifo.

Wanasaikolojia, hasa, wanaelekeza kwenye tafiti kadhaa zinazoonyesha kuwa kufikiria kuhusu kifo au "ufahamu wa kufa" kunaweza kuongeza hali ya mtu ya kujithamini, kuwafanya watu wasizingatie sana masuala ya pesa, na hata kuwafanya wawe wachangamfu na wenye ucheshi zaidi.

Kuhamasishwa kwa tafiti kama hizi, kumeibuka harakati za kijamii kama vile Death Cafés na kundi la Death Salon, ambazo huwapa watu nafasi ya kukutana na kuzungumza kwa uwazi kuhusu kifo.

Kwa namna nyingi, makundi haya yanafanana na falsafa za Mashariki ambazo kwa karne nyingi zimewahimiza watu kutafakari kuhusu kifo na udhaifu wa maisha ya mwanadamu.

Kwa mfano, Buddha alikuwa akihimiza kile kinachojulikana kama "kutafakari maiti", ambapo watu hutazama miili ya watu waliokufa katika hatua mbalimbali za kuoza.

Katika dhana ya "yin na yang" wazo la vitu viwili vinavyopingana kama "mwanga na giza", "moto na maji" na "maisha na kifo" inaonekana kuwafanya watu katika jamii kuthamini zaidi mambo ya kawaida ya kila siku .

Je, tunafikiria kuhusu kifo kwa njia isiyo sahihi? Ningesema, hapana. Kwa sababu hakuna njia "isiyo sahihi" ya kufikiria kuhusu kifo.

Lakini bila shaka, tunaweza kufikiria zaidi kuhusu kifo. Si lazima sana, bali kiasi ambacho kila mmoja wetu anaona inafaa. Kwa kufanya hivyo, mtazamo wetu kuhusu matukio ya kila siku inaweza kuboreka, hata kama kwa namna isiyodhihirika sana.

Kwa maana, kwa wale wanaotambua kwamba maisha hayadumu milele, hufurahia vitu vidogo maishani